Home KIMATAIFA Ugaidi ni mwendelezo wa ukatili duniani

Ugaidi ni mwendelezo wa ukatili duniani

557
0
SHARE

NA PROF. AZARIA MBUGHUNI, MAREKANI

UGAIDI si kitu kipya duniani. Katika historia ya binadamu kuna mifano mingi watu au kikundi cha watu wametumia imani zao kuhalalisha ukatili usio na kifani dhidi ya binadamu wenzao. Hakuna kikundi kilicho mwaga damu nchini Marekani kama kundi la KKK (Ku Klux Klan). 

Wakati Fulani nilipata nafasi ya kutembelea mji wa Pulaski uliopo katika jimbo la Tennessee nchini Marekani, kuona pahali ambako kundi la KKK liliundwa. Mji wa Pulaski uliopo kwenye jimbo la Tennessee ni mji ambao kikundi hichi cha kigaidi kilipoundwa. Ni kikundi kilichopata sifa kubwa ya uuaji wa kikatili, ubakaji, ulipuaji mabomu na mambo mengine mengi ya kikatili, kiliundwa mnamo mwaka 1866. 

Pamoja na kwamba zaidi ya miaka 150 imepita tangu KKK iundwe, uamuzi wa kutembelea mji na nyumba ambayo kikundi hicho kiliundwa haukuwa rahisi. Haikuchukua muda mrefu kuliona jengo ambalo wazungu wa kusini waliopigana vita vya mwaka 1861-65 kati ya Marekani ya Kusini na Kaskazini walikutana na kuamua kuanzisha kikundi chao. 

Moja ya sababu ya hivyo vita ilikuja kuwa utumwa. Mwanzoni watu wa kusini Marekani walitaka kuachiwa waamue wenyewe sera zao, pamoja na ya utumwa. Kwa upande wa Kaskazini, wao walikuwa wanataka kujaribu kupunguza utumwa. Vita vilipoanza mwaka 1861 ilikuwa kwa sababu sehemu za kusini zilitaka kujitenga na Kaskazini wakaanza vita ili kuhakikisha nchi haigawanyiki. 

Mwanzoni hata watu wa Kaskazini pamoja na raisi Abraham Lincoln hawakuwa na nia ya kuondoa utumwa. Nia yao ilikuwa ni kuhakikisha nchi inabaki moja. 

Baada ya kama mwaka mmoja wa vita, upande wa Kaskazini ukashtuka kwamba wa kusini walikuwa wanatumia watumwa kujijenga kwenye vita na kwamba wanaweza kuwashinda kusini kama wakitangaza utumwa umekwisha kusini. 

Hilo Lincoln alitanganza mwaka 1863. Vita hivi havikuanza kwasababu ya utumwa tu, ila utumwa ukaja kuwa sababu kubwa ya hiyo vita na chanzo cha ushindi wa kaskazini baadaye. 

Turudi kwa askari waliopigana upande wa kusini, mnamo mwaka 1866, karibu mwaka baada ya vita kuisha, kikundi cha watu walikutana kwenye Ofisi ya kinyozi wakaunda KKK huko Pulaski, Tennessee. 

Kikundi hicho cha kigaidi kilitumia nguvu, vitisho, umwagaji wa damu kuhakikisha watu weusi wanaoishi kusini wanarudi karibu na utumwa ingawa utumwa ulishakatazwa kutokana na sheria mpya za nchi. 

Katika mkutano wao wa kwanza mkubwa uliofanyika Nashville, Tennessee, viongozi walikuja kutoka miji mingi ya kusini, pamoja na Jenerali Nathan Bedford Forrest, mkuu wa majeshi ya kusini wakati wa vita. Jenerali Forrest alipewa cheo cha Grand Wizard wa KKK, yaani mkuu wa kwanza wa kikundi cha KKK. 

Kati ya mwaka 1868 na 1870, KKK ilihakikisha watu weupe wanashika sehemu zote za kusini kwa kutumia mabavu. Hatuwezi kujua watu weusi wangapi waliuliwa kikatili kuhakikisha watu weupe wanashika tena Marekani ya kusini. 

Wanasiasa karibu wote kuanzia Majaji na wakuu wa polisi (Sheriffs) wanaochaguliwa kwenye uchaguzi wote walikuwa wanachama wa KKK. Kulikuwa hakuna haki kwa mtu mweusi kuanzia polisi mpaka mahakamani. 

Walikuwa wanakuja mchana nyumbani kwa mtu, wanamchukua na kumuua wazi kikatili kwa visababu tafauti, kama mtu kamsalimia mwanamke mzungu au visababu vingine visivyo na msingi; cha muhimu, na nia yao kubwa, ilikuwa kuwatisha watu weusi wabaki chini.

KKK ilikuja kuwa na wanachama wengi zaidi mwanzo wa karne ya ishirini. Inasemekana walikuwa na wanachama zaidi ya milioni nne katika Marekani kipindi hicho. Wanasiasa wengi walikuwa wanachama wa wazi wa KKK hadi miaka ya 1920. Mmoja wao alikuwa ni Hugo L. Black, Jaji wa Mahakama Kuu ya Marekani. 

Ni vigumu kusema watu wangapi waliuliwa na KKK. Lakini kuna wanaosema watu 4000 waliuliwa na kikundi hicho. Ukweli hatutaujua, kwani kuna wengi zaidi waliuliwa na hamna aliyetoa ripoti. 

Kuna mauji ya kikatili ya mji mzima wa watu weusi huko Tulsa, Oklahoma mwaka 1921, mauaji ya Emmet Till huko Mississippi mwaka 1955, mauaji ya Medgar Evers, bomu lilioua watoto kanisani Birmingham, Alabama mwaka 1963, na mauaji ya Jason Smith huko Louisiana mwaka 2011, yote yalifanywa na wanachama wa KKK. 

Smith walimkuta ametolewa utumbo ingawa wanasema alizama kwenye maji. Mateso na taabu walizopata watu weusi Marekani kwa sababu ya hawa magaidi ni vigumu kueleza ieleweke. 

Leo hii kuna wazungu wengi ambao bado wanafuata sera za KKK ingawa wanajificha na sio rahisi kuwajua. Baadhi yao ndio wanaongoza nchi ya Marekani. Tafakari hawa watu wanaoendesha nchi hiyo wanaangaliaje watu weusi, Waafrika, na watu wengine wasio wazungu leo hii.

Nilipita na kupiga picha kwenye hilo jengo la KKK nikajiondokea Pulaski, Tennessee. Sina mpango wa kutembelea mji huo tena, labda nirudi kupigana vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wa binadamu wenzangu. Hapo nitarudi na kusimama na mkono mmoja juu.