Home Makala UPIGAJI KURA NI HIYARI, HAKI AU WAJIBU?  

UPIGAJI KURA NI HIYARI, HAKI AU WAJIBU?  

5732
0
SHARE

NA CASTORY BENEDICT


NITANGULIE kwa kueleza maana za maneno msingi yanayopatikana katika kichwa cha makala haya ambayo ni kura, wajibu, hiari na haki.

Kura ni karatasi ambayo hutumika katika zoezi la uchaguzi na karatasi hiyo ndio mpigaji wa kura hutumia kuonyesha amemchagua mgombea fulani na sio mwingine.na vilevile kura hutofautiana kadiri ya mazingira na chaguzi.

Wajibu ni kama hali ya kuaminika katika jambo fulani ambalo unalazimika kulitenda kwa faida bianfsi, faida ya mtu mwingine, jamii au kikundi fulani.

Wengi wetu tunaelewa maana ya neno ‘hiari’ kuwa ni hali ya kutenda au kufanya jambo pasipo shuruti au msukumo mara nyingi wa kutoka nje, na kinyume chake basi ndio maana ya lazima.

Neno la mwisho ambalo ni ‘haki. Ukikutana na swali haki ni nini? Unaweza kutoa majibu mbalimbali lakini kimsingi neno haki linaweza kutafsiriwa katika mitazamo mbalimbali mathalani kimaadili.

Katika mtazamo huo haki ni hali ya kutenda na kuamua kwa kuzingatia kanuni za maadili mema na sahihi. Kutenda kwa kuepuka yaliyo maovu au mabaya; au kutenda kwa kutimiza wajibu katika jamii.

Naomba nikiri kuwa maneno haya yana changamoto kuyaeleza kiundani katika lugha ya Kiswahili basi lengo kuu lilikuwa ni kudadavua maana za maneno ayo ili kuweka andiko ili kuwa lenye kueleweka zaidi.

Hivyo basi makala haya yanalenga kuibua uelewa, maswali na tafakuri juu ya uhusiano kati ya haki, kupiga kura na uhuru. Je kupiga kura ni haki zaidi kuliko wajibu?

Je mwananchi mwenye sifa za kupiga kura ana haki ya kuamua kutokupiga kura? Je wanaoamua kutokushiriki kupiga kura wanapoteza nini katika jamii wanayoishi? Je aliyetumia uhuru wake kutokupiga kura anapoteza haki zipi nyingine za msingi?

Nisiwachoshe kwa maswali zaidi lakini naamini maswali haya ni muhimu sana katika kutafakari andiko ili fupi.

Kwa kuzingatia dhana ya haki, uhuru na wajibu basi suala la kupiga kura linajipambanua kuwa ni wajibu zaidi kuliko haki na hivyo si la hiari kwani wajibu si hiari.

Kwakuwa binadamu tunaishi katika jamii kwa lazima yaani si kwa hiari basi mantiki hiyo inasababisha kila binadamu kupaswa kushiriki katika ustawi wa jamii kwa lazima maana jamii inapostawi ndio ustawi wa watu mmoja mmoja pia unatokea na kuendelea.

Hivyo kwakuwa katika kila jamii kuna uongozi ambao ndio unaendesha gurudumu la maendeleo ya jamii husika basi kila mtu mwenye sifa stahiki ana wajibu wa lazima wa kushiriki kuchagua uongozi katika jamii husika.

Pamoja na changamoto nyingine mbalimbali za masuala ya uchaguzi shindani  umuhimu mkubwa wa watu kupiga kura unabaki kuwa vile vile maana wengine hudiriki kutoa tafadhali na visingizio mbalimbali kama vile sitopiga kura kwasababu ya foleni kubwa, kwasababu uchaguzi sio wa haki n.k.

Sikusudii kupingana na uzito au wepesi wa visingizio hivyo bali nataka kujenga fikra kuwa pamoja na sababu hizo zote, kuacha kupiga kura si suluhisho hata chembe bali naweza kusema ndio linaongeza matatizo mengine zaidi.

Tukisema kupiga kura ni haki zaidi basi tutakubaliana kuwa kutokupiga kura pia ni haki maana haki haiwezi kuwa lazima maana mwenye haki hulani anaweza kuamua kutokuitumia haki yake.

Hivyo linapokuja suala linalopelekea ustawi wa jamii kwa ujumla nafikiri linapaswa kutokuwa la hiari zaidi bali wajibu wa kila mmoja.

Kwakuwa tayari fikra zetu unaelewa kuwa kutokupiga kura ni haki yetu pia hata pasipo sababu za msingi na tunaamini kuwa wengine watatuwakilisha katika kuchagua viongozi na serikali, basi hebu tujiulize wakati wa kulalamika pale uongozi ambao hatukutaka kushiriki kuchagua unapoenda kinyume na matakwa yetu tunajisikiaje?

Je malalamiko yetu yanapata msingi au uhalali upi ikiwa hatukupiga kura? Je tunaelewa nini kuhusu uhuru na wajibu? Kama tunatumia uhuru wetu kutokuchagua basi tuanze kuelewa kuwa kwa kufanya hivyo tunapoteza haki ya kulalamika dhidi ya utawala ambao hatukushiriki kwa makusudi kuuweka.

Msomaji anaweza kujiuliza kwanini niandike haya yote lakini ni wazi kabisa jamii yetu imefikia hatua mbaya katika kujenga dhana ya kuonyesha kupiga kura hakuna maana au umuhimu.

Natambua sababu zilizochangia hatua iyo lakini bado naona hitimisho hilo si sahihi maana halileti unafuu wowote zaidi ya kutoa nafasi kwa wachache kujiamulia kwa urahisi zaidi na kufanikiwa.

Napenda kusisitiza kuwa watu kurudi nyuma na kufikiri vizuri juu ya ulazima wa kila mwenye sifa kushiriki kupiga kura na kama ukiona hakuna nguvu au msukumo wa kukulazimisha kufanya hivyo basi walau heshimu dhamiri na fikra zako ambazo nina hakika  ukizingatia vizuri hauwezi kukuhitimisha katika haki ya kutokupiga kura.

Katika hali fulani namna pekee ya kuelewa jambo ni kupitia kuelewa ukinyume wa jambo hilo. Hivyo kama inatusumbua kuelewa umuhimu wa kupiga kura basi tujaribu kutafakari ubaya wa kutokupiga kura na kama hatuelewi ubaya wa kusema wengine watapiga kwa niaba yetu hebu tufikiri ikiwa wengine watafikiri vivyo hivyo matokeo yatakuwaje katika jamii?

Naamini msomaji atabaki na maswali mengi juu ya mawazo aya nami nawakumbusha tena kujiuliza maswali ndio namna pekee ya kufikia ukweli. Matatizo na changamoto hazipaswi kutatuliwa kwa njia ambazo zitaongeza au kuzalisha matatizo mengine.