Home kitaifa Ugaidi una sura nyingi usipuuze

Ugaidi una sura nyingi usipuuze

1060
0
SHARE
ASKARI WAKIWASAKA WAHALIFU KWENYE MAPANGO YA AMBONI JIJINI TANGA
ASKARI WAKIWASAKA  WAHALIFU KWENYE MAPANGO YA  AMBONI JIJINI TANGA
ASKARI WAKIWASAKA WAHALIFU KWENYE MAPANGO YA AMBONI JIJINI TANGA.

Na Yona Maro,

KATIKA kipindi cha miaka miwili nchini Tanzania kumekuwa na matukio kadhaa yenye viashiria vya ugaidi. Miongoni mwa matukio hayo ni pamoja na kutupwa kwa mabomu ya mkono mkoani Arusha, kumwagia watu tindikali visiwani Zanzibar, kuuawa kwa watu msikitini na hali ya hatari katika mapango ya Amboni.

Kabla ya tukio la watu kuingia msitikiti na kuua wenzao, kulisambaa habari za watu wanaojiita wafuasi wa Islamic state kuwa na makazi yao nchini, pia kumekua na video nyingi zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zenye mahusiano yanayofanana .

Ugaidi una sura nyingi na sababu nyingi ila muda mwingine ni watu wanaopigania maslahi na mengine ndani ya maeneo fulani ambayo walipoteza ushawishi sasa wanataka kurudisha, kuondoa serikali wasizozitaka, kutafuta maslahi ya kiuchumi na kutafuta njia ya kufanikisha biashara haramu za silaha, dawa za kulevya, kuuza binadamu na mengine mengi.

Kwa Tanzania  sababu za ugaidi au harakati za namna hiyo zinaweza kuwekwa katika makundi manne muhimu; Kwanza ni suala la bomba la gesi toka Mtwara kwenda dar  es salaam , pili kuna bomba la mafuta toka tanga kwenda Uganda, vuguvugu la kisiasa na maisha visiwani Zanzibar, na suala la kupambana na rushwa, ulanguzi na mengine linaloendelea kusimamiwa na serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli yenye kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu!

Miradi ya mabomba ya Tanga na Mtwara inajulikana kukwaza baadhi ya mataifa ya nje na wabia wao wengine waliokua wanategemea njia kupata kandarasi za kujenga mabomba na kuyasimamia kwa kipindi kirefu. Kama ikienda vizuri ina maana Tanzania na majirani zake wataacha kununua bidhaa hizo maeneo mengine duniani hasa Arabuni, kwa hiyo moja ya mbinu inayoweza kutumika na maaduni ni hii ya kuhujumu, kuanzisha vikundi vya kigaidi na waasi ambavyo vitakua vinacheza maeneo hayo yenye rasilimali mfano halisi wa hali hii angalia Niger delta nchini Nigeria, Libya, Syria, Iraq, Mashariki mwa Congo, Sierra Leone na Liberia, huko kote kuna rasilimali za aina mbalimbali.

Pia kuna suala la kundi la Islamic state kushindwa kwa kiasi kikubwa huko Iraqi na Syria, hapa wapiganaji na wafuasi wengine waliokua maeneo hayo wanakimbia na kurudi makwao kama Tanzania, Kenya, Uganda na kwingine hawa wanaporudi na mbinu, uzoefu na silaha wakati mwingine wanaweza kuanzisha vikundi vya kigaidi au vingine vya vurugu.

Sasa kama taifa la Tanzania tufanyeje? Huu ni ushauri wangu mfupi wa mbinu mbalimbali tunazoweza kutumia kukabiliana na hali hii kutokana na maelezo ya utangulizi niliyotoa hapo juu na mengine nitakayoongezea .

Kwanza tuboreshe mahusiano kati ya vyombo majeshi na raia au wananchi wa kawaida huko mitaani, kuboresha kwa maana ya kuwa na mfano mawasiliano ya bure yanayopatikana muda wote katika call centre ya polisi, kuwe na vitengo vinavyojihusisha na raia moja kwa moja kuanzia polisi, jeshi na wengine ambapo mwananchi anaweza kutembelea kuonana na wahusika kwa ajili ya kutoa taarifa na mengine ambayo anayo bila kutishwa, kuulizwa maswali ya kudhalilishwa na mengine ambayo hutokea mara kwa mara.

Kuna matukio yamewahi kutokea mwananchi anaweza kutoa taarifa polisi au kwa polisi lakini akaambiwa hamna tukio kama hilo, au anaambiwa jeshi hupata taarifa hizo kwa njia maalumu za kijeshi na wakati mwingine anaweza kuambia arudi kufanyia uchunguzi taarifa zake kisha awasilishe tena, yawezekana raia husika hajui chochote kuhusu upelelezi, uchunguzi na mengine ya kiusalama na hata vifaa na rasilimali nyingine hana kwa hiyo anaweza asitoe kabisa ushirikiano kwa kuhofia usalama wake na mengine yanayoweza kuhusika .

Jeshi la Polisi na idara nyingine zifungue milango ya mawasiliano kwa njia nyingine kama za mitandao ya kijamii kwa ajili ya kupokea taarifa, kujibu maswali na kutoa maelekezo ambayo yanaweza kusambazwa kwa makundi mengi ya watu maana si kila mtu anaweza kwenda kituoni , au kupiga simu au kufanya mawasiliano ya papo kwa hapo lakini kwa kutumia mitandao ya kijamii.

Pia kuna hitajika think tank yaani vikundi na taasisi kwa ajili ya kuandaa mijadala ya wazi kuhusu masuala mazima ya ulinzi na usalama, hapa wananchi wanaweza kualikwa kusikiliza hoja mbalimbali, kuuliza, kukosoa na kuelimishwa kuhusu masuala mbalimbali lakini Zaidi kukutana na viongozi wa jeshi la polisi, jeshi la wananchi, magereza na wadau wengine wa sekta hii kama viongozi wa dini n.k .

Hili la think tank limetumika na nchi nyingi hasa zile zilizoendelea katika propaganda, kutoa taarifa na mengine mengi kwa maslahi ya nchi zao. mijadala inaweza kuandaliwa ndani ya vyuo na maeneo mengine ya umma ambayo kila mtu anaweza kwenda .

Matukio ya kusambaza picha za kutisha hasa zinazohusu ugaidi na ukatili mwingine ni ya kuangaliwa pia, ingawa kila mtu ana uhuru wa kusoma na kusambaza picha kwa nia ya kujifunza na kuelimisha lakini hili linaweza kuchochea hasira, chuki, visasi na mengine kwa baadhi ya jamii kitu ambacho makundi ya kigaidi na maadui wanapenda kukitumia katika kutafutwa kuungwa mkono ili kutekeleza shabaha zao fulani fulani .

Katika tukio la Mwanza, tumeona picha za watu waliolala chini baada ya kuumizwa na wengine kupoteza maisha, wakati wa matukio ya kushambulia vituo vya polisi mkoa wa pwani na staki shari, hata matukio ya wakulima na wafugaji kupigana napo kuna watu walisambaza picha za kutisha na picha nyingine zimepigwa huku viongozi wa polisi, siasa wakiwa pembeni bila wasiwasi .

Kwa hili la picha tunaweza kujifunza kutokana na matukio ya ugaidi nchini Ufaransa na Ubelgiji hapa sijui nani aliona picha za miili zikisambazwa katika mitandao ya kijamii au magazeti ni kwa sababu wanajua athari zake za kusambaa kwa picha hizo ni ushindi kwa magaidi na wafuasi wao wengine.

Suala la picha za kutisha limeshafanyiwa marekabisho ya sheria nchini Kenya kutokana na Al Shabaab kutumia mbinu hiyo kutisha na kutafuta kuungwa mkono, kwahiyo ukiwa kenya na kusambaza picha za kutisha za ajali, matukio ya mabomu au chochote basi jela ina kungoja maana utakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dol .

Tuangalie suala la vikundi vya mikopo au vingine vinavyohusu fedha ambavyo havina usajili au hata vile vyenye usajili. makundi ya kigaidi na wahalifu yanaweza kutumia mbinu hii kuficha fedha, kusafirisha na hata kulipana lakini kwa njia ya mikopo na hapa tutaenda mbali zaidi hata kuchunguza mali na maisha ya baadhi ya watu ambao wanaweza kuwa mawakala wa magaidi na vikundi vya kihalifu kwa kujua au kutokujua .

Intelegensia lazima iingie ndani ya makundi ya wahalifu na sehemu nyingine mbalimbali ili kuweza kujua wahusika, zana walizo nazo, mipango yao ya baadaye na kuwa na nia ya dhati kabisa ya kuvimaliza kutokea katika mashina na mizizi yao. Mbinu hii ilitumika na uingereza baada ya kushambuliwa jijini London miaka kadhaa iliyopita, kwahiyo kwa sasa ni ngumu sana kwa mfuasi wa ugaidi na mawakala wao kukanyaga ardhi ya Uingereza bila kujulikana kisha kuripotiwa na polisi au idara nyingine kuchukua hatua kwa muda unaofaa.

Suala la kamera za usalama maarufu kama CCT, itungwe sheria ya kulazimisha wenye kumiliki vyombo hivi kuhifadhi video kwa muda fulani labda miezi 6 mpaka mwaka na endapo jeshi la polisi litataka basi lipatiwe rekodi husika kwa ajili ya kufanyia uchunguzi na mengine yanayoweza kuhitajika, maana tumeona matukio ya watu kuibiwa katika mabenki, maduka na maeneo mengine lakini baada ya muda video hufutwa au hukatwa vipande au kufanyiwa marekabisho kitu ambacho sio vizuri katika suala la ushahidi na ufuatiliaji.

Lazima kuwa na nia ya dhani ya kuelewa nia ya watu kujiingiza katika siasa kali na kuunda vyombo vya kushugulikia suala hili kwa kushirikiana na wadau wengine ambao wamefanikiwa katika kukabiliana na hili hii.

Ni jambo la muhimu kushirikiana na serikali nyingine ili kutengeneza njia sahihi za kuzuia kuenea kwa siasa kali. mfano mzuri ni jirani zetu kenya, Somalia na maeneo mengine ambayo yanakabiliwa na vitendo vya siasa kali na ugaidi.

Tunaweza kuomba msaada kutoka maeneo mengine kuhusu baadhi ya vitu katika masuala ya kisiasa, jamii ili kusaidia kutambua maeneo yenye siasa kali na kuwa na mipango endelevu ya kushugulikia ili isisambae na kuathiri jamii kwa ukubwa wake.

Katika maeneo ambayo siasa kali zinaendelea kushika kasi lazima kuwe na viongozi wa kuelimisha ili watu wabadilike dhidi ya siasa kali na vikundi vya vurugu.

Lazima serikali iwe na nguvu kwa kushirikiana na taasisi nyingine kutenga, kuingilia na kutengeneza maeneo maalumu ya kuponya watu walioingizwa katika siasa kali ili waweze kubadilika na kuwa watu wema waishi maisha kama ya wengine baadaye.

Mwisho ni kuangalia na kufuatilia vikundi vya kujitolea na watu wanaowaleta vijana wa kujitolea toka sehemu mbalimbali duniani. Inajulikana kwamba kuna majasusi, wapelelezi na maadui wengine wa nchi wanaoingia nchini kwa mgongo wa kujitolea kwa ajili ya kutafuta taarifa, kupata watu wa kuwaunga mkono na mengine mengi.

Sheria ya kujitolea lazima iangaliwe upya na kila anayekuja kujitolea ajulikane na awe anafuatiliwa kila hatua mpaka atakapoondoka kwa maslahi ya taifa.

Mwandishi wa Makala hii sio mwajiriwa wa chombo chochote cha ulinzi na usalama na kilichoandikwa humu ni mawazo yake binafsi .

                                                0786 806028