Home Habari Umuhimu wa sekta ya tatu ya umma katika maendeleo

Umuhimu wa sekta ya tatu ya umma katika maendeleo

573
0
SHARE

Na ANNA HENGA

HIVI karibuni nchi imeshuhudia mabadiliko ya sheria inayosimamia. Asasi za kiraia pamoja na sheria zingine saba. Katika mjadala mzito baada ya kuletwa kwa mabadiliko ya sheria hii, wengi wetu walikuwa wakijiuliza ni nini maana halisi ya asasi za kiraia na umuhimu wake katika maendeleo.

Kabla ya kuangalia umuhimu wa asasi za kiraia ni muhimu kujikumbusha historia ya hizo asasi. Historia ya asasi za kiraia inaanza kabla ya uhuru ambapo jamii zilikuwa zikiishi kwa kusaidiana na kulikuwa hakuna Serikali kwa mfumo huu kama ilivyo leo.

Wakati wa ukoloni, watu walikuwa wakikusanyana pamoja kutafakari hali waliyonayo ya kutawaliwa na wakoloni na kujifariji pia kujadiliana namna ya kuondokana na hali ile.

Karibia na uhuru baadhi asasi za kiraia ziligeuka kuwa vyama vya kupigania uhuru pamoja na masilahi mbalimbali mfano Tanganyika African Association, Tanganyika Farmers Association, vyama vya kutetea wafanyakazi na kadhalika.

Kukua kwa asasi za kiraia baada ya uhuru kulikuwa kwa ajili ya huduma zaidi. Ifahamike kuwa zipo aina mbili kuu za asasi za kiraia nazo ni asasi za kutoa huduma na zile za utetezi. Asasi za huduma ni zile zinazotoa huduma moja kwa moja kwa wanufaika kwa mfano kujenga shule, kuchimba visima, kusomesha watoto yatima, kuwa na vituo vya watoto yatima au walioko kwenye mazingira hatarishi na kadhalika.

Asasi za utetezi ni zile zinazotetea kuwepo kwa huduma mbalimbali kama shule bora, maji safi, kuwepo kwa sheria, sera na mienendo katika jamii yenye ustawi, haki na amani.

Kwa hiyo kwa miaka ya 1961 hadi 1980 asasi aina ya kwanza ndio zilizokuwa zimepamba moto. Mwanzoni mpaka katikati ya miaka ya 80 kulikuwa na mtikisiko wa uchumi nchini, baada ya vita vya Kagera pamoja na njaa iliyoikumba nchi yetu miaka ile.

Katika kujikwamua na hali hiyo nchi yetu ilifanya mabadiliko makubwa hususani katika sekta ya umma. Watu wengi walianzisha asasi za kiraia na pia kuwa wajasiriamali. Kipindi hicho ndicho huwa kinatamkwa kama ‘mushrooming of NGOs in Tanzania’ au kwa kiswahili kukua kama uyoga kwa azaki nchini.

Pia ikumbukwe mwaka 1984, nchi yetu ilifanya mabadiliko ya tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977, ambayo yaliweka hati ya haki za binadamu kwenye Katiba.

Kuwekwa kwa hati hiyo ya haki za binadamu pamoja na kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, kulisababisha asasi nyingi za utetezi kuanzishwa kutetea haki kwa mujibu wa Katiba.

Sheria zilizokuwa zinatumika kusajili azaki zilikuwa ni anuai ikiwemo sheria ya makampuni, sheria ya vyama vya kijamii, sheria ya udhamini na kadhalika. Mpaka mwaka 2002, kulikuwa hakuna sheria iliyokuwa inaratibu asasi za kiraia.

Mwaka huo 2002, ilipitishwa sheria moja iliyokuwa na lengo la kuziratibu azaki hizi. Kwa kuwa kulikuwa na azaki zilizokuwa tayari zimeshasajiliwa, kulikuwa na kifungu kilichokuwa kikizipa asasi hizo fursa ya kuendelea kusajiliwa na sheria zingine lakini pia kufuata masharti ya sheria ya asasi za kiraia (NGOs Act). Hii ilikuwa inaitwa ‘certificate of compliance’ kwa lugha ya kigeni.

Umuhimu wa asasi za kiraia haufichiki; kwanza asasi zimekuwa zikisaidiana na serikali bega kwa bega kuchangia maendeleo ya nchi kwa njia ya kutoa huduma mbalimbali mfano kujenga shule, kutoa elimu kwa umma, kutoa msaada wa sheria kwa wananchi na pia kutetea kuwepo kwa maendeleo kwa njia ya uchechemuzi.

Si hayo tu asasi za kiraia zimekuwa chachu kwani sekta hii huitwa sekta ya tatu yaani sekta ya umma ikiwa ya kwanza, sekta binafsi ikiwa ni ya pili na hii ikiwa sekta ya tatu katika mfumo wa utatu katika maendeleo.

Vilevile, sekta ya asasi za kiraia imechangia kwa kiasi kikubwa kulipa kodi kwani imekuwa ikiajiri maelfu ya wananchi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali. Si hivyo tu azaki zimechangia kutoa ajira nyingi kwa vijana na wanawake ambao walikuwa wameachwa na mfumo wa umma wa ajira.

Changamoto ambazo zimekuwa zikizikumba asasi za kiraia ni pamoja na zile za kukosa fedha za kujiendesha kwani nyingi zimekuwa zikitegemea michango ya wanachama na wahisani ambao wakati mwingine michango hiyo hukosekana kwa vile ni suala la hiyari kutolewa kwa fedha hizo.

Shime watanzania waanze kuona umuhimu wa kuchangia asasi hizi kwani zinasaidia wananchi sana. Changamoto nyingine za azaki ni kutokueleweka hasa zinapokuwa zinafanya utetezi, wengi hufikiri kazi ya azaki ni ya watu wa nje na kusahau kuwa haki ni stahiki za kila binadamu hivyo sio suala la kimagharibi, bali ni maisha halisia.

Hitimisho; kwa kuwa zoezi la kusajili upya limeshaanza, ni vyema kwa wananchi kuendelea kuziunga mkono asasi hizi na pia asasi kuendelea kujitolea kuwasaidia wananchi. Na katika zoezi linaloendelea la kusajili upya, natoa wito kwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuendelea kuzilea hizi kwani mchango wake ni muhimu kwa ustawi na maendeleo ya jamii.

Pia ni katika kutekeleza haki ya kukusanyika na kujumuika kama ilivyoainishwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyorekebishwa mara kwa mara.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).