Home kitaifa Ukawa tumieni Dar es Salaam kuelekea 2020

Ukawa tumieni Dar es Salaam kuelekea 2020

3177
0
SHARE

katuni rai matutuKAMA kuna jambo ambalo linatakiwa kushukuliwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKawa) ni hatua ya kufanikiwa kutwaa jiji la Dar es salaam.

Zipo sababu nyingi za kushukuru kwanza jiji hili ndilo ambalo ni uso wa nchi kwa kuwa ndilo kitovu cha biashara na kivitendo ndiyo mji mkuu wa nchi ukiondoa Dodoma ambayo ipo kinadharia.

Hivyo basi kama kuna ushindi ambao ninauchukulia kuwa mkubwa kwa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu uliopita ni hatua ya muungano huo kufanikiwa kutwaa jiji hili ambalo limekuwa likitawaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Ingawa kumekuwa na maneno ya kupotosha kutoka kwa baadhi ya watu, wapo ambao wamekuwa wakipotosha kwa makusudi wakijifanya kwamba hawatambui Rais wa jiji ni Meya wa jiji ambaye kwa sasa ni Isaya Mwita anayetokea Ukawa.

Wanaopotosha wanajifanya kusahau kwamba Rais wa Mkoa ni Mkuu wa Mkoa na badala yake wanavuka mipaka na kumkabidhi jiji, hii inasikitisha na kushangaza hasa kwa watu wanaojua na kufikiri sawasawa.

Wale wanaopotosha kwa makusudi wamekuwa wakitaka kuonyesha kwamba Meya si lolote katika jiji kwa sababu ametoka Ukawa ila wakati alipokuwa akitokea kwenye CCM walimuona kuwa muhimu na alitambuliwa kwa wadhifa wake stahili wa kiitifaki kwamba ndiye mwenye jiji.

Ili kuwafahamisha kwamba mwenye jiji ni Meya wakati alipokuwa amefika Rais barrack Obama nchini na wageni wengine wanapoingia kwa ugeni wa jiji kiongozi anayekuwa mbele katika mapokezi huwa Meya ambaye kiitifaki ndiye mwenye mji wake.

Wanapotosha wakati wanajua fika kwamba baada ya mfumo wa vyama vingi pamoja na mpango wa maboresho katika halmashauri za wilaya imefanya Wakuu wa mikoa na Wilaya kukosa kazi maalumu ya kufanya zaidi ya kuzunguka na kutoa ahadi zisizotekelezeka na kuingilia majukumu ya watu wengine.

Hufanya kazi nyingi zisizo rasmi za kukisaidia chama tawala kwa kuweka mikakati ya ushindi katika chaguzi mbalimbali ikiwemo mikakati ya ushindi wa kweli au wakati mwingine ya hila.

Kwa nini nasema wanaingilia majukumu ya wengine kwa kukosa kazi ya kufanya kiutendaji ni kwamba majukumu katika ngazi ya wilaya au Mkoa yana watendaji wake kwa mfano, shughuli zote za maendeleo zinasimamiwa na mkurugenzi na jopo la wataalam wake.

Wakati mkurugenzi na watu wake wanafanya shughuli hizi kwa utaalam, upande wa siasa wa kazi zao unafanywa chini ya mameya na madiwani wake hivyo kuwafanya kukosa kazi.

Pamoja na kuwa Mwenyekiti wa ulinzi na usalama lakini majukumu yake kivitendo husimamiwa vema na Ofisa usalama wa taifa katika wilaya (DSO) na kamanda wa polisi wa wilaya (OCD) wakati kwa Mkoa anayefanyia kazi ni Kamanda wa polisi wa Mkoa (RPC) kwani hawa wana utaalamu na maelekezo yaliyoandikwa kuhusu kazi hiyo.

Maelezo yangu ya juu nilitaka kuweka sawa kuhusu Rais wa kweli wa jiji ni nani kiutendaji na naamini nitakuwa nimeeleweka vema.

Kazi inayobaki kwa rais wa Dar es salaam ambaye ni Meya wa jiji kuhakikisha anafichua na kufanyia kazi tuhuma za ufisadi zilizofanywa na viongozi wa Jiji waliopita kwa kupora Mali za Jiji kama vile Shirika la usafirishaji Dar es Salaam (UDA), Mali za soko la Kariakoo, Viwanja na majengo ya Jiji.

Mstahiki meya Isaya unatakiwa kutambua kuwa wananchi wa dar es salaam wanatarajia kusikia ukifuatilia usitishwaji wa mkataba batili na maamuzi haramu yaliyofanyika ya kukabidhi hisa asilimia 76, mali na uendeshaji wa kampuni ya UDA kwa Kampuni ya Simon Group Limited.

Mstahiki meya Isaya wana- Dar es Salaam wanatamani kuona ukiwafichua na kuchukuliwa hatua kwa wale wote walioshiriki kuzuia serikali iwe kwa makusudi au kwa bahati mbaya kupata kodi stahili wakati wakiwa katika madaraka.

Wananchi wanaamini utafanikisha kutimia kwa ndoto alizokuwa nazo aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa, waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, za kufanya mabadiliko katika miji mbalimbali tofauti na ilivyokuwa kwa watendaji wa CCM.

Mstahiki Meya Isaya anatakiwa kufahamu kuwa utendaji wake ndio unaweza kuwapa matumaini wananchi ya kuchagua au kuikataa Ukawa katika uchaguzi ujao Mkuu ujao na nyingine ndogondogo.

Meya Isaya unatakiwa kutambua kuwa Dar es Salaam ndiyo imekuwa kioo cha Ukawa kujinadi katika chaguzi mbalimbali kwa kuthibitisha ilichokuwa ikikizungumza kwenye kampeni za uchaguzi uliopita.

Meya Isaya kumbuka kwamba umeingia kwenye uongozi ambao watu wa CCM hawakupenda Ukawa mkamate nafasi hiyo hivyo unatakiwa kuwa makini na ushike maneno yako kwa vitendo kuwa utaongoza kwa uwazi na wala hutampendelea mtu.

Jambo hilo lionekane kwa wananchi na watawala wa CCM ili Dar es Salaam iweze kuendelea kuwa ngome ya Ukawa ambayo itasaidia kupatikana kwa majiji na manispaa nyiongine nyingi na kaa ukijua kwamba wewe ni miongoni mwa matumaini machache ya umoja huu.