Home Uncategorized UKWELI ULIVYO KIBOKO ALICHOCHAPWA ABOOD KINAMSTAHILI MCHUNGAJI LWAKATARE

UKWELI ULIVYO KIBOKO ALICHOCHAPWA ABOOD KINAMSTAHILI MCHUNGAJI LWAKATARE

1103
0
SHARE

NA VICTOR MAKINDA

Mbunge wa Morogoro mjini, Abdulazizi Abood amekiri ‘kuchapwa kiboko’ na Rais Jonh Magufuli kuhusu kiwanda chake. Kiboko hicho kilimzindua kutoka katika usingizi mzito na kumfanya kuamka na kukimbia kwa kasi kuelekea kwenye sera ya kutimiza lengo la serikali ya awamu ya tano, sera ya Viwanda.

Hakuna asiyejua umuhimu wa viwanda katika kuifanya Tanzania kuwa ni nchi ya watu wenye kipato cha kati na hata cha juu. Viwanda vinatoa ajira kwa wingi katika sekta na nyanja tofauti tofauti.

Ukweli Ulivyo sera ya Tanzania ya Viwanda, inarejesha matumaini ya watanzania yaliyopotea katika nyanza ya uzalishazi wa bidhaa za kilimo ambazo ni malighafi na bidhaa za viwandani zinazotokana na mazao ya kilimo ambapo kwa ujumla wake sera hii ina utajiri wa ajira. Binafsi naiita sera hii ni sera ya Utajirisho kwa Watanzania.

Kichwa cha makala hii kimegusia juu ya kiboko cha Rais Magufuli kwa Mbunge wa Morogoro Mjini, Abdulazizi Abood na namna kiboko hicho kilivyomwamsha mbunge huyo kutoka katika usingizi mzito wa kumiliki kiwanda kisichozalisha/Kiwanda mfu na haraka kuanza uzalishaji.

Abood anamiliki kiwanda cha kuzalisha mafuta, kinachojulikana kama Moproco Factory kilichopo mjini Morogoro. Kiwanda hiki kwa muda mrefu kilifungwa, lakini ikumbukwe kuwa miaka ya mwanzaoni mpaka mwishoni mwa 90, kiwanda hiki kilikuwa maarufu sana ndani nanje ya nchi kwa uzalishaji wa mafuta ya kupikia yanayotokana na mbegu za Alizeti na kilikuwa kiwanda mahiri kwa uzalishaji wa sabuni, Komoa.

Mimi sijui kwa nini kiwanda hiki kilifungwa, lakini kwa maelezo yake mwenyewe Abood anasema kuwa ushindani wa soko huria, soko linaloruhusu bidhaa kutoka nchi za nje kuingia nchini, ndicho chanzo kilichopelekea kiwanda hicho kuzalisha kwa hasara na hatimaye kufungwa mwanzoni mwa miaka 2000.

Lengo la makala haya sio kuzungumzia kiwanda cha Moproco, hapana, lengo la makala hii ni kuizungumzia nguvu ya Rais Jonh Magufuli katika kuwasukuma wanaomiliki viwanda visivyozalisha kuanza uzalishaji wa haraka.

Akiwa njiani kutoka Dodoma, Rais Magufuli kama ilivyo desturi yake alisimama kusalimia wakaazi wa mkoa wa Morogoro, hususani Morogoro mjini. Hii ilikuwa ni mwanzoni mwa mwaka jana  2017. Rais Magufuli pamoja na mambo mengine alikemea vikali juu ya watu wanaomiliki viwanda ambayo vimegeuka kuwa magofu pasipo kuzalisha chochote. Rais Magufuli alitoa  karipio bila kuuma maneno kama ilivyo desturi yake, kwa mbunge wa Morogoro mjini tena kwa kumtaja jina kuwa anamiliki kiwanda ambacho hakizalishi.

Hatua hiyo ilimuasha Abood na kuanza ukarabati wa haraka wa kiwanda hicho na wiki iliyopita rais Magufuli akiwa mjini hapa katika ufunguzi wa kiwanda cha sigara kilichopo Kinguruwila, Abood alikiri kwa kinywa chake mbele ya Rais Magufuli, kuwa kiboko alichochapwa na rais kimemzindua na tayari sasa kiwanda chake kimeanza uzalishaji na kinatoa ajira kwa wingi.

Safu ya Ukweli ulivyo mwaka jana ilipata kutembelea kiwandani hapo kipindi kabla ya uzalishaji haujaanza. Nilichokiona ni ghala kubwa la kuhifadhi mbegu za Alizeti likiwa limesheheni maelfu ya magunia ya alizeti huku malori kutoka maeneo mbali mbali Tanzania yakimiminika kiwandani hapo kushusha mbegu za alizeti tayari kwa kuanza uzalishaji wa mafuta yanayotokana na zao hilo.

Mantiki ni nini? Hapa tunaona kuwa kwa kufunguliwa kiwanda cha Moproco, Abood, ametoa ajira kwa maelfu ya watanzani ndani na nje ya mkoa wa Morogoro. Mbegu za alizeti zinazoletwa kiwandani hapo zinatoka Singida, Manyara, Tabora na maeneo yote yanayozalisha alizeti kwa wingi kutia ndani mkoa wa Maorogoro.

Katika muktadha huo, wakulima wa alizeti wamepata soko la uhakika lakini pia wapo wafanyakazi katika nyanja na sekta tofauti walio ajiliwa kiwandani hapo.

Picha ya jumla ni kwamba kiwanda cha Adood Seeds kimezalisha ajira nyingi na kinaendelea kuboresha ajira na maisha ya wananchi wengi mahali pengi Tanzania.

Hivi ndivyo viwanda tunavyovihitaji na hii ndio dhima ya sera ya Tanzania ya viwanda. Nitakuwa mchoyo wa fadhira kama sitompongea kwanza Rais wetu Magufuli kwa msukumo wake mkubwa wa sera ya viwanda na pili Mbunge wa Jimbo la Morogoro, Abdulazizi Abood kwa hatua yake hii muhimu ya kukifungua na kuanza uzalishaji wa kiwanda chake.

Mkoa wa Morogoro ni mkoa uliokuwa kimbilio la wasio na ajira kutoka mikoa mingi Tanzania. Miaka ya 1970-80 mpaka mwanzoni mwa 90 mkoa huu ulikuwa na viwanda hai vingi. Viwanda hivyo vilitoa ajira nyingi na kuuchangamsha uchumi wa mkoa huu.

Kama alivyopata kutamka Rais Magufuli kuwa Watanzania tuliingiwa na ugonjwa wa ajabu. Viwanda vingi tuliviua pasi kujali umuhimu wa viwanda hivyo katika ustawi wa maisha ya watanzania.

Kwa uchache ninavikumbuka viwanda vikubwa vilivyokuwepo Morogoro. Morogoro Canvas, kiwanda cha maturubai ni moja kati ya viwanda vingi vilivyokuwepo, kuna  Moro Lather Board maarufu kwa utengenezajiwa wa Ciling Board, CIDO, kilikuwa kikizalisha  Mabegi na mikoba ya akina mama, Moro Shoe, kiwanda maarufu kabisa kwa utengenezaji wa viatu,     Ceremic, kiwanda maarufu kwa utengenezaji wa  vyombo vya nyumbani vya udongo na vingine vingi.Viwanda hivi vyote vimefungwa. Jiulize ni ajira ngapi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja zingezalishwa kama viwanda hivi vingekuwa vinafanya kazi?

Safu ya ukweli ulivyo hivi karibuni ilitembelea,kiwanda cha 21 Century kilichojulika kama Polyster hapo zamani. Kiwanda hiki ni cha mfano wa kuigwa  katika viwanda vinavyofanya kazi  na kutoa ajira kwa wingi.

Mmoja wa viongozi kiwandani hapo alinidokeza kuwa kiwanda hicho kimetoa ajira za moja kwa moja kwa wafanyakazi wapatao 2200. Hapa tunaweza kuona ni jinsi gani viwanda hai vinaweza kupunguza tatizo la ajira nchini. Kama kiwanda kimoja tu cha 21ST Century kimeajiri watu zaidi ya 2000 vipi kama tungekuwa na viwanda kumi vya aina hiyo?  Viwanda ni moyo wa maendeleo ya Taifa. Sera ya viwanda ni sera iliazimia kuwatajirisha Watnzania. Viwanda ni Utajirisho.

Rais Magufuli alimchapa kiboko Abood, Abood sasa kiwanda chake kama nilivyosema awali kimeanza uzalishaji. Rais Magufuli sasa kiboko chako kile kile ulichomchapia Abood, na ukitumie kumchapa Mama Getrude Lwakatare mbunge wa viti maalumu CCM, ambaye ni ni mwekezaji wa kiwanda mfu cha Mang’ula Machine and Mechanical Tools.

Kwa wasiofahamu, kiwanda hiki kipo kijijini cha Mang’ula B, Kata na Tarafa ya Mang’ula, wilayani Kilombero mkoa wa Morogoro. Kiwanda hiki ni miongoni mwa viwanda vilivyokuwa maarufu si tu Tanzania bali Afrika na duniani. Tunaokifahamu kiwanda hiki jinsi kilivyokuwa, tukitazama kilivyo leo, tunabubujikwa na machozi

Miaka ya 1970  mpaka mwanzoni mwa miaka ya 90, kiwanda hiki kilikuwa ni miongozi mwa viwanda nguli, bora na cha mfano wa kuigwa ndani nanje ya nchi kwa utengenezaji, uchongaji wa vipuri bora, imara mathubuti vya mashine za aina mbali mbali Duniani.

Kiwanda hiki kilibinafsishwa kwa Mama Lwakatare  baada ya uzalishaji kusimama kwa muda mrefu. Umuhimu wa kiwanda hiki katika suala la utoaji wa ajira hauelezeki, kwani ndicho kiwanda kilichouzaa mji wa Mang’ula na kuufanya ung’are na kupata wahamiaji wengi kutoka mahali pengi Tanzania.

Kufa kwa kiwanda hiki ilikuwa ni pigo kwa wakazi wa Mang’ula na Tanzania kwa ujumla. Tuliposikia kuwa kiwanda hiki kimepata mwekezaji, wengi tulifurahi na matumaini ya ajira yalirejea. Kinyume chake kiwanda hiki tangu kimebinafsishwa kwa Mama Lwakatare, kinachoendelea kiwandani pale ni kichekesho.

Sidhani kama kuna kipuri hata kimoja kinachozalishwa kiwandani MMMT kwa sasa,(nasema tena sidhani).

Awali baada ya kubinafsishwa, palikuwa na shule ya Sekondari na Msingi ya St Mary’s. Baadae sijui chuo cha ufundi, lakini kiukweli sijawahi kusikia muungurumo wa machine na kuona vipuri vikizalishwa pale. Nasema sijawahi kwa kuwa mimi ni mmoja wa wapangaji wa nyumba zilizokuwa za wafanyakazi wa MMMT wa zamani na sasa zimepangishwa watu binafsi (nikiwemo mimi), hivyo nipo karibukabisa na kiwanda hicho.

Nachelea kusema kuwa  kuna kinachoendelea kiwandani MMMT, na kwa mukktadha huo huo ninaungana na Mbunge wa Morogoro mjini Abdulazizi Abood kukuomba Rais Magufuli, kiboko kile ulichotumia kumchapa Abood na ukitumie kumchapa Mama Lwakatare aifufue MMMT ili sera ya Tanzania ya viwanda itimlike kwa vitendo.

Itaendelea wiki ijayo ambapo nitakuja na maelezo ya kina kuhusu kiwanda cha MMMT cha Mama Lwakatare.