Home Makala Kimataifa Ukiiba China utatangazwa nchi nzima

Ukiiba China utatangazwa nchi nzima

1857
0
SHARE

NA MUSA MAKONGORO, Shandong, China

MOJAWAPO  kati ya mambo ambayo wananchi wa taifa la China wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kabisa ni nidhamu ya Kazi na nidhamu ya muda. Kwenye matumizi ya muda tumezidiwa kwa kiasi kikubwa sana, jambo ambalo sisi watanzania hatuna katika jamii zetu. Haya ndiyo mambo hatuyaoni Afrika.

China wanaheshimu muda hakika sijawahi kuona wanadamu wana aina hii. Chukulia mfano suala la kula rshwa adhabu yake ni kifo, ikithibitika hivyo Mahakamani au kuhukumiwa kifungo cha maisha. 

Ifahamike, kabla ya rais wa sasa wa China, Xi Jinping kuisuka upya China, kulikuwa na kiwango cha kutupwa na wizi ulioshindikana. 

Tangu kuingia madarakani rais Xi Jinping, amedhibiti rushwa kwa kiasi kikubwa, hali ambayo imesababisha wawekezaji wengi kukimbilia bara letu la Afrika na wengi wanaokimbilia huko kwetu inaelezwa kwamba walikuwa wapigaji kutoka huku.

Kimsingi ni kwamba suala la rushwa bado ni tatizo kubwa hata Marekani. Takwimu zinaonesha hata China inashika nafasi ya 87 duniani katika kiwango cha mapambano dhidi ya rushwa. Hivyo vita bado inaendelea, kwahiyo hatuwezi kusema rushwa imetokomezwa moja kwa moaja lakini wamethubutu kupambana.

Rais Xi Jinping alipoingia mwaka 2013 Wachina zaidi ya milioni 1.3 wamekamatwa na kuchukuliwa hatua ikiwemo kunyongwa na vifungo vya maisha. Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama zaidi ya hamsini, akiwemo bilionea, Zhou Yongkong, wengine ni wakuu wawili wa Kijeshi wa ngazi za juu wamefungwa maisha baada ya kuthibitika na Rushwa.

Kwa China, wenyeji wananiambia ili uwe kiongozi lazima uthibitishwe pasi na shaka kwamba huna doa lolote kuanzia ngazi ya familia hasa katika masuala ya uongozi.

Kwa China suala la rushwa wanailiita ‘mizimu michafu na yenye mabalaa’, wafanyakazi wa umma wanaiogopa Rushwa kama kifo. Wachina wanafanya kazi kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa tano na dakika 45 asubuhi. 

Kisha wanakwenda kupata chakula cha mchana hadi saa nane kamili mchana. Halafu wanarudi kazini kuanzia saa nane kamili mchana hadi saa 11 kamili jioni. Katika muda huu hakuna ofisi yoyote ya umma inakuwa wazi labda kwa zile za kazi maalumu tu na Hospitali.

Wachina wengi muda wa kulala ni saa 4 usiku, wakichelewa sana ni saa tano. Lakini wakiwa ofisini wanafanya kazi kama nyuki na wana kasi ya ajabu. Simu haziruhusiwi wala kupiga gumzo wakati kazi.

Benki nyingi hakuna foleni ya kuchukua dakika 40. kila kitu kiko katika utaratibu na hata kufungua akaunti China ni kama dakika 15 unaondoka. Na wanatumia Automatic Banking System zinazofanya kazi saa 24 (kutoa na kuweka fedha) bure kabisa. Kama unatumia benki moja, yaani mfano kama unaangalia salio ni bure, kutuma na kutoa fedha benki hiyo hiyo ni bure na haraka. 

Katika maeneo ninayoishi ya mji wa Jiuqihe, katika jimbo la Shandong hapa China, kwa mwaka mmoja sasa sijawahi kuona umeme umekatika au kukosekana huduma ya Intaneti. Nimesahau kabisa mambo haya ambayo nilikuwa ninayashuhudia nyumbani Tanzania.

Katika mifumo ya kufanya kazi kwa watumishi wa umma hapa China na viongozi wa chama tawala cha China, CCP (Chinese Communist Party). China ina mifumo yake ya kijamii ya kudhibiti rushwa, moja ya mfumo huo, ni pamoja na kwamba kama mzazi wako amewahi kuiibia serikali na ikathibitika hivyo, basi familia nzima au ukoo wake haitakuja kupata chochote ndani ya China na mzazi huyo anafungwa maisha au kupewa adhabu ya kifo.

Mathalani kizazi chake hakitapewa mkopo benki, hawatanunua nyumba ndani ya China au gari au kiwanja au kuruhusiwa kufanya biashara yoyote au kupata Scholarship au huduma yoyote kama kumiliki kadi za bima, yaani jina lako linakuwa ‘Blocked’ kwenye mifumo yote na unatangazwa nchi nzima wewe ni mwizi.

Mfumo upo kuanzia ngazi za juu za uongozi kuanzia Rais mpaka wafagiaji wa chini kabisa katika ofisi za utumishi wa umma. Leo niishie hapa, kukusimulia ya ugenini nawe ukatafakari na kujifunza. Wakati mwingine ntajitahidi kueleza mfumo wa kuwapata viongozi nchini China unaoitwa ”Select and Appoint”.