Home Latest News Uhamiaji haramu na uhamaji haramu ni hatari

Uhamiaji haramu na uhamaji haramu ni hatari

1666
0
SHARE
Wahamiaji haramu wakiwa chini ya ulinzi

KATIKA siku za karibuni tumekuwa tukihabarishwa kuhusu matukio ya ujambazi na hata kuoneshwa katika mitandao ya kijamii picha za watu wanaodaiwa kwamba ni wezi wakiwa wamevishwa matairi tayari kwa ajili ya kuchomwa moto. Ni ukatili wa kutisha na ambao hautakiwi kufumbiwa macho.

Upo ushahidi kwamba si wote wanaokamatwa na kudaiwa kwamba ni wahalifu. Na hilo ndilo linalofanya umuhimu wa sheria kuachiwa kuchukua mkondo wake kuwa mkubwa zaidi. Tunaweza kuwa tunawachoma moto watu ambao hawastahili kuadhibiwa kwa sababu hawajatenda makosa. Ili tuweze kujua kuwa kosa limetendeka zipo mahakama na ni lazima tukubali kuziachia mahakama zetu zifanye kazi.

Lakini ili kesi ziweze kufika mahakamani ni lazima kuwa na mfumo mzuri wa usimamiaji wa utekelezaji wa sheria. Mfumo ambao utatuwezesha kuwa na mazingira mazuri na kuwa na jamii ambayo inafuata sheria.

Swali la msingi ni kwamba hivi inakuwaje watu ambao tunaishi nao wanafikia mahali tunawavisha matairi na kuwachoma moto hadi wanapoteza maisha na tunaliona hilo kama ni jambo la kawaida kiasi cha kusambaza kwenye mitandao ya jamii?

Ili kuwa na uhakika wa usalama wa watu na mali zao ni lazima watu watambuane. Ni vyema kila raia akajulikana na kutambulika kama sheria inavyotaka. Ili kutambulika huko kusiache hata chembe ya wasiwasi ni vyema mfumo wa kutambuana ambao uliwahi kutumika hapa nchini ukarejeshwa tena kwa kuboreshwa kisheria kama si kikatiba.

Hivi majuzi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alinukuliwa akisema kwamba kutafanyika uhakiki wa watu wanaoishi kwenye jiji, nyumba kwa nyumba. Baada ya tamko hilo ambalo limeacha kujadiliwa sana baada ya kutolewa ufafanuzi, kumekuwapo na tafsiri nyingi na moja ya hizo tafsiri ni kwamba sasa uhuru wa raia unaingiliwa.

Ni vyema kuangalia suala la usalama wa raia na mali zao kwa namna ambayo itasaidia kuondoa hii hatari ya watu wasiokuwa na hatia kuchomwa moto kwa sababu ya kujikuta wapo mahali ambako si sahihi kwa muda ambao si sahihi pia. Hatari hii ni kubwa na inaweza kumkuta yeyote yule. Hakuna anayeweza kusema kwamba hatokutana na balaa hilo hata kama si la kuchomwa moto bali na kubambikwa yowe la mwizi bila kujua ulikuwa unaiba nini.

Moja ya mambo ambayo ni muhimu kuyaangalia ni idadi ya wageni ambao wameingia nchini kwa njia zisizokuwa halali. Hivi sasa mitaa yetu imejaa wageni kibao kutoka nchi za mbali na jirani. Suala la uhamiaji wa holela si habari tena. Mitaa ya Kinondoni, Mwananyama, Sinza na hata Chalinze na Kibaha imejazana watu ambao bila ya kuingiza hisia zozote zile za kzenofobia ni kutoka nje ya Tanzania. Lakini suala la msingi ni kwamba kuna tatizo gani?

Utandawazi maana yake si kuachia mipaka yetu kuwa wazi kiasi kwamba hatujui nani ni nani. Tumeamua kuukumbatia utandawazi kwa namna ambayo inatugharimu maisha ya watu wetu na mali zao. Nitangulie tu kuweka angalizo kwamba simaanishi kwamba matatizo yetu ya usalama wa raia na mali zao ni kutokana na wahamiaji haramu tu. Hapana hata kidogo. Kuna matatizo ambayo wanaoyaleta ni watu wa ndani na hilo haliwezi kuachiwa tu kuonekana kama ni kawaida.

Mbali na hilo la uhamiaji haramu kuna suala la kuishi holela. Hiyo inamaanisha kwamba kumekuwapo pia uhamiaji holela wa raia wa Tanzania kutoka mahali pamoja kwenda kwingine bila ya utaratibu wowote ule. Hivi sasa mtu anaweza kuamka asubuhi akaenda katika shughuli zake akiwa mkazi wa Kinondoni na kesho akaamka ni mkazi wa Mbagala. Hiyo ina maana ameamua kuhama usiku na hakuna wa kumuuliza chochote.

Kwa hiyo kuna uhamiaji haramu unaofanywa na raia wa nje na pia kuna uhamaji haramu ambao unafanywa na raia wa Tanzania. Hakuna utaratibu wowote ule unaotambulika kisheria wa kuhakikisha kwamba mtu anatambulika makazi yake na kuyahama anaweza tu kufanya kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Hilo ni muhimu hata kiuchumi kwa sababu unapokuwa na raia ambao wanaweza kuhama watakavyo na bila ya utaratibu wowote basi hata vyombo vya fedha kama benki vinalazimika kuongeza riba kwa sababu ya hatari iliyopo katika biashara hiyo ya wateja kutokomea kwa kuhama bila kutoa taarifa.

Kama uhamiaji haramu unasababisha upotevu wa ajira kwa watu wetu, unaingiza tabia na desturi ambazo nyingine si za kuvutia lakini hakuna mfumo wa kuyadhibiti, unajenga mazingira kwa ajili ya kuingizwa kwa itikadi ambazo hatuzihitaji na zinapotapakaa tunakuwa hatuna namna ya kupambana nazo nao uhamaji haramu unatugharimu sana kiusalama na kiuchumi. Haishangazi kuona watu wanaotaka kupatiwa mikopo wanalazimika kuwa katika makundi kama ya kondoo ili wachungane. Huo ni ushahidi kwamba mtu mmoja mmoja haaminiki na moja ya sababu ni kutokana na wasiwasi wa makazi yanayohama bila kuwa na utaratibu maalum wa kisheria.

Hapa ndipo umuhimu wa kuwapo kwa sheria ya makazi kwa watu wa ndani unapokuwa muhimu sana. Hili suala la kuwa na sheria inayotambua uwepo wa mjumbe wa nyumba 10 linazungumzwa tu lakini halijafanyiwa kazi kikamilifu. Hili linatugharimu sana. Ni kwa nini Waziri wa TAMISEMI asilichukulie hili kwa uzito unaostahili na kuhakikisha kwamba sheria ya serikali za mitaa inafanyiwa marekebisho ili kuingiza nafasi ya mjumbe wa nyumba 10 ambayo ndiye atakuwa kiungo wa kweli kati ya wananchi na serikali?

Mjumbe wa Nyumba 10 ambaye nilipendekeza wakati wa mchakato wa katiba mpya na bado nitaendelea kupendekeza na kusimamia pendekezo langu ni mtu muhimu sana na ambaye anapopatiwa madaraka yanayostahili ama kisheria au kikatiba kama sheria mama atasaidia kuhakikisha kwamba taifa hili linasimama katika miguu yake na si rahisi kutetereka.

Katika mfumo wa serikali wa utawala wa chama kimoja cha siasa yapo baadhi ya mambo ambayo hayawekwi kisheria kwani uamuzi wa chama huwa tayari ni sheria. Maelekezo ya chama zama zile za chama kimoja yalikuwa yanatosha kuwa sheria na hilo ndilo lililokuwapo kwa nafasi ya mjumbe wa nyumba kumi. Mjumbe wa nyumba kumi alikuwa  ni mwenyekiti wa shina la chama. Shina la chama lilikuwa na kiongozi wake ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa shina. Ni huyo mwenyekiti wa shina ndiye aliyekuwa na kofia nyingine ya serikali ya ujumbe wa nyumba kumi. Huyu alikuwa ndiye kiongozi mkuu wa chama na serikali katika nyumba kumi ikimaanisha kwamba hizo nyumba kumi zilikuwa ni moja kwa moja chini yake.

Unapokuwa na kiongozi wa ngazi ya chini ambaye anao uhusiano wa kijamii na kisheria na anaowaongoza ni rahisi kuhakikisha kwamba kila mtu anayekuwa ndani ya eneo anajulikana na anawajibika kwa jamii ipasaavyo.

Mjumbe wa Nyumba 10 anakuwa ndiye mtu wa kwanza anayewajua watu wanaoishi ndani ya nchi hivyo haiyumkiniki kuwapo mtu katika eneo ambaye hajulikani ni wa mjumbe yupi.

Mjumbe wa Nyumba 10 ni nguzo na daraja la kuunganisha serikali ya mtaa na wananchi moja kwa moja na kwa mantiki hiyo basi ni kiunganishi cha uhakika cha wananchi na serikali yao katika ngazi zote hadi kwa Rais wa Jamhuri.

Katika mazingira hayo basi ni vigumu kuwa na wahalifu kwani kila raia atakuwa anakuwa na mjumbe wake wa nyumba kumi anayemjua vizuri. Akishukiwa mtu kwamba ni mhalifu kitakachofanyika ni kumtaka amtaje mjumbe wake na katika mazingira ya sasa ikibidi awe na simu ya mjumbe na hiyo itarahisisha mawasiliano na pengine kuokoa maisha ya mtu.

Tunasubiri nini kurejesha mfumo wa utawala wa Nyumba 10 kisheria kama njia iliyothibitika ya kupambana na uhalifu na kurejesha nchi katika mstari ulionyooka?

Hivi tujiulize kama Mjumbe wa Nyumba 10 angelikuwapo kisheria inawezekanaje katika nyumba zake kumi kukawepo kwa nyumba za kuuza unga, nyumba za ukahaba au nyumba za watu wanaofanya shughuli ambazo hazijulikani? Tusidanganyane hata kidogo kuhusu suala la ulinzi na usalama na kamwe tusijaribu kutafuta njia ya mkato.

Ni wazi basi kwa yote niliyoyaeleza hapo juu kwamba jibu la usalama wetu kama raia pamoja na mali zetu lipo mikononi mwetu. Tufike mahali basi walau itungwe sheria au yafanyike mabadiliko ya sheria ili kuhakikisha kwamba mjumbe wa nyumba kumi anarejeshewa hadhi yake kisheria. Ili awe ndiye nguzo na daraja kuu kati ya raia na serikali ya mtaa na bila shaka kwa uatartibu huo huo hadi huko juu kabisa. Ninaamini kwamba hatujapoteza kabisa urazini kiasi cha kukataa jambo ambalo lipo wazi kabisa kama hili la kutokuwa na udhibiti wa maisha yetu kwa kukataa kudhibitiwa. Kudhibitiwa ni muhimu kwa binadamu ye yote yule na kwa mantiki hiyo basi ni lazima na muhimu sana kuwarudisha wajumbe wa nyumba kumi watusaidie kuirejesha jamii kwenye mfumo unaoeleweka.