Home KIMATAIFA Udini, demokrasia vyabeba uchaguzi Mkuu India

Udini, demokrasia vyabeba uchaguzi Mkuu India

1262
0
SHARE

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.

NEW DELHI, INDIA

Mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi nchini India, nchi inayotajwa kuwa ni demokrasia kubwa zaidi duniani – kutokana na idadi kubwa ya watu (1.4 bilioni) na kwamba tangu ijipatie uhuru imekuwa ikiendesha chaguzi za kidemokrasia na hivyo kuwa mfano kwa nchi nyingi.

Hata hivyo chama cha familia ya Waziri Mkuu wa kwanza Jawahral Nehru cha Congress ambacho kimetawala nchi hiyo kwa jumla ya miaka 49 katika kipindi cha miaka 72 cha uhuru wa nchi hiyo kilishindwa uchaguzi wa 2014 kwa chama cha BJP chenye mrengo wa udini, na kilichoanzishwa mwaka 1980.

Katika miezi ya kuelekea uchaguzi wa mwaka huu (Aprili na Mei 2019) chama tawala kinachoongozwa na Waziri Mkuu Narendra Modi kimekuwa kikipoteza chaguzi za majimbo kadha, pia kujiuzulu ghafla kwa Gavana wa benki Kuu ya nchi hiyo Urjit Patel, mtu ambaye Modi alikuwa anamtegemea sana katika kuinua uchumi wa nchi hiyo.

Kujiuzulu kwake ghafla kulisababisha kuanguka ghafla kwa masoko ya hisa na kuyumba kwa uchumi lakini kikubwa ni kwamba mkuu huyo wa benki alikuwa anatofautiana sana na Modi katika masuala ya uchumi kwa ujumla.

Wadadisi wa mambo wanasema matukio hayo ni ishara ya hali mbaya ya chama hicho katika uchaguzi ujao. Miaka minne na nusu baada ya ushindi mkubwa wa BJP dhidi ya Congress, Modi bado anaendelea kujitangaza kwamba yeye ni mtoto wa muuza chai tu mgahawani, ni kiongozi asiye fisadi na anayejitahidi kuifanya nchi yake kuwa ya nguvu kwa kutembea kifua mbele.

Hata hivyo wengi wanaona kwamba India siyo kama ile ya zamani chini ya Congress ambayo itikadi yake ni kutokukumbatia dini yoyote (secularism), kwani itikadi hiyo, aliyoiasisi Nehru chini ya uongozi wa kiongozi wa kiroho Mahatama Gandhi ndiyo iliiwezesha nchi hiyo kusonga mbele kimaendeleo na kuwepo na umoja.

Gandhi alitambua kwamba suala la dini lingeweza kuiathiri nchi na alijitahidi sana kutojitenga kwa Pakistan ya sasa (iliyokuwa sehemu ya India wakati wa ukoloni wa Waingereza) na alikuwa radhi hata waziri mkuu wa kwanza atoke kwa Waisilamu. Hilo lilishindikana, Pakistan ilijitenga, na yeye Gandhi aliuawa mwaka 1947 na manazi wa Kihindu kutokana na msimamo wake huo.

Lakini sasa hivi suala la udini limerudi na alilolileta ni BJP na Modi, akitambua kwamba Wahindu ni asilimia zaidi ya 80 ya Wahindi wote.

Kwa mfano Modi katika kampeni zake za kupata kura za watu wa dini ya Kihindu ataibua sana suala la hekalu la Ayodhya ambalo limekuwa lina mzozo mkubwa na wa muda mrefu baina ya Wahindi na Waisilamu –  kila dini ikidai kwamba kihistoria lilijengwa na watu wa dini yao.

Kuhusu BJP kupoteza majimbo (states) matatu katika chaguzi ndogo hivi karibuni – majimbo ya Madhya Pradesh, Rajasthan na Chhattisgarh kunyakuliwa na chama cha upinzani cha Congress, viongozi wa BJP wamelaumu kampeni mbovu zilizofanywa na viongozi wa majimbo hayo.

Lakini wachunguzi wa mambo wanasema sababu kubwa ni kushindwa kwa serikali ya Modi ni hali duni ya wakulima latika majimbo hayo na kuongezeka kwa vijana wasiokuwa na ajira, kinyume na ahadi alizotoa Modi wakati wa kampeni za mwaka 2014.

Hata hivyo wadadisi wa mambo wanasema wapigakura 870 milioni wanaotarajiwa kupiga kura wataamua hatima ya ajenda ya Modi na chama chake cha BJP ya kuleta mageuzi na suala la udini ambalo huibuka sana wakati wa uchaguzi ikizingatiwa idadi ile ya Waisilamu wapatao 170 milioni watakaopiga kura.