Home Makala Urusi kuiweka mtegoni Tanzania

Urusi kuiweka mtegoni Tanzania

2787
0
SHARE

bolivia-nuclear_816x544Na Markus Mpangala

NAMTUMBO ni moja kati ya Wilaya tano za Mkoa wa Ruvuma. Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, ni Sheria Na. 7 ya mwaka 1982 iliwezesha kuanzishwa kwa Halmashauri ya Namtumbo ikiwa na eneo la kilometa za mraba 20, 375.  Wilaya nyingine za mkoa huo ni Tunduru, Songea, Mbinga na Nyasa.

Aidha, kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 wilaya ya Namtumbo ina jumla ya watu 201,639. Ukiacha wilaya hiyo tuje katika Kijiji cha Dar Pori kilichoko Wilaya ya Mbinga katika mkoa huo huo wa Ruvuma. Kijiji hicho kina wakazi takribani 6,000 na kipo kilomita 8 kutoka nchi ya Msumbiji, na kimekuwa maarufu kutokana na uchimbaji wa madini.

Baadhi ya wakazi waliokuwa wakiishi maeneo yenye madini walitakiwa kuhama na walilipwa fidia kupisha uchimbaji wa madini hayo. Pia kijiji hicho hakina kituo cha Polisi na kinategemea Zahanati ya Mpepo kupata matibabu yao ambayo ipo kilometa 11 kutoka makazi yao. Lakini kijiji hicho kinao utajiri wa madini.

Kwa wilaya ya Namtumbo na kijiji cha Dar Pori ni maeneo yanakopatikana madini ya ‘uranium’. Madini adimu ambayo hutafutwa na mataifa mbalimbali duniani ambapo hutumiwa kama vyanzo vya nishati ya umeme, mitambo ya mafuta, silaha, utafiti wa masuala ya kisayansi na utengenezaji wa mabomu ya nyuklia.

Kwa mujibu wa Shirika la Uzalishaji Madini ya Uranium, hadi mwaka 2014 ni nchi 19 ndizo zenye kiwango cha juu cha uchimbaji wa madini hayo, ambazo ni Kazakhstan (41.1%), Canada (16.2%), Australia (8.9%), Niger (     7.2%), Namibia (5.8%), Urusi (5.3%), Uzbekistan (4.3%), Marekani (3.4%), China (2.7%), Ukraine (1.6%), Afrika Kusini (1.0%), India (0.7%), Malawi (0.7%), Brazil (0.4%), Jamhuri ya Czech (0.3%), Romania (0.1%), Pakistan (0.1%), Ujerumani 0.1%), na Ufaransa (0.0%).

Orodha hiyo inaonyesha kuwa Bara la Afrika linazo nchi  tatu;- Namibia, Malawi na Niger, ambapo Tanzania inakuwa ya tatu kufuatia kugundulikana madini hayo, na yapo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, na sasa kunaifanya Tanzania kuwa taifa linalowindwa mno na mataifa tajiri duniani.

Ripoti ya Shirika la Nyuklia duniani (World Nuclear Association) Niger ilivumbua madini ya uranium huko mjini Azelik mnamo mwaka 1957 baada ya utafiti wa Bureau de Recherches Geologiques et Minières (BRGM) ya Ufaransa. Lakini uchimbaji rasmi ulianza mwaka 1971, ni katika taifa hili pia ambalo Marekani imeanzisha kambi za Mafunzo ya Kijeshi kwa kushirikiana na jeshi la nchi hiyo.

Kutokana na Wilaya Namtumbo kuwa na utajiri wa madini hayo, Tanzania ikigeuka kushoto kuna China inayotaka madini ya Uranium, ikigeuka kulia kuna Urusi pia, ikibaki katikati kuna Marekani, na nyuma yake kuna Japan, ambayo ni miongoni mwa mataifa yanayoongoza kwa kusaka madini ya uranium kwa udi na uvumba. Ni dhahiri pia suala hili linazigusa mno nchi hizo kiasi cha kunyukana kwenye ardhi ya mataifa ya kigeni ili kukuza uchumi wao.

MIAKA 11 ILIYOPITA

Kampuni ya Mantra Resources Tanzania Limited (MTRL) ilikamilisha uchimbaji wa madini ya uranium katika mradi wake huko Mkuju, wilayani Namtumbo. MTRL ilitarajiwa kuchimba takribani tani milioni 4.5 za madini ya uranium. Ipo chini ya kampuni mama ya Mantra Resources Pty Ltd (zamani Mantra Resources Ltd.) ambayo inashirikiana na kampuni nyingine ya Uranium One katika mradi huo. Uranium One inamilikiwa na serikali ya Urusi kwa asilimia 100.

Mwaka 2005 kampuni hiyo ilipewa leseni ya utafiti wa madini ya hayo hapa nchini. Mwaka 1993 wakala wa Mazingira nchini Marekani (EPA) iligundua nyumba za makazi zilizopo ndani ya maili moja kutoka machimbo ya uranium ambao walikuwa katika hatari ya kupata saratani.

UJIO WA URUSI 2016

Makampuni makubwa ya viwanda na uzalishaji kutoka nchini Urusi ya Russian Helicopters, United Aircraft Corporation (UAC) na United Wagon Company (UWC) yako tayari kuwekeza kwenye miradi ya viwanda nchini Tanzania kupitia miradi ya madini ya uranium.

Kwa mujibu wa waziri wa viwanda wa Urusi Denis Manturov aliyemtembelea nchini mwezi mmoja uliopita alisema nchi yake iko tayari kujenga matmbo wa nyuklia (Nuclear reactor) hapa nchini  kwa ajili ya tafiti na mambo ya afya.

Aidha, alibainisha kuwa mpango huo umekusudia kufufua uhusiano wake na nchi za Afrika ambao ulidorora kuanzia miaka 1990.

“Tanzania, ikiwa na idadi ya watu takribani milioni 40, soko lake linazidi kupanda na kupanuka katika eneo la Afrika mashariki, kusaini mikataba ya uzalishaji kama hiyo inachangia kuingiza bidhaa hapa,” alisema Denis Manturov na kukaririwa na gazeti moja la Kiingereza hapa nchini.

Waziri Manturov aliongoza ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Urusi ambao walitembelea hivi karibuni na kusisitiza kuwa tayari ujenzi wa kinu cha nyuklia.

“Tulizungumza na Makamu wa Rais kuelezea kusudio letu la kuhakikisha tunajenga kinu cha Nyuklia kwa lengo la kufanya utafiti wa kisayansi hapa Tanzania, ikiwemo miradi ya afya. Tunaamini wenyeji wetu wamevutiwa na mpango huu,”

Kwa mujibu wa waziri Manturov, Urusi imewekeza katika miradi zaidi ya 50 ya nyuklia, ambapo kati ya hiyo 20 iko nchini mwao, huku mingine 30 ikiwa katika nchi rafiki.

Aidha, waziri huyo alisisitiza umuhimu wa ukanda wa afrika mashariki katika maendeleo na kubainisha kuwa serikali ya Urusi inatarajiwa kuanza rasmi kujenga kinu cha nyuklia kwa matumizi ya kibinadamu ifikapo mwaka 2018 na unasimamiwa na kampuni ya Uranium One mali ya Urusi. Aidha, inatarajiwa kuanza kuzalisha tani 35,000 za madini ya uranium.

MADINI YA URANIUM NI NEEMA AU LAANA?

Migogoro mingi inayoikabili dunia ni kutokana na matumizi au kiu ya kumiliki Nyuklia. Matumizi ya Nyuklia yapo tofauti kwhaiyo kila taifa linakuwa na malengo yake.

Yapo mataifa ambayo yamekuwa yakiishi katika laana kutokana na utajiri mkubwa wa madini ya uranium, kwamba zinakuwa masikini huku wanaonufaika ni watu wa mataifa ya kigeni.

Malawi ni mfano wa karibu yetu, kwani ni taifa masikini kabisa lakini linashikilia nafasi ya 12 kati ya mataifa yenye kiwango kizuri cha uzalishaji wa madini ya uranium ikiwa na asilimia  0.7.

Kwa mujibu wa  ripoti ya Shirika la Oxfam ya mwaka 2014 iliitaja Niger ndilo taifa lenye kiwango kikubwa ch auzalishaji wa madini ya uranium, lakini ni masikini kupindukia.

Aidha, kwa miaka 40 tangu kuanza uchimbaji wa uranium Niger haijanufaika na zaidi ya tani 100,000 zilizochimbwa. Sababu kubwa inayotajwa ni umiliki wa madini hayo ambayo asilimia 80 ulikuwa wa Ufaransa, huku iliyobaki ni ya Niger.

Kwa hapa Tanzania, kampuni Uranium One ndiyo inayomiliki hisa kubwa ya mradi wa uchimbaji wa madini hayo huko Mkuju, Namtumbo. Ikumbukwe mradi huo pia unatumai Sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo ina vipengere vingi vinavyowabeba wawekezaji na ambavyo vimenakiliwa kutoka Benki ya Dunia.

Aidha, inatajwa kuwa Benki ya Dunia ni kikwazo cha Afrika kunufaika na madini kwa madai inazibana nchi hizo katika soko la dunia kwa madai kuwa serikali zake hazina uwezo wa kumiliki mfumo wa uchimbaji.

Inatajwa kuchangia pia kubadilisha sheria ya madini ya mwaka 1998 kwenda ya mwaka 2010, ambapo wawekezaji wanawezesha kuhamisha mitaji (profit Transfering).

MADHARA

Akizungumza na wananchi wa wilaya ya Namtumbo, aliyekuwa Makamu wa Rais, Dk. Gharib Bilal mnamo Februari 16, 2012 alisema kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ya uranium hauna madhara yoyote na kwamba watu waliokuwa wakifanya juhudi kupinga mradi huo wanapotosha wananchi. Hata hivyo pamoja na kauli hiyo ipo mifano hai inayothibitisha madhara ya madini na nyuklia kwa ujumla.

Machi 14, 2011 kulitokea mlipuko katika kinu cha kinukilia kilichoharibiwa na tetemeko la ardhi cha mji wa Fukushima. Mlipuko huo wa hewa ya Hydrogen ulitokea katika mtambo wa tatu.

Msimamizi wa kiwanda hicho aliviambia vyombo vya habari kuwa mlipuko huo haujaharibu kifaa kinacho hifadhi mtambo huo wa kinukilia.

Kiwanda hicho kinasema watu sita walijaruhiwa na wengine 22 walitibiwa kutokana na madhara ya kuharibika kwa kinu hicho cha kinyukilia ambacho kilihifadhi tani 6,000 za maji yenye kiwango cha juu cha mionzi ya nyuklia, jambo ambalo limekuwa janga nchini humo.

Aidha, serikali ya nchi hiyo iliamua kumwaga baharini tani 10,000 za maji yenye kiwango cha chini cha mionzi ya nyuklia. Ingawa kampuni hiyo ilidai kuwa kuendelea kula samaki walioko eneo hilo la bahari hakutaleta madhara makubwa kwa afya ya binadamu, lakini hatua hiyo imepingwa vikali na Korea ya Kusini iliyothibitisha madhara ya mionzi hiyo.

Hii inathibitisha kuwa uchimbaji wa madini ya uranium na baadaye ujenzi wa mitambo ya nyuklia unaleta maadhara makubwa kwa afya ya wanadamu.

Ni sababu hiyo tulishuhudia mapema Machi 11, 2011 serikali ya Ujerumani  ikitangaza kufunga Vinu 7 vya nyuklia vilivyoanza kufanya kazi tongu mwaka 1980, vitafungwa kwa muda.

Kansela Markel alichukua uamuzi huo baada ya kukutana na viongozi kadhaa wa mikoa ya Ujerumani kuhusiana na suala la nishati ya nyuklia, ambapo imepangwa kufungwa vyote ifikapo mwaka 2021.

Aghalabu Shirika la nguvu za Atomiki la Umoja wa Mataifa limekuwa likieleza kuwa mionzi inayotoka kwenye mitambo ya nyuklia inakwenda moja kwa moja katika hewa angani na kwa wastani mionzi hiyo inaweza kubaki hewani kwa saa 10.

Mtaalamu wa masuala ya Mazingira, Eliya Mtupile, anasema, “Ninao na mtazamo chanya katika uchimbaji wa urnium ila kwa angalizo. Ufanyike utafiti wa kutosha wa kimazingira. Nuclear katika mambo ya mazingira tunasema zina “long term irreversible negative impacts” madhara ya muda mrefu ambayo ni vigumu kuyadhibiti. Lakini hata hivyo hamna maendeleo yanayokuja pasipokuwa na gharama,

Hivyo ningependekeza zifanyike tathmini za kimazingira na za athari Environmental Impact Assessment (EIA) and Risks Impact Assessment (RIA) zenye weredi (nyingi zinafanyika kwa kutofuata maadili na weredi) ili sehemu kiwanda kitakapojengwa kisiweze kuleta athari kwa watu na viumbe wengine,”

TANZANIA KUWA KAMA IRAN?

Ingawa rekodi zinaonyesha kuwa serikali ya Iran ilianza ushirikiano na Marekani katik masuala ya nyuklia mwaka 1957, lakini mataifa hayo yamegeuka kuwa adui mkubwa. Urusi ni taifa ambalo limewekeza kwa nguvu kubwa ya mitambo ya nyuklia baada ya uchimbaji wa madini ya nyuklia.

Uhusiano mzuri wa Urusi na Iran haikuzifurahisha Israel na Marekani. Zaidi ni uamuzi wa Iran kurutubisha madini ya uranium kwa madai ya kutengeneza nishati ya umeme kwa manufaa ya wananchi.

Hata hivyo ilielezwa kuwa Iran ilikuwa imevuka kabisa kiwango cha Thorium ambacho kinakusudiwa kuunda bomu la nyuklia na siyo matumizi ya nishati ya umeme. Yapo mataifa yanayomiliki mabomu ya nyuklia na yalianza kwa sababu zilizotolewa na Urusi, “utafiti wa masuala ya kisayansi ikiwemo afya, pamoja na nishati ya umeme,’. Uingereza, ilijaribisha bomu lake la nyuklia mwaka 1952; Ufaransa ikajaribisha mwaka 1960; China (1964); India (1974 na 1998); Pakistan (1998);  Afrika kusini (1997) na Korea Kaskazini (2006).

Kwa vyovyote Mataifa ya magharibi yanaliangalia suala la nyuklia ya Tanzania kwa jicho la tatu. Kwamba mataifa hayo yakiongozwa na Marekani yamekuwa mpinzani wa muda mrefu wa Urusi.

Kuanzia Belarus hadi Kazakhstan, na baadaye Ukraine na Iran pamoja na Syria. Mzozo mkubwa wa nyuklia umekuwa kiini cha kugombana kwao kwani wanaona maslahi yao yanatibuana, hivyo suluhisho ni kuwekewa vikwazo kamazilivyofanyiwa Iran, Syria na Korea kusini.

Ujenzi wa mitambo ya nyuklia una maslahi na Urusi, wakati huo huo Marekani inahakikisha maslahi yake yanalindwa kwa nguvu zote, huku ikizidi kuipiga kumbo China ambayo imekuwa na ushawishi.

China inayo miradi ya bandari na reli, Urusi nyuklia, na Marekani inayo ya umeme na mingineyo hata hivyo suala hili linaiweka Tanzania kwenye mtego wa kupendelea upande fulani. Nyuklia ni bidhaa adimu ambayo inawindwa kila kona, ndiyo maana wawekezaji walikuwa tayari kutafiti kwa miaka 11 pamoja na kumiliki uwekezaji kwa asilimia 100.

Kwa vipi Tanzania itakwepa mtego huu? Sababu , kwa kukumbusha tu, mgogoro wa Iran ulishamiri zaidi baada ya kutaka kurutubisha madini ya uranium kwa asilimia 20, lakini nchi za Magharibi pamoja na China  zilitaka Irani isirutubishe madini hayo siyo zaidi ya asilimia 5.

Kwamba kuiruhusu Iran kurutubisha uranium kwa asilimia 20 ni kuruhusu kuundwa kwa silaha za nyuklia. Halikutegemewa kutokea Iran ambako walisema wanahitaji umeme tu, lakini linaweza kuwa vivyo kwa Tanzania.