Home Latest News Ugonjwa wa Covid-19 na athari za kiuchumi

Ugonjwa wa Covid-19 na athari za kiuchumi

244
0
SHARE
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango

NA LEONARD MANG’OHA

KUIBUKA kwa ugonjwa wa virusi vya Corona mwishoni mwa mwaka jana nchini China na kisha kuenea duniani kote, kumeathiri shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Mataifa mengi duniani yameshuhudia kusimamishwa kwa shughuli nyingi za uzalishaji, kijamii pamoja masuala ya michezo na burudani huku uchumi ukianguka kwa kiasi fulani.

Bara la Afrika kama sehemu ya dunia limekuwa sehemu ya janga hilo huku likitabiriwa kushughukia kiasi kikubwa cha vifo kutokana na mifumo dhaifu ya afya katika mataifa mengi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa huenda watu milioni 250 wataambukizwa virusi vya Corona katika kipindi cha mwaka mmoja barani humo ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa.

Kupitia mjadala wa kila mwaka wa kabla ya bajeti unaoratibiwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) uliofanyika hivi karibuni wadau mbalimbali wamejadili masuala kadhaa ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika bajeti ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza wakati wa majanga ikiwamo masuala ya sera za kifedha, hifadhi ya jamii na masuala muhimu ya afya.

Mhadhiri wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, anasema Corona imevuruga vyanzo vya mapato vya kikodi na visivyo vya kikodi pamoja na matumizi kwa kulazimisha Serikali kutoa fedha eneo moja na kuzipeleka eneo jingine kama njia ya kukabiliana na janga hilo.

Anasema hali hiyo itasababisha kushindwa kufikiwa kwa matokeo ya ukuaji wa uchumi yaliyotarajiwa hasa kutokana na kuvuruga kabisa robo ya mwisho ya mwaka wa fedha huku akikiri kuwa hali ya mfumko wa bei hapa nchini imeendelea kuwa nzuri ukiwa katika asilimia 3 hadi 3.5.

Profesa Ngowi anasema kuwa biashara ndogo ndogo na utalii na usafiri ndizo zimeathirika zaidi kutokana na njia zake kufanyika kwake kulazimika kufungwa kama njia ya mapambano ya Corona.

“Tumeshuhudia shule kuanzia vyuo vikuu hadi shule za msingi zimefungwa kwa hiyo wale watoa huduma wa cafeteria, wasambazaji wa mayai, mbogamboga, maji ambao wengi wao ni wanawake wamepoteza kazi,”anasema Profesa Ngowi.

Anasema haiwezikani kuelezea suala la kuathirika biashara bila kuitaja Covid-19 ambayo imeathiri baadhi ya biashara moja kwa moja huku zingine zikiathirika kutokana na hatua zinazochukuliwa kukabiliana na janga hilo ikiwamo kuzuia mikusanyiko ambapo biashara zilizokuwa zikifanyika katika mazingira ya mikusanyiko hazifanyiki tena.

Anasema kwa sasa sera pana za kikodi zinahitajika ili kunusuru biashara mbalimbali nchini kama ambayo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilivyofanya hivi karibuni kwa kupunguzia riba mabenki.

Profesa Ngowi anasema kwa sasa benki za kibiashara pia zinapaswa kushusha viwango vya riba kwa wafanyabiashara ili kuwezesha biashara zao kuendelea pamoja na kutoa unafuu kwa wafanyabiashara kulipa madeni yao ikiwa ni pamoja na muda wa kulipa madeni hayo kutoka mwaka mmoja hadi miwili.

“Mfano wakati wa mtikisiko wa uchumi mwaka 2008 kodi ya onezeko la thamani ambayo kihistoria ilikuwa asilimia 20 ilipunguzwa hadi asilimia 18. Sasa hili tulichukulie kama fursa ya kuweza kujifunza,”anasema Profesa Ngowi.

Anasema kuwa kutokana na madhara ya majanga wajasiriamali wanapaswa kupewa fedha zitakazosaidia kuokoa biashara zao jambo ambalo likifanyika katika baadhi ya mataifa ikiwamo Ghana.

Pia mifumo ya hifadhi ya jamii (social protection) inahitajika zaidi kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote jambo ambalo hapa nchini halijafanyika vya kutosha.

Mkuu wa Idara ya Jinsia na Fedha katika taasisi isiyo ya kiserikali ya FSDT, Anna Mushi anasema kuwa athari za kiuchumi yanapotokea majanga ya aina hii ni kubwa kwa sababu sekta nyingi huathirika.

Anasema kuwa tayari ripoti mbalimbali za kidunia likiwamo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) zinaonesha kuwa uchumi katika mataifa mengi duniani utaanguka na ukuaji wake utakuwa wa asilimia hasi tatu katika baadhi ya mataifa na huenda ukazidi wakati wa mdororo wa uchumi wa mwaka 2008.

Makundi ya wanawake, vijana na wanaume masikini anayataja kama makundi yatakayoathirika zaidi kutokana na janga hilo.

Anasema kutokana na hali hiyo, sekta ya fedha inapaswa kusaidia kunusuru hali hiyo ambapo anashauri BoT na TCRA kuja na mikakati wezeshi inayozingatia makundi ya pembezoni hasa kwa kuzingatia kuwa watu wengi wenye kipato cha chini hasa wanawake wanatumia huduma za fedha kupitia simu kuliko benki.

“Sera za benki haziwagusi watu wa chini kwa sababu si wateja wake badala yake wanaopoteza katika vikundina hutumia zaidi simu kutoka na kupokea fedha zao.  Watu wa chini hasa kina mama wakishindwa mikopo yao wasinyang’anywe mafriji yao ya kufanyia biashara.

“Huduma za simu kwa kutuma fedha kiwango kidogo zisiwe na makato kama njia ya kuwasaidia watu wa chini. Pia watoa huduma za kifedha ni muda wa kuja na bidhaa bora na kuanzia kuwa ambush wateja wao.

Anasema ni muhimu sasa kuwa na mfumo mzuri wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), ili kuangalia namna ya kuongeza mnyororo wa thamani katika sekta zinazoajiri watu wengi ikiwamo biashara za rejareja na kilimo ambazo zimeajiri idadi kubwa ya wanawake inayokaribiana na wanaume ambapo anaamini kuwa ikiwa mazingira yakiboresha itakuwa na manufaa kwa sababu biashara hizo zitakuwa na uhakika wa soko kwa sababu hutumiwa zaidi na watumiaji wa ndani.

Mkurugenzi wa Taasisi inayojihusisha na kuwawezesha wanawake na watoto wa kike kiuchumi, Jovita Mlay anashauri kuwa kutokana na changamoto zilizojitokeza katika sekta ya afya wakati wa kupambana na Corona anashauri kuongezwa kwa muda wa bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili kuangalia namna ya kuwasaidia walioathiriwa na janga hilo.

Anasema hilo linapaswa kufanyika baada ya kufanywa utafiti mdogo kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi ili kubaini athari zilizojitokeza.

“Pia TRA ibadili njia zake za ukusanyaji kodi kwa sasa ije na njia rafiki kwa wafanyabiashara kipindi hiki kuliko kuendelea kuwasumbua wateja wake wakati huu walioathirika kwa kiasi kikubwa,”anasema Jovita.

Anasema kuwa alitegemea katika bajeti iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo, ingeonesha jinsi gani wizara hiyo itashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kufikisha teknolojia vijijini ili kuwawezesha watoto wote kuendelea na masomo wakati huu wa Corona na majanga mengine yatakapojitokeza.

Jovita anasema kwa sasa ni kundi dogo tu la watoto wanaoweza kujifunza kwa kutumia njia ya kiteknolojia ikiwamo matumizi ya televisheni na intaneti na kwamba radar wanapaswa kupaza sauti zaidi ili kuhakikisha watoto wengi wanafikiwa.

“Serikali iwe na nguvu zaidi wakati huu ili kuwa na ufanisi kwenye elimu, afya na maji na kuweza na database ya kushughulikia mambo hayo,”anasema Jovita.

Mtaalamu wa Afya Jamii kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa Ifakara, Grace Mhalu anashauri Serikali kuwekeza zaidi katika tafiti na kwamba tafiti nyingi haziangalii masuala ya kijinsia kwa sababu eneo hilo halijapewa uzito wa kutosha.

Akitolea mfano janga la Corona, anasema tafiti zaidi zinahitajika kubaini kwanini wanaume ndiyo wametajwa kufariki kwa wingi ikilinganishwa na wanawake.

Anasema ikiwa wanaume wengi wanafariki na kuziacha familia zao ni wazi kuwa kutakuwa na madhara makubwa ya kijamii kwa sababu baadhi ya tafiti ambazo zimewahi kufanyika hapa nchini ukiwamo ule wa kidemokrasia zinaonesha kuwa kaya nyingi zinazoongozwa na wanawake peke yao zinakabiliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwamo watoto kutopata chanjo.

Pia anasema kuwa kwa kulitazama janga la Corona katika mrengo wa kijinsia wanawake wengi wanawekwa katika hatari zaidi kwa kuwa ndiyo walio wengi katika sekta ya afya ikilingalishwa na wanaume.

“Lakini kitendo cha watoto kubaki nyumbani mimba na ndoa za utotoni zinaongezeka kwa sababu wengine huozeshwa. Lakini pia mifumo ya afya inazorota hasa afya ya uzazi ikiwamo kuzidiwa na mimba kwa sababu rasilimali zilizokuwa zitumike kwenye afya zinahamishiwa kwenye majanga.

“Tulichukulie mfano DRC wakati wa mapambano ya Ebola vifo vya kinamama viliongezeka kwa sababu hakukuwa na huduma bora za afya. Majanga kama mafuriko huathiri kina mama na watoto kwa malaria pia huwazuia kushiriki katika shughuli za maendeleo,” anasema Grace.

Mratibu wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Makumbusho jijini Dar es Salaam, Janeth Mawinza, anasema umefika wakati wa kuwa na bajeti inayoonesha wazi mfuko wa majanga unaolenga makundi ya pembezoni wakiwamo watu wenye ulemavu na iwe na namna bora ya kushughulikia vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati wa majanga.

Janeth anasema ni vema kuwa na bajeti inayoweza kutoa fidia kwa wanawake waliojiajiri katika kilimo ili kuwapa nguvu ya kuendelea kama mwanzo kabla ya kutokea majanga.

“Kwenye afya kuwa na mfuko wa kutoa mafunzo maalumu ya kushughulikia majanga ili kuepuka kutoa fedha katika maeneo mengine,” anasema Janeth.