Home Makala UJENZI WA RELI YA TAZARA NA HISTORIA YAKE

UJENZI WA RELI YA TAZARA NA HISTORIA YAKE

2432
0
SHARE

NA HILAL K SUED

WAKATI Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli, ikiwa mbioni kufanikisha mradi kabambe wa kujenga reli mpya ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) kati ya Dar es Salaam kwenda Bara ambayo itachukua nafasi ya ile ya zamani iliyojengwa na wakoloni wa Ujerumani zaidi ya karne moja iliyopita, ni vyema tukajikumbusha reli nyingine iliyojengwa katika mradi mwingine kabambe zaidi enzi hizo, miaka 40 iliyopita.

Hii ni Reli ya Tazara inayomilikiwa kwa pamoja kati ya Tanzania na Zambia. Hivyo wakati tunaendelea na mradi huu wa sasa ni vyema ule wa zamani ukatupa somo la historia la kujifunza na hivyo kutilia maanani kwamba kujenga reli na kuiendesha ni masuala mawili yaliyo tofauti kabisa.

Kwani hakuna aliyewaza kwamba Tazara, inayomilikiwa kwa pamoja baina ya Tanzania na Zambia baadaye ingejikuta katika hali ya kupumulia mashine na kuendesha shughuli zake kutokana na misaada ya kifedha na kiufundi kutoka China, nchi iliyoijenga reli hiyo katika miaka ya 70.

Na kuhusu Reli ya Kati, kuna wanaohoji iwapo tulishindwa kuiendesha reli hiyo ambayo tulikabidhiwa na wakoloni kwenye sahani ya fedha, tungepata wapi utaalamu wa kuendesha reli nyingine mpya? Na tayari tuna somo la kujifunza hapa kuhusu ule ukodishaji wa TRC kwa RITES.

RITES walishindwa kuliendesha shirika letu la reli na waliondoka baada ya kutia hasara kubwa kwa wananchi. Na iwapo habari kamili ya yaliyojiri katika mkataba baina ya TRC na RITES utaanikwa hadharani, zitazishinda kashfa zote zilizowahi kutokea na kuiathiri nchi hii masikini kiuchumi katika miaka ya karibuni.

Reli ya Tazara, ambayo pia huitwa Reli ya Uhuru (Uhuru Railway), ilijengwa kati ya 1970 na 1975 kwa lengo la kuipa nchi ya Zambia iliyokuwa haina pwani ya bahari ‘kiunganisho’ hadi Bandari ya Dar es Salaam kama njia mbadala ya kusafirisha bidhaa zake zilizokuwa zikipitia Rhodesia (sasa Zimbabwe), Afrika ya Kusini na Msumbiji.

Ikumbukwe nchi hizo tajwa zilikuwa bado chini ya utawala wa kikoloni na/au wazungu wachache huku mapambano ya kudai uhuru yakiendelea. Kwa upande wa Tanzania lengo lilikuwa ni kusukuma maendeleo katika maeneo reli hiyo imgepita.

Hivyo mradi huu tayari ulikuwa na soko kuhusu matumizi yake (turnkey project) na uliwezeshwa na kugharamiwa na fedha kutoka Jamhuri ya Watu wa China. Jumla ya gharama ilikuwa Dola za Kimarekani milioni 500 (wakati ule) na hivyo kuufanya mradi huo kuwa ni mkubwa zaidi kuliko miradi yote ya China kwa nchi za nje.

PINGAMIZI ZILIZOJITOKEZA DHIDI YA MRADI

Baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, nchi hii, wakati huo ikiitwa German East Afrika ilikabidhiwa Uingereza kuitawala chini ya udhamini wa iliyokuwa Jumuiya ya Kimataifa (League of Nations – mtangulizi wa Umoja wa Mataifa (United Nations). Tangu enzi hizo, mipango ya kujenga njia ya reli ilikuwa inafikiriwa kuunganisha Tanganyika na iliyokuwa Rhodesia ya Kaskazini (sasa Zambia).

Hata hivyo, mipango hiyo ilikaa ndani ya makabati tu kutokana na kudorora kwa hali ya uchumi duniani katika miaka ya 1930. Baada ya Vita ya Pili ya Dunia (1939-45) wazo la kutandika reli hiyo liliibuka tena. Aprili 1949, ramani iliyochapishwa katika Gazeti rasmi la Reli (Railway Gazette), ilionyesha mchoro wa njia ya reli kuanzia Dar es Salaam hadi Kapiri Mposhi, Zambia na haikuwa mbali sana na njia ambayo miaka 20 baadaye ilianza kujengwa na Wachina.

Na Ripoti ya 1952 ya Sir Alexander Gibb na wenzake ilisema kwamba, reli kati ya Rhodesia na Tanganyika isingekuwa na tija yoyote kiuchumi kutokana na kiwango kidogo cha maendeleo ya kilimo katika maeneo itakayopita na kwamba reli zilizopo kutoka Rhodesia kupitia Msumbiji na Angola zinatosha kwa ajili ya kusafirisha madini ya shaba ya Zambia kwenda nje.

Na Ripoti ya Benki Kuu ya Dunia ya 1964 nayo pia ilihitimisha kwamba reli kati ya Zambia na Tanzania haikuwa na tija kiuchumi na ikapendekeza badala yake ijengwe barabara.

Wazo la kujenga reli kati ya Zambia na Tanzania lilipata msukumo mpya mwaka mmoja baada ya uhuru wa Zambia pale, mwaka 1965 utawala wa wazungu wachache wa Rhodesia chini ya mlowezi, Ian Smith, kujitangazia uhuru kutoka Uingereza (Unilateral Declaration of Independence – UDI) na hivyo kuhatarisha njia za kibiashara za Zambia.

Ndipo Rais Julius Nyerere na mwenzake wa Zambia, Kenneth Kaunda, walianza kufuatilia njia nyinginezo kujenga reli mbadala. Nyerere baada ya kutembelea China alipewa timu ya wapimaji wa ardhi ambao Oktoba 1966 walitoa ripoti yao fupi.

KAZI MUHIMU ALIYOFANYA ABDULRAHMAN BABU

Hata hivyo, Kaunda hakuwa na imani sana kuwahusisha Wakomunisti (utawala wa China) na aliona nchi za Magharibi ndiyo zingefaa zaidi katika kazi hiyo.

Hivyo uchunguzi wa anga uliofanywa na timu iliyojumuisha Waingereza na Wacanada ilitoa ripoti nzuri Julai 1966, lakini ahadi ya fedha za kugharamia mradi kutoka nchi hizo haikutolewa.

Tangu awali kiongozi wa China, Mwenyekiti Mao Zedong, alikuwa tayari kutoa fedha, wakati ile ilikadiriwa kuwa Dola za Kimarekani bilioni moja ili kujiongezea kura dhidi ya Urusi ya Kisovieti katika Mkutano wa Wakuu wa nchi za Asia na Afrika uliokuwa unafanyika Algiers mwaka 1966.

Hivyo baada ya kutembelea China Januari 1967, Rais Kaunda alilegeza upinzani wake dhidi ya kuihusisha China katika mradi huo wa reli. Aliyekuwa waziri wa biashara na uchumi katika Serikali ya Muungano, Abdulrahman Babu, alifanya kazi kubwa katika kufanikisha upatikanaji wa fedha kutoka China kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo.

Kutokana na kumbukumbu za kuaminika, Nyerere alikuwa anataka kujenga uhusiano wa karibu kati ya Zanzibar na China kwa faida ya nchi nzima (Jamhuri ya Muungano). Hivyo Abdulrahman Babu, aliteuliwa kuwa kiongozi wa ujumbe wa kibiashara ambao ulitangulia ziara ya Nyerere kwenda China.

Matokeo ya ziara hii ni makubaliano ya kibiashara ya pauni milioni tano kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano. Fedha hizi ni mbali na zile pauni za Uingereza milioni 11 za misaada ya kawaida.

Chini ya makubaliano haya Tanzania itakuwa inanunua kutoka China chochote kile wanachohitaji, nayo China itanunua kutoka Tanzania bidhaa za thamani ya pauni milioni tano kila mwaka.

Kutokana na uzoefu wake na Wachina na imani yake ya kiitikadi katika namna ya maendeleo yao, Babu alikuwa mtu stahiki kwa kazi hiyo. Aliwaeleza Wachina ugumu uliokuwapo kwa Tanzania kupata fedha za kugharamia mradi wa reli.

CHINA YAKUBALI KUGHARAMIA UJENZI

Julai 1, 1965, Serikali ya China ilitoa ahadi madhubuti kwa Serikali za Tanzania na Zambia ya msaada wa pauni milioni 150 kugharamia reli hiyo.

Septemba 6, 1967 makubaliano yalitiwa sahihi huko Beijing baina ya mataifa matatu; China, Tanzania na Zambia. China ilijitolea yenyewe kujenga reli hiyo katika mkopo wa bila riba utakaolipwa katika kipindi cha miaka 30.

Ujenzi ulianza mwaka 1970 na usafiri wa reli hiyo ulianza baada ya miaka sita. Reli ilianzia bandari ya Dar es Salaam na kupitia ardhi ya Tanzania mwelekeo wa Kusini-Magharibi. Reli hiyo ilipita katika maeneo mengi yasiyokuwa na makazi ya watu.

Tangu reli hiyo ianze kazi kumekuwepo maendeleo ya viwanda katika maeneo ilikopitia, pamoja na mtambo wa uzalishaji umeme wa Kidatu na kiwanda cha karatasi cha Mufindi.

Reli inapishana na barabara kuu ya kwenda Zambia karibu na mji mdogo wa Makambako na inakwenda sambamba nayo hadi Mbeya na mpakani mwa Zambia na inaingia Zambia na kuunganishwa na mfumo wa reli wa Zambia pale Kapiri Mposhi.

UBUNIFU WA UHANDISI TANGU VITA YA PILI

Jumla ya urefu wake ni kilomita 1,863 (maili 1,160) na inaishia ikiwa mita 1,400 juu ya usawa wa bahari. Upande wa Tanzania urefu wa reli hiyo ni kilomita 969 na Zambia ni kilomita 894. Reli hii ilikuwa inatajwa kuwa ni ubunifu mkubwa sana wa uhandisi hapa duniani tangu Vita ya Pili ya Dunia. Ilichukua miaka mitano tu kuijenga na ilimalizika kabla ya muda uliopangwa, mwaka 1975.

Upana wa reli ni mita 1.067 (futi tatu na inchi sita) upana ambao ni sambamba na mfumo wa reli wa Zambia na nchi nyingine za Afrika ya Kusini ambayo huitwa Cape Gauge. Reli yetu ya Kati ina upana wa mita moja. Kituo cha kubadili mifumo hii miwili inayohusisha magurudumu kilijengwa Kidatu mwaka 1998.

Mbali na upana wake, reli ya Tazara ilichukua mfumo wa reli nchini China katika miaka ya 70, hasa katika viunganisho vya mabehewa (couplings), mfumo wa breki, uzito wa mizigo kwenye magurudumu (axle loading – tani 20), aina ya chuma cha reli (high manganese steel) na mataruma (sleepers).

Mataruma ni ya zege zenye nondo ndani kwa reli nzima isipokuwa kwenye madaraja na maungio ambako mbao ndiyo ilitumika.

CHANGAMOTO ZA KAZI YA UTANDIKAJI RELI

Kabla ya kuanza kujengwa wapima ardhi 12 kutoka China, walitembea kwa miguu kwa miezi tisa kati ya Dar es Salaam na Mbeya ili kubaini njia ambayo reli ingepita.

Baada ya hapo, Watanzania wapatao 50,000 na Wachina 25,000 walihusishwa katika kazi ya ujenzi wa reli hiyo ya kihistoria. Katika, jua, mvua na upepo vibarua hao waliweza kutandika reli kupitia moja ya sehemu zenye milima mingi na mabonde barani Afrika.

Kazi hiyo ilihitaji kusafirisha tani 330,000 za reli ya chuma cha pua na ujenzi wa madaraja 300, mahandaki 23 ya chini kwa chini (tunnels) vituo vya treni (stations) 147.

Nguzo za kushikilia daraja la kuvukia Mto Mpanga zina urefu wa mita 49 kutoka chini na handaki (tummel) la Irangi lilikuwa na urefu wa kilomita 1.5 chini ya mlima. Sehemu kati ya Mlimba na Makambako ndiyo ilikuwa sehemu ngumu sana kupitisha reli, kwani ilikuwa ina milima mingi na mabonde ya kina kirefu na pia kuwa katika eneo la mvua nyingi. Mifumo madhubuti ya uondoshaji wa maji ya mvua ililazimika kujengwa.

Asilimia 30 ya madaraja yote, mahandaki na mitaro ya kuondoshea maji, pamoja na upasuaji mkubwa wa majabali ulikuwa katika kipande hiki kigumu cha urefu wa kilomita 16 tu.

Kambi za ujenzi ziliwekwa kila baada ya kilomita 64 na zilikuwa zinahamishiwa mbele jinsi kazi ya utandikaji reli ulivyokuwa ukiendelea. Mipapai na migomba ilikuwa inaoteshwa kwenye kambi hizo kwa ajili ya kujipatia chakula kwa vibarua ambao baadhi yao pia walilima bustani za mboga nyakati zisizo za kazi.

MANDHARI YA MAENEO RELI INAKOPITA

Kuanzia Dar es Salaam, reli hiyo ilipitia uwanda wa pwani kabla ya kuingia Hifadhi ya Mikumi na ile kubwa ya Selous kwa upande wa Kaskazini. Wasafiri wa reli hiyo hupata nafasi ya kuangalia aina mbalimbali za wanyamapori katika Hifadhi ya Selous – kama vile twiga, tembo, pundamilia, swala na kadhalika na baada ya miaka mingi wamekuja kuzoea kuvumilia mingurumo ya treni zinapopita.

Baada ya Hifadhi ya Selous, reli inapita Bonde la Kilombero lenye rutuba nyingi kwa kilimo na inapita kwa pembeni mbuga ya Kibasira kabla ya kuingia Mlimba na hatimaye Makambako.

Baada ya kupita maeneo ya Nyanda Juu za Kusini, njia ya reli inaingia katika tambarare ya Usangu na hapa hali ya hewa ni joto kidogo.

Kabla ya kufika Makambako, Hifadhi ya Milima ya Udzungwa inapanda hadi kufikia mita 2,137 kwa upande wa Kaskazini na milima ya Kipengere upande wa Kusini.

Makambako ndiyo makutano ya reli na ile barabara kuu ya kwenda Zambia na nyingine ikielekea Njombe na Songea. Baada ya Milima ya Kipengere, milima ya Uporoto inaonekana huku Bonde la Usangu likionekana upande wa kulia.

Kutokea Chimala, reli inaambaa hadi Mbeya kwa upande wa Kusini. Kutokea Mbeya reli inaendelea Kusini-Magharibi hadi Tunduma inapovuka mpaka na kuingia Zambia.