Home Makala Uratibu wa maeneo ya kufanyia kampeni uwekwe sawa kwa vyama vyote

Uratibu wa maeneo ya kufanyia kampeni uwekwe sawa kwa vyama vyote

259
0
SHARE
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage

NA NASHON KENNEDY

WAKATI tunaelekea kwenye uchaguzi Mkuu Oktoba 28 mwaka huu, yapo majukumu ya msingi ambayo endapo yatatekelezwa vyema ni dhahiri yatafanikisha vyema zoezi zima la uchaguzi mkuu kwa mujibu wa ratiba inayopangwa na kwa mujibu wa Sheria na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Maandalizi hayo ya usawa yatavifanya vyama vyote vya siasa na wagombea wao kushiriki kwenye uchaguzi huo pasipo kuwa na jazba, manung’uniko wala mitafaruku yoyote, hatua ambayo itaashiria kuwa uchaguzi umefanyika kwa huru na haki.

Ili kutosababisha kuwepo kwa changamoto na mitafaruku na uvurugaji wa mikutano ya kampeni wakati wa uchaguzi, ratiba ya mikutano ya kampeni ya vyama vyote vya siasa lazima iandaliwe na NEC kwa Tanzania Bara na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ZEC) kwa Zanzibar.

Aidha kwa upande wa wilaya ratiba hizo huandaliwa na Wasimamizi wa Uchaguzi ambao ni wakurugenzi watendaji wa wilaya, miji na majiji. Wadau wengine ambao pia wana jukumu la uratibu wa ratiba za kampeni wakati wa uchaguzi ni pamoja na Jeshi la Polisi, maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB), wakuu wa wilaya na mikoa.

Moja ya eneo hilo muhimu linalofanikisha uchaguzi ni pamoja na maeneo ya kufanyia mikutano. Haya yanaweza kuwa ni maeneo ya wazi kama maeneo ya viwanja vya mipira, yaliyotengwa kwa kazi zingine na Serikali na maeneo mengine muhimu. Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchaguzi, maeneo ya kufanyia mikutano ya uchaguzi huandaliwa na tume yakiwa na ratiba kamili inayotambulika kwa taasisi na watu wote wanaojihusisha na uchaguzi.

Lakini baadhi ya vyama vya siasa, labda kutokana na umaarufu wa wagombea wao, rasilimali fedha vimekuwa kwa makusudi vikikiuka taratibu kwa kuyachukua maeneo ya kufanyia mikutano ya kampeni kwa nguvu bila ya kujali na kuheshimu ratiba iliyotolewa na NEC.

Hatua hiyo huchochea vurugu na hamaki kwa maofisa wa vyama vya siasa, wagombea wao na maofisa wa NEC, hatua ambayo endapo suala hilo lisipofanyiwa uchunguzi na kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria litavuruga zoezi zima la uchaguzi.

Watu na taasisi zilizopewa na dhamana na NEC za kusimamia na kuratibu shughuli za uchaguzi ni lazima zihakikishe zinasimamia changamoto zote kwa kutenda haki kwa vyama vyote na wagombea wao bila upendeleo kwa kuzingatia sheria zilizowekwa.

Mambo ya aina hiyo ya baadhi ya wagombea wa vyama vya siasa kutotendewa haki ikiwemo kutopewa maeneo waliyopangiwa kufanyiwa kampeni zao kwa mujibu wa Ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu (LHRC) ya kufuatilia mwenendo wa uchaguzi ya mwaka 2015 yalijitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Katibu wa Chama cha UDP Mkoa wa Mwanza ambaye Oktoba 11 mwaka 2015, aliieleza tume hiyo kuwa eneo la mkutano kwa ajili ya kampeni yao lilipangwa kufanyika katika Kijiji cha Jojiro, Kata ya Ng’hundi jimbo la Kwimba Oktoba 10 liliingiliwa na Chama Cha Mapinduzi, ili hali kikielewa kuwa ratiba ya mkutano ilikuwa ya chama cha UDP.

Tukio la aina hiyo pia kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Tume lilitokea pia katika kijiji cha Malemve katika Kata ya Igongwa, wilayani Kwimba katika Mkoa wa Mwanza, ambapo CCM kilikwaruzana na UDP kwenye eneo moja la kufanyia mkutano wa kampeni.

Aidha kwa mujibu wa Ripoti hiyo, vyama vya CCM na Chadema vilikwaruzana kwenye eneo moja la kufanyia mikutano kati ya Septemba 14 na 17 mwaka 2015 katika vijiji vya Kasanga na Samazi, wilayani Kalambo mkoani Rukwa na sababu ya ugomvi wao haikuwekwa wazi, ingawa ilikuwa ni kung’angania eneo la kufanyia mkutano wa kampeni.

Aina hiyo ya sintofahamu husababisha wafuasi wa vyama vya siasa kuanzisha vurugu ambazo baadaye huhatarisha amani na hivyo kuharibu zoezi zima la uchaguzi.

Tanzania iliridhia mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa mujibu wa sheria mwaka 1992. Kila mamlaka na watu waliopewa dhamana ya kuratibu na kusimamia shughuli za uchaguzi lazima wahakikishe kuwa wanatoa fursa sawa za uchauzi kwa vyama vyote vya siasa pasipo hila wala jazba au kwa ushawishi wa kisiasa ama aina ya wagombea wanaowataka au waliowabeba mifukoni mwao.

Waliopewa dhamana ya kusimamia sheria, wakifuata kanuni na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria watakuwa wamewezesha kufanyika uchaguzi wa huru na haki na kuepusha vurugu ambazo mwisho wake ni kumwagika kwa damu isiyo na hatia na hivyo kuifanya nchi yetu kuingia kwenye rekodi ya nchi ambazo hazizingatii kanuni, taratibu za uchaguzi.

Lazima kila mtu, mpiga kura, chama cha siasa, mgombea, ofisa wa NEC na taasisi zilizopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi kwa pamoja watekeleze wajibu wao kwa kusimamia kikamilifu kanuni, taratibu na sheria zilizowekwa ili tuweze kufanikisha shughuli kubwa iliyo mbele yetu ya uchaguzi Mkuu. Mungu ibariki Tanzania na watu wake, naomba kutoa hoja.

0756 823 420/ 0684 214 114