Home Habari Ubora, udhaifu TPL 2018/19

Ubora, udhaifu TPL 2018/19

1157
0
SHARE

NA ZAINAB IDDY

MSIMU huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unazidi kuyoyoma, huku vita kali ikibaki kwa vigogo Yanga, Simba na Azam zinazouwania ubingwa.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa wababe hao, tayari African Lyon imeshashuka daraja licha ya kuwa na mechi nne mkononi.

Kama ilivyo kawaida, msimu wa 2018/19 ulikuwa na mambo mengi ya kupendeza na mengine ya kukwaza. Hivyo basi, katika mahojiano yao na RAI, makocha 20 wa timu zilizoshiriki TPL msimu huu wameibua kasoro na ubora walioubaini.

Abdallah Mohammed ‘Bares’ (JKT Tanzania)

“Udhaifu wa ligi msimu huu upo katika utoaji taarifa. Msimu uliopita hadi kipindi hiki tulikuwa tunajua timu nne zitashuka daraja lakini safari hii ni tofauti.

“Katika dakika za mwisho wa ligi, ndiyo tunaambiwa mbili zinashuka moja kwa moja na mbili zinakwenda kucheza ‘Play Off’ na zile za daraja la kwanza.

“Juu ya ubora, msimu huu ligi imekuwa ngumu, kila timu inahitaji ushindi ndiyo maana kwenye msimamo timu zimepishana alama chache.”

Abdul Migange (Azam FC)

“Kuongezeka kwa idadi ya timu kumeifanya ligi kuwa bora kwani wachezaji wanapata mechi nyingi za kucheza na kuimarika zaidi.

“Kwa upande wa udhaifu, kwangu sijayaona sana kwa kuwa ni ya kawaida na kila msimu yapo. Kikubwa ni TFF ijitahidi kuyafanyia marekebisho ili yasijirudie kila msimu.”

Abdulmutik Haji (Ruvu Shooting)

“Ubora upo katika ushindani ulioonekana tangu mwanzoni mwa msimu hadi sasa  lakini kwenye mapungufu ukiondoa matatizo ya waamuzi limeongezeka suala la ukata kwani tulisikia kuna timu ilishindwa kurejea kwao hadi pale ilipochangiwa.”

Aldof Rishard (Tanzania Prisons)

“Ratiba haikuwa rafiki kwa timu nyingi za Ligi Kuu msimu huu na hili liliifanya ligi isiwe na mvuto kutokana na wachezaji kucheza chini ya kiwango kwa kuwa hawana muda wa kupumzika.”

Ally Bizimungu (Mwadui FC)

“Ligi ya msimu huu haijawa bora zaidi ya iliyopita na hii imetokana na timu kuwa na ukata wa mara kwa mara. Ni kutokana na ligi kukosa wadhamini.

“Msimu uliopita, kulikuwa na njaa lakini wadhamini wachache waliokuwepo waliweza kusaidia. Lakini pia, maamuzi mabovu ya waamuzi yameiharibu ligi.

“Kwa upande wa ubora, licha ya ukata uliopo, bado wachezaji wameendelea kujituma uwanjani na hivyo kuifanya ligi kuwa ngumu.”

Amri Said ‘Stam’ (Biashara United)

“Ubora wa Ligi ni kwamba hakukuwa na timu iliyotaka kufungwa kirahisi lakini udhaifu ulioonekana ni kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kushindwa kuyatatua kwa wakati matatizo au kesi zinazopelekwa.

“Mfano, hadi sasa zipo kesi za baadhi ya timu kufanyiwa fujo zilipokwenda ugenini, waamuzi kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka…”  

Athuman Bilali ‘Bilo’ (Stand United)

“Ubora wa ligi msimu huu upo katika maandalizi ya timu kwani kila moja ilijitahidi kukiandaa kikosi chake na kukifanya kiwe na ushindani mkubwa, kiasi kwamba hata unapopata alama tatu unakuwa umezitolea jasho.

“Kwa upande wa udhaifu, ni kamati ya waamuzi ambayo imeleta watu wasio makini na wanaovuruga mechi, hivyo kupoteza ladha ya mashindano.”

Ettiene Ndayiragije (KMC)

“Msimu huu wa ligi ulikuwa na changamoto nyingi ndani na nje ya viwanja, ikiwamo ubovu wa viwanja katika baadhi ya mikoa, ukata kwa baadhi ya timu, maamuzi mabovu na upangaji wa ratiba.

“Lakini kwa upande wa ubora tumeona jinsi timu zilivyojituma kiasi cha kuyafanya mashindano kuwa magumu.”

Felix Minziro (Singida United)

“Sijaona tofauti yoyote katika ubora na udhaifu wa ligi msimu huu kwani matatizo ya siku zote yapo pale pale ambayo hata hivyo hayaondoi ushindani uliozoeleka.”

Jabir Suleiman (African Lyon)

“Licha ya changamoto lukuki zilizojitokeza, ligi kuu msimu huu, ikiwamo waamuzi kuingia na matokeo mfukoni, ukata na hata ratiba mbovu, ubora ulionekana kwani kila timu ilicheza kwa kujituma na kuonyesha ushindani.”

Juma Mgunda (Coastal Union)

“Ubora wa ligi msimu huu upo katika ushindani unaoonesha na kila timu, kila moja ikihitaji alama tatu na udhaifu ni waamuzi wanaofanya kazi nje ya taaluma yao.”

Khalid Adam (Ndanda FC)

“Udhaifu wa ligi upo kwa waamuzi na ratiba kutokuwa rafiki kwa timu zetu na hili linatuumiza sana sisi wa hali ya chini. Utakuwa Ndanda inatakiwa kucheza Dar es Salaam Jumamosi kisha iende Mara lakini pia irejee Mbeya kipindi hicho tunatumia basi. Huku ni kuwaumiza wachezaji.

“Kwa upande wa ubora, ligi imeweza kuwajenga wachezaji wetu kwa kuwa wanacheza mechi nyingi, tofauti na misimu iliyopita.”

Malale Hamsini (Alliance FC)

“Ubora wa ligi msimu huu upo viwanjani kwani kila timu imejipanga kupata matokeo, jambo lililosababisha hadi sasa isijulikane timu gani inashuka, tofauti na msimu uliopita.

“Kwa upande wa udhaifu, ni upangaji wa ratiba kwani licha ya kupigiwa kelele mara kwa mara, bado imeendelea kutokuwa rafiki kwa baadhi ya timu.”

Mecky Maxime (Kagera Sugar)

Mecky Maxime kocha wa Kagera anasema: “ Ubora wa ligi ya msimu umeonekana  kwenye ushindani ulionyeshwa na timu zote kwani wale wadogo hawapo tayari kufungwa na wakubwa, lakini kwenye madhaifu ni yale yale ya siku zote hivyo TFF inapaswa kuyafanyia kazi.”

Mwinyi Zahera (Yanga)

“Udhaifu uliojitokeza kwenye ligi ni waamuzi wanaozibeba baadhi ya timu na ratiba.

“Haiwezekani baadhi ya timu zicheze mechi zaidi ya 20, huku zingine zikicheza 10 tu, huku ni kupanga matokeo.”

Patrick Aussems (Simba)

“Ligi si mbaya kwa kuwa inaonesha ugumu kila unapokutana na timu nyingine lakini ratiba ni ratiba kwani si rafiki kwa Simba.

“Simba imekuwa ina ratiba ngumu msimu huu kwani imetoka kucheza mechi za kimataifa inakuja kwenye ligi ina mechi za viporo zaidi ya 10, huku ni kuwaumiza wachezaji. Msimu ujao TFF waliangalie hili hata kama wahusika si Simba.”

Ramadhan Nsanzurwimo (Mbeya City)

“Ligi ya msimu huu ina udhaifu mkubwa, hasa kwa upande wa waamuzi ambao wameshindwa kutafsiri sheria 17 za mchezo na hivyo kuzibeba baadhi ya timu kongwe.

“Kwa upande wa ubora msimu huu, sijaona kama ligi ni bora kwa kuwa kila siku unasikia timu zimekwama kusafiri, wachezaji wameshinda na kulala na njaa, wachezaji wanagoma na mengine mengi.”

Salum Mayanga (Mbao FC)

“Ligi ya msimu huu haina tofauti na ile iliyopita katika suala la ubora na mapungufu kwani ushindani upo pale pale na matatizo ya waamuzi na ratiba pia hayajamalizika.”

Seleman Matola (Lipuli FC)

“Udhaifu upo katika suala la fedha na hii imekuja baada ya msimu huu kukosekana kwa mdhamini mkuu.

“Kwa upande wa ubora, bado suala la ushindani limeendelea kuwepo licha ya ukata unaoziadhibu timu zetu.”

Zuber Katwila (Mtibwa Sugar)

“Kwa msimu huu, sijaridhishwa na waamuzi waliopewa jukumu la kuchezesha kwani wanaharibu burudani ya soka. Ingekuwa ni maamuzi yangu, kuna baadhi ya waamuzi, hasa wa kati, wangefungiwa.

“Kuhusu ubora wa ligi msimu huu, bado sijaona kwani licha ya timu nyingi kupambana uwanjani zinakwamishwa na miundombinu mibovu, ukata na ratiba mbovu.”