Home Makala Kimataifa UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: NI UCHAGUZI GHALI ZAIDI BARANI AFRIKA

UCHAGUZI MKUU KENYA 2017: NI UCHAGUZI GHALI ZAIDI BARANI AFRIKA

1266
0
SHARE

NAIROBI, KENYA

Uchaguzi mkuu wa Kenya mwezi ujao (August 8) unatarajiwa kuwa miongoni mwa chaguzi ghali zaidi Barani Afrika.

Gharama za uchaguzi huo zinatarajiwa kufikia Dola za Kimarekani bilioni moja na hivyo kuwa uchaguzi ghali zaidi katika kile kinachoitwa uwiano wa gharama kwa kila mpiga kura – (cost-per-voter basis).

Matumizi ya fedha kwa upande wa serikali na taasisi binafsi zote ziko juu kuliko wakati wowote katika historia za chaguzi katika nchi hiyo.

Kwa upande wa wagombea katika nafasi mbali mbali, mamia ya mamilioni ya Dola za Kimarekani zimetumika katika ngazi zote mbili za ugombea – ngazi ya uteuzi katika vyama vyao na ngazi hii inayofuata ya uchaguzi.

Ripoti mpya ya Matumizi ya Fedha iliyotolewa kabla ya uchaguzi, Hazina ya Taifa ya Kenya imesema maandalizi na kufanyika uchaguzi wenyewe utagharimu KSh 29.9 bilioni au dola za kimarekani 480 milioni – fedha za walipa kodi.

Sehemu kubwa ya bajeti hiyo ya uchaguzi imekwenda kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ambayo imepanga kutumia Ksh 43 bilioni au Dola 413 milioni kuajiri wafanyakazi, ununuzi wa vifaa vya kupigia kura, kuendesha zoezi la elimu kwa wapigakura, achilia mbali gharama katika ukusanyaji wa matokeo ya uchaguzi.

Fedha nyingine kiasi cha Ksh 4 bilioni zitatumika katika kuimarisha ulinzi na usalama hasa katika majimbo (counties) yenye viashirio vya uvunjifu wa amani na maeneo ya mipakanai, kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho vya taifa vya uraia na katika kuhakikisha utulivu na amani katika jamii wakati wa uchaguzi na pia baada ya uchaguzi.

Idara ya Mahakama, Usalama wa Taifa na Ofisi ya Rais ni baadhi ya taasisi zilizopewa mamilioni ya Dola katika gharama za moja kwa moja au zile zisizo za moja kwa moja.

Uchaguzi huu unakuja wakati ambapo uchumi wa nchi unatikiswa kutokana na hali ya ukame, kuongezeka kwa mfumuko wa bei za bidhaa na kushuka kwa mikopo katika sekta binafsi.

Madai ya nyongeza za mishahara kwa watumishi wa umma kama vile wauguzi na walimu, mbali na gharama kubwa ya kugharamia vikosi vya jeshi vilivyopo nchini Somalia, pia ni mzigo mkubwa kwa nchi hiyo.

Aidha Hazina ya Taifa imekuwa na hofu ya kuibuka kwa ghasia katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wenyewe, hali ambayo inaweza kuathiri imani kwa wawekezaji wa nje na wa nyumbani pia.

Kama kitovu kilichoimarika katika uchumi na demokrasia ya wazi katika kanda hii ya Afrika, uchaguzi wa Kenya umekuwa unafuatiliwa sana hata nje ya mipaka.

Mwaka huu utakuwa ni wa uchaguzi mwingine tena unaowapambanisha nguli wawili wa kisiasa nchini Kenya – rais aliye madarakani Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga – kama ilivyokuwa kwa uchaguzi wa mwaka 2013.

Na uchaguzi huu unahitimisha miaka 10 kamili tangu uchaguzi wa mwaka 2007 ulioibua ghasia kubwa zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,200.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba pamoja na kuwa na katiba nzuri na kupiga hatua kubwa katika demokrasia, gharama za kuendesha uchaguzi zimekuwa zikiongezeka. Wanasema hili linatokana na gharama kubwa katika uandikishaji wapigakura, usimamizi mbovu na ufisadi.

Kwa mfanao wanataja kwamba mwaka 2013 vifaa vya BVR vilivyonunuliwa kwa Dola za Kimarekani 95 milioni vilifeli katika dakika za mwisho hivyo kuharubu kabisa mwenendo wa uchaguzi mzima.