Home Makala UCHAFUZI WA HEWA

UCHAFUZI WA HEWA

3815
0
SHARE

Matumizi ya kuni ni mojawapo ya vyanzo vya uchafuzi wa hali ya hewa

*Afya za wakazi mjini zinatafunwa

NA GABRIEL MUSHI


Oktoba 30, mwaka huu, Shirika la Afya Duniani (WHO),  linatarajia kuwa na mkutano wa dunia kuhusu uchafuzi wa hali ya hewa. Katika mkutano huo ambao unatarajiwa kufanyika Geneva- Uswiss, wadau kutoka nchi mbalimbali, watajadili madhara ya uchafuzi wa hali hewa na namna yanayoathiri binadamu.

Kwa hakika uchafuzi wa hali ya hewa umeendelea kuwa tatizo sugu katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea, na huibua mjadala mpana kadiri siku zinavyosonga mbele, lakini madhara yake yameendelea kuitafuna dunia ikiwamo Tanzania ambayo kwa namna moja au nyingine, inaelekea bado haijatambua athari zake kinagaubaga.

Ikumbukwe kuwa uchafuzi wa hewa kwa asilimia kubwa, hunatokana na vitu vinavyochomwa moto. Moshi wenye kaboni monokside (hewa ukaa), ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya hali ya hewa. Moshi unaotolewa na vyombo vya moto, una hewa  nyingi zenye madhara kama vile, salfa, nitrojini dioksidi na haidrokabon amabayo ni sumu.

Vilevile uchomaji wa plastiki husambaza gesi za sumu hewani. Njia nyingine za uchafuzi wa hewa ni uozaji wa takataka ambazo huzalisha mitheni ambayo ina madhara zaidi kuliko gesi ya ukaa.

Kutokana na hali hiyo, ripoti mbalimbali zinadhibitisha kuwa uchafuzi wa hali ya hewa umeendelea kuwa hatari kwa afya ya binadamu na viumbe vingine.

Katika Ripoti ya Malengo ya Ustawi Endelevu – 2018 iliyotolewa hivi karibuni na WHO, ilibainisha kuwa uchafuzi wa hali ya hewa unakadiriwa kusababisha vifo visivyotarajiwa milioni saba kila mwaka duniani kote na kwa mwaka 2016 pekee ulisababisha vifo milioni 4.2 duniani kote

Pia ripoti hiyo ilibainisha pia kuwa asilimia 91 ya idadi ya watu duniani, wanaishi katika mazingira ambayo muongozo wa shirika hilo la afya katika ubora wa hewa, umezidi kiwango chao na kusababisha watu tisa kati ya 10 duniani kote kuvuta hewa isiyo safi.

Katika ripoti hiyo pia, ilibainisha kuwa uchafuzi wa hewa katika miji unaongeza hatari ya mtu kuugua saratani ya ini, mapafu; kuugua pumu na magonjwa mengine kama ya moyo ambayo husababisha kufariki zaidi ya watoto milioni tatu kabla ya kutimiza muda wa kuzaliwa.

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo ilibainisha kuwa, katika kipindi cha kati ya mwaka 2000 na 2014, jamii ya watu wa mjini waliokuwa wakiishi katika maeneo yasiyofaa na yenye msongamano mkubwa wa watu duniani, ilifikia milioni 883.

“Uchafuzi wa hali ya hewa unachangia asilimia 25 ya vifo na magonjwa yatokanayo na saratani ya ini, asilimia 17 ya vifo na mfumo wa upumuaji, asilimia 16 kutokana na kiharusi (stroke), asilimia 15 vifo na magonjwa ya moyo,” ilisema ripoti hiyo.

Wataalam: Madhara ya uchafuzi yanakuja kwa kasi

Ni dhahiri uchafuzi wa hali ya hewa sasa unazidi kuzorotesha afya za watanzania. Hoja hii inadhihirishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Crispin Kahesa ambaye anasema licha ya saratani itokanayo na vijidudu kuendelea kuongoza kwa asilimia 60, sasa hali ni tofauti kwani saratani inayosababishwa na vyanzo vitokanavyo na mfumo wa mazingira kama vile kemikali nayo imeanza kuja kwa kasi.

Anasema tatizo la saratani limekuwa likiongezeka siku kwa siku kwani taasisi hiyo inapokea wagonjwa wapya 6,000 kwa mwaka tofauti na miaka iliyopita ambayo ilikuwa ni wagonjwa 2,000 pekee wapya.

Anasema kiujumla wagonjwa wa saratani nchini wapo zaidi ya 50,000 lakini kulingana na hulka za Watanzania baadhi ya wagonjwa hawafikishwi hospitali bali huishia kwenye tiba za asili, waganga wa kienyeji au maombezi.

“Vyanzo vya saratani vipo vingi, ila kuna sababu za kibaiolojia, pia kuna sababu za kikemikali pia. Vyote hivi vinafanya kitu kinaitwa mazingira, yaani vitu vinavyotuzunguka.

“Kuna baadhi saratani zitokanazo na vijidudu na kemikali, kwa mfano kwenye taka ambazo zinatoka kwa njia ya hewa huzalisha carbon monoxide na peroxide ambazo zikiungana zinakuwa na madhara makubwa kwa mwili wa binadamu vivyo hivyo kwenye viwanda vinavyotoa moshi. Hata moshi wa tumbaku unatoa kemikali hatari.

“Pia taka sumu nyingine zinapatikana kwenye maji au mimea ambayo tunakula na kunywa. Cha msingi je, taka sumu zina kemikali gani? Je, ina kemikali ambayo inasababisha saratani?

“Kwa kuwa saratani ni suala mtambuka kwa sababu inachukua zaidi ya miaka 10 hadi 15 kutokea hivyo ongezeko hilo linaendana na mabadiliko ya maisha na mazingira,” anasema.

Aidha, mmoja wa wadau wa masuala ya mazingira kutoka taasisi ya Urban Environmental Development Association (UEDA), Didas Temu anasema ipo miji ambayo haijakua sana ikilinganishwa na jiji la Dar es Salaam, na kwa kuwa mpangilio wa miundombinu ya kuhifadhi taka si mizuri ni vema kuanza kujipanga mapema.

Anasema Dar es Salaam hali ni mbaya ila miji mingine kama Arusha inapaswa kujipanga mapema ili kusiwepo na uchafuzi wa hali ya hewa lakini pia serikali ihamasishe watu wote wanaojenga sasa waache maeneo kwa ajili ya kupanda miti.

Anasisitiza kuwa hali hii itasaidia watanzania wengi kupata ahueni kutokana na miti hiyo kwani asilimia kubwa ya hewa ukaa haitaathiri watu moja kwa moja.

Hata hivyo, katika siku za karibuni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri naye amekuwa mmojawapo wa viongozi wa kuigwa baada ya kuhamasisha maharusi pindi wanapofanikisha kufunga ndoa, kuwa wapande miti kama moja ya kumbukumbu kwao.

Pia kiongozi huyo, amefanikiwa kuanzisha kampeni ya kupanda miti ya matunda katika shule na taasisi mbalimbali za serikali jambo ambalo limekuwa na mwitikio mkubwa na kuwa mojawapo ya uhamasishaji usio kifani katika kuhakikisha miti inapandwa kwa wingi kulinda uharibifu wa mazingira.