Home Michezo Kimataifa Usajili wa Hazard, La Liga inavyoitesa EPL

Usajili wa Hazard, La Liga inavyoitesa EPL

1371
0
SHARE

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

USAJILI wa Eden Hazard umeendelea kuwa gumzo kwa siku kadhaa sasa lakini kubwa ni kwamba si tu Chelsea, bali hata Ligi Kuu ya England (EPL) imepoteza staa wake.

Hazard mwenye umri wa miaka 28 raia wa Ubelgiji, amekwenda Real Madrid, mabingwa mara 13 wa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya Chelsea kukubali kupokea kitita cha euro milioni 140.

Kwa upande mwingine, huo ni mwendelezo wa utemi wa Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ mbele ya EPL kwani ni miaka 10 sasa, Real Madrid na Barcelona zimekuwa zikijichukulia wanasoka wanaowika England.

Akiwa kwenye ubora wake katika kikosi cha Manchester United, Cristiano Ronaldo alielekea Madrid mwaka 2009, usajili wake ukigharimu kitita cha euro milioni 94.

Hadi anaondoka zake Santiago Bernabeu akielekea Juventus mwaka jana, akiwa amefunga mabao 450 na kuipa Madrid mataji manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, nyota huyo alikuwa ameipa umaarufu mkubwa La Liga, hasa kwa upinzani wake na Lionel Messi.

Baada ya Ronaldo, La Liga walipiga hodi kwa mara nyingi pale EPL na safari hii alikuwa ni Luka Modric waliyemng’oa Tottenham kwa ada ya euro milioni 35.

Akishirikiana na Toni Kroos katika eneo la kiungo, waliifanya Madrid kuwa tishio barani Ulaya na itakumbukwa kuwa mwaka jana alikuwa mchezaji wa kwanza kuibeba Ballon d’Or mbele ya Ronaldo na Messi.

Mwaka mmoja baada ya Modric kutimka EPL, Madrid walirejea EPL na kumchukua Gareth Bale, ambaye pia alikuwa mchezaji wa Tottenham. Hiyo ilikuwa mwaka 2013 na usajili wake uliigharimu Madrid kitita cha euro milioni 101.

Bale alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshinda taji la 10 la Ligi ya Mabingwa katika msimu wake wa kwanza, akifunga bao muhimu katika mchezo wa fainali dhidi ya Atletico Madrid.

Luis Suarez ni mchezaji mwingine aliyekuwa kwenye kiwango bora akiwa Liverpool lakini Barca walimfikia mwaka 2014 na kisha kumchukua kwa ada ya euro milioni 81.

Kutokana na ‘kombinesheni’ yake nzuri na Daniel Sturridge katika eneo la ushambuliaji, waliitikisa England na kukaribia kuipa Liverpool taji la Ligi Kuu msimu wa 2013-14.

Liverpool walijikuta wakilia tena mwanzoni mwa mwaka jana baada ya Barca kutua tena klabuni hapo, safari hii wakiitaka kwa staili yoyote huduma ya kiungo wa Kibrazil, Philippe Coutinho.

Bahati mbaya kwa EPL, Barca walifanikiwa kukamilisha usajili wake kwa kutoa euro milioni 130. Tofauti na wenzake waliokwenda La Liga, hayajaonekana kwenda vizuri kwake.

Msimu uliopita, ambao ni wa kwanza kwake tangu atua Camp Nou, Coutinho aliingi mara 22 tu katika kikosi cha kwanza cha Barca, takwimu za mechi za Ligi Kuu.

Hata hivyo, licha ya ubabe wa La Liga kwa EPL katika soko la usajili kuwa wa muda mrefu sasa, bado kuna kila dalili kuwa utaendelea. Unajua kwanini?

Kipindi hiki cha usajili wa dirisha kubwa, majira ya kiangazi, Madrid na Barca zinafuatilia baadhi ya mastaa wanaofanya vizuri England. Ni kwa maana kwamba, huenda Hazard anaweza kuwa si mchezaji wa mwisho kubebwa na La Liga.

Mfano mzuri ni kile kinachoendelea kati ya Madrid na nyota Paul Pogba, Christian Eriksen, David de Gea, Sadio Mane. Pia, usisahau kuwa Barca wanavutiwa na Alexandre Lacazette. Lolote linaweza kutokea.