Home Makala UFILIPINO: VITA DHIDI YA MIHADARATI YASAHAULISHA AJENDA YA MAENDELEO

UFILIPINO: VITA DHIDI YA MIHADARATI YASAHAULISHA AJENDA YA MAENDELEO

532
0
SHARE
Rais wa ufilipino Rodrigo Duterte.

NA HILAL K SUED


Maadili katika uendeshaji wa siasa yanaweza kuwa yanaporomoka duniani kote, lakini kumtaja Adolf Hitler kama mfano wa ‘msukumo’ (inspiration) hakukubaliki popote duniani.

Lakini hiyo haikumzuia Rais machachari wa Ufilipino, Rodrigo Duterte, ambaye September mwaka jana alitangaza hadharani kwamba atawashughulikia watu wanaotumia dawa za kulevya kama vile Hitler alivyowashughulikia Wayahudi.

Tangu aingia madarakani vita ya Duterte imeua zaidi ya watuhumiwa 7,000 wa dawa za kulevya ambao waliuawa na polisi, makundi ya wanamgambo na wengine kutokana na uhasama baina yao.

Sasa hivi Wafilipino wengi wana wasiwasi kuhusu usalama wao, na watu wengi nje ya nchi hiyo wamechukizwa na kampeni hiyo.

Lakini uipende usiipende, kampeni hiyo imeyapoteza kabisa mengine ya utawala wa Duterte unaotimiza miezi minane.

Hata hivyo ni ukweli kwamba Wafilipino hawakumchagua Duterte kutokana na msimamo wake wa ‘ki-cowboy’ dhidi ya vitendo vya uhalifu, lakini zaidi walimuona yeye angejaribu kuinua hali ya maisha ya mamilioni miongoni mwao na kuboresha miundombinu ambayo ilikuwa katika hali mbaya.

Na zaidi ya kusababisha mauaji makubwa ya raia bila ya michakato ya kimahakama, kampeni ya Rais Duterte dhidi ya watumiaji wa dawa za kulevya inaanza kuifanya serikali yake kusahau masuala mengi mengine ya msingi yaliyopo katika ajenda yake.

Miongoni mwa masuala mengine ambayo yanasahaulika ni marekebisho katika mifumo ya kodi hasa kupunguza kodi kwa wafanyakazi hasa wale wa kipato cha chini na kuwabebesha mzigo wa kodi matajiri na makampuni makubwa makubwa.

Waziri wa Fedha Carlos Dominguez anasema marekebisho haya ambayo yanasuasua Bungeni yataongeza mapato ya serikali pamoja na kupunguza kodi kwa watu wa kipato cha chini. Anasema upunguzaji wa viwango vya kodi kutapunguza ukwepaji kodi ambao ulikuwa unafanyika sana.

Alisema kuongezeka kwa mapato ya serikali ni muhimu katika mipango ya rais Duterte ya kuboresha miundombinu. Hii inatokana na ukweli kwamba kwa muda mrefu nchi hiyo haikuwa inawekeza sana katika miundombinu.
Vipaumbele vingine katika mipango hiyo ni pamoja na kuboresha viwanja vya ndege na njia za reli nchini kote – hasa katika maeneo ya nyumbani kwa Rais Duterte mwenyewe – visiwa vya Mindanao.Ripoti ya World Economic Forum ya hivi karibuni inaonyesha Ufilipino ni ya 95 katika uwekezaji katika sekta hiyo, ikiwa chini zaidi ya nchi nyingine katika eneo hilo la kusini mashariki mwa Asia – kama vile Indonesia, Malaysia, Vietnam na Thailand.

Vingine katika ajenda aliyoipigia debe wakati wa kampeni ya uchaguzi ni kuondoa vizuizi kwa watu wa nje kumiliki makampuni nchini, kurekebisha sheria za umiliki wa ardhi, kuboresha sekta za elimu na afya na kuharakisha maendeleo vijijini.

Aidha Duterte aliahidi kumaliza uasi uliokuwepo nchini kwa miaka mingi – hasa ule unaoendeshwa na Waisilamu katika kisiwa hicho cha Mindanao – eneo anakotoka ambapo tayari serikali yake imeshapeleka Bungeni muswada wa sheria utakaowapa Waisilamu wa Mindanao madaraka zaidi ya kujiamulia mambo yao wenyewe.

Hata hivyo wachunguzi wa mambo wanasema ili yakamilike, kunatakiwa nidhamu na muda wa kuyashughulikia kikamilifu, hali ambayo bado haipo kwa sababu muda mwingi unatumika katika masuala ya vita dhidi ya watumiaji wa dawa za kulevya.

Wananchi wengi walikuwa na matumaini kwamba hali hii ingebadilika, hasa pale mwezi Januari Rais Duterte alipoisitisha vita hiyo baada ya polisi kumuua mfanyabiashara maarufu wa Korea ya Kusini.

Lakini wiki iliyopita Mkuu wa polisi wa nchi hiyo alitangaza kwamba tatizo la utumiaji dawa za kulevya linarejea miongoni mwa jamii na hivyo Rais Duterte kaamuru mapambano yaendelee.

  • Makala hii imeandikwa kutokana na vyanzo mbali mbali vya Inteneti.