Home Makala UHURU, DEMOKRASIA NI MISINGI YA MAENDELEO YA KIUCHUMI

UHURU, DEMOKRASIA NI MISINGI YA MAENDELEO YA KIUCHUMI

6426
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA


“UTAFUTENI kwanza Uhuru wa kisiasa na mengine yote mtazidishiwa.” Haya ni maneno ya mwasisi wa harakati za mwanzo za uhuru barani Afrika, Rais wa Kwanza wa Ghana, Dk. Kwame Nkrumah, alipokuwa akiziasa nchi zilizokuwa chini ya ukoloni mkongwe miaka ya 1960. Kwa Nkrumah, “uhuru” ulikuwa  ufunguo wa yote – demokrasia na maendeleo ya kiuchumi.

Katika kipindi cha zaidi ya nusu karne ya uhuru wake, Afrika imeshuhudia mifumo ya kisiasa ikiamka na kuanguka; uchumi kudorora kiasi kwamba Afrika sasa ni masikini kuliko ilivyokuwa kabla ya uhuru.

Afrika inapoteza haraka utamaduni wake bila kujitambua, huku nchi za Magharibi zikielekeza mizinga yake kwa mbali kutoa pigo la mwisho kwa uhuru wa bendera uliopatikana na kuzirejesha kwenye ukoloni awamu ya pili.

Ugomvi na kuhasimiana kwa kambi mbili za enzi za vita baridi kufuatia Vita Kuu ya Pili ya Dunia, kati ya nchi za kibepari wa Magharibi na nchi za kisoshalisti za Mashariki kutaka kuzivuta nchi changa upande wake. Ugomvi huo ulitoweka baada ya anguko la Urusi kiuchumi na kijeshi, lakini umeibuka tena baada ya China kuibuka kwa nguvu na kuchukua nafasi ya Urusi.

Kinachotafutwa katika kinyang’anyiro cha rasilimali na uwekezaji usiojali  maslahi ya nchi changa, ni kukidhi ule usemi kwamba “Magharibi, au Mashariki inapopiga chafya, Afrika hupata mafua”. Ndivyo ilivyokuwa enzi za utawala wa Kisultani Zanzibar wakati wa biashara ya utumwa kwamba: “Zanzibar inapopiga chafya Bara hupata mafua.”

Yote haya yanatokea wakati nchi huru za Kiafrika zikijinasibu kama nchi huru kwa kupeperusha bendera kama mataifa yenye nembo ya taifa; wimbo wa taifa na viti katika Umoja wa Mataifa.

Lakini Afrika ni masikini na inaendelea kufukarika kuliko mwanzo, kinyume na utabiri wa Nkrumah.  Nini kimekwenda kombo? Kwa nini tuko juu juu tu kwa kufuatilia matatizo ya Ulaya kuliko tunavyosikiliza kilio cha watu wetu? Kwa nini tunapata mafua wanapopiga chafya Ulaya hadi tuagize dawa kutoka kwao wakati sisi ni watu huru?

Kwa mfano: Wanapopigana wao kwa wao huko Ulaya, au Mashariki ya Kati, Wafrika huwa kizabizabina kwa kuandamana kulaani mapigano yasiyowahusu, wala kuzielewa sababu za mapigano hayo. Lakini wanapopigana Wakongo kwa Wakongo, Warundi kwa Warundi, Wanyarwanda kwa Wanyarwanda; au inapotokea nchi ya Kiafrika kuvamiwa na taifa la nje, hatuandamani. Je, tumekuwa bendera kufuata upepo? Hakika sisi, kama andikavyo Franz Fanon, ni “Viumbe wa dunia waliolaaniwa.”

Tatizo kwa Afrika huru ni watawala. Tawala legelege zisizo na visheni wala mapenzi kwa Afrika.  Taarifa ya Benki ya Dunia (1979) ya Afrika chini ya sahara, “From Crisis to Sustainable Growth”, inauelezea mgogoro wa kiutawala na watawala barani Afrika kama ifuatavyo:- “Uwajibikaji mdogo, viongozi wamejali maslahi yao bila hofu ya kuulizwa; siasa imebinafsishwa na kuwa ya kivikundi vya vyama na vitabaka; uhuru wa habari umedhibitiwa na asasi za kiraia zimetiwa kibano au kupigwa marufuku. Serikali zinaendeshwa kiujanjaujanja; utawala wa Sheria na mfumo wa Mahakama umevurugwa katika nchi nyingi.”

Demokrasi imebinafsishwa na inatafsiriwa kumaanisha jinsi watawala wanavyopenda ieleweke.  Kwa hiyo, uhuru na demokrasi vimegeuzwa kichwa cha mwendawazimu kwa kila mtu kujifunzia kunyoa ndani ya jamii iliyojifunga.

Jamii hii inajiendesha kighafighafi nyuma ya migongo ya wananchi na kwa ngazi mbali mbali, kitaasisi na kiitikadi ambapo mambo ya kiumma huendeshwa kwa siri na uficho kwa kuwachukulia wananchi kama watazamaji tu na wapika majungu badala ya kuwaona kama washiriki na watoa hoja.

Uhuru na haki ya kujieleza umebanwa, vyombo vya habari vimedhibitiwa; uhuru wa mawazo unachukuliwa kama uchochezi, wakati haki ya kujua mambo imetoweka. Uwazi, ambao ni mmoja ya misingi mikuu ya jamii ya kidemokrasia, umeathirika na kuzaa utamacduni wa kisiasa wa uhasama na kutovumiliana. Matokeo ni kuyoyoma kwa umoja wa kitaifa ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi.

Afrika imezaa sampuli ya viongozi madikteta—Bokassa, Mobutu, Nguema, Museveni, Kagame na wengine ambao wanaona utawala ni haki yao ya kuzaliwa.

Demokrasiani neno la Kiyunani linamanisha “mamlaka” mikononi mwa watu”.  Waasisi wa taifa la Amerika, waliipanua tafsiri hiyo kuwa “Serikali ya watu kwa ajili ya watu, inayoongozwa na watu wenyewe”.

Kwa kifupi, demokrasia ni serikali kwa njia ya majadiliano na maridhiano, kati ya watu walio sawa – kwa njia ya uhuru, kwa kusema ukweli bila woga wala upendeleo na kwa uwazi.

Demokrasia ya kweli ya uwakilishi haina maana ya chama au vyama vingi vya siasa.  Unaweza kuwa na demokrasia ya kweli ndani ya chama kimoja imara pengine kuliko demokrasia ya vyama vingi, mradi tu chama hicho kiwe chama cha watu; na katiba ya nchi, sheria, mfumo wa utawala na utendaji usiwe unaobana uhuru wa watu.

Uwakilishi pia hauna maana ya kupitia vyama vya siasa pekee, bali ni uwakilishi wa mtu katika kuwasemea waliompa ridhaa hii.  Kwa hiyo, mgombea binafsi na kwa mtu kushiriki katika masuala yanayomhusu au kumgusa ni haki ya msingi ya kuzaliwa ya binadamu, ambayo ilikuwapo kabla ya katiba ya nchi na vyama vya siasa.

Ndiyo maana, Katiba yetu ya 1977, tangu mwanzo inatambua kwamba, haki ya mtu ya kushiriki katika uongozi haipotei kwa sababu tu ya mtu huyo kutojiunga, au kujiunga na chama cha siasa. Ibara ya 20 (4) inasema:

“Itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kulazimishwa kujiunga na Chama chochote au Shirika lolote….”.

Watawala wanaweza kuruhusu vyama vingine kufanya kazi kwa masharti yaliyowekwa na wao; lakini hiyo pekee haitoshi kuwakilisha matakwa ya wananchi wote au kurekebisha “maovu”, udhaifu na dosari za walio madarakani. Pamoja na kwamba tuna bahati yakuwa na amani na utulivu nchini, lakini hatujafanya vizuri katika eneo la demokrasia ya uwakilishi.  Hatari iliyopo mbele ni kwa siasa kubinafsishwa kwa watu au vikundi vya wenye fedha na kujengeka demokrasia ya kitabaka.

Katiba inapaswa kuzingatia matakwa ya muda mrefu ya watu na taifa, badala ya matakwa ya muda mfupi ambayo mara nyingi hukidhi haja za watu binafsi na za vikundi.  Marekebisho ya mara kwa mara kwa Katiba yetu ni ishara ya kwamba Katiba inaudhaifu, haiwezi kukidhi matakwa ya vikundi, badala ya matakwa ya watu na taifa.

Kama Katiba ya Marekani imefanyiwa marekebisho si zaidi ya mara matano tu tangu 1776 wakati wa utawala wa Rais wa kwanza, Jenerali George Washington, hadi rekebisho la mwisho mwaka 2001 wakati wa utawala wa George Walker Bush, iweje Katiba ya Tanzania ya 1977 [achilia mbali Katiba tatu za kwanza zilizoitangulia], isheheni viraka zaidi ya 20 katika kipindi cha miaka 15 kufikia mwaka 1992?

Katiba yetu haikidhi matakwa ya muda mrefu ya watu wake na taifa.  Inatakiwa Katiba ya kudumu, yenye visheni na madhubuti. Inakubalika miongoni mwa wanasheria wa mambo ya Katiba kwamba, namna pekee ya kulinda na kuendeleza matakwa ya wananchi, na ya kudhibiti udhaifu na matumizi mabaya ya madaraka kwa watawala, ni kulifanya Bunge [kama mwakilishi wa watu], kuwa na ukuu juu ya watawala [Parliamentary Supremacy/Sovereignty].

Sisi hatujafanikiwa kwa hilo kwa sababu Rais ni sehemu ya Bunge [Katiba – Ibara 63 (i)], na anashiriki pia katika kutunga Sheria za nchi, kwa maana kwamba, Muswada wa Sheria hauwezi kuwa Sheria hadi umetiwa sahihi na yeye [Ibara 91 (i)].  Na kama Rais ataukataa muswada huo, na Bunge likaamua kutokubaliana naye, inabidi alivunje Bunge lililowekwa na wananchi [Ibara 91 (4)].

Hapo je, ni nani mkuu, kati ya Rais na wananchi kupitia wawakilishi wao?  Yako wapi mamlaka ya watu chini ya demokrasia tunayoendesha licha ya kuahidiwa chini ya ibara ya 8 (1) (a) ya Katiba, kwamba “Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi?”

Angalia katika kujadili miswada bungeni: Mbunge mmoja atasimama kupinga kwa uchungu mkubwa, Muswada fulani usiowakilisha maslahi ya wananchi na maslahi ya Taifa kwa ujumla akisema: “…. Serikali lazima iweke mbele maslahi ya wananchi, Taifa, demokrasia na utawala wa Sheria kwa kuzingatia Katiba yetu. Muswada huu Mheshimiwa Spika, mimi naona unapingana na vyote hivi …., unakiuka haki za binadamu katika nchi yetu. Pamoja na hayo, Mheshimiwa Spika, naunga mkono muswada huu asilimia kwa mia” [Makofi kutoka kwa Wabunge wenzake!].

Mbunge wa aina hiyo yuko bungeni kuwakilisha maslahi ya waliomchagua kwa uhuru au yuko kutetea maslahi yake kwa njia ya nidhamu ya woga na kuangamiza demokrasia? Kama hivyo ndivyo, basi Bunge limekuwa taasisi ya kitabaka lenye kuwakilisha maslahi ya kisiasa.

Ili Bunge liweze kutekeleza jukumu lake la Kikatiba la kutunga Sheria, kwa nini Muswada wa Sheria uwe Sheria baada ya kutiwa sahihi na Spika wa Bunge? Hii itakuwa ni kutekeleza pia dhana ya “mgawanyo wa madaraka” na demokrasia kwa vitendo, na kwa kila mhimili kusimamia mambo yake.

Kwamba baadhi ya Viongozi hawawajibiki, na kuwa wanajali maslahi yao binafsi bila hofu ya kuhojiwa, ni hoja inayokaribiana na uweli. Tumeona jinsi Viongozi wasivyosituka wanapokabiliwa na kashfa za Kiuongozi.  Hali hii inasababishwa na mfumo dhaifu wa kushughulikia kashfa za Viongozi wasiozingatia maadili ya Taifa na ya uongozi. Sababu moja ni kuwa Bunge limeng’olewa meno, haliogopwi wala kuheshimiwa na “Viongozi” ambao wanaonekana kujiona wanawajibika zaidi kwa waliowateua na chama kinachowaingiza madarakani.

Pengine dawa pekee ya tatizo hili ni kwa uteuzi wa viongozi na watendaji wakuu wa umma, wakiwamo mawaziri, kuridhiwa na Bunge. Miiko na Maadili ya Viongozi yafafanuliwe vyema na kuingizwa katika Katiba ya nchi ili kulipa suala la uongozi umuhimu na nguvu linayostahili. Bunge liachwe kuwa chombo huru kinachojitegemea na kusimama kwa miguu yake, kwa sababu shughuli za Bunge ni za Kikatiba zaidi kuliko kisiasa; na Katiba ya nchi ipo kwa wote, wanachama wa vyama vya siasa na wasio na vyama.

Jazba za kisiasa na zile zinazotetea maslahi binafsi na ya vikundi, hazina nafasi katika enzi hizi za utawala wa Sheria. Watu watapenda kuoanisha matendo au matukio na Sheria zinazoruhusu matendo au matukio hayo, kuona kama yanashabihiana na madhumuni ya Muungano, demokrasia na haki za binadamu.

Tusiugeuze Muungano kuwa kichwa cha mwendawazimu au uwanja wa kujifunzia kupiga shabaha kwa wanasiasa wabovu, wenye kujitafutia umaarufu kwa njia ya ushabiki, kwa kuzua dhoruba na kujifanya mafundi wa kuzima dhoruba hizo.

Miaka 50 ya Muungano tungekuwa tunazungumzia nchi moja yenye Rais mmoja, Serikali moja, Waziri Mkuu mmoja, Bunge moja, badala ya Serikali mbili zisizokidhi azma na maana ya neno “muungano”.  Kwa nini?  Kwa sababu ya watu kuhodhi tafsiri ya “Muungano” na kujitafutia umaarufu.

Tumesema kuna hatari kwa demokrasia kutekwa nyara na wenye fedha kupitia vyama vya siasa [udikteta wa vyama], na kupitia chaguzi zilizodhibitiwa na kuongozwa [guideded elections]. Hii inaashiria vyama sasa kuwepo kwa ajili ya chaguzi tu; baada ya hapo vinakwenda likizo hadi uchaguzi unaofuata, kwa mbwembwe, nguvu na jeuri ya fedha.  Huo si uongozi, bali ni umamluki; tumefanywa kuchagua watu wasiofaa; tunachagua wafadhili badala ya wawakilishi kwa tamaa ya fedha.

La mwisho ni hili la uhuru na demokrasia ya kiuchumi, ambalo si tatizo kwa Tanzania pekee, bali ni kwa Afrika nzima na dunia ya tatu kwa ujumla.

Kama ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika, matatizo ya kiuchumi yanatokana na viongozi kutaka kuziendeleza nchi zao kwa misingi ya historia ya Ulaya na Amerika, na kwa manufaa ya mataifa hayo mawili bila kuelewa athari zake.  Hii imesababisha utegemezi mkubwa wa misaada kutoka nje, misaada yenye masharti yanayofanya tuuze uhuru wetu wa kujiamlia mambo yetu.

Udhaifu huu wa viongozi umewafanya wafadhili na mashirika ya kimataifa yawe na sauti na kauli turufu katika nyanja na sera za uchumi, siasa na jamii, kuliko wakati wowote wa uhuru wetu. Utawala bora tunaopigania katika ujenzi wa demokrasia, wenyewe pekee hautoshi katikati ya mzigo wa madeni kwa nchi [tegemezi], kushuka kwa bei ya mazao, uporaji wa rasilimali za taifa unaofanywa na wageni, ufukara usiotoa mazingira ya kukua kwa uhuru wa kujieleza, kutetea haki wala demokrasia, utawala wa Sheria na utawala bora. Ni utamaduni huu wa utegemezi unaojenga ufukura, kama tulivyosema, kwamba siasa na demokrasia sasa imekamatwa na wenye mitaji.

Katika mazingira kama haya, uchumi na maendeleo ya nchi hayawezi kumea na kukua kwa kukosa rutuba. Lakini Watanzania tunapaswa kujilaumu. Tumeiua wenyewe misingi ya Azimio la Arusha kwa Azimio la Zanzibar [1992], tukakosa dira, visheni na uwajibikaji.  Ni uzushi kudai kwamba Watanzania hatukuwa na uwezo wa kutunga sera sahihi, kama inavyodaiwa na mawakala wa ukoloni mamboleo, wa ndani na wa nje ya nchi.

Azimio la Arusha lilibeba sera shirikishi zilizoipa jamii nzima uwezo wa kujiamlia mambo yake yenyewe.  Leo, itawezekanaje taifa kuwa na demokrasia ya kweli wakati wafadhili na Mashirika ya fedha ya kimataifa yamepewa kiti cha mbele katika nyanja zote za maisha, na watu wetu hawaruhusiwi kujiamlia mambo yao?. Kama alivyosema Profesa Issa Shivji mahali fulani, “[uchumi na] maendeleo hayapimwi kwa kuwa na magari mengi na majengo makubwa, au kupatikana kwa bidhaa mbali mbali; bali uwezo wa kuzinunua”.

Kama kuna somo tunalopaswa kujifunza katika miaka 57 ya uhuru wetu, ni lile kwamba udemokrasishaji wa taasisi zote za kijamii ni muhimu ili kuepuka kudumaa au kuporomoka kwa uchumi. Hili linawezekana kwa wananchi kushirikishwa katika mchakato mzima wa kuleta demokrasia na maendeleo yao ya kiuchumi.

Mabadiliko yanayotakiwa katika mchakato huu si kwa njia ya kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa pekee, au ridhaa itolewayo na Serikali kwa jina la “demokrasia”; bali ni muhimu pia kuimarisha vyama vya kiraia katika ngazi zote za jamii, wakiwamo wakulima, wafanyakazi na Vyama vya Wanafunzi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali [NGOs], Vyama vya wanataaluma na vikundi vya wasomi. Lengo la kufanya hivyo ni kuamsha nguvu ya umma uweze kushiriki katika mchakato mzima wa demokrasia na maendeleo kwa wote; na katika kulinda na kuimarisha uhuru wetu.