Home Makala Kimataifa Umoja wa Mataifa wamsubiri Guterres

Umoja wa Mataifa wamsubiri Guterres

750
0
SHARE

Mapema mwezi huu uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulifanyika. Uchaguzi huu unalenga kuziba nafasi ya Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Ban Ki-moon ambaye ataachia nafasi hiyo rasmi Januari Mosi, 2017. Aliyepata nafasi ya kuchaguliwa ni Raia wa Ureno Antonio Manuel de Oliveira Guterres.

Uchaguzi wake unamfanya kuwa Katibu Mkuu wa tisa, na aliweza kupita katika mchujo uliofanywa na Kamati ya Usalama ya Umoja wa Mataifa kwa kupata kura 13 za ndiyo na mbili zilizompinga. Uchaguzi huo ulifanyika Oktoba 6, 2016.

Katibu Mkuu huyu mteule alizaliwa Aprili 30, 1949 na katika maisha yake amefanya kazi za siasa na diplomasia kwa kiwango cha juu. Alikuwa Waziri Mkuu wa Ureno kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 na kisha kushika wadhifa wa Kamishna wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya Wakimbizi kuanzia 2005 hadi Desemba 2015.

Guterres alizaliwa na kukulia Ureno katika jiji la Lisbon na baba yake anaitwa Virgílio Dias Guterres (1913–2009) na mama yake Ilda Cândida de Oliveira (aliyezaliwa mwaka 1923). Katika miaka ya awali ya elimu yake amewahi kuwa mwanafunzi bora katika Ureno na alihitimu masomo ya Uhandishi wa Umeme akichanganya pia na masomo ya Fizikia. Alipata shahada yake ya kwanza mwaka 1971 na kuanza kufundisha kama Mhadhiri Msaidizi akifundisha Nadharia katika Mawasiliano ya Simu kazi aliyoifanya kwa muda mfupi na kisha kuamua kujiunga na siasa.

Gutterres anaingia UN akikabiliana na suala la mripuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ulioikabili Haiti. Ugonjw aunaoelezwa kusababishwa na wasimamizi wa amani wa Umoja wa Mataifa walioenda huko kikazi. Walinda amani hao walipelekwa Haiti wakitokea Nepal na inaelezwa baadhi yao walikuwa na vimelea vya ugonjwa huo na hawakuweza kutibu uchafu waliokuwa wakiutupa hali iliyosababisha raia wa Haiti kuhathiliwa na Ugonjwa huo. Haiti inahitaji fidia na msimamo wa Katibu Mkuu huyu mpya ni kuwa, Walinda amani wanayo kinga lakini kinga hiyo haiwaondolei wajibu wao katika kulinda maisha ya watu.

Tena anakabiliwa na shutuma za ubakaji zilizofanywa na walinda amani katika nchi ya Afrika ya Kati. Suala hili limekuwa likiibua mjadala mkubwa huku Afrika ya Kati ikihitaji Umoja wa Mataifa uwapeleke mahakamani Askari wake waliokuwa huko na wakahusika na tukio hili la uvunjaji wa haki za binadamu.

Lakini pia anakuwa Katibu Mkuu katika kipindi ambapo nchi za Afrika zinapaza sauti kutaka nazo zipewe nafasi katika Baraza la Usalama la Umoja huo, hoja ambayo imekuwa ikipingwa mara kwa mara. Afrika inadai kuwa inazo sifa za kupata kiti licha ya kuwa nayo ina changamoto kubwa moja ikiwa kupata jina la nchi ambayo itapewa nafasi hiyo.

Kuemekuwepo na harakati za mara kwa mara kwa nchi zenye uchumi mkubwa katika Afrika ndizo kudai zikabidhiwe jukumu hilo, huku nazo zikiwa zimegawanyika kutokana na ukanda. Nchi hizo ni pamoja na Afrika Kusini, Nigeria na Misri.

Lakini pia lipo dai linalohitaji ipatikane nchi iliyo na msimamo wa kiafrika na inayofanana na Afrika kwa kila jambo ili iweze kwenda kwenye Baraza hilo na kusimamia madhila ya Afrika hasa yanayosababishwa na nchi zenye uchumi mkubwa.

Ni dhahiri zama za Ban Ki-moon ndizo zinaelekea mwisho na tayari nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeanza kuangaza na kujiandaa kumpokea Katibu Mkuu huyu mpya. Afrika nayo inasubiria ujio wake huku ikiangaza kuhusu sera za Katibu Mkuu huyo katika kuimarisha amani na kukabiliana na matukio kama vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoyakabili mataiafa mengi.

Pia nchi zenye umaskini na zile zinazokabiliwa na majanga kama vimbunga nazo zinamtazama Katibu huyu zikitarajia kuwa umoja huo utakuwa karibu katika utoaji wa huduma za kijamii pale inapotokea majanga au machafuko katika nchi hizo.