Home Makala UKUAJI WA TEKNOLOJIA UMERAHISHA MENGI

UKUAJI WA TEKNOLOJIA UMERAHISHA MENGI

746
0
SHARE

NA FARAJA MASINDE


KUKUA kwa teknolojia kunaendelea kuwa na matokeo mbalimbali ambayo yapo yanayojenga kwa maana ya kuwagusa watumiaji moja kwa moja kupitia kuinua uchumi wao huku kukiwa pia na matokeo hasi ambayo haya yanatokana na kundi dogo la watu ambalo limekuwa halioni mantiki ya kutumia mitandao hii kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla achilia mbali kupashana habari.

Hata hivyo, licha ya kuwapo kwa changamoto hizo bado kuna watu wachache ambao wameamua kufikiria zaidi na kugeuza uwepo wa mitandao hii ya kijamii kuwa fursa ya kuboresha yale wanayoyafanya katika kukuza vipato vyao.

Eneo la kilimo ni miongoni mwa sekta ambazo zimeweza kunufaika maradufu kupitia mitandao hii ya kijamii ambapo makundi mbalimbali yameanzishwa lengo likiwa ni katika kuwaweka wakulima wa Tanzania kwenye eneo moja.

Ni kupitia mitandao hii ya kijamii ndipo tunashuhudia tovuti na makundi mbalimbali yanayojihusisha na kilimo yakianzishwa ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ni chachu ya mafanikio kwa wakulima wengi kwa sasa.

Abdul Mkono, ambaye ni Bwana shamba na Mkurugenzi wa Kampuni ya uzalishaji matunda na mboga mboga ya Makaru Agro Ltd na mmoja wa waasisi wa kundi la mtandao wa kijamii kupitia Whatsap, linalojulikana kama kilimo cha kisasa, anasema kuwa kupitia mitandao hiyo ni wazi kuwa limekuwa ni jukwaa ambalo limesaidia wakulima wengi kuweza kujielekeza kwenye kilimo cha kisasa zaidi na chenye mafanikio.

“Ni wazi kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ni chachu kubwa mno ya mafanikio ya wakulima wengi kwani awali mwitikio ulikuwa ni mdogo wakati grupu hili linaaanza lakini kwa sasa kadiri siku zinavyozidi kwenda kunakuwa na mwamko mkubwa.

“Hii inachangiwa zaidi kwamba wakulima wengi kwa sasa wamekuwa wepesi wa kusoma mambo mbalimbali yanayohusiana na kilimo wanachofanya, hivyo utakuta kwamba kwa sasa wakulima ni rahisi zaidi kutumia njia ya mtandao wa kijamii kupata elimu ya kilimo kuliko hata kutafuta vipeperushi na magazeti, hivyo wengi wamekuwa wakiweka pale changamoto wanazokabiliana nazo na wanapatiwa suluhu jambo ambalo ni lakupongezwa zaidi,” anasema Mkono.

Mkono anasema changamoto kubwa ambayo bado ipo ni kwa namna ya kuwafikia wakulima ambao wamekuwa wahawatumii simu za kisasa na hivyo kulazimika kutengeneza vipeperushi licha ya kwamba bado si jambo jepesi kuwafikia tofauti na wale wanaomiliki simu za kisasa kwani wao wanakuwa na urahisi wa kupiga picha aina ya ugonjwa unaoshambulia mazao na kupatiwa suluhisho kutoka kwa wataalamu.

“Ni wazi kuwa kwa sasa si rahisi kwa wakulima kwenda darasani kusoma juu ya kilimo na hivyo kwa kutumia mitandao ya kijamii inakuwa ni jambo jepesi katika kuweza kurahisisha changamoto hii.

“Kwani kuna magonjwa mengi ambayo yanafanana kwenye kilimo hivyo iwapo mkulima anakuwa na simu inayomwenzesha kujiunga kwenye mitandao ya kijamii inakuwa ni rahisi kupiga picha ya ugonjwa na kushirikishana na wengine na hivyo hata mtaalamu inakuwa ni rahisi kujua ugonjwa wake.

“Hivyo simu sasa hivi zinasaidia sana katika kunyanyua kilimo na kukifanya kuwa cha kisasa zaidi huku wakulima wengi wakiendelea kuongeza faida ya namna gani ya kuwa na kilimo cha kisasa ambacho kitawasaidia kuepukana na umbali wa kutembea kutafuta wataalamu na hata soko kwani wakulima wengi wanatumia mitandao hii katika kuweka bayana mazao yao na hivyo kurahisisha zaidi upatikanaji wa soko,” anasema Mkono.

Msukumo huo wa mitandao ya jamii kwenye kilimo haujaishia kwenye makundi hayo tu katika kuwasaidia wakulima kuwa na kilimo chenye manufaa kwani bado hata tovuti mbalimbali zimeanzishwa katika kuhakikisha kuwa zinasaidia kufanya kilimo kuwa cha kisasa zaidi kama anavyobainisha Brian Filbert, ambaye ni kati ya waasisi wa tovuti ya kilimo Forum.

Anasema kulingana na kuwapo kwa uhitaji mkubwa wa taarifa zinazohusiana na kilimo ndipo wakaamua kuanzisha tovuti hiyo ambayo inawasaidia wakulima kupata soko moja kwa moja ambapo mkulima kwa kupitia simu yake ya kiganjani anaweza kutumia mitandao hiyo ya jamii katika kujenga wigo wa mafanikio.

“Ni wazi kuwa kumekuwapo na idadi kubwa ya watumiaji wa mitandao ya jamii ambapo hata hivyo kumekuwa hakuna ushawishi kwa watu kuanzisha majukwaa kwenye mitandao yanayohusiana ana kilimo moja kwa moja.

“Hivyo hiyo ndiyo ikawa chachu ya sisi kuanza kutengeneza tovuti hii ambayo licha ya kwamba ni tovuti changa lakini kila kukicha inaendelea kuwa na msaada mkubwa kwa wakulima wenyewe,” anasema Filbert.

Anasema kupitia mitandao hiyo ya jamii kwa kushirikisha tovuti hiyo, ni wazi kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa ambapo wakulima wengi wamekuwa wakitumia jukwaa hilo katika kubadilishana ujuzi na mambo mengine.

“Kwa mkulima wa sasa anayetumia mitandao hii ya kijamii na amefanikiwa kujiunga na majukwaa mbalimbali yanayohusiana na kilimo ni wazi kuwa atakuwa ameona mabadiliko makubwa kwenye kilimo chake kufuatia elimu kubwa na matokeo chanya ambayo imekuwa ikitolewa kwenye mitandao hiyo kuhusu kilimo.

“Hivyo ni vyema kwa wakulima ambao hawako kwenye mitandao hii ya kijamii wakajinyima kwa kipindi kifupi lengo likiwa ni katika kuhakikisha kuwa wanapata simu zitakazowasaidia kuongeza ujuzi wa namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwenye kilimo pamoja na kupata soko la mazao yao kiurahisi,” anasema Filbert.

Upande wake, Amon Daniel, ambaye ni mkulima wa mananasi mkoani Morogoro anafafanua kuwa kupitia uwepo wa mitandao hiyo ya kijamii kumekuwa na msaada mkubwa kwenye kilimo chake ambapo amekuwa akipata darasa kila siku kupitia mafundisho mbalimbali yanayoelezwa na bwana shamba.

“Sasa hivi mambo ni wazi kuwa yamekuwa mepesi kwani hakuna jambo linalokosa utatuzi pindi unapoliweka kwenye mtandao wa kijamii, hivyo unajikuta kwamba kutumia mitandao hii kunampa mkulima faida kubwa kwani mbali ya kwamba inajumuisha wataalamu mbalimbali wa magonjwa ya kilimo pia inasaidia katika kutoa elimu namna unavyoweza kupata soko la bidhaa zako kirahisi na namna gani unavyoweza kuhifadhi vizuri mazao yako ili yasiweze kuharibika.

“Kwani kupitia mitandao hii wapo ambao awali walikuwa hawajui namna ya kulima baadhi ya mazao, lakini kulingana na kwamba huku kunapatikana njia zote tangu mwanzo wa kuandaa shamba, kupanda, kumwagilia, kuvuna na hatua nyingine bila kusahau mahala pa kwenda kuuza,” anasema Daniel.

Mwisho