Home Latest News ULIPAJI DENI LA TAIFA NI UKOMBOZI WA UMASIKINI KWA WATANZANIA?

ULIPAJI DENI LA TAIFA NI UKOMBOZI WA UMASIKINI KWA WATANZANIA?

1147
0
SHARE
Mwanamama akichota maji katika mazingira hatarishi

NA PROF HANDLEY MAFWENGA,

MAANA ya Deni la Taifa ni mrundikano wa jumla ya mikopo yote ya Serikali baada ya kulipa baadhi ya madeni. Kipimo cha deni la Taifa ni mrundikano wa jumla ya matumizi yaliyofanyika kutokana na mapato yaliyokusanywa na Serikali. Kadiri mapato yanapozidi kuwa makubwa Serikali ndipo inapokuwa na uwezo wa kufanya matumizi, ikiwa ni pamoja na kulipa deni la Taifa. Serikali yoyote inayoweza kukusanya mapato yake vizuri kukidhi matumizi inakuwa na uwezo mkubwa wa kulipa deni la Taifa na kuwa na heshima.

Uhalisia wa kipimo cha deni la taifa, hupatikana pale ambapo unajumuisha uhamishaji baina ya Serikali husika kwenye soko na malipo ya riba za mikopo ambayo huongeza ukubwa wa mikopo. Na mara nyingi kitakwimu huoneshwa kwa jumla ya mwaka katika bei za soko la wakati huo. Kwa upande wa Tanzania, deni la Taifa hadi kufikia kipindi cha Mwaka 2016 lilifikia karibia asilimia 37 ya Pato la Taifa. Kimsingi Deni la Taifa hulipwa na raia wa nchi inayodaiwa deni ikiwa ni pamoja na kizazi kijacho katika Taifa husika. Nadharia ya Uchumi huwa inahitaji kuwepo kwa kiwango cha kumudu deni la Taifa ambapo uwiano wa deni la Taifa na ukuaji wa uchumi ndiyo huangaliwa zaidi.

Kabla hujaingia kutathmini deni la Taifa, ni vyema kuwa na kiwango kikubwa cha ukuaji wa uchumi. Na ulipaji wa deni la Taifa unategemea zaidi jumla ya deni ambalo Taifa inadaiwa. Na vyanzo vya kulipa deni la Taifa ni lazima kuwepo na kitu kinachoitwa ‘Seignorage’ ambacho ni kitendo cha kuifanya fedha ya nchi kuwa na nguvu kuhimili mfumuko wa bei na hii huwa ni uwepo wa uwezo wa mapato kuweza kulipa madeni mapya na madeni yaliyopo yaani ukuzaji wa uwekezaji katika mitaji na bidhaa na kupunguza madeni katika hati fungani hasa kwa kuangalia fedha za ndani kwa mfano shilingi ya Tanzania.

Uwepo wa deni la Taifa katika nchi ikiwemo Tanzania unasababishwa na kushuka kwa thamani ya shilingi, uwepo wa mikopo mipya yenye masharti nafuu na mikopo ya kibiashara ambayo Serikali inakuwa ikipokea na malimbikizo ya riba ya deni la nje kwenye nchi zisizo wanachama wa Kundi la Paris ambazo hazijatoa misamaha ya madeni kulingana na makubaliano. Hadi kufikia Desemba 2014, deni la Taifa kwa Tanzania lilikuwa Sh trilioni 33.6, ikiwa ni jumla ya deni la Serikali Sh trilioni 30.1 na lile la sekta binafsi Sh trilioni 3.5.

Kwa upande wa Tanzania pamoja na kukua kwa deni la Taifa, uwiano wa deni la Taifa na ukuaji wa uchumi umekuwa imara  kutokana na ukuaji mkubwa wa uchumi na gharama ndogo za ukopaji, yaani riba katika mikopo ya masharti nafuu. Jumla ya deni la nje na lile la ndani kwa Dola za Marekani limekuwa imara pamoja na kuwa deni la ndani limekuwa likikua kutokana na kushuka kwa thamani ya fedha za Tanzania ambayo umesababisha kushuka kwa uwiano wa deni la ndani likithaminishwa kwenye Dola za Marekani.

Kwa bahati mbaya, katika nchi nyingi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, soko la deni la ndani bado halijaendelea sana na linatawaliwa na washiriki wachache wakiongozwa na benki za biashara. Kwa Tanzania, benki za biashara zina asilimia karibia 50 ya madeni ya dhamana. Athari ndogo katika dhamana za Serikali ukilinganisha na ukopeshaji kwenye sekta binafsi unaonesha jinsi benki za biashara zilivyojikita zaidi kwenye soko la dhamana. Hii pia inasababishwa na ukuaji wa sekta ya kibenki. Benki Kuu ya Tanzania ni ya pili kwa zaidi ya asilimia 28 ikifuatiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii yenye zaidi ya asilimia 16.

Serikali pia hukopa kutoka katika vyanzo vya ndani kwa ajili ya miradi yake kama vile miundombinu. Serikali ya Tanzania kupitia mpango wa sera uitwao ‘Policy Support Instrument arrangement’ inaweza kukopa hadi kufikia asilimia moja ya kiwango cha ukuaji wa uchumi bila kuathiri uchumi na ukuaji wa uwekezaji katika sekta binafsi. Mikopo ya ndani ni chanzo kikubwa cha mapato kwa taifa, ingawa chanzo hiki kina changamoto zake kwa sababu fedha zinazoahidiwa na wahisani zinakuwa hazitoshi na hivyo kukosa dhana ya kujua uhalisia wa thamani yake kwa siku za usoni. Hii ni kwa sababu wafadhili wengi pia wanakumbwa na matatizo ya kiuchumi katika nchi zao. Kwa hali hiyo, utoaji wa ahadi zao umekuwa ukipungua. Kwa siku za karibuni ufadhili umekuwa mgumu na wenye kukosa tathmini ya kujua thamani yake siku za usoni.

Serikali ya Tanzania inakopa katika vyanzo vya mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya miradi yake ya kimkakati. Vyanzo hivyo ni kama kutoa hati fungani kutoka kwenye soko la kimataifa, kukopa mikopo yenye uhusiano wa kifedha na kiasasi yaani syndicated loans na mikopo ya kusaidia ukopeshaji kwa ajili ya kuuza bidhaa nje ya nchi. Hata hivyo, mikopo isiyo na masharti nafuu inaweza kuongezeka kutokana na kushuka kwa misaada kutoka nchi za wahisani. Hili pia ni suala la kuliangalia sana.

Kasi ya ulipaji wa madeni kwa Tanzania inaweza kusaidia kupunguza makali ya riba kwenye mikopo na kupunguza muda wa ulipaji wa mikopo hiyo na kuifanya nchi iwe na heshima na iweze kufanya mambo mengine muhimu zaidi. Ili Tanzania tujikomboe katika ukuzaji wa mapato, ni vyema kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli ya kufanya kazi kwa kasi na nguvu ili matokeo yake yaliepushe Taifa katika mzigo wa kulipa madeni yanayojitokeza.

“MUNGU IBARIKI TANZANIA! MUNGU IBARIKI AFRIKA”