Home Makala UCHAGUZI MKUU WA UINGEREZA: THERESA MAY AZIDI KUPOROMOKA KURA ZA MAONI

UCHAGUZI MKUU WA UINGEREZA: THERESA MAY AZIDI KUPOROMOKA KURA ZA MAONI

1197
0
SHARE
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May.

LOMDON, UINGEREZA


Wakati zimebaki siku saba tu hadi uchaguzi mkuu nchini Uingereza hapo Juni 8, kuna dalili kwamba uungwaji mkubwa mkono aliokuwa nao Waziri Mkuu Theresa May umeanza kuyeyuka na kwamba huenda akashindwa kupata uwingi wa kutosha katika Bunge.

Mapema mwezi uliopita Waziri Mkuu Theresa May aliitisha uchaguzi wa ghafla ili kupata kile alichokiita nguvu kubwa ya Wabunge wa chama chake kusimamia mchakato wa nchi hiyo wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (EU).

Mwaka jana serikali ya Uingereza chini ya aliyekuwa Waziri Mkuu David Cameron – ambaye alikuwa muumini mkubwa wa muungano wa Ulaya – aliendesha kura ya maoni iliyouliza iwapo nchi hiyo ijitoe EU au la.

Matokeo yalikuwa ni kwamba wananchi wengi walitaka ijitoe, hivyo akajiuzulu uwaziri mkuu kama alivyoahidi na kumuachia uwaziri mkuu Theresa May.

Baada ya kutangazwa tu kwa uchaguzi, pauni ya Uingereza ilipata nguvu kwa matumaini kwamba iwapo Theresa May atapata Wabunge wengi katika Bunge la House of Commons, basi atapata uhuru na nyenzo muhimu anazohitaji katika kupata mkataba wa namna bora ya kujitoa EU na hapo hapo kuwasuta wale wenye msimamo mkali.

Kwa kipindi fulani ilionekana kama vile mpango huu ulikuwa unakwenda vyema. Kura za maoni zilionyesha chama cha Conservative cha Waziri Mkuu Theresa May kilikuwa mbele kwa asilimia 20.

Lakini kampeni za chama hicho ambazo zilitegemea sana mvuto na umaarufu wa Theresa May zilibadilisha mambo. Uzinduzi wa ilani yake ya uchaguzi ulikuwa wa hovyo kwani ilijumuisha kuwatoza kodi wazee ili kugharamia huduma za jamii.

Hata hivyo hilo waliliondoa kwa haraka na May alikataa kukubali kwamba tukio hilo liliathiri madai ya uongozi wake bora.

Kwa upande wake, Jeremy Corbyn – kiongozi wa chama cha upinzani cha Labour alionekana kufaidika kwa haya baada ya awali kuonekana chama chake kingepata matokeo mabaya. Corbyn ameweza kusisitiza ilani yake – ya kuongeza bajeti ya huduma za jamii na kutoa mpango mzuri wa uchumi baada ya nchi hiyo kujitoa kutoka EU.

Matokeo ya haya yote ni kwamba kura za maoni sasa zaonyesha tofauti ile ya asilimia 20 ya Conservative kuwa mbele imeanza kupungua. Kura moja ya maoni mapema wiki hii ilionyesha sasa tofauti hiyo imefikia asilimia 8 tu.

Na iwapo kura hii ya maoni inatafsiriwa kwa viti vya ubunge, basi chama cha Conservative cha Theresa May kutapata uwingi wa viti viwili tu dhidi ya vyama vya upinzani.

Na kura hiyo ilifanyika baada ya tukio la ulipuaji bomu katika jiji la Manchester, tukio ambalo wengi walifikiri lingempaisha Theresa May.

Uwingi wa viti viwili ungeivuruga hoja ya kuwa na nguvu kubwa bungeni ya kulishughulikia suala la kuitoa nchi kutoka EU. Hata hivyo wadadisi wa mambo wanauliza: Ataziambia nini nchi zile nyingine 27 ambazo bado zimo katika EU?

Na wawekezaji wala hawaoni uwezekano kwamba hali hii itazidi kuwa mbaya kwa Theresa May au kwamba kura za maoni si sahihi. Lakini wachunguzi wa mambo wanasema kura hizi za maoni zikizidi kuwa mbaya kwa Conservatives, basi hapo ndiyo masoko ya hisa na ya fedha yataanza kutikisika.