Home Makala Urudishwe muundo wa Utumishi kuinua kiwango cha uendeshaji

Urudishwe muundo wa Utumishi kuinua kiwango cha uendeshaji

3647
0
SHARE

NA BALINAGWE MWAMBUNGU

‘Civil Service’ ndiyo injini ya kuendesha mambo ya serikali—hasa katika nchi zilizoendele na zenye ukimavu wa demokrasia.

Katika demokrasia komavu, huwa hakufanyiki madadiliko, muundo, taratibu, sheria na kanuni za kuendesha serikali—ndio maana unakuta katika baadhi ya nchi, kwa mfano Ujerumani, viongozi wa kisiasa walichukua muda mrefu mwaka huu, kuunda serikali baada ya uchaguzi mkuu kwa sababu hapakuwa na chama kilichokuwa na idadi ya Wabunge wa kutosha kuunda serikali peke yake, japo chama cha Kansela Angela Markel cha CDU (Christian Democratic Union) kilishinda uchaguzi. Katika kipindi hicho takriban cha miezi minne, Ujerumani haikutetereka kiuchumi na huduma za kijamii, kutokana na ‘stalemate’—hali ya kutopatikana mshindi wa moja kwa moja.

Zamani hapa Tanzania, kulikuwa na Idara ya Utumishi (Central Establishment), ambayo kazi yake kuu ilikuwa kusimamia taratibu, kanuni na sheria za utumishi, wa ajira ambazo hazikuangukia kwenye pensheni, hawa walikuwa wanalipwa kiinua mgongo. Wasomi walikuwa katika ajira za kudumu na kupata pensheni (permanent and pensionable staff).  Central Establishment, ilikuwa na Central Registry—kwa watumishi wote wa Serikali.

Kama kuna nafasi za kuteuliwa zilijitokeza, wanaopendekezwa kujijaza walikuwa ‘vetted’ kabla ya majina yao kupelekwa Ikulu kwa uteuzi. Sasa hivi inaonekana utaratibu huo haufuatwi, kama unafuatwa, basi hauzingatiwi. Watumishi wateule wanafanya kazi kwa wasi wasi—wana hofu ya kutumbuliwa. Matokeo yake ufanisi wa kazi unapungua—kwa sababu wanasiasa wanatoa amri—fukuza, simamisha, ondoa, hamisha, weka ndani—kinyume na kanuni, taratibu na Sheria ya Utumishi.

Halafu kulikuwa na kiapo (written) cha kutunza Siri (confidentiality). Sasa kama siri za uteuzi zinatamkwa kwenye majukwaa—inaonesha nini?

Nilifanya kazi serikalini japo kwa muda mfupi (nilishia ngazi ya Executive Officer Grade 1). Watumishi walipanda ngazi kwa kufuata sio kisomo tu, bali pia waliangalia miaka ya mtumishi (seniority) katika kazi. Aidha, nyongeza ya mishahara ilikuwa ni kila mwaka, labda kama mtumishi alikuwa na matatizo, mfano utoro kazini, mkubwa wake alikuwa namadaraka ya kupendekeza (apewe/anyimwe) nyongeza.

Kulikuwa na aina mbili ya mafaili ya mwajiriwa—ya siri (confidential), na wazi (open). Mwajiriwa alikuwa haruhusiwi kuliona faili lake la siri wala kupeleka faili lake la wazi kwa wakubwa. Kulikuwa na karani maalumu wa Masjala ya Siri. Masijala ilikuwa inatunzwa kama inavyotunzwa ‘strong room’—chumba cha kuhifadhia fedha katika benki. Mambo ya utendaji serikalini yalikuwa hayafuji. Ndio maana ya kuwa na msemaji mkuu.

Kila baada ya kipindi fulani, kilichapishwa kitabu chenye orodha ya watumishi wote wa serikali, kikionsha mahali akozaliwa, shule na vyuo alivyosoma, anwani zao, cheo, namba za simu za mezani. Simu za kiganjani hazikuwapo. Kitabu hicho cha Who is Who in the Civil Service, kilikuwa na wasifu wa kila mtumishi mwenye cheo zaidi ya gaedi ya karani ‘clerical staff’.

Kulikuwa na Kamati za Nyumba (Housing Committees) ‘A’ na ‘B’ chini ya Utumishi  kwa ajili ya watumishi wandamizi. Nyumba ziligawiwa kwa vyeo.

Nilipoingia Wizara ya Elimu kama Education Officer III, nilistahili kupewa nyumba Grade B au A kama ipo iliyo wazi. Kwenye shule za sekondari za bweni kulikuwa na nyumba za walimu—sasa hivi sijui hali ikoje. Kwa shule za mijini, walimu wakuu na walimu wandamizi, walipewa nyumba katika utaratibu ule ule wa Utumishi.

Shule za sekondari zilikuwa chini ya Ofisa Elimu Wilaya/Mkoa, ambaye aliwajibika moja kwa moja kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, tofauti na sasa ambapo shule zinaendeshwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa! Wizara ya Elimu—ambayo ilipaswa kuongoza elimu, haina uendeshaji wa shule wa moja kwa moja.

Walimu walikuwa wanalipwa mishara yao  moja kwa moja na Katibu Mkuu ndio maana hapakuwa na ucheleweshaji, isipokuwa mishahara ya walimu waliokuwa wanajiriwa kwa mara ya kwanza, lakini sio zaidi ya miezi sita.

Sasa hivi ni kawaida kwa mwalimu sio tu kucheleweshewa mshahara, kubugia vumbi la chaki miezi 12 bila mshahara, huku Hazina ikiwa imekwisha idhinisha fungu!

Kipindi cha Madaraka Mikoani, walimu walikuwa wanalalamika kwamba Wakurugenzi wa Maendeleo wa Wilaya—ma DDD, walikuwa wakipata dharura, walikuwa wanatumia mishahara ya walimu na kuwalipa fungu husika litakapo patikana. Hapo ndipo mvua ilipoanza kuwapiga walimu. Matokeo yake kazi ya uwalimu sasa inadharauliwa, haina maslahi ukilinganisha na tasnia zingine. Uboreshaji wa elimu uende sambamba na uboreshaji wa maslahi ya walimu—ikiwa ni pamoja na nyumba kujengwa maeneo ya shule.

Mfumo wa kijadi ulitumika kutatua matatizo ya ardhi vijijini. Machifu walikuwa na madaraka ya kuamua  masuala yote ya kijamii ikiwa ni pamoja migogoro ya mipaka kati ya mtu na mtu, au wilaya na wilaya kwa kushirikiana na mabwana shauri (district officers). Hawa walikuwa wanafaya kazi chini ya maDC. Hii inawezekana ni moja ya sababu ya kutokuwapo kwa rushwa enzi hizo—tofauti na sasa ambapo mfumo wa mabaraza ya ardhi yanalalamikiwa kwendeshwa kwa rushwa.

Vyeo vya DC na PC (district na provincial commissioners), havikuwa vya kisiasa. Waliteuliwa kwa kufuata ngazi katika utumishi wa serikali. Utaratibu huu ulikuja badilika baadaye—ma DC na PC kuwa ni wateule wa kisiasa. Wateule hawakuangalia CV ya mtu—bali uwaminifu wake kwa chama.  Wateule wengine waliishia darasa ‘O’ lakini  waliwasimamia wasomi bila vitisho na kukwaruzana.

Kenya hawakufanya makosa kama hayo, na mfumo wao wa machifu (katika sehemu zenye jadi hiyo), umeendelea kuwapo na serikali imefanya mabadiliko miaka michache iliyopita na kuleta mfumo wa Magavana (kama RC) wa kuchaguliwa. Hakuna watu kuhama hama ili kuzengea uteuzi.

Wasomi wenye uzoefu ndio waliteuliwa na Rais kushika nafasi za juu za utawala. Haikuwa rahisi kumteua mtu aliyekuwa mgeni kazini, akateuliwa kushika nafasi ya juu kwa sababu tu eti ana kisomo, ingawaje ni kweli kwamba walikuwa na ngazi ya kuanzia.

Tanzania hatutaweza kufikia malengo kama siasa itaendelea kupewa nafasi zaidi ya ujuzi katika kazi na kisomo. Uteuzi wa kulipa  fadhila, upendeleo, urafiki, udugu, ukanda na ukabila ni adui wa maendeleo.

Zamani kwenye Civil Service ofisa alikuwa ananzia ngazi ya chini, ili ajifunze—Waingereza husema ‘the tools of trade’ ili apande ngazi akijua kazi wanazifanya wa chini yake—Ingawaje kulikuwa na kitu kiliitwa ‘accelerated promotion’—kupanda ngazi kwa haraka. Hii ilitokana na juhudi na kujituma, nidhamu, uhodari na utii. Nadhani utaratibu huu bado upo kwenye majeshi yetu.

Lakini imefika mahali wateule wengine huwa hawajawahi hata kundesha ofisi—hawajui ku ‘move a file’. Civil service rules and regulations hawazijui, ndio maana kuna ‘kuagiza na kuamrisha’ kumfukuza kazi watumishi, kuwashusha maofisa vyeo bila maandishi na bila kufuata utaratibu. Mwajiriwa hufukuzwa kazi na mwajiri, kwa barua na kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za kiofisi.

Kuteua watu kutokana na usomi pekee ni kitendawili. Mwanajeshi (trained professional soldier) hupewa wadhifa uraiani  na kuwaacha waliosomea mambo ya utawala kunazua maswali.

Kuna haja ya kufufua Chuo cha Uongozi—kama ilivyokuwa Institute of Public Administration Mzumbe—kiliwapika watawala (admnstrators), ndio walipewa madaraka ya kundesha wilaya, mikoa, wizara na taasisi za serikali. Ilikuwa kosa kukibadili chuo cha Mzumbe (Institute of Development Stidies (IDM) kuwa chuo kikuu kama vyuo vingine.

Muda wa kumbadilisha mtu taaluma yake na kumfanya mtawala hatuna. Hili litazamwe upya. Zipo taarifa kwamba baadhi ya wasomi walioteuliwa kujaza nafasi mbali mbali—wakikuwa hawajui hata kuandika dokezo!

Ajira za serikali zilikuwa centralized—kupunguza upendeleo. Kulikuwa na Baraza la Ajira Serikalini—badala ya kuacha kila wilaya, halmashauri iwe na mamlaka ya kuajiri.

Mabaraza ya madiwani kumkataa mtumishi—ni kitu kipya. Hii ni kwa sababu ajira zimekuwa decentralized. Kitendo hiki kinawavunja moyo watumishi na kuwajengea woga. Kwa taratibu za Utumishi, mtu haondolewi kazini kwa matangazo. Kama ni uhamisho, zipo taratibu zake—sio kwa tangazo la madiwani la kumkataa.