Home Makala UHABA WA MAJI UNAKOLEZA UMASIKINI TANGA

UHABA WA MAJI UNAKOLEZA UMASIKINI TANGA

1440
0
SHARE
Uhaba wa maji unavyoathiri baadhi ya wanawake nchini

NA AMINA OMARI, MUHEZA

Maji ni moja ya rasilimali muhimu kwa ustawi wa binadamu pamoja na viumbe vyote duniani. Lakini maendeleo ya sasa yameifanya rasilimali hiyo kuwa finyu.

Uharibifu wa vyanzo vya maji ikiwamo kukata miti ovyo, kuchimba madini kwenye maeneo ya vyanzo vya maji ni sehemu ya changamoto zinazosababisha uhaba wa maji pamoja na uharibifu wake.

Licha ya rasilimali hiyo kuwa ni kiungo muhimu cha maendeleo miongoni mwa jamii, bado kuna wananchi wachache wenye tamaa ya mali wamekuwa wakiendesha shughuli zisiso rasmi kwenye vyanzo na kuviharibu.

Jiji la Tanga linategemea huduma ya maji kutoka katika milima ya Amani ambayo ipo wilayani Muheza na maji hayo hutiririka na kumwaga maji yake katika mto Zigi.

Hata hivyo, mto huo una vyanzo vingine vya maji ambavyo vinamwaga maji yake katika mto huo kama mto Kihuwi, unatoa maji yake katika maeneo ya Potwe, Mto Muzi unaotoa maji katika maeneo ya Wilaya ya Mkinga.

Lakini shughuli za kujiongezea kipato zimesababisha kuwepo kwa uvamizi katika vyanzo  ambao kwa kiasi kikubwa wameweza kuleta uharibifu wa maji yanatumiwa na wananchi wa Tanga.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira jijini Tanga (Tanga Uwasa), Mhandisi Joshua Mgeyekwa, anasema uharibifu wa vyanzo vya maji umesababisha tope jingi kuingia kwenye bwawa.

Anasema takribani wiki tatu wananchi wa Jiji la Tanga wameweza kupata adha ya huduma ya maji yenye rangi ya udongo kutokana na uharibifu uliofanywa kwenye vyanzo hivyo.

“Unajua kulikuwa na kiangazi kwa muda mrefu hivyo ilisababisha kupungua kwa utiririkaji wa maji kwenye milima ya Amani, hali hiyo wachimbaji waliweza kuchimba mashimo makubwa kwenye vyanzo hivyo kwa ajili ya kupata madini ya dhahabu,” anabainisha.

Mgeyekwa anasema kutokana na uchimbaji huo, mvua zilipoanza kunyesha kasi ya maji ilikuwa kubwa na kujaa kwenye mashimo yaliyoachwa na wachimbaji hivyo maji yalichafuka,” anasema Mkurugenzi huyo.

Anasema hali hiyo ilisababisha maji yaliyokuwa yanaingia katika bwawa la Mabayani ambalo ni maalumu kwa ajili ya kuhifadhi maji kabla ya kusambaza kwa wananchi kuwa na maji ambayo yamechanganyika na tope.

Mkurugenzi huyo anasema hali hiyo ilisababisha hata mtambo wa kusafisha maji kuweza kuzidiwa nguvu na tope ambalo lilikuwa limechanganyika na maji.

Anaongeza kuwa kutokana na kasoro hizo, mtambo huo licha ya kusafisha maji na kuweka dawa lakini maji hayo yalikuwa yanaenda kwa wateja yakiwa bado na rangi ya udongo.

“Tulikuwa tunaweka dawa kiwango cha NTU 100, lakini kiwango cha tope katika maji yalikuwa yanabadilika hadi kufikia NTU 400 hadi 600 ili kuweza kusafishwa na kuwa katika hali nzuri,” alibainisha Mgeyekwa.

Anasema kubadilika kwa kiwango hicho cha tope mara kwa mara kulisababisha baadhi ya maeneo ya Jiji la Tanga kupata maji ambayo yana rangi ya tope.

“Kutokana na changamoto hiyo walilazimika kupunguza uzalishaji wa maji ili kutoa nafasi kwa mashine kuweza kusafisha maji vizuri kutoka unit 29,500 kwa siku hadi kufikia unit 20,000.

Anasema hali hiyo ya uchafuzi wa maji imewalazimu mamlaka kuingia gharama ya kutumia dawa za kusafisha zaidi ya Kg 1200 ambazo ziliwagharimu kiasi cha Sh milioni 2.2  wakati awali kabla ya maji kuingia tope walikuwa wanatumia dawa kilo 200 kwa ajili ya kusafisha maji kwa siku tofauti na kabla ya maji kuchafuka.

Licha ya uharibifu tayari Tanga Uwasa ilikuwa imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali za uhifadhi wa mazingira katika vyanzo vyake ikiwemo kuwatafutia kipato mbadala wananchi wanaoishi karibu na vyanzo hivyo.

Ramadhani Nyambuka ni mtaalamu wa mazingira kutoka katika Mamlaka hiyo, ambapo anasema waliunda jumuiya za watumia maji. Jumuiya hizo zina wajibu wa kulinda nyanzo vya maji ikiwemo kuvilinda na kuhamasisha upandaji wa miti katika maeneo hayo ili kuvifanya vyanzo viwe endelevu.

Katika maeneo yaliyokuwa yanakabiliwa na shughuli za uchimbaji wa madini, wananchi hao walitafutiwa shughuli mbadala ikiwemo miradi ya vitalu vya miti.

“Mpaka sasa tuna kamati tatu za watumia maji ambazo ni Zigi Juu, Zigi Chini pamoja na Kihuwi ambazo zinawajibika katika kulinda uharibifu wa aina yoyote unaofanyika katika vyanzo hivyo.

“Kuna miradi ya uhifadhi tunayoitekeleza katika maeneo ya milima ya amani kuhusu uhifadhi wa vyanzo vya maji na kuacha kufanya uharibifukama uchimbaji wa madini,” anasema Nyambuka.

Lakini kwa sasa chanzo cha maji cha Mto Muzii kimechimbwa mashimo makubwa pembezoni, matokeo yake tope lote limesombwa na maji kuingia moja kwa moja mtoni na kusababisha madhara.

Mto Muzii unapakana na vijiji vya Mtilia vilivyoko katika kaya ya Bosha wilayani Mkinga ambapo mto huo umezingira na mashamba karibu pamoja na mahandaki kutoka na uchimbaji wa dhahabu.

Mwenyekiti wa Jumuiya wa Watumiaji Maji Zigi Juu, Philipo Mdoe, anasema moja ya mikakati waliyokuwa nayo ni kushirikina na viongozi wa vijiji na kata katika kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.

Anasema chanzo cha uvamizi wa vyanzo vya maji inatokana  na shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo kisichozingatia matumizi bora ya ardhi pamoja na uchimbaji haramu wa madini ya dhahabu.

Anasema tayari jumuiya hiyo imeweza kufanya mikutano na madiwani pamoja na viongozi wa vijiji kuhusu umuhimu wa kulinda vyanzo hivyo.

“Kwa sababu tunawajua wahusika wa uharibifu wa mazingira, hivyo tumewapa jukumu viongozi wa vijiji ambapo maeneo yao yanaendelea na uharibifu basi wahakikishe wanawachukulia hatua stahiki wahusika wote wa vitendo hivyo,” anasema Mwenyekiti huyo.

Anasema Mto Muzii ndio ambao umeathiriwa sana na shughuli zauchimbaji licha ya juhudi mbalimbali wanazozichukua lakini bado viongozi wa vijiji wamekuwa wakiwalinda wahalifu hao.