Home Latest News USAJILI SIMBA, YANGA UCHUNGULIE KIMATAIFA

USAJILI SIMBA, YANGA UCHUNGULIE KIMATAIFA

1609
0
SHARE

NA HASSAN DAUDI

KWA miaka mingi, timu za soka za Tanzania zimekuwa zikishindwa kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa, huku sababu mbalimbali zikitajwa, ikiwamo maandalizi duni.

Katika hilo, kujua ni kwa namna gani  soka la Bongo limekuwa likishindwa kufua dafu kwenye ngazi ya kimataifa, zifuatilie klabu kongwe za Simba na Yanga, kwani mara nyingi ndizo zimekuwa zikipata nafasi ya kwenda kuiwakilisha nchi.

Timu hizo zenye mashabiki wengi ndani na nje ya Tanzania zimekuwa zikivurunda kila zinapotia mguu kwenye  mashindano yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf); Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.

Mafanikio makubwa ya Tanzania katika katika mashindano ya Shirikisho hilo ni Wekundu wa Msimbazi walipofika fainali ya Kombe la Caf (sasa Kombe la Shirikisho) mwaka 1993.

Licha ya Yanga kushiriki mara 11 Ligi ya Mabingwa Afrika, imefanikiwa kutinga hatua ya makundi mara moja pekee na hiyo ilikuwa mwaka 1998.  Mara nyingi safari ya Wanajangwani hao imekuwa ikiishia raundi ya kwanza au ya pili.

Kwa upande wa wenzao Simba, wamecheza michuano hiyo mara sita, lakini ni mara moja pekee waliweza kutinga makundi (2003), wakiishia raundi ya kwanza mara nne.

Kwa mara nyingine, katika michuano ya mwakani ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, ni Yanga na Simba ndizo zitakazokwenda kuipeperusha bendera ya Tanzania.

Yanga, ambao msimu uliopita walitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wataelekea kwenye kivumbi cha Ligi ya Mabingwa, huku mahasimu wao Simba walioshika nafasi ya pili wakijaribu kulisaka taji la Kombe la Shirikisho, ikiwa ni mara yao ya kwanza kucheza michuano ya kimataifa tangu mwaka 2011.

Hata hivyo, kuelekea mashindano ya kimataifa, dirisha dogo la usajili linatarajiwa kufunguliwa Novemba 15, kipindi ambacho kinaweza kuwa muhimu zaidi kwa timu hizo.

Ni kipindi ambacho makocha Omog na mwenzake George Lwandamina ‘Chicken’ wa Yanga wanatakiwa kuwa ‘bize’ kuvifanyia marekebisho vikosi vyao.

Ikumbukwe kuwa baada ya kipindi hicho cha usajili kitakachomalizika Desemba 15, wakufunzi hao hawatakuwa na nafasi nyingine ya kuongeza wachezaji kwenye vikosi vyao.

Kwa mujibu wa kanuni za Caf, baada ya kipindi hiki cha usajili, Simba na Yanga zitaweza kusajili wachezaji wengine endapo zitaweza kutinga hatua ya makundi.

Je, licha ya kuuanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Bara, ni kweli ubora wa vikosi vya Simba na Yanga unaakisi ugumu wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho?

Aina ya wachezaji waliopo Yanga na Simba wanaweza kuzisaidia timu hizo kufanya vizuri  katika michuano hiyo mikubwa? Hicho ndicho wanachotakiwa kujiuliza makocha George Lwandamina na Omog kabla na hata wakati wa usajili ujao.

Ukiitazama Simba, utagundua kuwa licha ya ubora wake, bado kikosi hicho cha Omog kimekuwa na kasoro na kama Mcameroon huyo hatazifanyia kazi, basi huenda kikaishia kuwa wasindikizaji kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.

Tatizo kubwa lililopo kwenye kikosi cha Wekundu hao wa Msimbazi ni katika safu yake ya ushambuliaji, ambayo kwa kiasi kikubwa imekuwa ikimtegemea Emmanuel Okwi.

Takwimu zinaonesha kuwa mastraika Jonh Bocco na Laudit Mavugo wameshindwa kwenda sambamba na kasi ya mpachika mabao huyo raia wa Uganda.

Wakati Simba ikiwa imeshafunga mabao 21 tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Okwi ameshazipasia nyavu mara nane akiwaacha mbali Bocco na Mavugo ambao kwa pamoja wamefunga mabao matatu pekee, yaani zaidi ya mara mbili ya mwenzao huyo.

Mabao mengine sita yamefungwa na safu ya kiungo; Shiza Kichuya aliyetupia matano na Muzamir Yassin mwenye mawili.  Kwa takwimu hizo, ni wazi mbio za Simba katika kuufukuzia ubingwa zinaweza kuzima endapo Okwi atakuwa majeruhi.

Unawezaje kwenda kwenye michuano ya kimataifa ukiwa na aina hiyo ya utegemezi wa mshambuliaji mmoja? Ni wazi Omog anatakiwa kuliangalia hilo kwa jicho la tatu.

Lakini pia, Yanga nayo inaelekea kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa ikionekana wazi kutompata mtu sahihi aliyeweza kuziba pengo la kiungo wake wa pembeni Simon Msuva ambaye alitimkia Morocco kujiunga na Difaa El Jadidi ya Ligi Kuu nchini humo.

Kwa bahati mbaya, si Emmanuel Martin, Pius Busita wala Baruani Akilimali, aliyeweza kuvivaa viatu vya winga huyo wa zamani wa Mtibwa, japo wamejaribu kwa uwezo wao kuisaidia Yanga.

Kwa kuzingatia ugumu wa michuano ya Ligi ya Mabingwa, hakuna shaka kuwa Lwandamina atahitaji kukitumia kipindi cha dirisha dogo la usajili kuziba pengo la Msuva, ambaye Yanga waliutegemea zaidi upande wake wa kulia kupandisha mashambulizi.

Lakini pia, Lwandamina atalazimika kuliangalia upya eneo lake la kiungo, ambalo huenda udhaifu wake umefichwa na uwezo mzuri wa Papy Tshishimbi raia wa  Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

Nyota huyo wa zamani wa Mbabe Swallows ni kiungo wa ulinzi na amekuwa akiifanya kazi hiyo kwa ustadi mkubwa tangu alipotua nchini, lakini anahitaji ‘patna’ wake katika eneo hilo.

Suala la kiungo mshambuliaji Yanga ni kama halionekani kuzungumziwa sana ingawa ukweli ni kwamba eneo hilo sasa haliwezi kumtegemea tena mchezaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Thaban Kamusoko.

Licha ya uwezo wake mzuri wa kumiliki mpira na kupiga pasi ‘zenye macho’, umri mkubwa alionao na majeruhi vinaweza kuwa vikwazo kwake kukabiliana na mikimiki ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Rafael Daudi, ambaye msimu uliopita alikuwa moto wa kuotea mbali katika safu ya kiungo ya Mbeya City, akifunga mabao nane, ameshindwa kuwa kwenye kiwango chake tangu alipotua Jangwani.

Huenda mapungufu yaliyopo kwenye vikosi vya timu hizo yakaonekana si makubwa sasa kutokana na udhaifu wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini, kama Omog na Lwandamina hawatalitumia vema dirisha la usajili litakaloanza Novemba 15, basi huenda ubora wa timu zilizopo kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho ukaibua kasoro hizo na hatimaye Simba na Yanga kurudi nyumbani mapema.