Home Makala UFISADI WAIGAWA KNCU KILIMANJARO

UFISADI WAIGAWA KNCU KILIMANJARO

1482
0
SHARE

NA SAFINA SARWATT, KILIMANJARO

G32 ni Vyama 32 vya ushirika wa wakulima wa kahawa Mkoani Kilimanjaro, ambavyo vilijitenga na Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) kutokana na ufisadi mkubwa unaoendelea ndani ya chama hicho.

Hata hivyo,  ufisadi huo wa mali za  wanachama  ulisababisha vyama  hivyo kugawanyika ambapo vyama 76 kati ya 92 vilijiondoa na kuamua kukoboa kahawa kwenye viwanda binafsi huku vyama 18 vilivyo chini ya G32 na 29 vya watu binafsi vikikoboa kahawa zao TCCCO.

Ufisadi huo uliigharimu KNCU kukosa mweleko hali iliyochangia kuyumba kwa chama hicho kikuu cha ushirika  mkoani Kilimanjaro na kukumbwa madeni makubwa ya benki ya CRDB, Mishahara wafanyakazi pamoja na madeni ya vyama vya ushirika.

Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kwamba G32 kwa sasa imekuwa kimbilio na faraja kwa wakulima wa kahawa mkoani Kilimanjaro na mkombozi wa vyama vya ushirika baada ya KNCU kukosa mweleko.

Aidha, G32 ni miongoni mwa vyama vya ushirika 92 vilivyojitenga na KNCU na kuanzisha umoja wao kwa lengo la kuendeleza kilimo cha kahawa na kurudisha uhai wa ushirika ambao ulikuwa mkombozi wa wananchi mkoani Kilimanjaro.

G32 kwa sasa imechukua jukumu kubwa wakukifufua kiwanda cha kukoboa kahawa cha TCCCO ambacho kilishindwa kujiendesha kutokana na ufisadi uliofanywa na viongozi wa KNCU pamoja na baadhi ya watumishi hali iliyowapelekea wakulima kuacha kupeleka kahawa zao kwenye kiwanda hicho.

Meneja wa G32, Gabriel Ulomi anasema kuwa  vyama hivyo 32 viliamua kujitenga kutokana na wizi wa kahawa za wakulima pamoja na ufisadi ulioko ndani ya KNCU.

Anasema baada vyama hivyo kuondoka na kuanzisha umoja wao unaitwa G32 Kilimanjaro new Co-operative initiatives-JVE LTD kiwanda cha TCCCO kilikosa kahawa na kushindwa kujiendesha hali ambayo ilichangia kiwanda hicho kusimama kwani hata wakulima waliobakia walikuwa hawapeleki kahawa.

“Wizi wa kahawa za wakulima na ucheleweshwaji wa malipo ya kahawa za wakulima ndiyo iliyochangia wakulima kimbilia kwenye viwanda vya watu binafsi kukihama kiwanda chao ambacho ndiyo mali ya ushirika,”anasema Ulomi.

Anasema kuwa G32 iliandikishwa rasmi mwaka 2008 ambapo mpaka sasa inamtaji mkubwa wakujiendesha wenyewe.

“Sisi  G32 ndiyo tumewalipa mishahara mitano wafanyakazi wa kiwanda cha  TCCCO lengo ni kukifufua kiwanda hicho na kuendeleza ushurika ambao ulikuwa mfu kwa muda mrefu,”anasema Ulomi.

Anasema G32 wamerudisha kukobolea kahawa zao kwenye kiwanda cha TCCCO LTD na kwamba hakuna wizi tena kama ilivyokuwa awali  kutokana na kahawa hizo zinakobolewa kwa ulisimamizi wa G32.

Anasema tunatengemea vyama vinavyokoboa kahawa yao katika viwanda binafsi vitakobolea kahawa yao TCCCO LTD chini ya usimamizi wa G32.

Anasema kuwa vyama hivyo tayari vimeshakubali kurudi TCCCO lengo ni  kurudisha uhai wa ushirika na kuimarisha ushirika wakati serikali ikiendelea kuwashughulikiwa wafisadi waliokitafuna ushirika na kujinufaisha wenyewe.

Akizungumzia mafanikio tangu kuanzishwa kwa G32 anasema kuwa wameweza kujiendesha kibishara na hali ya uzalishaji  wakahawa inaendelea kuwa nzuri.

Anasema kuwa G32   vimeweka makisio ya kuuza nje kahawa bora kilo 153,600,yenye dhamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.6 kwa msimu wa mwaka 2017/2018.

Anasema kuwa kwa msimu huu wanatarajia hali ya soko la nje kuwa nzuri zaidi kuliko msimu uliopita kutokana na bei ya kahawa kupanda katika soko la dunia.

Ulomi anasema kuwa katika msimu ulipita wa mwaka 2016/2017 waliuza nje makontena manne ya kahawa yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 878.7 ambapo bei iliyolipwa kwa wakulima ilikuwa sh 4,000 hadi 5,000 kwa kilo kutegemea na ubora wa kahawa.

Kwa upande wa soko la ndani kwa msimu wa 2017/2018, G 32 inatarajia kuuza kahawa safi kilo 120,353 sawa na magunia 2407 ambayo  ni zaidi ya shilingi milioni 837.6.

“Licha ya jitihada nyingi ambazo tumekuwa tukifanya za kutafuta masoko ya nje lakini wanunuzi wengi pia wanahitaji kahawa bora huku tukikabiliwa na changamoto ya ukame na matunzo hafifu  pamoja na wanunuzi kuhitaji kahawa ambayo  imesajili.

“Bodi na menejimenti wanaendelea na mikakati ya kutafuta masoko ya nje katika nchi za China, Japani, Zambia, Amerika, Finland, Korea na Afrika Kusini,”

Anasema kuwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa soko la nje pia kuna changamoto ya uzalishaji mdogo wa kahawa kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabia ya nchi.

Anasema kuwa chama kinaendelea kutoa taarifa sahihi kwa Serikali juu ya kushuka kwa bei ya kahawa pamoja na kuiomba Serikali kuweka ruzuku ya pembejeo kwa zao la kahawa ili kumpunguzia mkulima gharama za ununuzi wa pembejeo na kutokata tamaa kutokana na gharama za uzalishaji.

Mradi wa pamoja wa vyama 32 vya ushirika  ulibuniwa msimu wa mwaka 2002/2003 baada ya sheria ya ushirika na ile ya kahawa kubadilika mwaka 1994 hivyo kuruhusu wakulima kuuza kupitia ushirika, watu binafsi au kampuni kupitia sheria mpya iliyoruhusu soko huria.

Anasema kuwa makosa yaliyofanywa na Bodi ya TCCCO iliyopita yameathiri wakulima wa kahawa na uchumi wa Taifa kwa ujumla, ni aibu ya karne na kwamba haya hayapaswi kurudiwa tena.

Kaimu Meneja Mkuu wa TCCCO, Mhandisi Japhet Ndossi, anasema kujiondoa kwa vyama hivyo kukoboa kahawa zao kiwandani kulipelekea mapato yake kushuka.

Anaongeza kuwa hali  hii ilisababisha kiwanda kuwa na madeni makubwa ambayo inadaiwa na taasisi mbalimbali kama vile mamlaka ya mapato nchini (TRA), mfuko wa jamii NSSF na wafanyakazi ambao hawajalipwa mishahara yao kwa mwaka mmoja sasa.

Aidha, anasema kahawa iliyopokelewa katika kiwanda hicho chenye uwezo wa kukoboa tani za kahawa 50,000 kwa mwaka, ni tani 726.15 tu, ikilinganishwa na tani 65,736 msimu wa 1980/1981.