Home Latest News Udhubutu, misimamo ya JPM ni kioo cha ukombozi Afrika

Udhubutu, misimamo ya JPM ni kioo cha ukombozi Afrika

392
0
SHARE

NA DEOGRATIAS MUTUNGI

NIANZE makala haya kwa kusema na kusimamia ukweli usio kuwa na chembechembe yoyote ya unafiki, ushabiki, itikadi au undumila kuwili  kuwa Tanzania na Afrika tunaye kiongozi ambaye ni kioo cha viongozi wa Kiafrika, mwenye udhubutu na kusimamia fikra endelevu za kiafrika ambazo zimekuwa zikipiganiwa kwa miaka mingi na viongozi wa Kiafrika, ingawa Afrika ya zama hizi imepoteza viongozi wengi wenye hulka kama za Rais John Magufuli ukilinganisha na zama za miaka ya 1960-1988, uthubutu na misimamo iliposhika hatamu na Afrika ikawa tishio kwa mataifa ya ughaibuni.

Sharti ukweli usemwe kuwa Afrika ya leo ina ombwe la ladha ya viongozi mithili ya Rais Magufuli na wengineo waliowahi kuwepo na kuitangaza vyema Afrika, lakini zipo sababu nazo ni ukosefu wa viongozi wazalendo, uwepo wa viongozi wala rushwa, wenye viburi na  tamaa ya madaraka, ukosefu wa viongozi wenye hofu ya Mungu na ombwe la utawala bora kwa baadhi ya viongozi wetu ni kati ya sababu nyingi zinazosababisha kukosekana kwa viongozi wenye udhubutu na misimamo katika kusimamia mambo ya msingi ndani ya  mataifa yao.

Kwa ufupi tukirejea kwenye mantiki halisi ya Umoja wa Afrika (AU) kuchukua nafasi ya OAU kwa maana ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika ulioundwa Mei 25 mwaka 1963, sera kuu ni mataifa ya kiafrika kuwa na misimamo dhabiti juu ya nchi zao sambamba na dhamira ya kuhakikisha kuwa Bara la Afrika linatoka kwenye mikono ya wakoloni na kuhimiza maendeleo na umoja kati ya nchi wanachama wa umoja huo,  kwa sasa ndio njia anayopitia rais wetu JPM ndani ya utawala wake kutokana na misimamo  aliyonayo kwa taifa na watu wake.

Udhubutu na misimamo ya JPM ndio misimamo inayohitajika katika Afrika ya leo, aidha ndio dira yenye kuikomboa Afrika kutoka kwenye ukoloni mambo leo, misimamo ya namna hii ni kichomi na sumu kwa mataifa ya Magharibi na Amerika ambapo kwao ni kigingi cha unyonyaji wa rasilimali zilizopo Afrika badala yake tunachonganishwa kwa waafrika wenyewe kwa wenyewe na tunakubali kuchonganishwa kwa wepesi huu ni uhayawani kabisa kwa mwafrika mwenyewe. 

Hata hivyo lazima ukweli usemwe kuwa huyu ndiye rais tuliyebaki naye Afrika ambaye kwa kweli kijiko bila kupindisha chochote na ndio watu ambao Mwalimu Nyerere na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe waliwahitaji watu wa namna hii katika kuipigania Afrika ya sasa na hapo baadaye.

Aidha kwa bahati mbaya au kwa makusudi sisi Watanzania hatujatambua umuhimu wa kiongozi tuliye naye kama ana vinasaba vya kipekee katika falsafa za uongozi na usimamizi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yenye mantiki ya ukombozi wa mtu mweusi hasa mnyonge na masikini, bado tunadhani ni kiongozi mwenye misimamo isiyo na dira jambo ambalo kimantiki si la kweli, hata hivyo maandiko matakatifu yanasema nabii hakubaliki kwao rejea Marko 6:4 ndio hiki ninachokiona kwa baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa hawakubaliani na kila sera, mipango na harakati za serikali ya awamu ya tano, wapo baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa mstari wa mbele kusifia misimamo ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuliko misimamo ya rais wa taifa lao huu ndio utumwa wa fikra tulio nao baadhi ya Waafrika ambapo tusipobadilika inaweza kuchukua karne nyingine nyingi Afrika kuwa wamoja na wenye mawazo sawa ya kujitegemea. 

Afrika tunahitaji kubadilika na kusimamia kile tunachokiamini bila kujali falsafa na mirengo ya Ulaya na Amerika, kamwe falsafa na mirengo ya Afrika hazijawahi kuigwa wala kipaumbele cha mzungu, Afrika nani katuroga, Afrika tatizo letu ni nini hasa?

Mbali na hayo kwa jinsi mantiki ya ukweli ilivyo kwa sasa huwezi kutenganisha misimamo ya Rais Magufuli na viongozi nguli wa kisiasa za ukombozi wa kiafrika kama rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Robert Mugabe, Mwalimu Nyerere, Rwagasore, Kamuzu Banda, Kanali Gaddafi, Keneth Kaunda na viongozi wengineo wa kiafrika ambao mawazo yao yalikuwa na misimamo ya kupinga utumwa wa kifikra kutoka kwa mataifa ya Magharibi na Amerika.

Inawezekana kabisa wanaobeza misimamo na mawazo pevu ya Rais Magufuli kwa sasa hasa kwa kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Covid-19  wanafanya makusudi au wamesahau historia ya viongozi wetu wa kiafrika walivyokuwa na ujasiri wa kipekee katika kuipambania nchi na bara letu kwa ujumla wake, viongozi hao walijitoa mhanga kuitengeneza Afrika kama Rais JPM alivyojitoa kimasomaso kuirejeshea hadhi yake Afrika.

Kwa ujumla wake mantiki kuu ya makala haya inasimamia kufafanua na kuelezea kwa kina misimamo ya Rais Magufuli dhidi ya uamuzi wake wa kutoifunga nchi maarufu kama “lockdown” na badala yake kuachia Watanzania waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali na kujiongezea pato binafsi na la nchi kwa ujumla wake.

Uamuzi huu umezua tafrani na mijadala ya moto sana, aidha tumesikia mengi na kila aina ya hoja zikijengwa na kuibuliwa ndani ya kipindi hiki cha Covid-19, hata hivyo makala haya yanaweza kuigawa mijadala hii katika makundi makuu mawili, Mosi kundi la wanasiasa wenye itikadi za mrengo wa kupinga kila kitu iwe kizuri au kibaya wao ni kupinga tu ambao agenda yao kubwa husimama katika kutafuta umaarufu wa kisiasa zaidi badala ya kusaidia watu kujikomboa na tatizo fulani kisiasa huu ni uhuni na utapeli wa kisiasa.

Kundi la pili ni kundi ambalo linaundwa na wanaharakati ambao wao kwa lugha moja au nyingine wanasimama katika tabaka la uwakala wa uhujumu serikali kwa maana ya kutumika aidha na mataifa ya nje au na baadhi ya watu ambao walikuwa na mifumo ya kinyonyaji iliyobanwa na utawala uliopo madarakani. 

Kwa ufupi makundi haya yote mawili ni hatari kwa ustawi wa nchi kutokana na sera zake kuwa za kukwamisha maendeleo ya dola iliyopo madarakani aidha ndio makundi ambayo hujitoa kimasomaso kuichafua serikali ya JPM nje na ndani ya nchi yetu ukiwasikia watu hawa huwezi kutambua kama ni Watanzania lakini ukweli ni Watanzania wasio wazalendo na nchi yao si jukumu ya makala haya kuwalaani bali kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili waweze kubadilika kitabia na kuwa waungwana na wazalendo.

Hata hivyo ukiachana na nia ovu ya makundi hayo mawili niliyoyafafanua hapo juu ni wazi kuwa serikali ya awamu ya tano kwa ujumla wake imeweza kuwa mfano wa kipekee katika bara la Afrika kwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya kulinda uchumi wa Watanzania kwa kuzingatia historia ya hali ya Watanzania, giografia ya maeneo na uchumi wa nchi katika kipindi hiki cha Covid-19.

 Kupitia makala haya unaweza kutambua uamuzi huu wa serikali kuwa ulikuwa ni wa hekima kubwa kuliko uamuzi uliochukuliwa na baadhi ya mataifa ya Afrika na hata duniani kote.

Ingawa zipo nchi ambazo zilionyesha wasiwasi dhidi ya uamuzi huu wa JPM, lakini bado misimamo ya serikali iliweza kuonyesha mafanikio makubwa mpaka sasa tofauti na mataifa mengine yalivyotegemea, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kupitia kwa mkurugenzi wake, Tedros Adhanom anasema tuizoee Covid-19 maana itachukua muda kuisha ndani ya jamii zetu.

Kwa mantiki hiyo makala haya yanakiri kuwa serikali ya Tanzania imechukua uamuzi wa kipekee na kihistoria katika kupambana na Covid-19 kutokana na kutoiga mbinu, mifumo na utaratibu wa mataifa mengine zaidi ya kufuata miongozo ya kiafya kutoka WHO na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa afya tofauti na mataifa mengine ya Kiafrika yaliyoamua kuiga na kutumia utaratibu wa mataifa ya Magharibi na Amerika.

Mathalani mifano ipo wazi nchini Uganda, Kenya na Rwanda tulishuhudia baadhi ya ghasia zilizojitokeza baada ya uwepo wa “lockdown” aidha katika mataifa haya tuliona takwimu za vifo vilivyotokana na nguvu za dola katika kukabiliana na raia walioamua kutotii amri ya kukaa ndani na kuamua kwenda mitaani kujitafutia ridhiki ya kujipatia kipato.

Pengine tujiulize swali ipo wapi mantiki ya kulinda uhai wa raia dhidi ya Covid-19 kwa kuweka zuio la kutotoka ndani na kuua wale waliotoka kwa sababu ya kwenda kutafuta ridhiki ya kuendesha maisha yao kujikimu, nini mantiki yake bila shaka swali hili linafikrisha sana na linaonyesha zaidi ombwe la ukosefu wa viongozi imara na madhubuti katika kusimamia kile wanachokiamini bila kuiga ya mataifa mengine na ndipo unapoona mantiki na hekima ya serikali ya awamu ya tano chini ya  JPM kuwa zuio la “lockdown” kwa Watanzania lilikuwa na maana kubwa na kuacha historia ambayo itaendelea kuwa alama kwa JPM na Tanzania kwa ujumla kutokana na misimamo na udhubutu wa rais wetu, makala haya yanatoa rai kwa viongozi wetu wa kiafrika kuwa na misimamo na uthubutu usiolegalega pale linapokuja tatizo la ndani linaihusu Afrika na watu wake.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania

0717718619 

 HYPERLINK “mailto:dmutungid@yahoo.com” dmutungid@yahoo.com