Home Habari kuu Umuhimu wa kujenga vijana wenye maadili, wazalendo

Umuhimu wa kujenga vijana wenye maadili, wazalendo

332
0
SHARE

Na ANNA HENGA

TAKWIMU zinaeleza vijana duniani kote wanafikia idadi ya bilioni 1.2 ambao ni sawa na asilimia 16 ya watu wote.

Idadi hii inakadiriwa kuongezeka hadi kufikia bilioni 1.3 mwaka 2030 kama ilivyoelezwa na Malengo Endelevu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa.

Hapa nchini idadi ya vijana inakadiriwa kuzidi asilimia 50 kulingana na takwimu zilizopo na tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika. Hapa ndipo tunapopata uhalali wa hoja yetu juu ya umuhimu wa kujenga vijana wenye maadili, wazalendo na wanaoheshimu haki za binadamu hapa nchini.

Kwa kuwa vijana ndio msingi wa taifa lolote duniani na ndio tumaini la mafanikio kwa maendeleo ya leo na kesho, basi kama taifa hatuna budi kuandaa mazingira wezeshi na vijana kuwa washika bendera, waongoza njia na wachochea mabadiliko ambayo yatasababisha taifa letu kupata maendeleo kwa kasi na kujikwamua kutoka uchumi wa sasa kuelekea wa kati ambao ndio ndoto yetu na ya Serikali ya awamu hii ya tano.

Kwa sababu hizo, tuna haja sasa ya kuandaa taifa la vijana wenye maadili kwa kuwa maadili ndiyo nguzo ya taifa lolote endelevu.

Maadili ni kanuni, miongozo au taratibu zinazotambulika kuwa nzuri na muhimu kwa jamii fulani na ndani yake hubeba nidhamu, heshima, upendo, utu n.k.

Kimsingi maadili huathiri mwenendo mzima wa tabia ya mtu. Ni vema tukajenga maadili ya vijana kwanza, ili kuwafanya watambue misingi ya taifa lao.

Maadili yatatufanya  tujue ni taifa gani tulilo nalo kwa sasa, ni kizazi kipi tunakijenga na ni taifa gani tutakuwa nalo baada ya leo.

Ikiwa taifa halitajengwa na maadili imara basi litazalisha kizazi cha ovyo na kizazi hicho ndani yake kitatoa viongozi wa ovyo na maisha ya watu wa taifa hilo yatakuwa ya ovyo pia. 

Inawezekana matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa tuliyonayo sasa Tanzania, yanatokana na misingi mibovu ya vijana wa zamani ambao hawakujengwa katika maadili sahihi.

Vijana wetu tutakapowajenga vyema kimaadili, itasababisha utii na heshima kwa misingi ya utu na haki za binadamu. Mtu yeyote mwenye maadili mema hawezi kuzipuuza haki za watu wengine.

Hivyo,ikiwa vijana wa Tanzania watajengwa katika misingi ya kuzijua na kuziheshimu haki za binadamu, italeta tija katika maendeleo ya taifa letu

Kwa kuwa haki za binadamu zinagusa kona zote za maisha ya binadamu, kuwawezesha vijana kuzijua na kuziheshimu haki za binadamu ni njia bora  ya kuwaandaa viongozi wa baadaye watakaokuwa na mtazamo chanya juu ya haki na usawa.

Pia,itawezesha kukuza sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni kwa kuwa haki za binadamu zinazungumza kuhusu yote hayo.

Ukisoma vema Sera ya taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, inalenga kuwainua vijana na kuwafanya kuwa waelevu, wenye hamasa na uthubutu kuhusiana na mambo mbalimbali yanayopelekea maendeleo  binafsi na ya taifa.

Hili halitawezekana ikiwa vijana hawa hawatakuwa na misingi mizuri ya kutambua haki zao, wajibu wao na fursa zilizopo nchini mwao.

Itapendeza sana ikiwa kila jambo tunalotaka kulitekeleza katika jamii yetu tukaangazia misingi ya haki za binadamu  kama vile; usawa wa kijinsia, uhuru wa mtu binafsi kuamua juu ya mambo yake binafsi, ulinzi wa utu wa mtu bila kujali hali yake ya kiuchumi au hadhi yake katika jamii husika.

Kwani jamii yetu itadhurika na nini tukisema kama taifa tunatakiwa kuwahamasisha wasichana na wanawake kushiriki michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na mingineyo? Au tukisema ajira zitolewe kwenye misingi ya usawa kwa kujali ufanisi na weledi pasi na kujielekeza kwenye jinsia ya mtu tutapungukiwa nini? Je, tutakuwa tumetengeneza taifa la namna gani ikiwa kijana ataamini kwa sababu ya jinsia yake au hali yake ya kifedha au cheo cha mzazi wake ndio sababu yeye anastahili kupata kitu fulani na mwingine hastahili?

Au Serikali ikitaka kufanya uwekezaji bila ya kufanya tathimini ya mazingira na madhara kwa umma, kisha uwekezaji huo ukaleta madhara ya kiafya kwa wananchi, je itakuwa sawa? Hio ndio maana ya kufuata na kuheshimu misingi ya haki za binadamu. Tunatakiwa kulizungumzia suala hili la haki za binadamu kwa upana zaidi kuliko kulitazama kama ni suala la wapinga Serikali au wapinga maendeleo. Hakuwezi kukawa na maendeleo bila ya kuziheshimu haki za binadamu.

Maendeleo yote yanaletwa na watu kwa ajili ya watu, sasa kwanini tusijenge misingi ya kuwalinda watu? Lakini hili litawezekana tu ikiwa kizazi chetu tutaanza kukilea katika maadili ya kuziheshimu haki za binadamu na hivyo, kuwafanya waone hilo ni suala la lazima na kuamini kwamba wana wajibu wa kulielezea, kulitetea na kulilinda kama tunu na msingi wa taifa letu.

Hebu tuzieleze haki za binadamu kama tunavyozielezea ilani za vyama vya siasa, tuziwekee mipango, mikakati na mbinu za uenezi ambazo zitafanya kila mtu kujua haki zake na kuheshimu haki za wenzake.

Kama taifa, tunatakiwa tukiri kwamba tumelenga kuwaandaa vijana wetu huko nyuma na ndio anguko letu la leo ambapo tuna kizazi cha vijana ambao hawana uelewa sahihi wa maadili ya taifa lao, hawana mioyo yenye utu na ndio maana matukio ya ukatili na uhalifu  yanaongezeka.

Lakini pia kasoro yetu ya kutokuwaandaa vijana wetu vema kwenye suala la maadili na haki za binadamu ndio chanzo cha viongozi wabovu na wasiofuata sheria, kanuni na taratibu za nchi zilizowekwa na Bunge na mamlaka zingine za nchi.  

Leo hii kila kiongozi ni msemaji wa taifa, anaongea analojisikia bila kujali liko sawa kisheria au atakuwa amemvunjia mtu mwingine haki zake. Kwa kuwa yeye ni kiongozi basi amepata kinga ya kusema chochote.

Hii sio sawa kwenye nchi ya watu waliostaarabika, nchi inayofuata misingi ya kidemokrasia, utawala wa sheria na utii wa misingi ya haki za binadamu.

Ili tuweze kujenga taifa imara, haja ya kuwaandaa vijana wetu kuanzia leo ni muhimu sana, ili kesho yao iwe bora zaidi ya kesho yetu ambayo inatugharimu sana.

Hatuwezi kuwa na vijana wenye uzalendo kwa taifa lao, ikiwa hawatakuwa na maadili na heshima juu ya misingi ya utu. Kama taifa tunawajibika kuwaandaa vijana wetu katika maadili bora ya kitanzania na kuwafundisha kuziheshimu haki za binadamu ili tuifikie jamii yenye haki na usawa.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC). Anapatikana kwa namba; 0765 471 006