Home Habari ‘UKIMWI bado tishio kwa vijana’

‘UKIMWI bado tishio kwa vijana’

290
0
SHARE

MWANDISHI WETU

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), limewatahadhirisha vijana kuachana na ngoni zembe kwani ugonjwa wa Ukimwi bado ni tishio kwao.

Tahadhari hiyo imetolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa wadau wanaotekeleza afua za wasichana balehe na wanawake vijana Tanzania.

Akimwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Maimuna Tarishi kwenye mkutano huo uliofanyika mwanzoni mwa wiki hii  jijini Dar es salaam, Beng’i aliwataka vijana kuwa wabunifu pamoja na kutumia teknolojia katika shughuli zao wanazotekeleza katika kujipatia kipato ili kuendana na mazingira ya sasa.

Being alisema Ukimwi  umeendelea kuwa tishio la uchumi na maendeleo ya nchi na madhara yake yanaendelea kuwa changamoto katika kufikia malengo ya mpango wa MKUKUTA.

Ameongeza kuwa Maambukizi ya VVU ni matokeo ya mchanganyiko wa sababu nyingi za kibaolojia,masuala ya kijamii, kimila na kiuchumi.

“UKIMWI unaathiri mtu binafsi, familia, jamii na nchi kwa ujumla, kwahiyo uthibiti wake unahitaji nguvu za pamoja zoezi la kuumaliza  ugonjwa huu lipo mikononi mwetu sote”. alisisitiza Beng’i.

Aidha kulingana na utafiti wa viashiria vya UKIMWI kwa mwaka 2016/17, Tanzania ina jumla ya vijana milioni 12 wa umri wa miaka 10 hadi 19 ikiwa ni asilimia 24 na milioni tano wa umri wa miaka 20 ikiwa ni asilimia 31 ya idadi ya Watanzania wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 44.

Beng’i aliweka wazi kuwa utafiti umeonesha kuwa maambukizi mapya yameongezeka kwa kiwango kikubwa kwenye kundi la vijana wenye umri wa miaka10 hadi 24 ambapo ni sawa na asilimia 40 na kati ya hiyo asilimia 80 yako kwa wasichana wa umri wa miaka 15-19.

Miradi ya majaribio inayolenga wasichana balehe na wanawake vijana imekuwa ikitekelezwa katika mikoa tisa ya Shinyanga, Dar es Salaam, Kagera, Dodoma, Morogoro, Singida, Mbeya, Iringa na Halmashauri 24 nchini, kwa ufadhili wa Serikali ya watu wa marekani kupitia PEPFAR, UNICEF na Mfuko wa Dunia wa UKIMWI, Kifua kikuu na Malaria(GFATM)

Mkutano huo ni wa kwanza kufanyika nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla chini ya uratibu wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania Bara (TACAIDS) ambapo wadau mbalimbali kutoka Serikalini, Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo ikiwa ni pamoja na Asasi za Kiraia wanaotekeleza afua mbalimbali za kusaidia Wasichana Balehe na Wanawake Vijana wamekutana na kujadili namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakumba vijana hao.

 Pamoja na kuendelea kuboresha Uratibu wa Sekta mbalimbali ili ziendelee kusimamia utekelezaji mipango yao ya afua zinazohusiana na Wasichana/vijana balehe na vijana kama zilizoainishwa katika Mkakati wa Nne wa Kudhibiti UKIMWI Tanzania.

Maeneo mengine waliyoyaangalia ni pamoja na kuangalia tathimini ya matokeo yaliyopatikana na wadau wanaotekeleza afua kwa ajili ya wasichana balehe na wanawake iijana katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2018. kutambua maeneo ambayo hayajafikia makundi mbalimbali katika kutekeleza afua za kupambana na athari za UKIMWI ikiwa ni pamoja na wasichana balehe na wanawake vijana na wenzi wao.

Aidha wasichana balehe na Wwnawake vijana wamekuwa  wahanga wakubwa wa athari zinazotokana na mdororo wa kijamii na kiuchumi ambazo husababisha  kujiingiza katika vitendo vinavyo weza kuhatarisha afya na maendeleo yao kutokana na mazingira duni yasiyowawezesha kukabiliana na changamoto zinazowazunguka kama vile ukosefu wa Sera mahususi  kwa ajili ya kuwawezesha, changamoto za mila na desturi, usawa wa kijinsia, athari zinazotokana na maumbile yao, changamoto za kimfumo zinazowakwamisha kufikia malengo yao kwa namna moja au nyingine.

JENISTA  MHAGAMA AZINDUA TAARIFA

Wakati huo huo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amezindua taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya UKIMWI wa mwaka 2016 – 2017 (Tanzania HIV Impact Survey).

Taarifa hiyo imezinduliwa Jijini Dodoma wiki iliyopita, ambapo alieleza kuwa utafiti huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali imeendelea kupambana na ugonjwa wa UKIMWI kwa kuonesha juhudi za kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya na kupungua kwa vifo vinavyotokana na UKIMWI nchini.

“Tafiti zinaonesha maambukizi mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 80,000 mwaka 2012 hadi kufikia watu 72,000 kwa mwaka 2017, vilevile takimu zinaonesha kupungua kwa vifo vinavyotokana na UKIMWI kutoka watu elfu 70 kwa mwaka kwa mwaka kufikia mwaka 2010 hadi kufikia vifo elfu 32 kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2017,” alieleza Mhagama

Alisema kuwa katika kuthibitisha hilo, kiwango cha maambukizi ya UKIMWI nchinikinazidi kupungua ambapo mwaka 2012 matokeo ya utafiti kama huo yalionesha kuwa kiwango cha maambukizi kilikuwa ni asilimia 5.1 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 na matokeo ya mwaka 2016 – 2017 kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7. Waziri Mhagama alieleza kuwa matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa watu waliopima afya zao kwa hiari wanaongezeka kutoka tafiti moja hadi nyingine, kati ya watu hao wanawake waliopima ni wengi kuliko wanaume