Home Uchambuzi UMUHIMU WA KUTENGANISHA CHAMA NA SERIKALI

UMUHIMU WA KUTENGANISHA CHAMA NA SERIKALI

2219
0
SHARE

NA HILAL K SUED

Takribani miaka saba iliyopita wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010, niliwahi kuandika katika gazeti hili kwamba chama tawala (CCM) bado kinajiona kiko katika zile enzi za mfumo wa demokrasia wa chama kimoja, enzi za chama kushika hatamu katika masuala yote ya nchi pamoja na maisha ya wananchi.

Hivyo mfumo wa demokrasia ya ushindani, mfumo ambao una kanuni na miiko yake kwa lengo la kuleta haki na usawa kwa vyama vyote, bado ulikuwa ni kitendawili kikubwa kwa chama hicho ingawa sahihi zaidi ni kusema kwamba kilikuwa hakiutaki na hilo limeendelea hadi leo. Naweza nikasema sasa hivi hali hiyo imezidi.

Kuiheshimu miiko hiyo CCM inaona ni sawasawa na kujipatia tiketi ya kutokomea nyikani bila ya matumaini ya kurudi. Na hali inakuwa mbaya zaidi pale mgombea mmoja wa urais ni rais aliye madarakani (incumbent) kama tulivyoona katika chaguzi za 2000 na 2010.

Bila shaka CCM ilipata somo kutoka kwa kilichokuwa chama swahiba (UNIP) cha Zambia ambacho katika uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1991, kiongozi wa chama hicho na aliyekuwa rais wa nchi, Mzee Kenneth Kaunda ambaye aligombea nafasi ya urais alishindwa na mpinzani wake Frederick Chiluba (sasa marehemu) wa chama cha MMD.

Kwa kukumbusha tu katika kampeni zile, Kaunda mwenyewe alisisitiza kwa wapambe wake kufuata miiko na maadili ya demokrasia ya vyama vingi, alikataa matumizi ya vyombo vya usafiri vya Serikali katika kampeni zake na kadhalika. Hivyo vyama vyote viwili vikuu (UNIP na MMD) vilifanya kampeni katika hali ya usawa kabisa.

Aidha, inadaiwa hata baada ya upigaji kura kumalizika na kuonekana kila dalili za yeye kushindwa, alikataa wito/ushawishi wa wapambe wake wakuu kufanya kile baadhi ya nchi barani humu hufanya, kupindua matokeo na yeye kutangazwa mshindi.

Hata hivyo, huenda hakufanya hivyo kwa sababu utamaduni huo haukuwepo kwa kuwa Zambia ilikuwa ni nchi ya kwanza barani Afrika kufanya uchaguzi chini ya demokrasia ya vyama vingi. Lakini hakuna nchi nyingine iliyotaka kuiga hayo bali kuwa funzo kubwa kwa vyama tawala vikongwe vingine barani Afrika kutofanya makosa kama yale, ya kusimamia miiko, kanuni na maadili ya demokrasia ya vyama vingi. Viliona huko ni kujinyonga kweupe!

Mbali na CCM ambayo ilitikiswa sana na NCCR-Mageuzi katika uchaguzi wa 1995 pamoja na kuikataa miiko hiyo, huko Kenya nako katika uchaguzi wao wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, Rais Daniel Arap Moi wa chama tawala cha KANU alipita kwa tabu, kwa kupata asilimia 35 ya kura yaani chini ya nusu ya kura zote. Wakati ule sheria yao ya uchaguzi ndiyo ilivyokuwa, kwa sasa hivi isingewezekana uchaguzi lazima ungerudiwa.

Lakini kama nilivyosema katika nchi nyingi barani Afrika, bado hali ni hiyo hiyo, hata Afrika ya Kusini ambayo ilipata utawala wake wa walio wengi takriban miaka 20 iliyopita. Katika uchaguzi wa 2014 nchini humo hali kama hiyo ilijitokeza.

Chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), kilitoa malalamiko makali kwa Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo kikilalamikia kwamba mgombea wa ANC, Rais Jacob Zuma alikuwa akitumia magari na ndege za Serikali katika kampeni.

Hapa Tanzania katika vyama vya upinzani vimekuwa vikilalamika kwamba chama tawala kilikuwa kinatumia mali na nyenzo nyingine za Seikali katika kampeni hasa zile za urais. Kwa mfano mwaka 2010 vililalamika kitendo cha mke wa rais, Salma Kikwete kutumia ndege ya Serikali kwenda mikoani kumfanyia kampeni mume wake na hapo hapo kupokelewa uwanja wa ndege na wakuu wa Serikali (Mkuu wa Mkoa na maofisa wengine wa Serikali).

Majibu ya tuhuma hizi yaliyotolewa na Meneja wa Kampeni ya CCM, Abdulrahman Kinana, kwamba ndege ilikuwa imekodiwa na CCM, hayakuwa ya kuridhisha kwa sababu hakutoa ushahidi thabiti wa malipo hayo.

Yote haya yanaonyesha kwamba ule mstari unaotakiwa kutenganisha chama tawala na Serikali yake umeshindikana kuandikika takriban robo karne ya demokrasia ya vyama vingi. Kuna watendaji wakuu wa chama hicho tawala ambao bado wanapenda kuonekana kama watendaji wa Serikali.

Si kwamba tu wangependa kauli zao za kichama zichukuliwe kama maagizo kwa Serikali, bali pia hata wangependa kuwaaminisha wananchi kwamba miradi mbalimbali ya Serikali inayotumia fedha za walipa kodi au za misaada kutoka nje ionekane inatokana na nguvu au ufadhili wa chama yaani bila uwepo wa CCM, miradi hiyo hakuna.

Pengine hii ni kujaribu kujipatia unafuu wa kujitangaza kisiasa na kujiimarisha kwa kupitia mgongo wa Serikali katika lengo la kuvipiku vyama vya upinzani.

Miaka michache iliyopita katika ziara za kichama katika maeneo mbalimbali huko mikoani, Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, alikuwa akikagua miradi ya maendeleo ya Serikali kwa kile alichosema kusimamie ilani (na si tena ahadi) ya uchaguzi ya chama hicho.

Katika ziara yake, moja runinga zilimuonyesha akikagua majengo ya ziada ya hospitali ya Serikali ya mjini Tabora na kuanza kuwahoji kwa namna ya kuwawajibisha wakandarasi na watendaji wakuu wa Serikali ya mkoa kuhusu ucheleweshaji na ubovu wa kazi yenyewe. Kazi hiyo ingefanywa na rais, waziri mkuu au waziri yeyote wa Serikali isingeleta shida.

Lakini hivi karibuni baada ya ujio wa Rais John Magufuli, angalau mwanga ulionekana wa kutenganisha chama na Serikali iwapo tu angekisimamia kwa dhati kile alichokisema.

Mwaka uliopita akihutubia mkutano mmoja mjini Singida pamoja na kwamba haikuwa katika njia ya wazi, alionyesha kusisitiza masuala ya chama yawe mbali na yale ya Serikali. Yalikuwa matamshi yaliyobeba kila ishara za kuwa mtihani mkubwa kutokana na hali ilivyozoeleka.

Alisema yeye ni rais wa Watanzania wote na kwamba atawatumikia bila kuweka itikadi ya chama na kuwataka watendaji wengine wafanye hivyo. Alisisitiza mikutano yake na wananchi itakuwa ya kiserikali tu na kuwataka viongozi wa chama wakae mbali.

Ulikuwa mwanzo mzuri ingawa ulionekana mtihani mkubwa kama nilivyosema. Wiki mbili tu baadaye katika mkutano wake mikoa ya Kanda ya Ziwa, Rais Magufuli alionekana jukwaani akiwa na viongozi kadhaa wa chama chake na kuna mmoja aliruhusiwa kuhutubia kuhusu masuala ya upotevu wa fedha za chama.

Na hali iliendelea kuwa hivyo, makada wa chama katika sare zao wamekuwa wakijazana katika majukwaa ya mikutano yake.

Hata hivyo, mtihani mkubwa utakuwa wakati wa kampeni za uchaguzi ujao (2020) iwapo ataamua kugombea. Akisimamia alichokisema basi tutarajie usawa wa vyama katika kampeni. Lakini masuala kama haya yanatakiwa kusimamiwa na Msajili wa Vyama vya Siasa chini ya Sheria ya Vyama ya 1992.

Kifungu 5(1) (i) cha Sheria hiyo, kinavitaka vyama vya siasa kuepuka kutumia mamlaka, rasilimali za Serikali, vyombo vya dola au wadhifa wa kiserikali, kisiasa au ufadhili wa nje ama wa ndani kwa namna yoyote ile ili kukandamiza chama kingine.

Na kwa upande wake Msajili wa Vyama Vya Siasa, Jaji Francis Mutungi baadaye alikuja na taarifa ya kukemea kauli alizoziona ni ‘kali na zisizofaa’ za viongozi wa Chadema za kutaka kufanya mikutano na maandamano na kutaja vipengele kadhaa vya Sheria ya Vyama ya 1992 anayoisimamia.

Lakini aliacha kutaja vipengele vingine vya sheria hiyo hiyo inayokataza chama cha siasa kutumia nyenzo na rasilimali za Serikali katika masuala yasiyo ya kichama.

Angalau rais aliyemtangulia Jakaya Kiwete aliwahi kukerwa na uwepo wa makada na wanachama wa chama chake katika ziara zake za Serikali.

Mwaka 2014 akikagua mafuriko katika bonde la Jangwani, Dar es Salaam Kikwete aliwageukia wafuasi wa chama chake waliokuwa wamejazana hapo wakiwa katika sare za chama na kuwaambia waondoke, kwani shughuli ile haikuwa mkutano wa chama na aliwahoji iwapo walikuwa hawana kazi ya kufanya.