Home Latest News UCHAGUZI MKUU DRC: HOFU YA VISASI VIGINGI VINAVYOMTAFUNA BEMBA

UCHAGUZI MKUU DRC: HOFU YA VISASI VIGINGI VINAVYOMTAFUNA BEMBA

5627
0
SHARE

NA NDAHANI N. MWENDA


Tangu ipate Uhuru mwaka 1960 nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) haijawahi kutulia hata kidogo. Sasa ni zaidi ya nusu karne nchi hiyo imekuwa na vita visivyo na ukomo, na vyote hivyo ni katika kugombea madaraka ya taifa hilo tajiri kwa madini duniani.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu nchini humo wa 23 Disemba 2018 kumekuwa na sintofahamu kama uchaguzi huo utaicha salama nchi hiyo yenye watu wanaokadiriwa kufikia millioni 80 kwa sasa.

Mnamo 8 Agosti mwaka huu Rais wa sasa Joseph Kabila alitangaza rasmi kutogombea Urais wa nchi hiyo na chama chake na vyama vinavyomuunga mkono vikamteua Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani Bwana Emmanuel Ramazani Shadary kupeperusha bendera katika kinyang’anyiro hicho.

Idadi ya wagombea katika uchaguzi huo ambao unatupiwa jicho kutoka kila pande za dunia una wagombea 25 lakini waliothibitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya nchi hiyo (CENI) ni wagombea 19 pekee, wagombea 6 wameondolewa kwenye kinyang’anyiro hicho huku mmoja akizuiwa kuingia nchini hivyo hakuchukua fomu kabisa.

Wagombea walioondoelewa ni pamoja na mbabe wa kivita na Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo Jean-Pierre Bemba (wa chama cha MLC), Mawaziri Wakuu wa zamani wa nchi hiyo Samy Badibanga, Adolphe Muzito, Antoine Gizega na Marie-José’ Ifoku Mputa, tajiri Moise Katumbi Chapwa (mmliki wa Klabu ya M[ira ya TP Mazembe) ambaye hakuchukua fomu kabisa kwa sababu amezuiliwa kuingia chini hadi sasa na serikali ya DRC licha ya kujaribu mara kadha.

Kati ya wagombea wote waliondolewa mmoja ndiye anaonekana mwenye nguvu na kuondolewa kwake kunaweza kuleta madhara makubwa kwa DRC ambayo kidogo inaonekana kutulia. Huyo si mwingine bali ni Jean-Pierre Bemba ambaye amerejea nchini DRC 1 Agosti mwaka huu akitokea Uhamishoni nchini Ubelgiji ambapo amekuwepo kwa takribani miaka 10 tangu aondoke nchini humo.

Jean-Pierre Bemba ni nani?

Pierre Bemba ni mzaliwa wa Bokada-Nordi Ubangi DRC, alizaliwa 04 Oktoba 1962. Mwaka 1998 aliunda kundi la wapiganaji wa msituni lilojulikana kama Movement Liberation for Congo (MLC) ambapo baadae alikuja kugeuza kuwa chama cha siasa nchini DRC. Kikundi cha MLC kilianza mapigano Jimbo la Orientale kisha kuhamia Jimbo la Equator  ambapo kundi hilo liliteka jimbo hilo na kulitawala huku mashirika ya Kimataifa yakisaidia ujenzi wa huduma za kijamii kama shule na zahanati.

Katika kutafuta maridhiano nchini DRC miaka ya 2000, Bemba aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa serikali ya mpito ya DRC kati ya 17 Julai 2003 hadi Disemba 2006 ambapo Uchaguzi mkuu ulifanyika huku yeye (Bemba) na Joseph Kabila wakichuana.

Katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika 30 Julai 2006, ulijumuisha wagombea 33, Bemba na Kabila ndiyo walikuwa wanaungwa mkono na watu wengi.

Agosti 20 2006 Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilitangaza matokeo na Kabila alipata kura 44% huku Bemba akipata kura 20%. Katika Uchaguzi wa marudio wa 29 Oktoba 2006 ambao uliwahusisha Bemba na Kabila Bemba alibwagwa na Kabila kwa kura 58.05% alizopata Kabila kwa mujibu wa Tume kwa matokeo waliyoyatangaza 15 Novemba 2006.

Upande wa Bemba ulilalamikia rafu na hivyo kwenda Mahakamani lakini Mahakama iliyatupilia mbali malalamiko hayo 27 Novemba 2006 na Kabila kuapishwa 06 Disemba 2006 huku Bemba akisusia sherehe hizo.

Licha ya hayo serikali ya DRC ilijaribu kutaka kuondoa uhai wa Bemba 21 Agosti 2006 alipokuwa na ujumbe wa mabalozi 14 wa Uingereza, Ufaransa, Ubelgiji.

08 Disemba 2006 MLC ilitangaza Pierre Bemba kugombea Useneta wa Jimbo la Kinshasa, na Bemba alishinda na kuwa Kiongozi wa Upinzani.

Machi 2007 yalitokea mapigano baina ya Majeshi ya serikali na MLC katika makazi ya Bemba na kupelekea maelfu ya raia na wanajeshi kupoteza maisha huku Bemba akikimbilia Ubalozi wa Afrika Kusini.

Inadaiwa pia hata Bemba aliumia mguu hivyo aliomba Baraza la Seneti ruhusa ya kwenda kutibiwa, na April 11, 2007 alikwenda uwanja wa ndege akisindikiwa na kikosi cha kulinda amani cha umoja wa mataifa (UN-MONUSC) Seneti lilimpa Bemba siku 60 lakini Brussels, Ubelgiji zaidi ya hizo siku akidai kuwa kulikuwa na njama za kutaka kumuua.

Akiwa Brussels, Ubelgiji 24 Mei 2008 alikamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Kiuhalifu wa Kivita (ICC) ya The Hague lakini mwaka 2009 alipewa ruhusa ya kwenda kumzika Baba yake aliyefariki akiwa Ubelgiji. Bemba alikaa kizuizini tangu mwaka 2008 mpaka Uchunguzi ulipokamilika na 21 Machi 2016 alikutwa na hatia ya makosa matano katika ushiriki wa vita ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 2003 alipotuma Majeshi yake kumsaidia Rais wa CAR kwa kipindi hicho Ange-Felix Patasse.

Bemba alikutwa na makosa ya uuaji, ubakaji, utesaji, uporaji na 21 Juni 2016 alihukumiwa kifungo cha miaka 18 na kulipa faini ya Euro 300,000 lakini 28 Septemba 2016 Bemba alikata rufaa na 8 Julai 2017 aliachiwa huru na Mahakama hiyo.

Bemba alirejea DRC 01 Agosti 2018 kugombea Urais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu nchini humo utakaofanyika Desemba 23.

25 Agosti 2018 CENI ililiondoa jina la Jean-Pierre Bemba kwa madai kuwa alitenda uhalifu wa kivita. Makosa ambayo ICC imemwachia huru baada ya kukata rufaa.

Je, uchaguzi huu utaiacha DRC salama?

Uchaguzi huo kwa mara ya kwanza utafanyika bila ya Rais Joseph Kabila kugombea, swali linakuja licha ya Kabila kutogombea uchaguzi huo utaicha DRC salama?

Mpaka sasa kuna sintofahamu baada ya Bemba na wenzake kuenguliwa katika kinyang’anyiro hicho. Tayari Bemba ameshakwenda Mahakama ya juu kupinga kuenguliwa kwake. Siku ya Jumatatu (wiki hii) upande wa Bemba waliwasilisha malalamiko yao. Mose Katumbi na Jean-Pierre Bemba wamesaini maazimio ya kumtaka Joseph Kabila asiingilie Mamlaka ya Tume ya Uchaguzi.

Pia Mawaziri Wakuu wawili wa zamani wameondolewa katika kinyang’anyiro hicho kwa madai ya kuwa wana uraia-pacha (dual citizenship) hivyo hawana sifa ya kugombea. Pia mwanasiasa mkongwe na Waziri Mkuu wa zamani Samy Badibanga (92) ameondolewa katika orodha ya wagombea kwa madai ya kukosea kujaza fomu ya Urais.

Duru za kisiasa zinadai kuwa Joseph Kabila anafanya kila liwezekanalo ili Emmanuel Ramazani ashinde uchaguzi huo. Ramazani ni mtiifu kwa Kabila hivyo inatarajiwa Kabila hataishi kwa shida pindi atakapoondoka Ikulu ya Kinshasa.

Pia inadaiwa serikali ya DRC inamzuia Bemba kuwania Urais kwa kuwa ana ushawishi mkubwa hivyo anawezakushinda na kuwa Rais na kulipiza kisasi. Aidha, Bemba anahusishwa kutumiwa na mataifa ya Magharibi kwani amekuwa karibu sana na mataifa hayo tangu aanze harakati zake za kugombea madaraka.

Na kinachowapa wasiwasi watawala wa DRC, ni jinsi Bemba alivyofutiwa mashitaka na ICC mapema mwaka jana. Inaonekana Bemba ni kibaraka wa Magharibi hivyo watawala wa DRC wanafanya wawezalo kumzuia asishike madaraka ndani ya taifa hilo lenye utajiri wa madini ya kila aina.