Home Habari Ukimya wa Ruto unakishindo Kenya

Ukimya wa Ruto unakishindo Kenya

614
0
SHARE
William Ruto

NA ISIJI DOMINIC

KWENYE siasa kuna msemo maarufu usemao ‘hakuna rafiki au adui wa kudumu’ na hili hudhihirika zaidi nchini Kenya pindi inapokaribia uchaguzi mkuu. 

Katiba ya Kenya inaruhusu vyama vya siasa kuunda miungano ndiyo kwa maana haishangazi tangu chama kongwe cha Kanu kushindwa katika uchaguzi mkuu, serikali ambazo zimeingia madarakani zote zinatokana na muungano wa vyama vya siasa. 

Uchaguzi Mkuu nchini Kenya umepangwa kufanyika mwaka 2022 na japo muda bado ni mrefu, wanasiasa wameshaanza kujipanga. Hali si shwari ndani ya chama tawala cha Jubilee na sasa ni dhahiri Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto hawapo tena karibu kama ilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017. 

Washirika wa Ruto wanadai Uhuru amemsaliti mtu aliyemfanyia kampeni na hana dalili ya kutekeleza makubaliano waliyoafikiana wakati wanaunganisha vyama vyao kuelekea uchaguzi mkuu wa 2013. 

Nao washirika wa Uhuru wanadai Ruto amejitenga kumsaidia Rais kutimiza majukumu yake kwa manufaa ya taifa na badala yake amekuwa akizunguka nchi nzima akifanya kampeni. Kitendo hicho ndicho kinadaiwa kuwa chanzo cha Uhuru kuanza kushirikiana na viongozi wa vyama vya upinzani akiona ni bora apate upinzani kutoka ndani ya chama chake kuliko wapinzani wa chama chake kuungana na wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Katika kuhakikisha anadhihirisha yeye ndiye kiongozi wa chama cha Jubilee na miswada ya Serikali isipate upinzani bungeni, Rais Uhuru alifanya mabadiliko ya viongozi wakuu ndani ya Bunge la Seneti huku mabadiliko zaidi yakisubiriwa kwenye Bunge la Taifa na hata baraza la mawaziri.

Waliyoguswa kwenye mabadiliko katika uongozi kwenye Bunge la Seneti, ni wanasiasa wanaomuunga mkono Naibu Rais Ruto. Aliyekuwa Kiongozi wa Waliowengi na Seneta wa Elgeyo Marakwet, Kipchumba Murkomen, aliondolewa kwenye nafasi hiyo ambayo sasa inashikiliwa na Seneta wa Pokot Magharibi, Samuel Poghisio huku Seneta wa Nakuru, Susan Kihika akiondolewa nafasi ya Kiranja wa Waliowengi ambayo sasa ipo chini ya Seneta wa Murang’a, Irungu Kangata. Kama hiyo haitoshi, Naibu Spika wa Bunge la Seneti, Kithure Kindiki, alipigiwa kura ya kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

Ruto ambaye anafahamika kuweka wazi hisia zake kama alivyofanya kujitenga na maamuzi ya chama aliyodai kufanywa na Mwenyekiti Nelson Dzuya, Makamu Mwenyekiti David Murathe na Katibu Mkuu Raphael Tuju kwa kisingizio cha kupata baraka kutoka kwa Rais Uhuru, hajatamka neno lolote tangu washirika wake kuondolewa kwenye nafasi hizo nyeti ndani ya Bunge la Seneti.

Sio kawaida lakini Naibu Rais ameamua kukaa pembeni na kutokujihusisha na kile kinachoendelea lakini Murkomen katika moja ya mahojiano na chombo cha habari nchini Kenya, alisema Ruto alimwambia abaki imara licha ya kuondolewa kwenye nafasi yake nyeti bungeni. 

Mbunge huyo wa Elgeyo Marakwet alibainisha kuwa wakati anauelezea Naibu Rais yale yaliyojiri, Ruto alimshauri kuwa ‘kila mtu aliye imara lazima apitie changamoto’. 

“Alinipa mfano wa kile alichokipitia akiwa na Rais. Alisema matatizo yangu ukilinganisha na ICC (Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai), ugaidi, maandamano ya upinzani aliyoyapitia ni mambo madogo,” alisema Murkomen.

Bado linabaki kitendawili kuhusu lini Naibu Rais atakapoibuka na kutoa tamko mabadiliko yaliyofanyika Bunge la Seneti na ‘sekeseke’ wanaopitia wanasiasa wanaomuunga. Je, tamko atakalolitoa litatikisa na kuzidi kupandisha joto la siasa nchini Kenya? 

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Jeremiah Kirui, alisema utaratibu aliyoamua Ruto kuutumia itawaacha maadui wake wakishangaa. 

“Ukimya ni aina ya mawasiliano ambayo ni madhubuti. Hakuna anayejua nini mtu anachokipanga, hatua atakayoichukua na watu gani anaoongea nao kabla ya kuibuka,” alinukuliwa Kirui. 

“Wakati unapokuwa kimya ilhali muda wote umekuwa ukionekana, watu wataanza kufikiria mipango yako. Kwa hali ya kawaida, mashabiki wako watakupambania, wale ambao si mashabiki wako watakuona huna hatia na utapata huruma yao.” 

Naye mchambuzi mwingine wa siasa, Profesa Makau Mutua, aliandika kwa mtandao wake wa kijamii kuwa Ruto ataibuka na atatikisa akisisitiza ni muda ndiyo kila kitu kwenye matukio kama haya yanayomkabili. 

“Naibu Rais ataitikisa siasa za Kenya katika staili ambayo haijawahi kutokea na atajibu mapigo pasipo uoga,”aliandika Makau ambaye kitaaluma yeye ni Profesa anayefundisha sheria Marekani. 

Tangu kuripotiwa kisa cha kwanza mgonjwa wa virusi vya Corona nchini Kenya Machi 13 mwaka huu, Ruto hajajitokeza katika shughuli za Serikali akiwa pamoja na viongozi wengine wa Serikali, ishara ya kwamba yupo pekee yake hususan alipotoa hotuba ya njia za kujikinga na Covid-19 Aprili 9 mwaka huu. 

Wachambuzi wengi wamekuwa wakitoa maoni yao wakisema Ruto ni mtu ambaye kwa sasa hatakiwi serikalini na hivyo angejiuzulu kabla ya kulazimishwa kujiuzulu. 

Mfano, Profesa Herman Manyora alisema Rais Uhuru ataendelea kuwanyoosha washirika wa Naibu Rais na kuwavua madaraka kadri anavyoendelea kubaki madarakani. Alimshauri Ruto kupunguza kasi yake kisiasa na kutekeleza majukumu machache anayoshikilia kama Naibu Rais ikiwemo pia kuweka wazi kuwa hatagombea 2022. 

“Kama hatajiuzulu, Uhuru ataendelea kuwanyoosha washirika wake. Anahatarisha kuwapoteza washirika wake kwa sababu wataanza kuamini Naibu Rais hana msaada na kile anachoweza kufanya ni kuwaona wakishughulikiwa,” alisema Manyora na kuongeza kwamba kilichowatokea Murkomen na Susan ni mwanzo tu. 

Rais Uhuru ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Jubilee sasa ameamua kuwa mkali hususan akiwa amebakisha takribani miaka miwili na nusu ya utawala wake na akiwa na lengo la kuacha kumbukumbu nzuri pindi atakapokabidhi madaraka kwa Rais wa awamu ya tano. 

Haishangazi kuona baadhi ya wachambuzi wakimshauri Ruto kusalimu amri kwa sasa ukizingatia aliandika kwenye mtandao wake wa kijamii maandiko yaliyoashiria kupingana na bosi wake kwa kutaka kujua hoja ya kujihusisha na shughuli za siasa wakati nchi inakabiliwa na madhara ya Covid-19 na mafuriko yaliyoua na kuwafanya Wakenya wengi kukosa makazi maeneo mbalimbali nchini. 

Kwa sasa Ruto ameamua kutulia na inasemekana yupo kwenye makazi yake akipata muda mzuri na familia yake. 

“Hii Serikali ni ya Uhuru, anafanya lile analotaka, alete yule anayemtaka na amfute kazi wale ambao hawahitaji. Ruto kimamlaka ni msaidizi wake na kwa wakati huu yupo na familia yake,”alinukuliwa moja wa mtu wake wa karibu. 

Wakati huu Ruto ameamua kuangalia mambo yanavyoenda akiwa pembeni, washirika wake wameapa kuendeleza mapambano. 

Mfano, Mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa, mtu wa karibu na Naibu Rais, alisema Ruto ameagiza timu ndogo ambayo inakutana na viongozi Wakenya mbalimbali japo kinachojadiliwa hakijawekwa wazi. 

“Mlango wake wa siasa bado unabaki wazi kwa viongozi wote ambao wako tayari kuungana naye kwa nia njema ya nchi na bila shaka malengo yake ya 2022,”alinukuliwa Barasa na moja ya chombo cha habari nchini Kenya.