Home Makala Umasikini chanzo cha mtoto wa kike kutothaminiwa

Umasikini chanzo cha mtoto wa kike kutothaminiwa

1133
0
SHARE

NA PENDO FUNDISHA-MBEYA

UMASIKINI ni hali ya ukosefu wa mahitaji ya msingi ya binadamu. Familia masikini inakosa uhakika wa kupata chakula bora, malazi safi na mavazi yenye staha.

Haya yote msingi wake ni kukosa fedha hali inayosababisha kukosekana uhakika wa kupata elimu bora, maji salama na huduma za afya.

Umasikini hauishii kwa familia tu, unaweza kutamalaki kwa mtaa, wilaya, mkoa na hata taifa na hivyo ndivyo ilivyo kwa nchi nyingi za Afrika. Zinatazamwa kama nchi masikini pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha kuwa matajiri.

Ingawa kumekuwa na jitihada za mara kwa mara za nchi masikini kupambana na kadhia hiyo, lakini bado mafanikio si makubwa.

Tafiti zinaonyesha kuwa miaka 10, Tanzania ilijitahidi kuupunguza umasikini kwa asilimia 20, hata hivyo hali bado ni mbaya kwa jamii zinazoishi vijijini.

Umasikini wa nchi unaiathiri pakubwa jamii, hali inayochangia kukosekana kwa huduma zote muhimu ikiwamo chakula na hata elimu.

Mathalani takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka 1991/99 na 2000/01 umasikini wa chakula kwa Taifa (National Food Poverty Line) ulipungua kutoka 21.6% hadi 18.7%.

 Aidha idadi ya kiwango cha Watanzania wanaoishi chini ya kiwango cha mahitaji muhimu (National Basic Needs) kilipungua kutoka 38.6% hadi 35.7%.Takwimu hizi zinaonesha umasikini bado upo.

Tathimini za umaskini zinaonyesha yapo makundi ya watu ambayo yapo katika hatari ya kuathirika zaidi kuliko makundi mengine.

Makundi hayo ni watoto, wazee, watu wenye ulemavu, wanawake wajane, vijana na watu waishio na virusi vya Ukimwi.

Mbali na makundi hayo, lakini pia inaelezwa kuna tofauti za viwango vya umasikini kwa mikoa, wilaya na hata vijiji kulingana na idadi ya watu,rasilimali zilizopo, hali ya hewa na ubovu wa miundo mbinu.

Utafiti uliofanywa na kitengo cha Uchumi cha chuo Kikuu cha Dar es Saalam juu ya mikakati ya kuwawezesha wananchi MKURABITA ilieleza kuwa mwaka 2000 iliandaliwa mikakati mbalimbali ya kupunguza umaskini.

Mwaka 2000-20033 mkakati wa kupunguza umasikini uliandaliwa, ukihususisha msamaha wa madeni chini ya utaratibu wa Benk ya Dunia na shirika la Fedha la Kimataifa.

Lengo la msamaha huo lilikuwa ni kuondolea mzigo kwenye sekta ya Elimu, Afya, Kilimo, Barabara za vijijini, Maji na Mahakama .

Baadae uliundwa mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA),ambao ulikuwa shirikishi.

Katika kuhakikissha umasikini unatokomezwa ukaibuliwa mpango wa “Tekeleza sasa katika Matokeo Makubwa” Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ndie aliuzindua.

Mambo makuu yaliyopewa kipaumbele kwenye awamu hii, ni Elimu, Nishati, kilimo, Maji, Uchukuzi na ukusanyaji  wa Mapato.

 hapa naipongeza serikali kwa kuwa na mikakati mizuri kwani wakati huo mkakati ukiendelea Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora mwaka 2016  ilikuja na Mpango wa kuzinusuru kaya masikini awamu ya tatu.

Mpango wa kuzinusuru kaya masikini chini ya TASAF bado uaendelea, malengo yakiwa ni kuzijengea uwezo kaya masikini kwa kuziwezesha ruzuku ya fedha, kupitia sekta ya afya na elimu kwa watoto kuanzia miaka 0-5 na wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita kwa kila mwezi kutolewa sh. 10,000.

 TASAF inatoa fedha kwa mtoto au watoto wenye umri chini ya miaka 18 na wanaongeza kiasi cha shilingi 4000 hata kama mtoto hasomi, mtoto chini ya miaka 0-5 atalipwa shilingi 4000 kwa kuhudhuria kituo cha afya au Zahanati kwa mwezi na watoto wanaosoma shule ya msingi watalipwa shilingi 2000 kwa kila mtoto kwa watoto wasiozidi wanne.

Hata hivyo, kwa watoto wanaosoma shule za sekondari kidato 1-4 watalipwa shilingi 4000, kila mtoto kwa watoto wasiozidi watatu kwa mwezi huku mtoto au watoto wa kidato cha 5-6 watalipwa shilingi 6000 kila mtoto kwa watoto wasiozidi wawili kila mwezi.

Mikakati yote imefanyika na kuendelea kufanyika lengo likiwa ni kuisaidia jamii kuondokana na umasikini.

 Umasikini umekuwa kichocheo kikubwa cha familiza kuwaozesha watoto wa kike ili kupata fedha hatua inayokatisha ndoto ya mtoto wa kike.

 Jambo hili linatajwa kuwa kikwazo kikubwa kwa elimu na afya ya mtoto wa kike kwani upo uwezekano wa kupata mimba akiwa mdogo.

Zipo sheria zinazomlinda mtoto wa kike, lakini mambo yanbakuwa magumu kutokana na umasikini, jamii inashindwa kutii sheria kwa sababu ya kusukumwa na tamaa ya kipato.

Sheria ya kumlinda mtoto ya mwaka 2009 sura ya 95 imetoa mamlaka kwa jamii kuripoti vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto, huku sheria ya jinai sura ya 130 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inasema mtoto aliyechini ya miaka 18 hana ridhaa ya kufanya mapenzi na endapo kitendo hicho kitafanyika kitakuwa ni ubakaji.

Sheria zote hizi zimeundwa kwa lengo la kumlinda mtoto wa kike aweze kusoma au kuishi kwa amani na kutimiza malengo yake, lakini kinachosikitisha ni kutotekelezeka kwa sheria hizo kwa asilimia 100 kutokana na baadhi ya wahusika kushindwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola.

Ukiangalia takwimu za mimba zilizotolewa na Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, zinasema mwaka 2017/18 jumla ya wanafunzi 212 walipata mimba huku sababu kubwa ikitajwa ni hali ya umasikini iliyozikumba familia hizo.

Mkuu wa shule ya Sekondari Imezu Wilayani Mbeya, Tibus Makona, anasema kwa mwaka 2017/18 shule hiyo inajumla ya watoto saba ambao wameshindwa kuendelea na masomo kutokana na tatizo la mimba na jambo la kushangaza ni kwamba wahusika wa mimba hizo hawajachukuliwa hatua zozote za kisheria.

Baadhi ya watoto, wanawataja wanaume waliowapa mimba lakini mzazi au mlezi anamtishia mtoto kwa kumtaka asimtaje kwenye vyombo vya dola kwani atakapokamatwa na ufungwa, hakutakuwa na mtu wa kumlelea mtoto pindi atakapozaliwa.

 “Sasa hapa unaona, mtoto kapata mimba wakati akitekeleza majukumu ya kifamilia na dola inapotaka kuchuua hatua za kisheria inakosa nguvu kutokana na ushirikiano hafifu toka kwa mtoto, mzazi na mlezi, sasa kama hawa watu watagoma kutoa ushahidi unadhani nani atasimama mahaamani,?,” alihoji Mwalimu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Imezu, Gorge Waziri, anasema miongoni mwa watoto waliopata mimba ni mtoto wake anayemlea Hanifa Waziri (15), ambaye alishindwa kuendelea na masomo ya kidato cha pili mwaka jana baada ya kupata ujauzito na sasa analea mtoto wa kiume wa miezi miwili.

 Waziri anasema changamoto kubwa inayochangia tatizo la mimba kwa watoto wa kike ni mazingira yanayowazunguka, hali duni ya kipato katika familia na lingine ni tamaa za kimwili, hata hivyo anakiri kwamba kwa tukio la mtoto Hanifa limetokana na uduni wa maisha wa familia hiyo ya kake yake na baya zaidi ni pale mtoto anaposhindwa kumtaja muhusika kutokana na shinikizo kutoka kwa mama yake.

“Mtoto anakuambia akiwa shule alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume zaidi ya mmoja na hata yeye hafahamu nani alimpa mimba, lakini ukifuatilia kwa undani unagundua kwamba hapo kunaviashiria vya muhalifu  kulindwa,na hapo ndipo vyombo vya dola vinapopata wakati mgumu wa kusimamia sheria hizi za watoto,”anasema.

SIMULIZI YA HANIFA NA ASHA JUU YA MIMBA

Hanifa Waziri ni miongoni mwa wanafunzi walioathiriwa na mazingira na hali duni ya kipato kutoka kwa wazazi hivyo kujikuta akishawishika na kuingia kwenye mikono ya baadhi ya wanaume waharibifu na kupata mimba na kupoteza ndoto zake.

Anasema wazazi wake wanajishughulisha na biashara ya pombe kilabuni hivyo wakati mwingi hubaki nyumbani pekee yake akiendelea na shughuli za nyumbani na shambani, lakini kila alipokuwa akijiitahidi kutekeleza majukumu hayo ya kifamilia anakutana na changamoto ya kifedha katika kukidhi mahitaji yake muhimu ya shule kama vile, daftari, mafuta, dawa ya meno, nguo za ndani, pedi na chakula.

“Nikitoka shule mama ananitaka niende shamba nikirejea nyumbani chakula hakuna, bado mafuta ya kupaka, sabuni, daftari na pedi kwa ajili ya kujisitiri sina, hivyo nafikiria nitavipata wapi hapo ndipo nilipojikuta nikiingia kwenye mahusiano na wanaume wawili ambao walikuwa wakijitahidi kunitimizia yale niliyokuwa nikiyahitaji,”anasema.

Anasema mwanaume mmoja ni mkulima na mwingine ni dereva bodaboda ambao wote walikuwa wakimsaidia. Hata hivyo ana wakati mgumu kutaja baba wa mwanaye kwani ana hofu atakamatwa na kufungwa wakati yeye atabaki na mzigo wa kulea mtoto.

“Kutaja baba wa mtoto ni ngumu, na siwezi kwani ninafikiria nani atamtunza mtoto kama atafungwa? Wazazi hawahangaiki na mimi?  Natamani kurejea shule lakini sioni msaada wowote tena,” anasema.

Asha Jamali (17) alishindwa kuendelea na masomo yake baada ya kupata mimba akiwa kidato cha tatu katika shule ya sekondari ya Ilongo Wilayani Mbeya, anasema  serikali inapaswa kuwasaidia kwa kuwachuulia hatua  wazazi ambao wamekuwa wakiwatumikisha watoto wa kike kwa kuwabebesha majukumu ya kifamilia na pamoja na Taasisi ya kupambana na Rushwa  (TAKUKURU) kuwabana wazazi wanaopokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa.

“Kidato cha kwanza na cha  pili, nilisoma kwa taabu sana lakini nilipoingia kidato cha tatu hapo ndio ilikuwa balaa kwani wakati mwingine ukimuomba mzazi fedha za mahitaji muhimu ya shule, malzi na chakula anakuambia hata wewe ni mwanamke umekuwa unaweza kwenda kutafuta au anakuambia kabisa umeshakuwa mkubwa na wewe ni mama wa familia unapaswa kuwalea wadogo zako,”anasema.

Anasema, alipopata ujauzito aliwaeleza wazazi wake ambao walimfuata muhusika na kumalizana naye kwa makubaliano ya kulea mimba hiyo kwa kutoa shilingi 2000 kila siku na kumtaka yeye asithubutu kumtaja mlengwa wa mimba hiyo kwani tayari njaa imemalizika nyumbani.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Mbeya na Diwani wa kata ya Imezu, Mwalingo Kisemba, anasema serikali ya kijiji inashindwa kutekeleza sheria zinazomlinda mtoto kwa kukosa ushirikiano kutoka kwa wazazi wakati wa operesheni ya kuwakamata wahusika waliowapa mimba wanafunzi na wakati mwingine wanashirikiana kuwatorosha na kuwatisha watoto wasiwataje wahusika.

“Wazazi na walezi hawatoi ushirikiano na wakati mwingine wanashiriki kuwatorosha wahalifu kwa makubaliano na haya yote yanafanyika kutokana na hali duni ya maisha kwani familia zinazojiweza zimekuwa zikishirikiana vizuri na vyombo vya dola katika kuwabaini wahalifu wa watoto wa shule,”anasema.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika, anasema  serikali imeweka mikakati madhubuti ya kumkomboa mtoto wa kike kwa kutekeleza kwa vitendo sheria ndogo zitakazo wabana wazazi watakaobainika kuwa watoto wao wamepata ujauzito wakiwa shule.

Anasema ukiangalia sheria ya mtoto ya mwaka 2009 sura ya 95 imetoa mamlaka kwa jamii ya kuripoti vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto, sheria ya jinai sura ya 130 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inasema mtoto aliyechini ya miaka 18 hana ridhaa ya kufanya mapenzi na endapo kitendo hicho kitafanyika kitakuwa ni ubakaji.

Mdau wa Maendeleo Mkoa wa Mbeya, Amani Mwansasu anasema changamoto kubwa ni ushirikiano wakati wa kuwabaini wahalifu lakini serikali inaangalia utungaji wa sheria ndogo zitakazo wabana wazazi na walezi wa watoto ambao watabainika kupata mimba wakiwa shule.       

Anasema, adhabu hiyo inatolewa  ikiwa na lengo la kutoa fundisho kwa wazazi kwani  wamekuwa ni kikwazo kwa  kuendekeza tamaa ya fedha mbele pale wanapogundua  binti zao wanamimba na kutokwenda kutoa taarifa ya tukio hilo  kwenye vyombo vya dola ili sheria ichukue mkonda wake.

Kweli ni mikakati mizuri sana hasa sheria hizi zitafanya kazi na kusimamiwa ipasavyo na wahusika ambao ni watendaji wa serikali kuanzia ngazi ya Kata mpaka Taifa, wazazi , walezi na walengwa wenyewe ambao ni watoto kwa kutoa ushirikiano mara tatizo linapotokea.

Naye mdau wa maendeleo ya elimu, kutoka ofisi ya wanasheria wa kujitegemea, Emanuel Peter, anasema wazazi pia wanapaswa kutupiwa lawama katika tatizo la  mimba za utotoni kutokana na kuwaficha wahusika wa vitendo hivyo na kuwazuia mabinti wasitoe ushahidi mahakamani.

“Watendaji wanajitahidi kuwatia nguvuni wahusika wa matukio hayo lakini wazazi wa pande mbili wakishakubaliana, vyombo vya dola vinakuwa havina nguvu tena kwani suala hilo linakuwa la kijamii zaidi,”anasema.

Watoto wako katika hatari mara mbili zaidi ya kuishi kwenye umaskini uliokithiri ikilinganishwa na watu wazima. Hii ni kwa mujibu wa utafiti mpya kutoka Benki ya Dunia na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF.

Utafiti huo ukiangazia watoto wanaoishi kwenye umaskini uliokithiri unaonyesha kuwa mwaka 2013, asilimia 19.5 ya watoto katika nchi zinazoendelea walikuwa wakiishi katika kaya zenye kipato cha dola 1.90 kwa siku au chini, ikilinganishwa na asilimia 9.2 kwa watu wazima.

Kwa mantiki hiyo UNICEF na Benki ya Dunia wanapendekeza pamoja na mambo mengine, mara kwa mara kupima umaskini miongoni mwa watoto katika ngazi ya kitaifa na serikali za mitaa na kuzingatia watoto katika mipango ya kitaifa ya kupunguza umasikini kama sehemu ya jitihada za kukomesha umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2030.

Mwisho.