Home KIMATAIFA Ukimwi bado tishio, fedha zaidi zahitajika

Ukimwi bado tishio, fedha zaidi zahitajika

354
0
SHARE

NA LEONARD MANG’OHA NA MITANDAO

RIPOTI ya Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi vimepungua kwa asilimia 33 tangu mwaka 2010 lakini fedha zaidi zinahitajika ili kuzuia kuenea kwa maradhi hayo.

Katika ripoti ya kila mwaka ya UN iliyozinduliwa hivi karibuni imeeleza kuwa vifo vinavyosababishwa na Ukimwi vilipungua kwa takriban vifo 770,000 sawa na asilimia 33 ya vifo vilivyotokea mnamo mwaka 2010 ambapo watu milioni 1.2 walifariki dunia

Miongoni mwa maeneo ambayo ripoti hiyo imeonesha kupungua kwa vifo vinavyosababishwa na Ukimwi kwa kiasi kikubwa ni pamoja na nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika, ingawa visa vya maambukizi bado ni vingi.

Katika nchi za Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini na Ulaya Mashariki vifo hivyo vinadaiwa kuongezeka kwa asilimia tano.

Licha ya ripoti hiyo kuonesha kupungua kwa vifo hivyo maambukizi mapya yameongezeka hasa Mashariki ya Kati na Ulaya Mashariki.

Kutokana na hali hiyo Umoja wa Mataifa umeitaka jumuiya ya kimataifa kuweka mkazo katika juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo hatari. Ripoti hiyo inaonesha kuwa kiashi cha watu milioni 37.9 wanaishi na virusi vya Ukimwi  kote duniani huku watu milioni 23.3 wenye virusi hivyo wanatumia dawa za kufumbaza virusi hivyo.

Umoja wa Mataifa umesema licha ya hatua hiyo ya mafanikio iliyopigwa, juhudi za kuutokomeza ugonjwa huo zimelegalega kutokana na ufadhili wa fedha wa kiwango cha chini na pia kutokana na watu walio katika baadhi ya maeneo kutopata huduma muhimu za afya.

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na Ukimwi, Gunilla Carlsson, anahimiza kuwapo dhamira ya kisiasa katika juhudi za kupambana na ugonjwa huo na kwamba dhamira hiyo ni muhimu katika juhudi za kuwasaidia watu walio katika maeneo yaliyoachwa nyuma.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo maambukizi yameongezeka miongoni mwa watu wasiopata huduma za kuepusha maambukizi na kuonesha kuwa fedha zaidi zinazohitajika  ili kutoa huduma za kupambana na Ukimwi.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa ifikapo mwakani zaidi ya Dola za Marekani bilioni 26.2 zitahitajika katika juhudi za kupambana na ugonjwa huo kutoka Dola bilioni 19 zilizotolewa mwaka jana.

Mwaka jana ripoti ya umoja huo ilionesha kuongezeka kwa idadi ya watu wenye virusi vya ukimwi wanaopatiwa dawa ambapo watu milioni 21.7 wanaogua maradhi hayo duniani kote wanaliripotiwa kutumia dawa hizo.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watu walioathirika na virusi vya ukimwi, (UNAIDS)  lilibainisha kuwa katika kila watu watano wenye virusi hivyo, watatu wanatumia dawa hizo duniani kote.

Kiasi cha watu milioni 36.9 walikuwa na virusi vya Ukimwi hadi mwaka 2017 kote duniani, kati ya hao milioni 15.2 hawakuwa wanapata dawa walizohitaji.

Hadi sasa kiasi cha watu milioni 80 wameambukizwa virusi vya Ukimwi na milioni 35.4 wamefariki dunia tangu visa vya kwanza vya ugonjwa huo viliporipotiwa katika miaka ya 1980.

Katika ripoti yake ya mwaka jana shirika hilo Shirika hilo lilitoa tahadhrisha juu ya hatari ya kukwama au kurudi nyuma kwa juhudi za kupambana na ugonjwa huo ikiwa fedha zaidi hazitapatikana sambamba na kupuuzwa kwa juhudi hizo.

Mkurugenzi wa UNAIDS wakati huo, Michel Sidibe, shirika hilo lilipungukiwa kiasi cha Dola bilioni saba zilizohitajika katika kuendeleza mafanikio yaliyopatikana na kufikia malengo ya  shirika ifikapo mwaka 2020.

Alibainisha kuwa endapo fedha hizo hazitapatikana kutakuwa na uwezekano mkubwa wa kurudi kuongezeka kwa idadi kubwa ya maambukizi.

Lengo la shirika hilo hadi kufikia mwaka 2020 ni kuwawezesha asilimia 90 ya watu wenye virusi vya ukimwi kutambua hali zao, asilimia 90 miongoni mwao kupatiwa dawa za kufubaza  makali ya virusi vya hivyo na asilimia 90 kati yao kuwa wamefubaza virusi hivyo.