Home kitaifa Usafi ni uamuzi, uchafu hujirudia

Usafi ni uamuzi, uchafu hujirudia

937
0
SHARE

Rais John Magufuli akikusanya takatakaNa M.M MWANAKIJIJI

UKIONA mji msafi au mtu msafi au mahali fulani pasafi unaweza kufikiria usafi ni tabia ya asili ya vitu. Viumbe vingi havina tabia ya asili ya usafi; vipo bila ya shaka viumbe ambavyo vinapenda usafi. Mwanadamu kwa asili yake si kiumbe msafi; tangu kutungwa kwake mimba hadi kuzikwa kwake mwanadamu anazungukwa na uchafu. Ukimwacha mtoto peke yake dakika chache utaona ukweli huu; ataenda kwenye uchafu hata pale anapotumia vitu ambavyo vinaweza kumfanya awe msafi!

Hata mtu mzima asipoamua kujisafisha haichukui muda mrefu kila mtu pembeni yake ataanza kuhisi kuwa huyu fulani ni mchafu. Kimsingi basi utaona uchafu ni zaidi ya tabia; ni hali. Ni hali ambayo si rahisi kuiondoa kwani inabidi uiondoe kwa kuleta hali nyingine ambayo si ya asili; usafi ni hali isiyo ya asili ya vitu vingi. Jambo jingine ambalo tunaweza kusema kuhusiana na uchafu ni kuwa ukizoeleka kwa muda mrefu usafi hautafutwi; mtu akizoea uchafu ni vigumu kumfanya aone umuhimu wa usafi. Hata ukisafisha mara moja usishangae mtu atarudi pale pale kwenye uchafu.

Ni ukweli huu wa pili unaonifanya niseme kuwa uchafu unatabia moja mbaya sana; hupenda kujirudia. Wiki iliyopita watu wengi walionekana wamehamasika kuanzia Ikulu hadi mitaani nchi nzima wakienda kushiriki kampeni ya usafi. Watu walivaa sare, walipiga picha na tushukuru mitandao wakajionesha kuwa kwa siku moja watu wamehamasika kusafisha mazingira yao – ambayo bila ya shaka wote walikuwa wanajua na waliyazoea katika hali yake ya asili – ya uchafu.

Tuliwaona watu wameshika mafagio, mafyekeo, mapanga, reki, mapipa ya kubebea takataka… wote wakihamasika na kuhamasishana kuwa “leo” ni siku ya usafi. Na kweli; walizibua mifereji na mitaro iliyoziba, walikusanya mifuko iliyochakaa ya plastiki (mojawapo ya vitu vinavyoharakisha uchafu wa mazingira kwa haraka) na kukusanya kila aina ya takataka zilizoweza kukusanywa na kuzichoma moto. Nchi nzima kulikuwa na harufu ya moshi karibu kila eneo kwa sababu watu waliamua kwa pamoja kufanya usafi na kuondokana na mazingira machafu. Kwa siku hiyo moja.

Kama nilivyosema uchafu una tabia mbaya  ya kujirudia. Huwezi kuoga siku moja ukasema umeoga daima; huwezi kukata kucha mara moja ukasema hutokata tena; huwezi kujipangusa sehemu zile zisizotajika ukasema kesho hutajipangusa tena! Uchafu kwa asili yake hujirudia. Tatizo ni kuwa usafi hauna tabia ya kujirudia wenyewe! Usafi hurudiwa kwa uamuzi wa lazima.

Sasa watu wale wachafu; waliozoea uchafu; walioona uchafu na kuuvumilia; waliojua kuwa jamii yao ni chafu na wakaishi kana kwamba hawaoni wakaamua kuwa wasafi kwa siku moja kwa kweli wanastahili kupongezwa. Lakini hili halisemi kitu hasa kwani tunajua nini kitakachojirudia bila kulazimishwa; uchafu. Watu hawa ambao leo huko maofisini bila ya shaka wanasimuliana jinsi walivyoshiriki usafi wanaweza kabisa wakakuta mtu anatupa taka kwenye eneo walilosafisha lakini wasiseme kitu kwa sababu siku ya “usafi” imepita. Wale walioenda mahakamani kudai kulinda kura yao katika mita 200; sidhani kama leo wanaweza kuona umuhimu wa kulinda maeneo yao waliyoyafanyia usafi hata kwa dakika mbili.

Uchafu utajirudia. Takataka zitatupwa kiholela, mifereji na mitaro itaziba tena, watu watatupa mabaki ya chakula ovyo, na kama ilivyokuwa juzi (siyo jana) watu wataanza kusahau umuhimu ule wa usafi na haja ya urudia rudia usafi kiasi kwamba hata watakapokuwa wamezungukwa tena na uchafu hawatojua. Hadi Magufuli akasirike tena na kuwakumbusha haja ya kuwa na usafi.

Ni kwa sababu hiyo naamini – na nina uhakika wengine wamependekeza vile vile – suala hili la kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa masafi kila wakati linahitaji uamuzi wa serikali kutangaza kuwa siku mbili ndani ya mweli ziwe ni siku za usafi katika jamii yote na Watanzania wote washiriki na bila ya shaka zisiwe tena siku za kazi na kuhakikisha kuwa kila ofisi inaweka utaratibu wa kutafuta siku hizi mbili za kuhakikisha mazingira yake – ndani ya mita fulani – hakuna uchafu wowote. Lakini zaidi ni lazima utafutwe utaratibu wa kudumu wa kushughulikia uchafu kwani kwa kadiri binadamu wapo uchafu utakuwepo.

Na hata ukiondoa leo kwa mbwembwe na heshima zote; uchafu utarudia tena.

Swali ni nini kitafanyika utakaporudi; siyo kama utarudia. Tunaposifia mahali, miji au jamii fulani kuwa ni safi tujue tu ni kwa sababu walirudia usafi kuliko kuacha uchafu ujirudie.

Baruapepe; klhnews@klhnews.com