Home Makala Umuhimu wa “Flow Meters” katika sekta ya mafuta, gesi,

Umuhimu wa “Flow Meters” katika sekta ya mafuta, gesi,

1134
0
SHARE

NA MWANDISHI WETU 

FLOW METER ni teknolojia ya mitambo ya kuhamisha umiliki kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi (custody transfer) inayopima kiwango cha ubora na ujazo wa mafuta na gesi pamoja na vimiminika vingine. Teknolojia sahihi ni ile inayoweza kutumika kutoa ushahidi ili kumaliza ubishi kwenye migogoro baina ya mletaji na mpokeaji, muuzaji na mnunuzi ama mlipa kodi na mtoza kodi. 

Akizungumzia kuhusu teknolojia hiyo mtaalamu wa Kampuni ya Emerson yenye Makao Makuu nchini Marekani, William Fernandes anasema teknolojia ya Flow Meters zipo za aina nyingi tofauti yake ni ubora na kutohitaji matengenezo baada ya kufungwa kwa lengo la kupunguza gharama kwa mnunuzi. 

Anasema hadi sasa Flow Meters zinazoaminika kuwa na usahihi wa hali ya juu katika upimaji wa viwango vya ubora na ujazo wa mafuta na gesi ni Micro Motion Coriolis  Flowmeters na Daniel Ultra Sonic Flowmeters. 

Mtaalamu huyo wa Emerson, Fernandes anafichua kuwa mgunduzi wa teknolojia ya Coriolis flowmeters zaidi ya miaka 50 iliyopita ni Kampuni ya Emerson inayowakilishwa hapa nchini na Kampuni ya kizalendo ya Petrogas Field Services Limited.  

Anasema Emerson imekuwa gwiji katika sekta ya ugunduzi wa teknolojia ya flowmeters kutokana na kujikita kwa muda mrefu kwani teknolojia zake nyingine zimedumu kwa muda wa miaka zaidi ya 130 hadi sasa.  

Fernandes anaeleza kuwa katika muda huo Emerson ndio waliogundua teknolojia ya Positive Displacement na baadaye kuiuza kwa kampuni nyingine duniani ambazo zinauza kwa Kampuni nyingi na mashirika mengi ya serikali teknolojia hiyo ambayo Emerson walishaacha kuwauzia wateja wao tangu walipobaini matatizo yake. 

Anasema kuwa miongoni mwa matatizo waliyobaini yanayotokana na teknolojia ya Positive Displacement ni pamoja na kuharibika mara kwa mara hivyo kumsababishia mteja gharama kubwa za kusimamisha mitambo na kuingia gharama za matengenezo na hivyo kusababisha upotevu wa mapato kwa upande wa serikali na hasara kwa wafanyabiashara wa mafuta na gesi. 

“Baada ya kubaini kwamba teknolojia hiyo inaingiza hasara kwa wanunuzi tukaamua kutengeneza teknolojia ya mita ambazo ni rafiki kwa wanunuzi zisizowaingiza katika gharama za kuharibika na kulazimisha kuzimwa kwa mitambo na zenye usahihi wa juu wa kupima mafuta, gesi na vimiminika vya aina mbalimbali.” Anasema  Fernandes.  

Katika kuhakikisha wataalamu wa sekta hiyo ya nishati na gesi wanafahamu umuhimu wa matumizi ya mita hizo za kisasa, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni za Petrogas Field Services Limited na Kilimanjaro International Inc., Greyson Kiondo anasema kampuni ya Petrogas kwa kushirikiana na Emerson wataendelea kutoa kozi mbalimbali kwa wataalamu wa sekta hiyo. 

Alisema katika kuwawezesha wataalamu wa Tanzania ili kuendana na dhana ya serikali ya awamu ya tano ya Tanzania ya viwanda Petrogas kwa kushirikiana na Emerson wameendelea na utoaji wa kozi kwa wataalamu wa sekta hiyo ili watambue faida za kutumia teknolojia mpya ya Micro Motion Coriolis  Flow Meters.  

“Kwa mara ya kwanza Emerson na Petrogas tulitoa elimu ya teknolojia ya mita  za Coriolis na Daniel Ultra Sonic, mwezi Novemba 2018, jijini Dar es Salaam ambapo wataalamu zaidi ya 50 walinufaika na mafunzo hayo ikiwemo na wateja kununua mita hizo.” Anasema Kiondo. 

Anasema mwaka huu wamepanga kufanya mafunzo mengine Aprili 29, mwaka huu ikihusisha wataalamu mbalimbali wa sekta hiyo ya nishati ya mafuta, gesi na umeme wakiongezeka kutoka 50 wa mwaka jana na kufikia zaidi ya 70 kutoka kampuni mbalimbali nchini. 

Tofauti na kongamano la mwaka jana kampuni ya Petrogas na Emerson wamejipanga kutoa uelewa mpana zaidi kwa wataalamu wa sekta hiyo nchini ili kuwawezesha kupata utaalamu wenye tija na faida kwa kampuni binafsi na mashirika ya umma na kuokoa taifa na hasara zinazotokana na matumizi ya mita zilizopitwa na wakati na ambazo hazitambuliki na wakala wa vipimo kwa mujibu wa sheria za nchi. 

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kushiriki mafunzo hayo, Meneja Uhandisi wa kampuni hiyo Baraka Mohamed Mkamba alisema kutakuwa na njia mbili za kuwapata washiriki ikiwemo kuleta maombi makao makuu ya ofisi za Petrogas zilizopo barabara ya Haile Selassie Masaki au kwa barua-pepe info@petrogasfield.com 

Faida ya Teknolojia ya Coriolis Flowmeters 

Akizungumzia kuhusu faida ya teknolojia ya Coriolis, mtaalamu wa Emerson, William Fernandes alisema teknolojia ya “Micro Motion Coriolis  Flowmeters” ni suluhisho la kudumu endapo zitatumiwa na wafanyabiashara  na wateja wao (kama vile kampuni za madini na ujenzi wa reli), mashirika ya umma na bandari zetu katika upimaji wa mafuta na gesi wakati wa kupakuliwa kutoka kwenye meli, malori, mabomba, ama matenki na kuhifadhiwa kwenye bohari kabla ya kuingizwa sokoni kwa mlaji mmoja mmoja. 

Anasema sababu za kupendekeza kufungwa kwa teknolojia hiyo ni kwamba zinafanyakazi kwa ufanisi mkubwa huku gharama zake za matengenezo zikiwa ni ndogo sana ikilinganishwa na teknolojia ya “Positive Displacement (PD)” ambayo inatatizo sugu la kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara. 

Iwapo teknolojia hiyo ya PD itaendelea kutumiwa italeta hasara kwa kampuni za mafuta na mashirika ya umma na serikali kwa upande wa mapato ya kodi. 

Anafafanua kwa undani kuwa, “sifa hizo ambazo Emerson pekee tu ndio tunazo, inawawezesha wateja wetu (muuzaji na mnunuzi)  kubaini mafuta na gesi endapo vimechakachuliwa kwa kuchanganywa na vimiminika vingine haramu kama maji au mafuta ya taa. Kukosekana Kwa Micro Motion Coriolis Flowmeters yenye ubora wa viwango vya kampuni yetu kutamsababishia mteja alipie maji, hewa, povu, matope na uchafu mwingine vilivyo ndani ya mafuta na gesi wakati wa kupakua kutoka kwenye meli ama kupokea kutoka kwa kampuni ama mamlaka nyingine,” 

Anafafanua kuwa ni muhimu kuzingatia kigezo cha Accuracy (usahihi) katika ununuzi wa flowmeters ili kutotoa mwanya wa kuibiwa ama kupunjwa katika uhamishaji wa umiliki wa mafuta na gesi. Kigezo kikingine cha kuzingatia ni kwamba siyo kila mtengenezaji wa Coriolis flowmeters amethibitishwa kuwa na hadhi ya kutengeneza na kufunga mitambo inayokidhi viwango vya kimataifa vya mizani na vipimo (Custody Transfer Approved).  

Kigezo hiki ni muhimu sana kwani huondoa migogoro ya kisheria juu ya mizani na vipimo (legal metrology) ambayo inaweza kujitokeza mara kwa mara katika uagizaji na upokeaji wa mafuta na gesi baina ya serikali na Kampuni kubwa za kimataifa kwa upande mmoja na baina ya Kampuni za mafuta nchini kwa upande mwingine.  

Fernandes anaongeza kwa kusema, “pamoja na ubora wake, Coriolis flowmeters zote hazitengenezwi kwa usawa kwa sababu kampuni zinazidiana kiteknolojia na uzoefu haswa kama sio wagunduzi na waasisi wa teknolojia husika. Ni sawa na kusema kwamba simu-janja zote hazilingani kwa ubora. Mnunuzi ataokoa gharama kubwa sana akifungiwa teknolojia ya flowmeter na Kampuni moja tu yenye ujuzi, uzoefu wa miaka mingi, na uwezo wa kifedha wa kusanifu, kuunda, kutengeneza, kujenga, kufunga, kukabidhi, na kuihudumia mitambo hiyo na kuchukua dhamana na wajibu wa kuitunza badala ya kutumia kampuni za mchanyato wa teknolojia (systems integrators) zinayokusanya utitiri wa mitambo na vipuri kutoka watengenezaji mbalimbali na kukabidhi mfumo mchanyato kwa mteja na kuondoka. Pasipo umakini mkubwa, mteja atajikuta anataabika wakati wa matengenezo baada ya kipindi cha uangalizi kuisha na kukabidhiwa mtambo na kampuni ya mchanyato wa teknolojia. Kimsingi, mteja ataepuka gharama lukuki kabla, wakati, na baada ya kufungwa kwa mfumo wa mita za mafuta na gesi endapo atachagua miongoni mwa kampuni zinazotengeneza zenyewe chini ya nembo zao Coriolis flow meter, flow computer, valves, smart transmitters, densitometer, gas chromatograph, prover, pamoja na skid.” 

Anaelimisha zaidi Fernandes kwa kusema, “upotevu wa mafuta na gesi kwa njia za wizi ama miundombinu mibovu vinaweza kuepukwa sasa kwa kutumia mitambo ya Coriolis flowmeters. Zipo kampuni chache sana duniani zinazoweza kumpa mteja na wadau wake mfumo wa mita wenye uwezo wa kuona mwenendo mzima wa mihamala ya mafuta na gesi inavyoendelea kufanyika wakati wowote kupitia kwenye kompyuta na simu-janja bila mteja na wadau wake kama mamlaka za serikali za udhibiti, usimamizi, uchunguzi, na kukusanya kodi kulazimika kwenda kwenye meli ama kupanda ngazi ndefu kueleka angani kuchungulia ndani ya matenki makubwa na marefu kwenye bohari zinazopokea na kutoa mafuta na gesi. Teknolojia ya Micro Motion Coriolis Flowmeter ina uwezo wa kufanya hayo yote na zaidi kwa sababu itabaini kama mabomba ama matenki ya mafuta na gesi yametoboka kwa hujuma ama ubovu wa miundombinu.  

Anahitimisha Fernandes, “kikubwa zaidi, teknolojia ya Micro Motion Coriolis Flowmeter imetumika kutoa ushahidi na kumaliza ubishi mahakani duniani kote kwenye migogoro baina ya mletaji na mpokeaji, muuzaji na mnunuzi ama mlipa kodi na mtoza kodi”. 

Historia ya Petrogas Field Services Limited 

Akizungumzia kuhusu historia ya Petrogas, Kiondo alisema kampuni hiyo ni ya kizalendo kwa asilimia 100 ikiwa imeanzishwa mwaka 2013 jijini Dar es Salaam. 

“Tulianza kwa kutoa mafunzo na ushauri kuhusu masuala ya sekta ya mafuta na gesi lakini kwa sasa tumefanikiwa kuwa wasambazaji na wafungaji wa mitambo na vipuri vinavyotokana na sekta hiyo kwa kushirikiana na Emerson. Tunaendelea kutoa mafunzo, ushauri, huduma za kihandisi, mitambo, vipuri na teknolojia nyingine katika sekta za nishati ya umeme, mafuta, gesi, bandari, madini, na viwanda vya kusindika na vinginevyo kwa kushirikiana na kampuni nyingine za kimataifa tunazoziwakilisha Tanzania zinazotengeneza mitambo na vipuri pamoja na zile zinazotoa ushauri, mafunzo, huduma za kihandisi, na ujenzi kwa viwango vinavyotambulika na kukubaliwa na kampuni kubwa za nje zilizo nchini Tanzania katika sekta husika”, anasema Kiondo. 

“Petrogas imejiandaa vizuri katika kuhudumia sekta ya viwanda inayokuwa kwa kasi chini ya Serikali ya Rais John Magufuli. Tuna uhakika wa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda kuja Tanga, Tanzania na katika ujenzi wa mitambo ya kuchakata gesi asilia mkoani Lindi kwa kutumia mitambo ya kisasa ya Micro Motion Coriolis  Flowmeters na Daniel Ultra Sonic Flowmeters ambayo itazuia taifa kupunjwa ama kuibiwa mapato katika uhamishaji wa umiliki wa mafuta na gesi kutoka kwa muuzaji kwenda kwa mnunuzi”, anamalizia Kiondo.