Home Makala UMOJA WA AFRIKA ULIUNDWA KWA SHINIKIZO LA MAREKANI?

UMOJA WA AFRIKA ULIUNDWA KWA SHINIKIZO LA MAREKANI?

1007
0
SHARE

NA JOSEPH MIHANGWA

WAAFRIKA hawajawahi kuunda umoja wao kwa hiari, uwe wa bara zima au wa kikanda, bila nguvu ya Ubeberu wa nje, hususani ule wa Kimarekani; kuanzia na jaribio la Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki mwaka1963, Jumuiya ya Uchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Umoja wa Nchi huru za Afrika (OAU) na hata Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni matokeo ya juhudi zilizoshindwa za kutaka kuunda Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki (EAF) lililoshindwa.  Itakumbukwa miaka michache kabla ya Uhuru wa Tanganyika, Rais wa kwanza wa Tanganyika, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alinukuliwa akisema, alikuwa tayari kuchelewesha Uhuru wa nchi yake kusubiri Kenya, Uganda na Zanzibar zipate Uhuru ili nchi hizi nne ziunde Shirikisho.

Ni yeye Mwalimu Nyerere na Rais Milton Obote wa Uganda, waliokwenda kwa Rais Jomo Kenyatta wa Kenya mwaka1963 na kumwambia: “Tuko tayari kwa Shirikisho la Afrika Mashariki” lakini Kenyatta akawabeza, hakutaka Shirikisho kama ambavyo tu Dakta Hastings Kamuzu Banda wa Malawi alivyopigana kufa na kupona kuua juhudi za Wakoloni walioondoka za kuunda Shirikisho la Rhodesia  Nyasaland kwa masilahi yao.

Afrika bado inakumbuka ugomvi kati ya Nyerere na Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkrumah, kwenye mkutano wa pili wa OAU mjini Addis Ababa, juu ya njia ya kufikia Shirikisho la kisiasa la Afrika, nusura washikane mashati hadharani.

Wakati Nkrumah akitaka Shirikisho hilo liundwe sawia kabla viongozi hawajanogewa madaraka ikawa vigumu kuyatoa ‘sadaka’ kwa Shirikisho, Nyerere alipinga vikali akisema, Shirikisho hilo lifikiwe kwa kuanza na miungano ya kikanda, likiwamo Shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.  Hoja ya Nyerere ikashinda; Nkrumah akalalama kwa Afrika kufanya kosa kumsikiliza Nyerere, kwamba kwa kosa hilo, Afrika haitaungana kamwe.

Ikumbukwe pia kwamba, wakati Mapinduzi ya umwagaji damu ya Zanzibar yakitokea, Januari12 mwaka 1964, Nyerere alikuwa mjini Nairobi akitupa karata yake ya mwisho kwa Kenyatta kuona Shirikisho la Afrika Mashariki linaundwa.

Kitu gani kilimsukuma Mwalimu kuendelea kupigania Shirikisho la Afrika Mashariki, wakati Kenyatta hakutaka?  Je, ilikuwa moyo wa umoja wa Afrika au ilikuwa kuepusha kushindwa kutekelezeka kwa hoja yake dhidi ya hoja ya Nkrumah?

Ni kwamba, wakati harakati za uhuru na juhudi za muungano kwa nchi za Afrika zikiendelea miaka ya1960, dunia ilikuwa ikipita kipindi kigumu cha vita baridi  kati ya nchi za kibepari za Magharibi zikiongozwa na Marekani na nchi za kisoshalisti za Mashariki zikiongozwa na Urusi na China.

Moja ya hofu kuu Afrika Mashariki kwa nchi za Magharibi, Marekani na Uingereza, ilikuwa juu ya Zanzibar kuwa mikononi mwa wanaharakati wa siasa za Ki-Karl Marx, kama vile kina Abdulrahman Mohamed Babu, Abdullah kassim Hanga, Salim Ahmed Salim na wengine, kwamba ingetokea hivyo, Zanzibar ingekuwa Cuba ya Afrika chini ya ushawishi wa Urusi.

Kwa hiyo, msukumo wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki ulilenga kuimeza Zanzibar ndani ya tumbo pana la Shirikisho ili isiangukie mikononi mwa Wakomunisti. Mipango yote hii iliendeshwa na kuratibiwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la kijasusi la CIA na Serikali ya Uingereza kupitia balozi zake nchini Kenya na Tanganyika.

Wala kushindwa kwa juhudi za kuundaEAF hakukuiondolea Marekani hofu hiyo, kwani uwezekano wa Urusi kuiteka Zanzibar kupitia wanaharakati wake ilikuwa bado mbichi.  Kwa sababu hii, Marekani ilibadili mbinu kwa kuhakikisha kwamba Zanzibar inaungana na Tanganyika ili visiwa hivyo vimezwe ndani ya tumbo pana la Tanganyika visifurukute.

Mkakati wa Marekani kufuatia Mapinduzi ya Zanzibar ulikuwa mpana kuhakikisha Mapinduzi hayo yanadhibitiwa.  Mikakati hiyo ilikuwa ni pamoja na kuivamia Zanzibar chini ya Mpango maalum ulioandaliwa kwa pamoja kati ya Marekani na Uingereza, uliopewa jina ‘Zanzibar Action Plan’ (ZAP).

Pili kumuua kinara wa Mapinduzi na Mkomunisti wa kutupa Zanzibar, Abdulrahman Babu pamoja na kuchochea mitafaruku ndani ya Serikali mpya.

Mbinu hizo ziliposhindwa, Marekani na Uingereza ziligeukia ushawishi wa kuundwa Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar.Mratibu Mkuu nchini Zanzibar alikuwa Balozi, gwiji la CIA, Frank Carlucci, aliyehamishiwa huko kutoka Congo ya machafuko kuja kudhibiti Ukomunisti Zanzibar na Afrika Mashariki.

Miaka ya karibuni (1987), Carlucci, aliyeweza baadaye kupanda cheo kufikia Mkuu wa CIA nchini Marekani, alinukuliwa kukiri hili akisema: “Ilikuwa lazima kwa Marekani kuzima nguvu ya Ukomunisti Zanzibar kwa kuanzisha Muungano, bila hivyo Zanzibar ilikuwa mbioni kugeuka Cuba ya Kiafrika kuweza kuambukiza Ukomunisti Afrika nzima”.

Ni kusema kwamba, juhudi za Waafrika  za kuunda Umoja kwa ujumla, mfano OAU, Shirikisho la Afrika Mashariki (EAF) na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, hazikuasisiwa na Wazalendo kwa hiari, bali kwa msukumo wa ubeberu wa nchi za Magharibi. Kwa vipi kuundwa kwa OAU kunaingia katika mkumbo huu tofauti na Muungano wa Tanzania?.

Kufuatia minyukano ya nchi za Ulaya wakati wa vita kuu ya pili, nchi hizo zilitoka zimejeruhiana, zikichechemea na kutoka damu, wakati Marekani, Urusi na China zikiimarika kiuchumi na kijeshi. Wakati huo huo Uingereza na Ufaransa zilipoteza umaarufu na hadhi ya kimataifa, ingawaje ushawishi wake barani Afrika kama nchi za makoloni, ulibakia.

Juhudi za nchi hizo kujikusanya upya na kuelekeza nguvu katika  kulinda masilahi yake dhidi ya Marekani iliyokuwa ikinyemelea kuiteka Afrika kwa njia ya ukoloni mamboleo zilikuwa zimeanza kutekelezwa. Ulaya iliitumia hofu bandia ya Afrika ya kutaka kutelekezwana dunia, ikabuni mbinu ya misaada ya danganya toto kwa kuzishirikisha nchi kwenye Jumuiya ya Uchumi ya nchi za Ulaya [EEC,sasaEU] ziweze kubakia upande wake.

Lakini kwa sababu nchi za Ulaya zilikuwa bado dhaifu, ziliendelea kuipigia magoti Marekani kwa misaada ya kufufua uchumi kupitia Mpango wake wa ‘Marshall Plan’ na kuzifanya tegemezi ndani ya mzingo wa KiMarekani.

Pamoja na utegemezi huo wa Ulaya kwa Marekani, mataifa haya katika ujumla wake, yalikuwa na jukumu la pamoja kuhakikisha, kupitia umoja wao wa kijeshi, -NATO, kwamba Ukomunisti haufurukuti, lakini wakati huo huo Marekani ikiona Afrika ilikuwa muhimu mno kuachwa mikononi mwa nchi dhaifu za Ulaya.

Na ili kuhakikisha kwamba Afrika haiangukii mikononi mwa Ukomunisti na kuzima ndoto ya Nkrumah ya kuunda Umoja imara wa Afrika, Marekani ilibuni kwa ajili ya Afrika, Umoja wa Mataifa ya Afrika (Organisation of African States-OAS), kwa misingi ile ile ya Organization of American States (OAS), kabla ya kuitwa USA.  Huo ndio ulikuwa Umoja wa Afrika wa kwanza kabla ya kubadili jina na kuwa OAU, Mei 25, 1963.

Kuundwa kwa OAU kulitishia masilahi ya nchi za Ulaya barani Afrika na kumlaumu Nkrumah kwa kuiweka Afrika mfukoni mwa Marekani. Na ili kulinda maslahi hayo,  nchi za Ulaya ziliazimia ama kuivunja kabisa OAU, au  kuhakikisha kwamba viongozi wa Kikomunisti barani Afrika, wakiwamo Nkrumah na Ben Bella (Algeria), wanafutiliwa mbali au kuondolewa madarakani.  Sambamba na mpango huo, nchi za Afrika zenye kuzungumza lugha ya Kifaransa ziliunda Umoja wake -OCAM, ili kuidhoofisha OAU na kupinga kila kitu alichopendekeza Nkrumah.

Wanaharakati wengi wa siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx waliuawa kwa msaada wa mabeberu.  Miongoni  mwa waliouawa ni Dakta Felix Moumie wa Kameruni, Pio Pinto wa Kenya na Abdullah Kassim Hanga wa Tanzania.

Dakta Moumie aliongoza Chama cha Umoja wa watu wa Kameruni (UPC), kuchukua nafasi ya Ruben Um Nyobe aliyeuawa kwa kupigwa risasi hadharani na Wafaransa, Septemba 13,1958.Novemba 3,1960, Dakta Moumie naye aliuawa kwa kulishwa sumu na kikundi cha kigaidi cha Wafaransa kilichoitwa “Red Hand”, kwa kusaidiwa na mawakala wa ndani ya Kameruni.

Ernest Oundie aliyechukua uongozi baada ya Moumie alikamatwa na Serikali ya Rais Ahidjo  Agosti19,1970na kunyongwa Januari15, 1971.

Nchini Kenya, mwanasiasa wa mrengo wa Ki-Karl Marx, Pio Pinto aliuawa kikatili mbele ya nyumba yake mjini Nairobi wakati akijiandaa kumkpeleka mtoto wake kwenye shule ya chekechea.Pinto alihariri pia gazeti mahiri la ‘The Clonicle’ lililounga mkono mapambano ya Mau Mau dhidi ya wakoloni wa Kiingereza; na aliongoza harakati kupinga kujiingiza kwa CIA katika vyama vya Wafanyakazi Afrika Mashariki kupitia kwa wakala wa Shirika hilo, Tom Mboya wa Kenya.

Kuuawa kwa Tom Mboya, Waziri wa Mipango wa Kenya, kuliashiria mfarakano kati ya Ulaya na Marekani barani Afrika. Mboya ambaye alikuwa mwanaharakati wa vyama vya Wafanyakazi Afrika Mashariki, alifadhiliwa na CIA kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi la Marekani A.F.L – C.I.O na alikuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Kenya na Afrika Mashariki. Na kama asingeuawa kwa njama za nchi za Ulaya, yeyote ambaye angechukua madaraka baada ya Kenyatta angekuwa na wakati mgumu kuubadili uchumi na siasa za Kenya wakati akiwapo.

NchiniTanzania, Mwanaharakati mwingine wa siasa za mrengo wa Ki-Karl Marx mwenye kuheshimika Afrika Mashariki, Abdullah Kassim Hanga, aliuawa 1970 baada ya kuwa kuzuizini visiwani Zanzibar tangu1967. Hanga, pamoja na wanaharakati wenzake, alishiriki kuung’oa utawala wa Sultani wa Zanzibar, Januari 12, 1964na kuteuliwa Makamu wa Rais wa Zanzibar hadi Zanzibar ilipoungana na Tanganyika. Kuuawa kwake kunahusishwa na kuendeleza “chokochoko” za Kikomunisti Visiwani kufuatia Muungano.

Alikamatwa akiwa Tanzania Bara na kupelekwa Zanzibar kujibu mashtaka ya uhaini kwa kutaka kupindua Serikali na kutaka kumuua Rais Abeid Amani Karume.  Nyerere alimrejesha Zanzibar akiamini kwamba haki ingetendeka Mahakamani, lakini badala yake akauawa kikatili bila kushitakiwa, yeye na wanaharakati wengine, kina Abdul Aziz Twala, Mohamed Abdullah Meki, Abdullah Macho na wengine.

Nchini Sudan wanaharakati wa kimataifa, Ahmed Mahgoub na Joseph Garang (si marehemu John Garang) wa Chama cha Kikomunisti cha Sudan waliomweka  madarakani Rais Jafar Numeiri mwaka1970, waliuawa na Numeiri mwenyewe mwaka 1971pamoja na Halmashauri Kuu yote ya Chama hicho, pale Rais huyo alipoanza kupoteza ushawishi na umaarufu nchini humo.

Wanaharakati wengine waliouawa barani Afrika na CIA kwa hofu ya Ukomunisti ni pamoja na Patrice Lumumba wa Congo (DRC), Ben Barka wa Morocco na Amilcar Cabral wa Guinea Bissau, wakati Nkrumah na Ben Bella walipinduliwa na majeshi ya nchi zao na kufia ugenini.

Afrika haiwezi kuungana kamwe kama itaendelea kufanya kazi kwa mipango inayoandaliwa na kupandikizwa kwake na mataifa ya nje, hasa Marekani,  kinyume na matakwa na maslahi ya Waafrika. Kihistoria, ni sera za nchi za Magharibi kuzitenga Afrika ya Mashariki pamoja na Afrika ya Kati na nchi za Kiislam za Afrika Kaskazini kwa hofu ya kujengeka Umoja wa Kiafrika/Kiarabu wenye nguvu kuweza kuzuia mataifa makubwa kupenya ndani ya Afrika.

Ukidadisi kwa makini hiki kinachoitwa ‘Ugaidi’ (terrorism) wenye chimbuko la nchi za Kiislamu dhidi ya ubabe wa Kimagharibi, ambao umesababisha Afrika ilazimishwe kutunga Sheria dhidi ya ugaidi bila kufafanua maana yake kwa mazingira yetu, ni sehemu ya mkakati huo wa kuzigawa nchi huru za Kiafrika.

Sera hizi zimekwenda mbali zaidi kwa njia ya uchonganishi na kibaguzi kwa misingi ya rangi kama ilivyo visiwani Zanzibar na Sudani, kati ya Waarabu na Waafrika. Ni kwa njia hii ya uchonganishi kwamba nchi za Ulaya na Marekani, zilimwona Kanali Muamar Gadaffi kutostahili kuongoza AU, eti kwa sababu tu ni Mwarabu na mwanaharakati wa Ki-Karl Marx na hivyo ni gaidi.

Pamoja na kujidai kwetu kutofungamana na mataifa makubwa, ukweli ni kwamba tumechagua kuwa sehemu ya ubepari kwa maangamizi yetu.  Matokeo yake ni kwa sisi kugharamia migogoro yote ya mfumo wa ubepari wa dunia; tumegeuzwa wanyama wa nguvu kazi wa mfumo huo. Tunalilia  uhuru, lakini tunafanyia kazi utegemezi; tunasumbukia neema lakini tunajijengea umasikini.  Umoja wa Afrika unafanya nini wakati wote huo?

Ni dhahiri, baada ya vita vya ukombozi kumalizika barani Afrika, inaelekea chombo hiki hakina kazi tena kutokana kwamba hakikuandaliwa tangu mwanzo kwa harakati za ukombozi wa kiuchumi. Maazimio yanayotolewa kwenye vikao vyake  yanasahauliwa au kutupwa jalalani mara tu viongozi wa nchi za Afrika wanapotua kwenye miji mikuu ya nchi  zao. Ni kwa sababu hii Afrika itazidi kuangamia chini ya Mitume wa Marekani; WB na IMF na nchi za Ulaya. Kujikomboa na hali hiyo, Afrika inatakiwa kuanzisha harakati za ukombozi awamu ya pili.

jmihangwa@yahoo.com/0713-526972