Home Makala UCHAGUZI MKUU BURUNDI 2020 Ni vita ya demokrasia kati ya waasi walioichafua...

UCHAGUZI MKUU BURUNDI 2020 Ni vita ya demokrasia kati ya waasi walioichafua Burundi

251
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

JANA raia wa Burundi waliitumia haki yao ya Kikatiba kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku kiti cha urais kikionekana kutolewa macho zaidi na wafuatiliaji wa siasa za nchi hiyo, Afrika na ulimwenguni kote.

Huo unakuwa uchaguzi mkuu wa sita kufanyika barani Afrika kwa mwaka huu, ikikumbukwa kuwa Comoro, Cameroon, Togo, Guinea na Mali zilishatangulia kufanya mchakato huo kidemokrasia.

Matokeo ya chaguzi zote hizo yalikuwa mabaya kwa upande wa upinzani, licha ya kwamba ushindi wa vyama tawala ulikumbana na ukosolewaji mkubwa kwa kile kilichoelezwa ulipatikana kwa ‘bao la mkono’.

Itoshe kufahamu pia, endapo uchaguzi wa Burundi utaepuka machafuko, basi hii itakuwa mara ya kwanza tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka kwa Wabelgiji mwaka 1962.

Kile ambacho Serikali ya Burundi ilikikataa, jumuhiya ya kimataifa ilitaka uchaguzi huo usogezwe mbele kwa kuwa nchi hiyo ni moja ya zile zinazokabwa koo na janga la Corona.

Licha ya Serikali kutangaza idadi ya waathirika kuwa ni 42, huku mmoja akifariki, wakosoaji wanaamini takwimu hizo zimechakachuliwa kwa lengo la kuficha ukubwa wa tatizo.

“Serikali inataka uchaguzi ufanyike kwa gharama yoyote. Haitaki kuanika ukweli ikihofia watu wanaweza kuogopa kujitokeza katika kampeni au kupiga kura,”anasema mmoja kati ya wanaharakati nchini Burundi.

Hoja inayoibuliwa juu ya Serikali kulazimisha uchaguzi ufanyike katika mazingira haya yasiyo rafiki ya taharuki ya ugonjwa huo ni kujibakiza madarakani kwa njia zisizofaa.

Zaidi ya hilo, hofu nyingine kutoka kwa wakosoaji ni namna ambavyo uwanja wa siasa umekuwa finyu hasa kwa wapinzani katika miezi ya hivi karibuni kuelekea uchaguzi.

Wakati huo huo, mazingira mengine yanayotia shaka ni kitendo cha waangalizi wa nje kuwekewa figisu, kikiwamo kigezo cha kukaa karantini, ikiaminika kuwa ni mbinu za kuwazuia kushuhudia kwa jicho la karibu uchaguzi wa mwaka huu.

Kutokana na mlolongo huo, wapo waliopoteza imani, licha ya kwamba ni mapema, wakihisi huenda uchaguzi wa safari hii ukagubikwa na wizi wa kura, vitendo vya rushwa, sambamba na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kama ilivyotangulizwa katika aya ya kwanza ya makala haya, Uchaguzi huu hautofautiani kwa kiwango kikubwa na zingine za Afrika kwani kiti cha urais ndicho chenye mvuto. Makala haya yatajikita hapo.

Ni kweli kuna wagombea saba wa nafasi ya urais lakini macho ya wengi yako kwa chama kikuu cha upinzani, National Congress for Liberty, na kile kilicho madarakani, CNDD-FDD.

Mvuto wa pande mbili hizo unatokana na aina ya wagombea waliopewa nafasi ya kupeperusha bendera za vyama vyao katika kuifukuzia tiketi ya kwenda kuiongoza Burundi. Kwa upande wa upinzani, mwakilishi wao ni Agathon Rwasa (56), wakati chama tawala kinawakilishwa na Evariste Ndayishimiye (52).

Rwasa na Ndayishimiye wanakumbukwa na wengi kutokana na namna walivyokuwa chachu ya machafuko yaliyodumu kwa takribani miaka 12 (1993-2005) nchini Burundi.

Makabila ya Wahutu na Watutsi yaliingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi (1993). Kwa kujikumbusha, chanzo ni ukomo wa miaka 25 ya rais Michel Micombero, ambaye wakati wa utawala wake, Serikali ilionekana kutawaliwa na Watutsi.

Sasa, baada ya uchaguzi wa vyama vingi, kisha uongozi wa Micombero kutolewa madarakani, Wahutu kupitia chama cha Burundi Workers (UBU), wakaona ni wakati mwafaka kwao kulipiza kisasi. Wakaanza kuua Watutsi, kisha ukatokea mwendelezo wa machafuko baada ya wenzao hao kujibu mapigo.

Hata hivyo, nyuma ya machafuko hayo ya miaka 12 yaliyogharimu maisha ya watu 300,000, huwezi kuwaweka kando wagombea urais wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, nikimaanisha Rwasa na Ndayishimiye.

Hiyo inatokana na ukweli kwamba Rwasa ndiye aliyekuwa kiongozi wa Wahutu, wakati Ndayishimiye alikuwa akiliongoza kundi la Watutsi lililoona linaonewa na uongozi ulioingia madarakani kupitia mfumo wa vyama vingi.

Kutokana na hilo basi, hofu inayoonekana wazi kutanda katika siasa za Burundi ni kwamba ushindani wao wa sasa, licha ya kwamba ni wa kidemokrasia, unaweza kuibua hisia za ukabila, ambazo zimepotea tangu pande mbili hizo zilipomaliza tofauti zao mwaka 2005, kisha Pierre Nkurunziza kuingia madarakani.

Kwa kiasi kikubwa, utawala wa Nkurunziza utakumbukwa kwa mafanikio yake ya kutokomeza dhana ya ukabila, hasa katika sekta za serikali, ikiwa ni pamoja na watumishi wa jeshi kuwa ni mchanganyiko wa Wahutu na Watutsi.

Upande wa uzoefu wa kisiasa kati ya wawili hao kuelekea uchaguzi huu, wengi wanamfahamu Ndayishimiye kwa ushawishi wake katika ulingo wa siasa za Burundi, akiwa ndiye Katibu Mkuu wa chama kilicho madarakani, achilia mbali wadhifa wa Jenerali wa Jeshi la nchi hiyo.

Ukiacha kuwa aliwahi kuwa waziri wa Mambo ya Ndani na Ulinzi, Ndayishimiye ni swahiba mkubwa wa Nkurunziza, ikiaminika ndiye aliyefanikisha kumweka kwenye kinyang’anyiro cha kiti cha urais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Ukaribu wake na kiongozi huyo unawafanya wengi wabaki wakijiuliza, ni kweli Nkurunziza ameiachia Burundi, au atamtumia Ndayishimiye kuitawala nchi hiyo kwa mlango wa nyuma?

“Nkurunziza amejiuzulu tu, hajaondoka kabisa (serikalini). Bado ataendelea kufanya kazi akiwa nyuma, atajaribu kuilinda familia na yake na utajiri aliochuma,” anasema Charles Nditije, aliyekuwa waziri, ambaye kwa sasa ni mmoja kati ya vigogo wa UPRONA, chama kingine cha upinzani Burundi.

Nguvu ya Ndayishimiye ndani ya chama tawala iko kwa vijana. Lakini, mara kadhaa wamekuwa wakilalamikiwa kuwachezea rafu wenzao wa vyama vya upinzani, malalamiko hayo yakiripotiwa zaidi katika huko vijijini.

Ukija kwa Rwasa, si wa kupuuzwa na chama tawala hata kidogo kwani kwa awamu mbili zilizopita (2010 na 2015), alishika nafasi ya pili, licha ya mara zote hizo kugomea matokeo akiamini alishinda na kuporwa kura na Nkurunziza.

Mwaka 2015, aliteuliwa kuwa naibu spika wa Bunge la Burundi, hivyo ni mwanasiasa mwenye ushawishi wa kutosha, ambao hakuna ubishi unapaswa kumnyima usingizi Ndayishimiye.

Wakati kampeni zilipoanza mwezi uliopita, wagombea wa vyama vyote walipata nafasi ya kunadi sera zao, ingawa ni kipindi ambacho mataifa ya Magharibi yalipiga kelele juu ya mikusanyiko kwa kile ilichosema inarahisisha kasi ya maambukizi ya virusi vya Corona.

Kama ilivyo katika mataifa mengi ya Afrika, ahadi zilizojikita zaidi katika kulinda amani, kuondosha umasikini, kupatia ufumbuzi suala la uhaba wa ajira, na kukomesha vitendo vya rushwa vinavyoonekana kutawala zaidi katika taasisi za Serikali.

Kujikita katika hilo la umasikini, inafahamika kuwa Burundi ni moja kati ya mataifa ya Afrika yenye asilimia kubwa ya raia wanaoishi maisha ya ‘kuungaunga’, licha ya Serikali kutawaliwa na kashifa za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Zao la kahawa ndilo pekee linalotegemewa na Burundi kujiingizia fedha za kigeni, ikiwa iko wazi kuwa hata sehemu kubwa ya matumizi ya serikali yake yamekuwa yakisubiri misaada kutoka nje.

“Rekodi ya uchumi kwa miaka 15 ya Nkurunziza akiwa madarakani ni mbaya mno. Ameirudisha nyuma Burundi katika kila idara.  Ameiondosha Burundi katika nchi za asili zilizokuwa zikiisaidia, zingine zikiwa ni jirani kabisa. Ni majanga,” anasema kada wa upinzani, Aime Magera.

Mbali ya hayo, ahadi ya kufikisha nishati ya umeme katika maeneo ya vijijini nayo iliwavutia wananchi wengi wa Burundi, sambamba na ile ya kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Mwisho, wadau wa ulingo wa siasa hawataki kuona Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ukigubikwa na kile kilichotokea mwaka 2015. Licha ya madai yao kupuuzwa na Serikali ya Nkurunziza, uchaguzi huo ulikosolewa kwa kile walichodai ulitawaliwa na vitendo vya kihuni.

Si tu wanasiasa wa upinzani, bali hata jumuhiya za kimataifa, ikiwamo UN (Umoja wa Mataifa), haikuvutiwa na ushindi wa Nkurunziza uliosababisha mamia ya raia wa Burundi kuikimbia nchi yao.

Ripoti ya UN ilikuja na chunguzi zilizobaini mauaji, mateso, na vitendo vya ubakaji vilivyokuwa vikitekelezwa dhidi ya viongozi au raia waliokuwa wakiunga mkono upinzani.

Aidha, kama Wasemavyo Waswahili, kwamba dalili ya mvua ni mawingu, viashiria vya machafuko viliripotiwa mara kadhaa wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka huu zilizochukua siku 21.

Haijasahaulika kwamba lipo tukio la wanachama na wapenzi wa Chama tawala, CNDD-FDD, kuingia kwenye mapigano na wenzao wa upinzani, siku ambayo watu wawili walitajwa kupoteza maisha.

Hiyo iliwafanya wanaharakati wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) kusimama na kupaza sauti ya kukemea, wakisema lazima Serikali ya Burundi na Chama tawala waache mara moja mateso yao dhidi ya upande wa pili, kwa maana ya upinzani.

“Kuna shaka kidogo kuamini uchaguzi huu utakwenda sawa kabisa bila kuwapo kwa matukio ya uonevu. Ni kwa sababu viongozi wa Burundi na wale wa Umoja wa Vijana (wa Chama tawala) wanatumia fujo kukibakiza madarakani chama tawala,” anasema Lewis Mudge, Mkurugenzi wa Human Rights Watch kwa Ukanda wa Afrika ya Kati.

Vilevile, baada ya kusema hakuona burasa ya kususia uchaguzi, mpinzani mwenye nguvu zaidi, Rwasa, alianika wasiwasi wake juu ya matokeo yatakayotangazwa, akisema haoni kama kuna haki itakayotendeka.

Landa hofu ya Rwasa, viongozi wengine wa upinzani na wakosoaji wa mwenendo mbovu wa siasa za Burundi wanakerwa na mfumo uliopo kikatiba katika kuunda tume ya uchaguzi (CENI), ikifahamika wazi kuwa ni chama tawala ndicho kinachohusika katika kuteua uongozi wake.

Je, Uchaguzi wa mwaka huu utaandika historia mpya ya siasa za Burundi kwa kumalizika kwa amani, au ni mwendelezo wa kile ambacho kimekuwa kikitokea na kugharimu maisha ya watu?

Lakini pia, ukiwa ni mpango mzuri wa kukabiliana na balaa la umasikini, Serikali mpya itafanikiwa kuzirejesha Marekani na Umoja wa Ulaya (EU), ambazo ziliiwekea vikwazo Burundi wakati wa utawala wa Nkurunziza?

NAFASI YA NKURUNZIZA

Wakati wananchi wa Burundi wakiendelea kusubiri matkeo ya uchaguzi wa juzi ambayo yatawapa rais mpya baada ya kipindi cha miaka 15 ya utawala wa Nkurunziza, tayari imehaelezwa kwua katia kustaafu kwake atapewa nafasi muhimu ya kuwa “msahauri wa ngazi ya juu wa uzalendo “.