Home Habari Umasikini kikwazo cha elimu vijijini

Umasikini kikwazo cha elimu vijijini

1070
0
SHARE

NA ELIZABETH KILINDI, NJOMBE

‘’Nilikuwa napenda kusoma, lakini mazingira yalikuwa shida. Nilikuwa naishi na bibi, naye alikuwa hajiwezi. Kwa hiyo kuna kipindi nilihudhuria masomo, na siku nyingine nilikuwa siendi kabisa, badala yake nilikwenda stendi kutafuta kazi yoyote ya kufanya.”

Haya ni maneno ya mmoja wa wanafunzi aliyeathiriwa na ukosefu wa kipato uliomfanya asitishe masomo akiwa darasa la nne.

Anaongeza mwanafunzi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina:  ‘’Ikitokea nimekwenda shule, basi nilikuwa nakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo kukuta nyumbani hakuna chakula. Bibi yangu ni mzee, hivyo nikawa natoka kwenda kutafuta chochote.’’

Anasema hajutii kuacha shule kwa sababu hakuna mtu ambaye alikuwa akimfuatilia kwa kuwa bibi yake amezeeka sana, na yeye sasa ndiye amebeba jukumu la kumsaidia.

‘’Sasa hivi nimeshasahau kuhusu shule kwa kuwa nafanya kazi ambazo zinanipa kipato kinachoniwezesha kumsaidia bibi,’’anasema.

Hali ngumu ya kiuchumi na ukosefu wa mahitaji ya msingi, unawalazimu watoto wengi kuingia katika ajira za utotoni ambazo mara nyingi ni za kinyonyaji, manyanyaso au zinazofanywa katika hali hatarishi kama vile kwenye migodi, uvuvi, mashamba au kazi za ndani.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya katika Kata ya Imalinyi, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe, umebaini umasikini wa kipato katika kaya ni chanzo cha wanafunzi kukosa fursa ya kupata elimu.

Takwimu za mwaka jana katika Kata hiyo, zinaonyesha kwamba wanafunzi 103 walishindwa kufaulu, huku 20 wakiacha shule na sasa hawajulikani waliko.

Wazazi waliozungumzia  tatizo hilo wanasema umasikini wa kipato ni tatizo kubwa kwa familia nyingi.

Steven Ngole, anasema kama katika familia kuna hali ya umasikini, maana yake mtoto atashindwa kupata mahitaji ya kila siku ambayo yatasababisha ashindwe kumudu masomo.

Ngole anasema mwanafunzi akipata mahitaji muhimu, kunamwezesha kufikiria maswala ya shule, si ya nyumbani. Lakini kama hali ni duni nyumbani, maana yake mtoto akili yote itakuwa nyumbani, na hawezi kushiriki masomo vizuri.

‘’Kama, kwa mfano, huu utaratibu wa chakula shuleni, kuna wazazi wengine hawamudu, kwa hiyo inapotokea wenzake wanakula, yeye hawezi kula, anaanza  kujinyanyapaa yeye mwenyewe.  Kwamba sisi ni masikini kiasi hiki, wenzetu wanakula sisi tunawaangalia. Hudhani wanaokula ni watoto wa matajiri hali hiyo haiwezi kumsaidia mtoto,’’ anasema Ngole.

Anaongeza: “Katika kufanikisha elimu bora kwa mtoto tuhakikishe mambo ya msingi yanakuwapo, kama mlo na mavazi. Vinginevyo elimu bado itapatikana kwa shida”.

Naye Sadoki Mwanda, anasema umasikini unachangia sana kushuka kwa elimu kwa sababu mtoto anapokuwa shuleni muda mwingine anakuwa hapati mahitaji ya msingi na hivyo kusababisha kushindwa kuhudhuria masomo kwa wakati.

‘’Wazazi wajitahidi, kwani hawa ndio Taifa la kesho kwa hiyo tunapaswa kuendelea kuwapatia mahitaji yao ya msingi na muhimu, hasa ukiangalia hivi sasa shule za msingi na sekondari, watoto wanapata chakula shuleni lakini wale ambao hawajachangiwa wanalazimika kurudi nyumbani kufuata chakula…kwa hiyo ule umbali wa kutoka shuleni kwenda nyumbani, anarudi akiwa amechoka na anapoingia kwenye vipindi analala tu darasani badala ya kumsikiliza mwalimu,’’ anasema Mwanda.

George Mbilo, anasema wanafunzi wengi wanaacha shule kwa sababu ya mzunguko hafifu wa fedha uliopo vijijini ambao unasababishwa na shuguli za kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo nyanya.

‘’Si unawaona hao watoto hapo, wameacha shule, hawataki kusoma, na akienda shule anashindwa kwa sababu hapa kuna mzunguuko mkubwa ya fedha, hivyo wanashinda tu hapa kijiweni kwa kujua kuwa watapata kazi yoyote, hata kuosha magari,’’ anasema Mbilo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Imalinyi, Onesmo Liandala, anasema wakazi wa Kata hiyo hawapangilii vizuri mapato na matumizi yao, hali inayowafanya kushindwa kutekeleza majukumu kwa watoto wao.

‘’Tatizo lililopo watu wa huku hawaishi kwa bajeti, kwa hiyo mtu hawezi kuelewa maisha  yake anaendeshaje ma kwa shilingi  ngapi? Ikitokea sasa anakwenda shuleni kwa sababu anakaa hosteli huko huko kwa hiyo tunapomwambia achangie chakula na kupiga hesabu, anaona kama ni gharama za maisha,’’ anasema Liandala.

Anaongeza: ‘’Hata suala la milo, kwa mfano, kuwa na milo mitatu kwa siku, na mahitaji ya nguo kwa mtoto katika familia zao, si kitu cha lazima. Anapata mpya baada ya zamani kuchakaa sana.

‘’Kwa hiyo, mtu anapoanza kumpangia kwa utaratibu huo, anajikuta kama ni gharama za maisha ambazo zimekuja bila kuzitarajia.’’

Anasema mara baada ya kugundua changamoto hiyo, walianzisha mpango wa kuondoa umasikini katika kila kaya.

‘’Baada ya kugundua watu tunaowaongoza wana umasikini wa kipato ambacho kinawafanya kushindwa kukidhi mahitaji ya lazima katika maisha yao…tulianzisha mradi wa kulima zao la parachichi kwa kila kaya, ili waweze kujikwamua kiuchumi,’ anasema Liandala.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe, Antoni Mawata, anasema sababu kubwa ya wanafunzi kushindwa mitihani lina sababu nyingi tofauti tofauti.

‘’Mkakati tuliojiwekea katika Halmashauri ni kuhakikisha tunaelimisha familia moja moja, ili waelewe umuhimu wa elimu kwa watoto wao, maana mengine wamekuwa wakisema fedha za kuwahudumia wakiwa sekondari hawana,’’ anasema Mawata.

Umaskini ni ukosefu wa mahitaji ya msingi ya binadamukama vile chakula, maji salama, huduma za afya, mavazina nyumba kutokana na kukosa uwezo wa kuvinunua.

Umasikini wa kadiri ni kuwa na rasilimali chache zaidi, au mapato madogo zaidi kulingana na watu wengine katika jamii au nchi au hali ya wastani duniani.

Hali hii pia hujulikana kama umasikini halisi au unyonge.

Umasikini linganishi, ni hali ya kuwa na rasilimali chache, au kipato cha chini kuliko wengine kwenye jamii au nchi, au ikilinganishwa na wastani duniani kote.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughilikia masuala ya Watoto, Unicef, limekadiria kwamba nusu ya watoto wote duniani (bilioni 1.1), wanaishi kifukara.

Utafiti wa Twaweza wa mwaka 2017, umeeleza kwamba wananchi wametaja umasikini/hali ngumu ya kiuchumi inayokabili Tanzania kwa sasa kuwa 60%, huku upungufu wa chakula /njaa ukiwa 57%, elimu ni 22%.

Watoto walio katika umri wa kwenda shule wanakabiliwa na changamoto na vikwazo vya kijamii na kiuchumi. Wanakabiliwa pia na ukiukwaji wa haki za kibinadamu na vitendo vyenye madhara, ikiwa ni pamoja na ajira za watoto, ambazo zinasababisha  suala la kupata elimu kuwa gumu au kushindakana kabisa.

Mwaka 2015 na 2016, Tanzania ilikuwa mwanzilishi wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kukomesha Ukatili dhidi ya Watoto, ambao unatokana na dhamira ya kumaliza suala la ukatili dhidi ya watoto ifikapo mwaka 2030.

Aidha, watoto wanaotoka katika familia masikini, wanakabiliwa na changamoto za utofauti wa kiuchumi ambao kwa kiasi kikubwa una athiri upatikanaji wa elimu yao.