Home Latest News UKAWA NDIO MWANZO WA KIFO CHA NCCR-MAGEUZI

UKAWA NDIO MWANZO WA KIFO CHA NCCR-MAGEUZI

1238
0
SHARE

NA ADO SHAIBU,

WASWAHILI wanasema: “Mbaazi zikikosa maua, husingizia jua”. Nimesoma nukta kwa nukta ya uchambuzi wa Ndugu Abdulrahman Lugone, ambaye amejitambulisha kuwa ni afisa wa ngazi ya juu wa Chama cha Wananchi (CUF), uchambuzi ambao ulibandikwa kwenye ukurasa wa Ndugu Julius Mtatiro, ambaye naye anajitambulisha kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF.

Awali nikiri kumfahamu Ndugu Lugone kiasi. Mara kadhaa nimehudhuria naye mafunzo ya vyama vya siasa chini ya mwamvuli wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD). Kwa siku chache nilizokaa naye, ninaweza kusema pasi shaka hata punje, kuwa yeye amejidhihirisha kuwa ni mtu muungwana anayehusudu hasa mapambano ya hoja badala ya “viroja”.

Lakini, kwenye andiko lake ambalo pamoja na mambo mengine, linajaribu kujibu hoja ya wale wanaodhani kuwa UKAWA umeiangamiza NCCR-Mageuzi, Ndugu Lugone, kwa makusudi, au kwa kutojua, ameamua kutoa habari ambazo zikiachwa kubaki kama zilivyo, zinaweza kuupotosha umma. Nami nitamjibu ndugu yangu Lugone kwa hoja bila viroja.

Kwenye andiko husika, Ndugu Lugone alikuwa akijibu hoja (nadhani ya Prof. Lipumba), kuwa kama UKAWA ulikuwa wenye manufaa kwa vyama vyote (bila kujali jitihada za miaka mingi za kuimarisha vyama husika), na kwa nini haukuwa na manufaa kwa NCCR-Mageuzi na NLD?

Waumini wa hoja hii ambayo Lugone anajaribu kuipangua, wanaamini kuwa licha ya faida za UKAWA, mzizi hasa wa matunda ambayo CUF imevuna, umetokana na jasho la Wana-CUF walilojitolea kujenga chama chao kwa miaka nenda rudi, kwenye maeneo yenye ngome za chama hicho. Hawa wanaamini kuwa UKAWA ungeikuta CUF legelege kama NLD na NCCR, basi isingeambulia kitu!

Kwenye kujibu hoja ya kufeli kwa NCCR, Ndugu Lugone amejenga hoja kuwa kudondoka kwa chama hicho kwenye majimbo yake, ati kulisababishwa hasa na ACT-Wazalendo kusimamisha wagombea kwenye majimbo hayo. Lugone anashangaa kwa nini ACT kilisimamisha wagombea kwenye majimbo ambayo yalikuwa ya vyama vingine vya upinzani?

Kwa maoni ya Ndugu Lugone, ACT, kwa kusimamisha wagombea ubunge, kilifanya kazi ya kuyumbisha ushindi wa vyama vyenzake vya upinzani. Hoja ya Lugone ina mapungufu kadhaa kama nitakavyoainisha hapa chini.

  • Mosi, ACT-Wazalendo haikuwa sehemu ya UKAWA. Kukitaka chama hiki kutosimamisha wagombea wa ubunge na udiwani ili kuwaachia wengine, ni kukitaka “kijiue kisiasa”.

ACT kilijaribu kuviandikia vyama vya UKAWA kuhusu utaratibu wa kujiunga UKAWA. Kama kingejibiwa, suala hili lingejadiliwa kwenye vikao vya chama na uamuzi wa kujiunga, ama kutojiunga ungefikiwa. UKAWA hawakujibu.

Kwa maoni ya Ndugu Lugone, licha ya kutojibiwa, bado sisi tulipaswa kuiacha fursa adhimu ya kunadi sera zetu na kutosimamisha wagombea! Sisi tuliamua kusimamisha! Mwishowe, kwa uwiano wa wabunge na madiwani, Chama chetu, wakati huo kikiwa na uhai wa mwaka mmoja tuu kimepata madiwani wengi zaidi nchi nzima kuliko NCCR Mageuzi!

  • Pili, si kweli kuwa vyama vingine vya UKAWA (ikiwemo CUF) havikusimamisha wagombea kwenye majimbo yote ya Kigoma waliyokubaliana kuachiana. Mifano ni mingi! Kwa mfano, kwenye majimbo yafuatayo ambayo walikubaliana kuachiana, vyama vya UKAWA vilikuwa na wagombea tofauti kama ifuatavyo:

Kasulu Mjini: MACHALI Moses Joseph – ACT , NSANZUGWANKO Daniel Nicodemus – CCM

CHUBWA: Mbonimpaye Optatus – CHADEMA -KASYOME Ester Obedi – CUF-FATUMA Hamisi Magulati – DP BUNYAGA Gideon Boniface – NCCR MAGEUZI.
YASSIN Kisembe Samwel – NRA Buhigwe:
GOODLUCK Alphonce Kimali – ACT
OBAMA Albert Ntabaliba – CCM
BASILIUS Ntizirusha Budida – CHADEMA
THOMAS D.C Malima – CUF
AZORY Nditije Mwomela Mteko -NCCR MAGEUZI

Buyungu: LEOPOLD Heneriko Muhagaze – ACT; Eng. CHIZA Christopher Kajoro – CCM; BILAGO Kasuku Samson – CHADEMA; MAWAZO Metusela Athanas – NCCR Mageuzi.

Hali hii ilikuwepo pia kwenye majimbo mbalimbali nchini. Kwa mfano, mkoani Mtwara, majimbo yafuatayo yalikuwa na wagombea wa vyama mbalimbali vya UKAWA; Mtwara Mjini, Masasi Mjini, Newala Mjini, Lulindi, Ndanda, Nanyumbu na Newala Vijijini. Hata hapa Dar es salaam, Vyama vya UKAWA “vilitunishiana misuli” na kusimamisha wagombea kwenye majimbo ya Segerea, Ubungo, Ukonga, Ilala, Kawe na Kigamboni. Ingekuwa vyema Ndugu Lugone avihoji Vyama washirika wa UKAWA Kwa nini vilitunishiana misuli majimboni kabla ya kunyoshea kidole ACT.

Ninaweza kuendelea na orodha ndefu ya majimbo ambayo vyama mbalimbali vya UKAWA vilikubaliana kuachiana lakini bado vilisimamisha wagombea. Ni hali ya ajabu kwelikweli kwa Wana-UKAWA kuituhumu ACT kuweka wagombea hata kwenye maeneo ambayo hata vyenyewe navyo vimesimamisha wagombea na kushindana!

  • Tatu, Mifano ya Ndugu Lugone juu ya jinsi kura za vyama vya wapinzani kwenye baadhi ya majimbo zilivyowanyima ushindi wapinzani wenzao ni ya kibaguzi. Kwa makusudi, Lugone ameamua kufumbia macho mifano ya majimbo ambayo UKAWA vilinyimana ushindi kama vile Segerea na Newala Mjini kama ifuatavyo:

Segerea: BONNAH Moses Kaluwa CCM (94,640), MTATIRO Julius CUF (75,744),
ANATROPIA Lwehikila Theonest CHADEMA (48,623). Kura za Mtatiro na Anatropia zingetosha kumpa Mtatiro ushindi!

Newala Mjini: MKUCHIKA George Huruma – CCM (18,817), NAKALE Ambrose Nkwabi – CHADEMA (1,602),
MANGUYA Juma Sadick – CUF (18,261).
Kura za CUF na CHADEMA zingeweza kuifanya CUF kuibuka kidedea!
Nne, Ndugu Lugone hasemi ukweli Kuwa Vyama vya CUF na CHADEMA vilisimamisha wagombea kwenye majimbo yote ya Masasi, Lulindi na Ndanda ambayo kwenye makubaliano ya UKAWA yalikuwa Chini ya NLD. Wagombea hawa walisimamishwa hata kabla Mzee Emmanuel Makaidi hajafa.

Kilichoimaliza NCCR

Ukweli ni kwamba mbali na vyama mbalimbali kunufaika na UKAWA, NCCR-Mageuzi hakikuvuna kitu cha maana. Binafsi nimewahi kukaa na kuzungumza na viongozi kadhaa wandamizi wa NCCR. Wala hawafichi hisia zao juu ya jinsi UKAWA ulivyopigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la chama chao! Maneno haya yalianza kusemwa tangu wakati wa uchaguzi.

Kwa mfano, katika kampeni, takribani viongozi wote wa juu wa NCCR (Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu na wajumbe kadhaa wa Halmashauri Kuu yake, waliutangazia umma kuwa UKAWA umekiathiri chama chao na kutoa hoja zifuatazo:

  • Kwamba licha ya makubaliano ya UKAWA kuwapa NCCR majimbo 12, vyama vingine vya UKAWA vilisimamisha wagombea kwenye majimbo 6.
  • Kwamba hata kwenye majimbo 6 yaliyosalia, vyama vya UKAWA havikuwaunga mkono na walipingwa waziwazi majukwaani
  • Kwamba Mwenyekiti James Mbatia, aliwatelekeza wagombea wake wa ubunge na badala ya kuwa na mikakati ya ushindi kwenye majimbo ya NCCR, aligeuka kuwa Msemaji wa CHADEMA. Kupuuzwa kwa hoja hizo ndiko kulikoifikisha NCCR hapa ilipo.

Nasaha zangu kwa Lugone (Licha ya ukinda wangu kiumri), ni kuwa haihitaji kuokoteza takwimu ili kuishambulia ACT-Wazalendo. Kama hasa anataka kusisitiza umoja wa vyama, avue viatu vyake vya CUF, na afanye uchambuzi usio na upande.

Akifanya uchambuzi wa namna hiyo, atagundua kuwa Kasulu Mjini, ACT hakikuathiri UKAWA, bali UKAWA ulikiathiri ACT.

Mwisho niseme kuwa umoja wa kweli baina ya vyama vya upinzani ni jambo jema, na utaweza kupatikana iwapo vyama vitajifunza kuheshimiana.