Home Habari Ubunge CCM mgumu 

Ubunge CCM mgumu 

1852
0
SHARE

MWANDISHI WETU

NAFASI ya kuwania uongozi na hasa ubunge  ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye chaguzi zijazo ukiwamo uchaguzi Mkuu ujao, kwa sasa inatajwa kuwa ngumu kuliko nyakati zote ambazo chama hicho kimepitia.

Ugumu wa jambo hilo hilo unatajwa kusababishwa na misimamo ya viongozi wa juu wa chama hicho, ambao kwa kiasi kikubwa wanaamini kiongozi ni yule anayekubalika machoni pa watu bila kuwashawishi.

Mbali na imani hiyo, lakini pia mbele ya wakubwa hao wa chama, imani yao ni kuona kila kiongozi haongozwi na tama na uchu wa madaraka bali ni dhamira ya kweli ya kuwatumikia wananchi hasa wale waliomchagua.

Tayari Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dk. John Magufuli ameshawaonya viongozi wa kuteuliwa hasa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na wakurugenzi wao, kuacha tamaa ya madaraka.

Akiwa katika moja ya vikao vya ndani vya chama hivi karibuni, Rais Magufuli  alimtaja Naibu waziri wa zamani wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Mkuu wa mkoa wa zamani wa Tabora, Ludovick Mwananzila kuwa ni mwenye tamaa nyingi sana.

Mwananzilia alishika nafasi ya Unaibu Waziri katika  awamu ya kwanza ya utawala wa Serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Jakaya Kikwete na katika awamu ya pili ya utawala wa Kikwete aliteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa  baada ya kukosa ubunge mwaka 2010.

Mwaka 2015 alirejea tena kwenye siasa hata hivyo alianguka hatua ambayo imetafsiriwa na Mwenyekiti wa CCM kama tamaa ya madaraka huku akijua wazi Watanzania wako zaidi ya milioni 50.

“Palikuwepo Mwananzila,  alikuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora, alikuwa Naibu Waziri baade akateuliwa na mzee Kikwete akawa mkuu wa Mkoa, akaona ukuu wa Mkoa hautoshi, akaenda kugombea kwenye jimbo, kule akashindwa, sio kwamba Mwananzila nilikuwa simjui, nilikuwa namjua , lakini nikaona huyu ni mtu mwenye tamaa  sana, hafai hata Katibu Tarafa, na ndio maana Mwananzila amepotea.

“Kwa hiyo hawa wanaojipanga kwenda kugombea,  Wakurugenzi, sijui ma RC wanani,  ninyi waacheni tu nendeni kule, chapeni kazi zenu,  nataka niwahakikishie, kwa sababu huwezi ukawa na vyote, Watanzania tuko milioni 55, nyie chapeni kazi zenu.”

Kauli hiyo ya Rais na Mwenyekiti wa CCM, inatajwa kuzidisha ugumu wa nafasi ya ubunge ambayo inatazamwa kama njia rahisi ya kisiasa ya kuonekana machoni pa viongozi wa nchi.

Kauli ya Mwenyekiti wa CCM imewiana kabisa na ile iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa chama hicho  Dk. Bashiru Ally, ambaye amewawekea ugumu wanachama waliojipanga kununua kura ili wateuliwe kugombea nafasi za udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Dk. Bashiru ameweka wazi kabisa kuwa watakaonunua kura za uteuzi, wajiandae kwa vita kali kwani kuna baadhi ya watu ndani ya CCM, wana ugonjwa wa vyeo na tayari orodha ya wagombea nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo ile ya urais wa Zanzibar huku wengine wakijificha kwenye kivuli cha kutoa misaada na zawadi wanayo.

Alisema watu hao wameshafunguliwa mafaili, kinachosubiriwa ni muda tu wa kushughulika nao.

Aliitangaza vita hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita  jijini Dodoma, katika mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari, baada ya kuulizwa swali kuhusu uwepo wa makundi ya watu wanaoanza kupanga safu za kuwania uongozi.

“Mimi Bashiru sina umaarufu ndani ya CCM, nguvu na uwezo inayotoka ndani yangu ni ya CCM, labda niseme hapa hapa kwa sababu nimeyasikia yanayosemwa barabarani kwa namna nyingine, maana ndani ya CCM, baadhi ya watu wana ugonjwa na vyeo vya urais.

“Tupo mwaka 2019, mtu amepanga safu ya urais ya mwaka 2025, kule Zanzibar kuna watu wanatafuta urais, sasa wamepasua visiwa vyote, mpasuko wa Pemba na Unguja haujaisha.

“Unguja kule kuna wanaoutafuta urais wa Unguja Kaskazini, kuna wanaotafuta urais wa Unguja Kusini na kuna wanaotafuta urais wa Unguja Mjini na Pemba,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Bashiru alisema watu hao wasitegemee kubebwa na viongozi wa ngazi za juu ndani ya CCM, kwani jukumu kubwa ni kuhakikisha katiba, umoja unalindwa ndani ya chama hicho kikongwe barani Afrika.

“Sikubebwa na sitabeba mtu, Rais Dk. John Magufuli hajabebwa na hatabeba mtu, Rais Dk. Shein hajawahi kubebwa na hatabeba mtu, Mzee Philip Mangula hana haja ya kubebwa, anasimamia uongozi aliopewa.

“Hao ndio viongozi wanne kikatiba na wote wana uwezo wa kichama, kazi tatu kubwa tunazifanya, kwanza kuhakikisha tuna umoja ndani ya chama na tunauimarisha kwa kuwaondoa watu wanaotafuta uongozi kwa ajili ya maslahi, kwa hiyo hakuna CCM ya Bashiru wala Magufuli, ni CCM ya wanachama. Mtu aliyejiandaa kununua kura kupitia CCM kwa kuteuliwa katika ngazi yoyote, anajiandaa kwa vita kali,” alisisitiza.

Dk. Bashiru alisema hatua hiyo ni katika kuhakikisha misingi ya kidemokrasia inazingatiwa wakati wa mchakato mzima wa uteuzi ndani ya chama.

Akijibu madai ya baadhi ya watu kutaka Rais Dk. Magufuli aongezewe muda wa kubaki madarakani baada ya muda wa kikatiba wa miaka 10 kumalizika na wale wanaodai kuwa Dk. Bashiru amekirejesha chama kwenye mstari wakati wengine walikibomoa, alisema CCM ina taratibu zake.

“Nimeshatolea ufafanuzi, Rais Magufuli anafanya maajabu na  miujiza, hivyo miaka 10 haimtoshi, mitano hajamaliza na sisi ndani ya chama anatakiwa kuomba ridhaa kwa mujibu wa katiba.

“Unazungumziaje miaka 10 kwamba haitoshi. Kuna minong’ono hiyo hiyo, kwamba Bashiru amekiweka chama pazuri, wengine walikiua. Mimi si  muuaji wala si mkombozi wa CCM, mimi ni mtumishi tu, tena utumishi wangu si wa kuchaguliwa, saa yoyote naweza nikatoka, wenzangu wengine wa kuchaguliwa ni miaka mitano, anaweza kuondolewa kwa sababu fulani ya kimaadili, mimi wala hutikisi nchi kuniondoa,” alieleza Dk. Bashiru.

Katibu Mkuu alisisitiza: “Nitaondoka kama nilivyoingia bila ya kubebwa, lakini nikiwa nimekalia kiti hiki, nitasimamia umoja wa chama, fikra ya chama na chama kukubalika kwa umma.

“Hii ndio naitafuta, mtusaidie chama kikubalike kwa umma, kama CCM ingekuwa inakufa, ingekufa baada ya Mwalimu (Julius Nyerere) kuondoka, jabali lile la kisiasa hata yeye aliwahi kusema CCM si mama yake, sasa Bashiru mimi kiduchuduchu hata mwaka mmoja sijamaliza mimi ni nani?”

Aidha, alisema akiondoka katika nafasi yake, hatoshika cheo chochote cha kuteuliwa wala kuchaguliwa kisiasa, atarejea darasani kufundisha.

Vile vile, alibainisha kuwa, utaratibu wa wagombea nafasi za kisiasa ndani ya chama kupigwa kura za maoni, umebadilika ambapo sasa watapigiwa kura na wajumbe wachache.

Alisema utaratibu hautakuwa kama wa awali, wagombea walipigiwa kura za maoni kwenye jimbo zima, lengo la kufanya hivyo ni kupunguza gharama na kuhakikisha haki inapatikana.

“Wagombea watachujwa, maana wapo wengine wanahesabu, wanakwenda na namna wajumbe kama wapo 700, kwa hiyo anajiwekea anao wajumbe 450, yeye atakuwa namba moja. Wapo wengine ambao hawataona hata sanduku la kura katika mchujo, kwa hiyo waache kufanya kazi ya unajimu.

“Lakini hata watakaoshinda kura za maoni, wasishangilie mpaka wateuliwe, kuna uzoefu kura zimerudiwa katika maeneo fulani na kuna uzoefu watu wameshinda kura za maoni na hawakuteuliwa. Kazi kubwa ni kuhakikisha mchakato huo unatenda haki, huo ndio mtihani,  unaweza kuwa wanne na ukateuliwa wa kwanza, wa pili wa tatu wakaongoza kura za maoni wasiteuliwe,” alisema.

Aliongeza: “Tumefanya hivyo Korogwe Vijijini, Songea Mjini kwenye uchaguzi mdogo na ukitaka kuthibitisha kwa nini hatujakuteua na ukitaka isiwe siri, tunakutangaza. Kuna wale wanaopitapita wengine wana makambi ya vijana, wanapeleka khanga na mashuka zimeandikwa majina yao, wengine wanapeleka mpaka hospitali za umma zimeandikwa majina yao. Tumewafungulia mafaili na mtunzaji wa mafaili hayo mnamjua? Ni Mzee Mangula, tunataka kuwapa wananchi uongozi wanaostahili.”