Home Makala Ujamaa falsafa isiyofutika katika mioyo ya Watanzania

Ujamaa falsafa isiyofutika katika mioyo ya Watanzania

947
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU

Falsafa ni jaribio la kuelewa na kueleza kwa kutumia akili inayofuata njia ya mantiki, Falsafa ni mantiki inayoelezea hatua zake ikiwa tayari kuchungulia upya kila hatua iliyochukua, hivyo falsafa ni njia ya uibuaji wa maswali.

Kwa hiyo, falsafa za ujamaa hapa Tanzania punde tu baada ya kupata uhuru mwaka 1961, zililenga kutumia akili na mifumo bayana ya kuunganisha jamii moja kuelekea nyingine ili ziweze kuishi kwa pamoja kizalendo, kifikra na kuzalisha uchumi imara kwa ustawi wa taifa letu.

Sera imara za ujamaa zilizalisha tabaka la waungwana wenye uzalendo wa taifa lao, ni nyakati za ujamaa upendo, kuaminiana na matendo ya amani yalishika hatamu na kuiletea heshima Tanzania.

Aidha tunaendelea kuwaona baadhi ya viongozi waliopita kwenye mkondo wa ujamaa wanavyohubiri itikadi za ujamaa na kujaribu kuwafanya watanzania wayaishi matendo ya kijamaa kwa maslahi ya taifa lao.

Ni wazi kuwa Watanzania na Wafrika kwa ujumla wamewahi kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa historia ya dunia katika falsafa za ujamaa ingawa mchango wao hautajwi sana katika ulimwengu wa sasa uliotekwa na ubepari mambo leo.

Mawazo ya ujamaa kama itikadi na dira ya maendeleo ni mchango mkubwa uliowahi kutolewa na Watanzania katika ulimwengu wa siasa za kifikra na zenye kunuia kuleta maendeleo ya pamoja yasiyokuwa na ubaguzi ndani yake chini ya kiongozi wao shupavu na imara, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Ikumbukwe kuwa mataifa mengi ulimwenguni, yaliichukulia kwa umuhimu wa pekee nadharia ya uchumi na siasa iliyoasisiwa na magwiji wa ushoshalisti Karl Marx na Frederick Engles kwa kuunda sera mbadala dhidi ya uchumi wa kibepari.

Mfumo wa ubepari ulioanzia ulaya Magharibi na kusambaa dunia nzima ulikuza hali ya maendeleo yasiyokuwa na ulinganifu, Nchi changa zilizoletewa mfumo wa ubepari nazo ziliingizwa katika hali ya kuwa tofauti kimajaliwa.

Kutokana na tofauti hizo za matakwa ya kusambazwa matunda ya uhuru viongozi mbali mbali wa Kiafrika ikiwemo Tanzania, walitunga itikadi na sera mbadala za kulikomboa taifa kiuchumi.

Mwalimu Nyerere kwa mfano, aliasisi Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa lengo la kujenga taifa lenye watu wanaopata mahitaji yao muhimu kwa usawa na haki ili kujenga taifa la kijamaa.

Mathalani, Ujamaa ulitafsiriwa katika lugha nyingi duniani, kutokana na umuhimu wake, kwa lengo la kuiwezesha jumuia ya kimataifa kuufahamu umuhimu wa Ujamaa ambao una misingi imara katika maendeleo ya jamii yoyote.

Hapa Tanzania, Ujamaa ulifafanuliwa zaidi katika Azimio la Arusha la mwaka 1967, ambapo mambo makuu manne ya msingi yalitajwa, (a) Hakuna unyonyaji, (b) Njia kuu za uchumi ni chini ya wakulima na wafanyakazi, (c) Kuna demokrasia, (d) Ujamaa ni imani.

Misingi hii minne ilijenga taifa lenye kuishi kwa mshikamano, haki na usawa bila kujali matabaka yaliyokuwepo wakati huo ni nyakati ambazo Tanzania ilisonga mbele kwa kasi kimaendeleo na uchumi imara ulishika hatamu na kuzalisha viwanda na ajira kwa watanzania.

Bahati mbaya badaye mwaka 1992, Azimio la Arusha liliporwa kifikra na kimantiki, na badala yake likaletwa Azimio la Zanzibar ambalo kiafya halikuwa na tija kama maudhui ya Azimio la Arusha yalivyokuwa hapo awali.

Inawezekana kabisa waliopitisha Azimio la Zanzibar na kuua Azimio la Arusha, hawakufahamu fika chachu na malengo ya Mwalimu Nyerere kuanzisha Azimio hilo la Arusha, kwa mantiki hiyo, ni vema tukajikumbusha kwa ufupi sababu hizo.

Sababu za uanzishwaji wa azimio hilo zilikuwa ni pamoja na; (i) Sera ya uhuru wa maendeleo kwa wananchi, (ii) Muungano wa Tanzania na Zanzibar mwaka 1964, (iii) Mgogoro wa kidiplomasia baina ya Ujerumani Magharibi na Mashariki na (iv) Tukio la jeshi la King’s African Rifles (KAR), tulilolirithi kutoka kwa mkoloni. Hizi ni miongoni mwa sababu zilizochangia kuwepo kwa Azimio la Arusha.

Pia ifahamike kuwa Ujamaa una asili ya mtindo wa maisha ya Kiafrika, kuanzia karne ya nyuma zaidi tangu enzi za mababu zetu ambao waliishi katika mfumo wa maisha ya jadi, kabila na koo zilizojenga moyo wa upendo na kuheshimiana katika maisha ya kila siku.

Mantiki ya Mwalimu Nyerere, kuutumia mfumo wa kijamaa ni matokeo ya mitindo na maisha ya Watanzania walioyaishi kabla ya kuingiliwa na tamaduni za kigeni, ambapo mali iliyopatikana kwa wakati huo, ilikuwa ikihesabika kama sehemu ya jamii husika.

Maisha ya kila siku ya Kitanzania yalizingatia kufanya kazi, ili kupata mahitaji muhimu kwa kila mwanajamii kwa kuzingatia upendo, kushirikiana na kugawana kila kinachopatikana kutokana na kazi ya kila mmoja.

Nyakati hizo Watanzania walikuwa na muundo wao wa kimaisha waliokuwa wakiishi kama jamii moja iliyo katika makundi, lakini waliweza kuelewana kama jamii moja iliyokuwa na umoja unaojumuisha makundi ya koo, jadi na kabila bila kubaguana, au kudai mahitaji zaidi kuliko wanajamii wengine, wala kujilimbikizia mali zaidi ya mahitaji ya lazima kwa kila kaya , koo na kabila.

Ushirikiano huo wa kuishi pamoja kwa kuheshimiana kama jamii moja, ikiongozwa na utashi wa maamuzi ya pamoja kuhusu masuala muhimu, na kuzingatia matakwa ya wanajamii wote kwa njia za kidemokrasia, ulifanya watu wote wawe na moyo wa upendo na kuwa kama jamii moja.

Ujamaa ulifanikisha kwa kiasi kikubwa, kujenga utu na uzalendo wa kisiasa wa kutokuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali, wanajamii walijijengea roho ya kijamaa pasipo kutanguliza maslahi binafsi kama ilivyo nyakati za sasa.

Zama hizi za ubepari, mambo ni tofauti kabisa—mali ni kwa lengo la kuwatawala na kuwanyonya wanyonge, wasaliti hutumiwa na mabepari kufarakanisha amani ya utaifa na uzalendo uliopo.

Mtajiwamabepariniuchonganishi na fitina, na kufarakanisha jamii moja kwenda nyingine—kwa mantiki hiyo, matokeo yake huzalisha chuki, ugonvi na machafuko, ambavyo huweza kuhatarisha amani ya nchi na kupoteza uhai wa watu wasiokuwa na hatia.

Haja ya Ujamaa ilikuwa ni haki na usawa. Ujamaa umepoteza ladha nyakati hizi. Tabaka la wanyonyaji na walafi, limeongezeka sana, dira ya sasa ni tofauti na enzi za Mwalimu Nyerere. Mfumo upi unaofuatwa hivi leo? Haueleweki kabisa kama ni Ujamaa au ubepari.

Kwa mantiki hiyo, ni vema watawala wakarejea falsafa , sera na itikadi mbadala ambazo Mwalimu Nyerere aliziishi na kuzipigania bila kuchoka, Japo rais wa sasa, John Pombe Magufuli, anaonekana kufuata nyayo zake, ni vema Serikali na taasisi zake, zikalifanyia kazi jambo hili, ili kufanikisha Ujamaa wa kisasa kushika hatamu.