Home Makala ‘Umemejua’ msaada kwa wanyonge

‘Umemejua’ msaada kwa wanyonge

1515
0
SHARE

Kituo cha daladala cha SIMU 2000 kilichopo Ubungo jijini Dar es Salaam, ni mojawapo ya mfano wa kuigwa katika matumizi ya taa za umemejua (solar).

GABRIEL MUSHI

WAKATI kaya za Mkoa wa Dar es Salaam zikiongoza kwa zaidi ya asilimia 99 kwa kuunganishiwa umeme wa gridi ya Taifa, barabara za jiji hilo nazo zinaongoza kwa kutumia umemejua ‘solar’ katika matumizi mbalimbali ikiwamo taa za kuongoza magari.

Kwa mujibu wa ripoti ya Energy Access Situation (EAS) ya mwaka 2016 iliyoandaliwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) asilimia 99.3 ya kaya za mkoa wa Dar es Salaam zimeunganishiwa umeme wa gridi ikifuatiwa na mikoa ya Rukwa (91.2%) na Kilimanjaro (88.0%).

Kaya ambazo mikoa yake inashika nafasi za mwisho kuunganishiwa umeme wa gridi ni pamoja na Lindi (24.5%), Njombe (36.6%), Mtwara (38.9%) na Katavi (41.1%).  

Aidha, kaya za mikoa ambayo inatumia umemejua kwa zaidi ya asilimia 50 ni Dodoma, Ruvuma, Katavi, Mtwara, Njombe na Lindi.

Kaya za mikoa ya Dar es Salaam, Rukwa, Kilimanjaro, Kigoma, Arusha, Morogoro na Mbeya zinatumia umeme jua chini ya asilimia 20.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA), Mhandisi Mathew Matimbwi anasema barabara za Mkoa wa Dar es Salaam ndizo zinazoongoza kwa kutumia umemejua.

Anasema ingawa mkoa huo umeunganishiwa umeme kwa zaidi ya asilimia 99, bado zipo kaya zinazotumia umemejua na pia Halmashauri mbalimbali za mkoa Dar es Salaam zinatumia umeme jua katika barabara zake kwa kuwa ni nishati endelevu na ya uhakika.

Anaongeza kuwa hadi sasa barabara za Halmashauri ya wilaya ya Kinondoni ndizo zinazoongoza kwa kutumia nishati ya jua.

“Nishati hii imeanza kuingia mjini, hata Dar es Salaam, sasa hivi ufungaji wa taa za barabarani, zinazotumia umemenuru, umekuwa mkubwa.. hasa Halmashaiuri ya Kinondoni inaongoza. Sasa hivi barabara zote zinazojengwa upya ndani ya wilaya ya Kinondoni zinafungwa taa za solar.

“Taa nyingi za kuongoza magari barabarani ni za solar vilevile. Kwa mfano maeneo Bamaga, Sayansi, Mnazi Mmoja, Barabara ya Nyerere mpaka kuelekea kule Uwanja wa Ndege na Gongo la Mboto kuna taa za solar,” anasema Matimbwi aliyekuwa akizungumza kuhusu sera na sheria zinazosimamia maendeleo ya nishati jadidifu katika mafunzo maalum ya wanahabari ya nishati.

Mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam yameandaliwa na Shirika la Hivos East Africa kwa kushirikiana na kampuni ya teknolojia na habari ya Nukta Africa na kituo cha kijamii cha Energy Change Lab kwa lengo la kuongeza wigo wa kuripoti habari za nishati jadidifu zitakazowasaidia wananchi hasa wa vijini kuondokana na umaskini. 

Matimbwi anasema uhakika wa upatikanaji wa umemejua kwa mfano katika kituo cha daladala cha Simu 2000, ni moja ya sababu inayoongeza hamasa ya matumizi ya nishati hiyo jadidifu nchini.

“Wakati wa usiku mwanga unatakiwa uwepo wa uhakika kwa ya sababu ya usalama. Ndiyo maana katika kituo hicho hawakutumia taa zinazotumia umeme wa Tanesco,” anasema.

Itakumbukwa kuwa vyombo vivyorushwa angani kufanya tafiti ndivyo chimbuko la umemejua kwani vinahitaji umeme.

Matimbwi anafafanua kuwa maendeleo ya teknolojia ya umemejua imeweza kufikisha umeme mahali ambapo umeme wa gridi hauwezi kufika kwa wakati.

“Hata wananchi wa mijini, majumbani mwao wamefunga mifumo ya akiba ya umemejua ili umeme wa gridi unapokatika wasikose angalau mwanga,” anasema.