Home kitaifa UHABA WA MAJI WACHANGIA MIMBA ZA UTOTONI

UHABA WA MAJI WACHANGIA MIMBA ZA UTOTONI

4044
0
SHARE

 

NA JOHANES RESPICHIUS


MAJI ni neema ya kiuumbaji tuliyopewa na Mwenyezi Mungu bure lakini wanasayansi hupenda kusema kuwa maji ni molekuli yenye atomi mbili za haidrojeni na atomi moja ya oxygen.

Kimiminika hiki kinaweza kuwa na maana fupi sana lakini kina umuhimu mkubwa kwenye mwili wa mwanadamu na kutokuwapo kwake kunaweza kuleta athari kubwa katika nyanja zote anazopitia binadamu kama vile kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kisiasa.

Maji hutumika katika shughuli nyingi kama kunywa, ukaoga, ukapikia, ukaoshea, ukanyweshea pia shughuli za kiroho kama kubatiza, kusilimisha, kutibu, kuapisha.

Kutokana na maji hitaji namba moja katika maisha ya binadamu Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umefanya uchunguzi uliobaini kuwa ukosefu wa maji ya uhakika inachangia ongezeko la mimba za utotoni.

Uchunguzi huo umefanywa katika maeneo mbalimbali ya nchi ambayo kuna tatizo la upatikanaji wa maji umetanabaisha uwepo wa mimba za utotoni. Ambapo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa mwaka 2017 mikoa inayoongoza kwa mimba za utotoni ni Katavi unaongoza kwa asilimia 45, Tabora asilimia 43, Dodoma asilimia 39, Mara asilimia 37 na Shinyanga asilimia 34.

Mimba za utotoni zimeendelea kuwapo licha ya serikali kuanzisha kampeni ya kuzuia mimba za utotoni iliyozinduliwa Octoba 11, mwaka jana jijini Dodoma.

Deo Temba ni Afisa Program, Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP, anasema kulingana na takwimu za DHS zinazoonesha kwamba mikoa yenye tatizo la mimba za utotoni ni ile inayokabiliwa na ukosefu wa maji hivyo serikali inatakiwa kuanza kushughulikia kwanza upatikanaji wa maji.

Anasema kuwa kuna uhusiano mkubwa wa ukosefu wa maji na upatikana wa ujauzito kwa wasichana wenye umri mdogo.

“Serikali ni vyema ikahakikisha kunakuwapo na upatikanaji wa maji safi na salama kulingana na mpango mkakati wa Sera ya Maji ya Taifa (NAWAPO) ya mwaka 2002 na Malengo ya Maendeleo ya Kudumu (SDG) ya kuhakisha tatizo hilo linakwisha,” anasema Temba.

Anasema ripoti hiyo ya chunguzi ya mwaka huu imejipambanua kwa mapana katika kuangalia hali ya tatizo hilo na namna gani linaweza kutatuliwa ambapo ni lazima kuwe na miundombinu rafiki katika sekta ya elimu, afya na hata maji kwa kulinganisha na bajeti ya 2018/19.

Anasema pamoja na elimu kuwa miongoni mwa vipaumbele ambapo imekuwa ikitenge kiasi kikubwa cha fedha ili kutoa elimu bura kwa kila Mtanzania bado kumekuwa na changamoto.

“Serikali imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha katika sekta ya elimu kwenye Pato lake la Taifa (GDP) ili kujaribu kuweka miundombinu mizuri ya kujifunzia lakini kuna changamoto ambazo zinahitaaji kushugulikiwa.

“Katika maeneo hayo ambayo hayana maji wanafunzi wamekuwa wakishindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao kutokana na kupoteza siku 3 hadi 7 wanapokuwa kwenye hedhi. Mbali na wanafunzi lakini wanawake wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi kutembea umbali mrefu kutafuta maji hivyo kushindwa kushiriki katika shuguli za kiuchumi,” anasema Temba.

Anasema kuwa ucheleweshwa au kupelekwa kiwango cha chini cha fedha ambazo zinakuwa zimetengwa kwenye bajeti kushugulikia masuala hayo ni moja ya sababu ya sekta ya maji kukabiliwa na changamoto kubwa.

“Mfano katika bajeti ya elimu ya mwaka 2017/18 walitengewa asilimia 75, lakini hadi kufikia Februari 2018 ilikuwa imetolewa asilimia 53 pekee.

“Pamoja na bajeti ya maji ya mwaka 2018/2029 kukaribia kuwa asilimia 7 ukilinganisha na bajeti ya mwaka 2017/2018 tatizo linaweza kuendelea kama hakutakuwa na jitihada za makusudi za kuwakomboa wasichana na wanawake changamoto hii hivyo kumtua mwanamke ndoo kichwani,” anasema.

Anasema ili kutatua tatizo hilo TGNP inaishauri serikali mfumo rasmi wa kutambua na kuwathamini wanawake na wasichana ambao utaeleza kwa kina  ‘Taarifa ya Bajeti ya jinsia na mifumo ya ufuatiliaji’.

Aidha, anasema tatizo la upatikanaji wa maji ni mzigo kwa mwanamke na msichana ambao ndio wanatumia muda mrefu kuyatafuta kwa kutembea umbali mrefu hadi ulipo mto au kisima ili kukidhi mahitaji ya familia kwamba wamelivalia njuga kushauri serikali hadi itengenezea njia madhubuti ya kulishughulikia kwa vitendo.

Kwamba kutokana na wanawake kutembea umbali mrefu kutafuta mji wamekuwa wakikabiliwa na hatari kubwa ikiwamo kutekwa, kubakwa jambo ambalo linaweza kusababisha kupata mimba zisizotarajiwa na hata kuambukizwa magonjwa.

“Ukosefu wa maji ya uhakika na salama kwa muda wote katika maeneo muhimu ya kijamii kama maeneo ya huduma za afya, nyumbani, shule, Vituo vya watoto yatima na katika makazi ya wazee ni hatari kwa jamii.”

“Katika shule nyingi ambazo hazina maji ya kutosha , hali hiyo imekuwa ikichangia wasichana kukosa kufika sshuleni wakaati wanapokuwa kwenye siku zao ambapo wanaweza kutumia siku 3 hadi 7 jaambo ambalo limekuwa likiwasababishia kushindwa vizuri kwenye mitihaani yao,” anasema.

“Mwaka 2014/15 iliasisiwa kampeni ‘Mama tua ndoo kichwani’ kwa lengo la kuvishawishi vyama vya siasa, wagombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kueleze namna watakavyopambana kutatua tatizo la maji iwapo watapata ridhaa ya kuongoza.

“Kampeni hiyo ilifanikiwa na kujikuta ikitumiwa na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli aliyeitumia kama kauli mbiu ’Mama tua ndoo kichwani’,” anasema.

Anasema wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Phillip Mpango, anasoma bajeti ya serikali ya mwaka 2018/19 hakueleza namna atakavyotatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo ambapo wanawake ndio waathirika wa kwanza.

“Ni jukumu la sekta ya maaji na mazingira kushirikiana na sekta nyingine za maendeleo ili kufikia matarajio ya kitaifa katika Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP II) na dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ambaayo inatambua Malengo Mapya ya Maendeleo (SDG) katika kutatua suala la maji.

“kwa muda serikali imekuwa ikijipambanua kutekeleza sera ya kushirikisha sekta mbalimbali kwa kuingiza masuala mbalimbali ya kijinsia ya maji na usafi wa mazingira katika bajeti na mipango yake. TGNP tunashauri kuwa jambo hilo litengenezewe sheria na kufuatiliwa kwa ufanisi ikiwemo kujenga taasisi husika.

“Kwa kuwa Tanzania ina lengo la kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda ni vyema serikali ikahakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma ikiwemo wanawake na watoto kwani ili kufikia mpango wa kitaifa wa mendeleo ni muhimu kuimarisha usawa wa kijinsia.

“Tunaamini, hili linapaswa kuwekwa wazi katika mipango ya serikali, bajeti na ufuatiliaji, kwani kilichotarajiwa kuonekana ni utatuzi wa suala hilo kwa kupewa uzito katika bajeti na sio kuonekana likiwa limechomekewa.” anasema.

Anasema kuwekeza katika sekta ya maji kutapunguza tofauti za kijinsia ambapo kila mmoja atashirikia sawa katika shuguli za kimaendeleo na kiuchumi.