Home Habari UCHAGUZI MONDULI: CCM DHIDI YA LOWASSA

UCHAGUZI MONDULI: CCM DHIDI YA LOWASSA

2345
0
SHARE

NA ABRAHAM GWANDU, ARUSHA            |           


UCHAGUZI wa marudio unaotarajiwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu katika Jimbo la Monduli unatarajiwa kuwa na hamasa ya kipekee kutokana na historia ya kisiasa ya  jimbo hilo.

Jimbo la Monduli ni eneo muhimu kimkakati katika siasa za Kanda ya Kaskazini na nchi kwa ujumla hususan kwa vyama vikuu vya siasa hapa Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Monduli  ina historia ndefu ya kisiasa  kufuatia kuwahi kuongozwa na Mawaziri Wakuu maarufu, Edward Sokoine aliyefariki Aprili 12 mwaka 1984, na Edward Lowassa aliyeongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 20 kabla ya kukihama CCM na kugombea Urais mwaka 2015 kupitia Ukawa mara hii itarudi kwenye pilika za uchaguzi utakao amua hatma ya upinzani hapa nchini .

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanau elezea uchaguzi huo kuwa vita baina ya Waziri Mkuu wa zamani, Mbunge wa Monduli kwa muda mrefu  na sasa  Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa dhidi ya kijana wake aliyeasi na kurudi CCM Julius Kalanga.

Kalanga mmoja kati ya vijana waliokuwa watiifu kwa Lowassa pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa halmashauri ya Monduli Issack Joseph ‘Kadogoo’ambao wote walihama CCM sambamba na Lowassa na kujiunga Chadema hivi karibuni walirejea katika chama hicho tawala.

Aidha, inaelezwa kuwa ikiwa ni vitani basi uchaguzi wa Monduli tofauti na chaguzi zingine tangu Lowassa ahamie Chadema ni kama risasi ya mwisho iliyobaki katika silaha yake katika siasa za ushindani.

Kitendo cha mtoto wa Lowassa, Freddy kuchukuliwa fomu na kuirejesha akiomba ridhaa ya kuwania ubunge kupitia Chadema katika uchaguzi huo sio tu kimeongeza msisimko na hamasa ya uchaguzi huo lakini pia upande wa CCM wamedhamiria kuonyesha kuwa mkongwe huyo wa siasa za nchi hii yuko upande usiokubaliwa na wananchi kisiasa.

Akizungumza na RAI kwa njia ya simu mwishoni mwa wiki Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema pamoja na watia nia wengine ambao majina yao yatapelekwa kamati kuu jina la Fred Lowassa limesisimua mchakato mzima.

“Baada ya hapa Monduli Jumamosi tuna mkutano wa wilaya wa kura ya maoni ambao utafanyika Kata ya Migungani, halafu siku hiyohiyo kamati ya utendaji ya wilaya itakaa na kuweka mapendekezo yake na nitachukua ofisi yangu ya Kanda na kuzipeleka makao makuu kwenye kikao cha Kamati kuu ya chama kwa maamuzi,” alisema Golugwa.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Septemba 16 mwaka huu baada ya aliyekuwa Mbunge wake Julius Kalanga (Chadema), kuhama Chama hicho na kujiunga na CCM, Julai 31 mwaka huu, huku akidai sababu zilizomfanya kujiuzulu chama hicho na kujiunga na CCM ni siasa za uhasama, malumbano na chuki ndani ya Chadema na kudai kuwa anajiunga na CCM ili kuunga mkono juhudi za Rais Dk. John Magufuli.

Kalanga ambaye alikuwa Mbunge katika Jimbo hilo kwa kipindi cha kwanza mwaka 2015 alishinda kwa kupata kura 35,024 dhidi ya mpinzani wake ambaye ni mtoto wa Sokoine, Namelock Sokoine (CCM) aliyepata kura 29,925.

KATIBU MKUU CCM BASHIRU ALLY AKOLEZA MOTO

Kitendo cha Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally kulinganisha upepo uliokumba CCM kiasi cha wanachama wake maarufu kukihama mwaka 2015 mara baada ya mchakato wa kumpata mgombe nafasi ya Rais kuwa sawa na pepo mchafu kimedaiwa kukoleza vita baina ya pande hizo.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa ziara yake Mkoani Arusha, Dk. Bashiru aliwaambia wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Monduli kuwa baada ya upepo ule ulioambatana na siasa chafu misingi ya taifa na CCM ilitikiswa.

“Tangu hapo nchi yetu haijapona, tunayo kazi ya kuifanya ili kurejesha misingi ya Taifa, ujasiri wa kurejea CCM tena ukitokea Monduli si kazi rahisi kama mnavyofikiria hapa tumetikisa upinzani kwelikweli .”

“Unaporejea CCM ndani ya Monduli unakuwa umerejesha uhai na heshima ya CCM kwa Taifa zima kwa sababu tuna historia ndefu hapa, hii umetupa heshima kubwa nasi tunakuahidi tupo nyuma yako katika mapambano yanayokuja ya  kulirejesha Jimbo hili”   alinukuliwa akisema Dk. Bashiru.