Home kitaifa Upinzani unajengwa na wapinzani wa ukweli

Upinzani unajengwa na wapinzani wa ukweli

1132
0
SHARE
MGANA MSINDAI

Na Innocent Hezekiah,

NIANZE makala  yangu kwa kukipongeza chama tawala kwa kufanya mkutano wake muhimu wa kukabidhiana kijiti cha uongozi na kumuwezesha Rais wa awamu ya tano, John Magufuli, kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho kikongwe zaidi nchini.

Pamoja na sifa zote kwa chama hicho, lakini niwaseme kidogo katika eneo moja kubwa ambalo ni la kutumia muda mwingi kuzungumzia wapinzani. Kiukweli mnawapa sifa bila kujua, maana majina yao yanabaki pia katika kumbukumbu za wanachama wenu.

Nirudi katika lengo mahususi la makala haya kwamba upinzani wa kweli hujengwa na wapinzani wa ukweli. Neno  wapinzani wa ‘ukweli’ ni neno maarufu kwa rika la vijana wakimaanisha mtu makini (tafsiri yangu).

Si vyema kuliacha hili neno kutumika huko tu, hata katika medani za kisiasa linaweza kuwa na mashiko pomoni, ili kufikisha ujumbe kusudiwa. Wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, kulitokea vuguvugu kubwa la wanasiasa wakubwa kwa wadogo kuhama kambi zao na kujiunga na kambi nyingine.

Vuguvugu hilo liliibua mtifuano mkubwa katika harakati za kuwania nafasi mbalimbali katika uongozi wa nchi yetu. Kuna waliofanikiwa na wengine kuangukia pua kama si kupigwa mweleka usiokuwa na kifani.

Lakini wengine baada ya kuona mambo hayako sawa kule walikokwenda waliamua kurudi walikotoka, kama hadithi katika kitabu cha Biblia kuhusu mwana mpotevu aliyeamua kurudi kwa baba yake baada ya kuwa kapewa urithi wake, lakini maisha yakamwendea kombo huko alikokwenda kuishi.

Upinzani nchini umekuwa na safari ndefu hadi kufikia hapa ulipo, na haya matunda yametokana na harakati mbalimbali, baadhi ya watu wamepoteza maisha, wamepata ulemavu wa kudumu huku wengine wakiingizwa jela katika siasa hayo ni sehemu ya maisha.

Hakika hakuna namna kwa vyama vya upinzani kupata matunda kwa njia ya lelemama—ni  lazima watafute mbinu mbalimbali, ili waweze kusonga mbele hata kama wenye dola hawatapendezwa, kwa kuwa ndio maisha waliyochagua.

Hivyo basi, ili kuwa mpinzani wa ukweli, ni lazima ukutane na misukosuko mingi katika kufanikisha malengo yako ya kisiasa. Kwa kutambua hilo zifutazo ni sifa muhimu za kumtambua mtu au kiongozi aliyeko upinzani na si mpinzani wa ‘ukweli’. Nitapingwa kwa hoja mahususi.

Kwanza; wale wanaojiunga upinzani kwa malengo ya kupata fedha na vyeo, hawa si watu sahihi kwa upinzani, kwani vitu walivyovitaka visipopatikana wanaweza kuusaliti upinzani, ili kupata waliyoyakosa katika kambi ya upinzani, na kuyafuata huko yanakopatikana.

Pili; wapo waliojiunga upinzani kimkumbo bila kujua kwanini wako upinzani. Watu wa aina hii hubadilika muda wowote, na katika mazingira yoyote—ndio wale wakisikia mahubiri na sera mpya, hubadilika mara moja.

Tatu; pia kuna wale waliojiunga upinzani kama mawakala wa vyama au chama tawala. Hawa ni watu makini kidogo, hudumu kwa muda mrefu kwa kuwa wao ni muhimu sana kwa watawala. Wapo viongozi, lakini hata wanachama wa kawaida pia wapo katika kundi hili.

Nne; ni wale walioko upinzani kwa kuwa wazazi, wapenzi au marafiki wako huko. Hawa wapo wapo tu, wala hawana machungu kwa chama, lakini wapo kuwaridhisha wale wanaowapenda au kuwategemea.

Tano; ni watu wanajiunga na upinzani kwa tukio fulani, lakini si wakazi wa kudumu wa huko, hubadilika kulingana na upepo.

Sita; wapo waliojiunga na upinzani kwa sababu za machukizo ya kule watokako, lakini wana mapenzi ya dhati ya kule walikotoka, ni suala la muda tu kurejea walikotoka.

Katika kundi hili wengine wamepewa vyeo kwenye vyama vya upinzani, lakini ni miongoni mwa watu watakaowaliza watu pindi watakapoamua kurudi nyumbani.

Nimalizie kwa kusema kuwa wapinzani wa kweli wapo, na wanaishi katika misingi ya itikadi zao, na wanaishi katika ukweli. Hivyo upinzani Tanzania unalo jambo la kujifunza kwa matukio ya hivi karibuni—maana wahenga walisema: Ukiumwa na nyoka hata ujani ukikugusa unashituka.

Siku njema.