Home Latest News UMEME WA GESI WAWA SHUBIRI MTWARA

UMEME WA GESI WAWA SHUBIRI MTWARA

832
0
SHARE

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA 

MKOA wa Mtwara ni moja kati ya Mikoa inayotumia umeme utokanao na uzalishaji wa nishati ya gesi, hali inayopelekea wakazi wa mkoa huo na mikoa ya jirani kunufaika na kutumia umeme wa nishati hiyo.

Upatikanaji wa gesi na umeme wa uhakika umeweza kuongeza idadi ya wawekezaji mkoani humo, huku ongezeko la watu likipelekea uzalishaji wa nishati hiyo kuanza kusuasua na kufanya ukatikaji wa mara kwa mara, hali ambayo inalalamikiwa na wananchi  na wafanyabiashara mbalimbali.

Kusuasua huko kumetokana na kuzidiwa kwa mitambo hali inayopelekea baadhi ya huduma kukosekana ama kupatikana kwa uchache ndani ya mikoa hiyo ikiwemo mashine za kusaga, maji.

Kukatika mara kwa mara umekuwa mwiba kwa wafanyabiashara wa mabarafu, hoteli, mashine hali ambayo inaonyesha wazi kuwa lipo tatizo kubwa katika uzalishaji wa mitambo hiyo ambayo inatumia gesi.

Miaka ya hivi karibuni umeme unaotumiwa na mikoa ya Lindi na Mtwara umekuwa ukikasirisha watumiaji huku shirika la umeme Tanzania likiwa kimya bila kutoa ufafanuzi kwa wateja wake, huku watumiaji wakikumbwa na athari nyingi zitokanazo na kukatika kwa umeme hivyo kupelekea gharama za uendeshaji kuwa kubwa.

Nestory Chilumba mkazi wa Ndanda wilayani Masasi anasema kuwa, tatizo la kukatika kwa umeme limekuwa sugu na limeongeza changamoto kwa wafanyabishara wala haionyeshi kuwa nishati hiyo inazalishwa hapa mkoani.

Anasema kuwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapaswa kurahakisha marekebisho wanayofanya ili kuweza kuwaondolea adha inayowakabili wakazi wa Mkoa wa Mtwara.

“Jamani Mtwara hatuna raha na umeme yaani umekuwa kama vile mafundi wako chuo cha mafunzo VETA dakika 2 umewaka, 2 umekatika tunafahamu yapo marekebisho yanaendelea  ya kutenganisha laini lakini tunaiomba serikali wanaweza kuyafanya kwa wakati hivi sasa………

“Tunao vijana wanamiliki Gereji wanahitaji kuchomelea, Saluni, Migahawa, Stationary, Gym na miradi mingine mbalimbali inayohitaji nishati hiyo kwa staili hii wanawezaje kujikwamua kiuchumi, tena ukienda wilaya ya pembezoni hali ni mbaya  zaidi ya hapa mjini hasa Masasi na Nanyumbu………..

“Hii sasa ‘its too much’ sisi pia hatupendezwi na hali hiyo inafikia wakati hili jambo lifanywe haraka hasa ukizingatia kuwa tunakaribia katika msimu wa mvua ambao utakuwa na ugumu katika kurekebisha mitambo ya umeme wanapaswa wajue kuwa  Umeme ndio uchumi ukiyumba umeme na uchumi ndio umeyumba,”  anasema Chilumba

Anasema kuwa kitendo cha umeme kukatika mara kwa mara bila taarifa imekuwa ikikwamisha vijana wengi kufanya shughuli za ujasiliamali zinazotumia nishati hiyo hivyo kukosa mapato.

Chilumba anaongeza kuwa, wanatambua kuwa shirika hilo lina majukumu mengi lakini wanapaswa kufanya shughuli zao kwa uangalifu na kutoa taarifa kwa watumiaji wa huduma hiyo ili kuwaweka tayari hatua ambayo itawafanya wajipange.

“Sisi tunajua kuwa wanajenga kinu kingine Mnazi Mmoja lindi lakini wanapaswa kutoa taarifa na muda sasa watakaomaliza umeme kuwa kero kwa watumiaji. Unakatika mara kwa mara hali ambayo inawapa wananchi kutokuwa na imani na shirika hilo.

“Sisi ndio tulitakiwa kujidai kwa kuwa umeme wetu unazalishwa kwa kutumia gesi lakini sisi tumekuwa hatuna tofauti na mikoa mingine. Umeme umekuwa shida kuliko hata wengine wasio na vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo,” anasema Chilumba

Naye Fatuma Napome Mkazi wa Indiani Kota Mtwara Mjini anasema kuwa, tatizo la kukatika kwa umeme na ukosefu wa maji limekuwa kubwa hali ambayo inapelekea wananchi kutembetembea kutafuta maji kutokana na maeneo wanayoishi kutokuwa na visima.

Wananchi wamekuwa wakihangaika bila kuwa na taarifa yoyote juu ya kukatwa kwa maji ambapo wamekuwa wakikaa wiki mbili bila kupata maji hatua ambayo inahangaisha wananchi.

Umeme na maji vimezidi kukatika mara wakate mara warudishe hata hawaoni huruma kwa watumiaji kuwa wanatumia vifaa vitokanavyo na umeme na vinaweza kuungua bora tukose umeme kuliko maji,” anasema.

Gazeti hili lilifika kwa baadhi ya wafanyabiashara wa hoteli katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambao  wamedai kuwa, wako hatarini kupunguza wafanyakazi iwapo tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara  lililoanza mwishoni mwa mwaka jana, litandelea kutokana na kutumia  umeme wa genereta ambao ni gharama kubwa huku shiriKa la umeme Tanzania  mkoa wa Mtwara likishindwa kutoa ufafanuzi kuhusiana na hilo.

Eric Shumbusho Meneja Msaidizi hoteli ya Tifanny Diamond anasema kuwa, kukatika kwa umeme kumekuwa kukisababisha shughuli za biashara kusimama huku baadhi watumia gharama kubwa kuziendesha.

Anasema kuwa, wamekuwa wakitumia shilingi 1, 200,000 kwa kununua mafuta ili kuwasha genereta kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme hali ambayo inayowafanya washindwe kujiendesha kwa faida.

“Tanesco wajue kuwa hii ni huduma pia, tunalipa kodi na ni watumiaji wakubwa wa umeme. Hili tatizo linapaswa lishughulikiwe kikamilifu, tukiendelea tunaweza kupata athari kubwa kwakupunguza wafanyakazi ili kupunguza ongezeko la gharama za uendeshaji”

Rukia Lipanduka mmiliki wa kiwanda cha kusaga nafaka anasema kuwa, tatizo la umeme limekuwa kubwa hali inayowafanya wao kupata hasara hasa wakati ambao unataka kukoboa mahindi.

Kitendo hicho cha kukatika umeme mara kwa mara kimekuwa kikipelekea wao kuingiza hasara kubwa, kutokana na kutokuwa mbadala wa umeme hivyo ukatikaji wa mara kwa mara hukwamisha usagaji na ukoboaji wa nafaka.

“Sawa wanasema wana matengenezo lakini hauyo matengenezo yataisha lini? Tunataka kujua hatma ya sisi kuishi bila kujua hatma ya umeme maana kunatukosesha mapato maana unaweza kumwaga mahindi ya kukoboa umeme ukikatika yanahabaribika, hii ni shida kubwa kwa mkoa wa Mtwara.”

Tatizo hilo la umeme pia limetajwa  kuleta  athari kwa mamalaka ya maji safi na maji taka -MTUWASA baada ya Mhadisi wa Maji wa Mamlaka hiyo kudai wanalazimika kuzalisha maji pungufu kutokana na kukosa umeme wa   Tanesco.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mafi na Maji Taka Mtwara (MTUWASA) Mashaka Sitta, anasema kuwa, hivi sasa maji hayatosherezi kutokana kushuka kwa uzalishaji wa maji kutoka lita milioni tisa hadi lita milioni 7.5.

Anasema kuwa kushuka kwa uzalishaji huo, kunatokana na tatizo la umeme hivyo kuwalazimu kufanya uzalishaji usiku tu kwa masaa 15 badala ya masaa 24 ya awali.

Sitta alisema kuwa mitambo ya mamlaka hiyo inashindwa kusukuma maji na kulazimika kubadili ratiba za ugawaji wa maji kutokana na tatizo la umeme ambalo linawalazimu kusukuma maji masaa ya usiku tu.

“Hitaji la maji ni lita milioni 14  sasa tunazalisha million 9 kwa siku sasa milioni 7.5  maji hayatoshelezi tuna uwezo wetu ni mdogo tunazalisha lita milioni 9 kwa siku hitilafu za umeme zimeongeza tatizo katika mji wa Mtwara.

“Sasa hivi tunagawana umeme na wananchi mchana mzima. Sisi hatufanyi kazi tunapewa umeme usiku saa chache sana ambapo uzalishaji wake hautoshelezi lita tulizokuwa tukizalisha awali hali ambayo imeharibu ratiba ya watu kugawiwa maji kwa masaa 24 sasa hivi tunazalisha masaa 15 tu,” alisema Sitta

Akitolea ufafanuzi taarifa hiyo Meneja wa Shirika la Umeme Mkoa wa Mtwara Azizi Salum alisema kuwa, kutokana na hitilafu ya mtambo wamelazimika kutoa umeme kwa mgao wa vipindi vipindi. Anasema kuwa mahitaji ya nishati hiyo yameongezeka hivyo kufanya matumizi wakati wa usiku kuwa makubwa zaidi na kupelekea mitambo kuzidiwa.

“Unajua mji wa hivi sasa kuna wimbi kubwa la ongezeko la watu hata matumizi yameongezeka pia hasa inapofikia usiku matumizi huongezeka mara dufu hupelekea mitambo kushindwa kubeba mzigo hivyo kushindwa kubeba mzigo………

“Umeme upo sio kwamba watu hawapati huduma hapa na wanapata ila ndio wanapata kwa vipindi vipindi hasa kuanzia saa 12:30 hadi saa 4 mashine yetu mbovu hadi mwezi wa pili itakuwa imekamilika kwakuwa vipuri vya kuitengeneza tumesha viagiza  ili kuweza kupunguza tatizo la umeme” alisema Azizi