Home Makala USAJILI WA MELI NI CHANGAMOTO MPYA YA MUUNGANO

USAJILI WA MELI NI CHANGAMOTO MPYA YA MUUNGANO

1369
0
SHARE

NA HILAL K SUED

‘Bendera ya Urahisi’ – (kwa Kiingreza Flag of Convenience) ni aina ya biashara ambapo mmiliki wa meli huisajili meli yake ya shughuli za kibiashara (merchant ship) katika nchi nyingine isiyo makazi ya mmiliki huyo, na meli hiyo hupeperusha bendera ya nchi hiyo nyingine na huitwa ‘bendera ya nchi’ (flag of state).

Sheria za kimataifa zinataka kila meli ya kibiashara kujisajili katika masijala iliyofunguliwa na mojawapo ya nchi zinazosajili meli na baada ya kusajiliwa meli hizo hulazimika kuheshimu sheria za nchi hiyo, sheria ambazo hutumika iwapo meli itakiuka sheria kuhusu usajili wa majini na sheria nyingine.

Mtindo huu wa ‘Bendera ya Urahisi’ ulianza tangu miaka ya 50 na sababu kubwa ya wamiliki wa meli kuzisajili meli zao nchi nyingine ni katika jitihada za ama kukwepa gharama kubwa, ushuru na kodi nyingine, au kukwepa sheria na kanuni kali za nchi yake kuhusu usafiri wa majini na usalama wa mabaharia wake.

Hapa Tanzania usajili wa meli wa aina hii sasa hufanyika na mamlaka ya Zanzibar ya Usafiri wa majini – Zanzibar Maritime Agency (ZMA) chini ya taasisi ya Tanzania Zanzibar International Register of Shipping (TZIRS). Lakini usajili wa meli ambao umekuwa ukifanywa na taasisi hiyo kupitia wakala wake kampuni ya Philtex ya Dubai umekuwa ukikumbwa na matatizo ya mara kwa mara.

Kukamatwa hivi karibuni kwa meli zilizosajiliwa Zanzibar na kubeba bendera ya Tanzania na maandishi ubavuni mwake ‘ZANZIBAR TANZANIA’ ambazo moja ilikutwa inabeba shehena ya dawa za kulevya na nyingine silaha si tukio la kwanza katika ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Kutokana na uzito wa suala zima kwa Jamhuri ya Muungano tayari Rais John Magufuli ametoa maagizo kadha yakiwemo mamlaka husika za usajili kisitisha zoezi la kusajili wa meli na kwamba zile zote zilizosajiliwa tayari zifanyiwe uchunguzi iwapo zinafanya kazi zao kufuatana na masharti ya usajili wake.

Hata hivyo ni suala gumu sana kuchunguza mamia ya meli zilizosajiliwa hapa nchini iwapo zinafanya shughuli halali kutokana na meli hizo kuzagaa sehemu mbali mbali duniani huku ukubwa wa dunia yenyewe unajulikana.

Akizungumza na gazeti moja la Kiswahili la kila siku wiki iliyopita, Waziri wa Mawasiliano na Miundombinu katika serikali ya Zanzibar, Rashid Seif Suleiman, alikiri meli hiyo iliyobeba dawa za kulevya kusajiliwa Zanzibar mwaka 2011.

Lakini alidai katika biashara ya meli, hizo ndizo changamoto ambazo zinaikabili, ya kukosa uwezo wa kutambua mmiliki au wafanyakazi wa meli hizo wanabeba nini.

Alisema biashara ya meli ni ngumu kwani meli ikishasajiliwa ni vigumu kujua wafanyakazi wa meli hiyo wanabeba nini, wakati mwingine hata mmiliki wa meli husika hajui, lakini alidai jambo hilo linafanyiwa kazi.

Mkurugenzi wa ZMA, Abdi Maalim, alinukuliwa na gazeti hilo akisema kuwa kupitia Philtex, hadi mwaka jana Zanzibar ilikuwa imesajili meli 400 na kati yao zingine ni mbovu, zimeondolewa sokoni na nzingine kuuzwa na kubaki meli 170 ambazo zinafanya kazi.

Aidha alikanusha kwamba mfumo wa usajili na sheria ya Zanzibar zinavyotumika kusajili meli hizo ni dhaifu na kuwa matatizo ya kukamatwa kwa meli hizo yangeweza kutokea mahali popote.

Kauli yake ya mwisho ni kweli tupu. Ukiukwaji wa sheria za kimataifa kuhusu meli zilizosajiliwa hauiandami Tanzania tu, hutokea kwa nchi mbali mbali nyingine. Lakini kwa Tanzania kuna kitu kimoja kinachojitokeza kila ukiukwaji huu unapoibuka – nani wa kubeba lawama kati ya Serikali ya Zanzibar (SMZ) na ile ya Tanzania (Jamhuri ya Muungano).

Usajili wa meli unaofanywa na mamlaka za Zanzibar na yanayotokea baadaye yanakumbusha methali moja ya Kiingereza inayosema, “huwezi kufaidi mazuri ya dunia zote mbili” (‘you cannot have the best of both worlds’). Zanzibar haiwezi kufaidi mambo yote mawili wakati mmoja – yaani muungano na uhuru kamili.

Kama nilivyosema hapo ZMA imekuwa ikisajili meli kupitia wakala wake wa usajili ambaye ni kampuni ya Philtex ya Dubai. Utaratibu huo, ulianzishwa baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kujitoa kwenye Sheria ya Usafiri wa Majini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2003, na kuunda sheria yake ya Usafiri wa Bahari ya Zanzibar ya mwaka 2006 ambayo
iliunda ZMA.

Sheria ya awali ya Muungano, iliweka masharti magumu kidogo ya usajili ambayo ni pamoja na kutoruhusu usajili wa chombo chochote cha baharini chenye umri wa zaidi ya miaka 15.

Aidha, sheria hiyo pia iliweka masharti ya kuweka sharti kwamba kila chombo cha baharini kinachosajiliwa Tanzania, kiwe na hisa ya asilimia 50 kwa Mtanzania na lengo likiwa ni kuweka udhibiti wa mchezo mchafu unaoweza kufanywa kupitia vyombo vya kimataifa vya maji.

Kuna madai kwamba udhaifu wa Sheria ya Mamlaka ya Usafiri wa Baharini ya Zanzibar (ZMA) ya mwaka 2006, umekuwa ukiichafua Tanzania katika usafiri wa majini duniani, baada ya sheria hiyo kutoa nafasi ya kusajiliwa ovyo kwa meli za kimataifa bila udhibiti.

Sakata la hivi karibuni la kukamatwa kwa meli zizlizosajiliwa na mamlaka ya serikali ya Zanzibar zilizobeba shehena haramu si tukio la kwanza lililotokea na kuiweka serikali ya Muungano katika mtihani mkubwa katika ya mahusiano yake na nchi za nje na taasisi nyingine duniani.

Karibu miaka sita iliyopita (2012) Tanzania (kwa maana serikali ya Jamhuri ya Muungano) ilijikuta ikijibu lawama ya kusajili meli za Iran zilizokuwa zikibeba mafuta kwenda sehemu mbali mbali duniani, meli ambazo zilisajiliwa Zanzibar.

Ikumbukwe kwamba wakati huo Iran ilikuwa imewekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa (Baraza la Usalama) kufuatia na msukumo wa nchi za magharibi ambazo zimekuwa zikidai kwamba Iran inaendeleza mradi wake wa nyuklia kwa ajili ya kutengeneza zana za kivita, tuhuma ambazo nchi hiyo ilikuwa ikizikana. Nchi za magharibi, hususan Marekani, Uingereza na Ufaransa zina ushawishi mkubwa katika Baraza hilo.

Vikwazo hivyo vilikuwa vinasimamiwa na nchi hizo za Magharibi, hususan Marekani na vilihusisha vikwazo vya uchumi – hususan sekta ya mafuta ya Iran. Nchi hizo za magharibi zilisusia kununua mafuta kutoka Iran na kuzionya nchi nyingine kutoiwezesha Iran kukwepa vikwazo, ikiwemo hili la kusafirisha mafuta yake.

Hivyo kwa mtazamo wa Marekani, Tanzania kusajili meli za Iran zinazosafirisha mafuta ni kinyume cha vikwazo vilivyowekewa Iran, na hasa ni kukiuka Amri ya Rais Barack Obama (Executive Order) ambayo aliisaini mapema mwaka 2012 ya kuiwekea vikwazo nchi yoyote itakayokiuka maazimio ya Baraza la Usalama kuhusu Iran. Hivyo Marekani iliionya Tanzania kwamba ni lazima ifute usajili wa meli hizo la sivyo nayo ingepambana na vikwazo.

Barua ya onyo hilo ilipelekwa kwa rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, na si kwa rais wa serikali ya Zanzibar. Bila shaka hii inatokana na ukweli kwamba kimataifa, Zanzibar haitambuliwi kama nchi huru.

Kwa upande wake, serikali ya Zanzibar, kupitia taarifa iliyosomwa katika Baraza la Wawakilishi na Waziri wake wa Miundombinu na Mawasiliano (wakati ule), Hamad Masoud Hamad, ilijitetea kwa hatua hiyo ya kuzisajili upya (re-registration) meli hizo ingawa inasema meli zote zile 11 zilizopewa usajili hazikuwa za kampuni za Iran, bali ni za makampuni ya nchi nyingine kama vile Malta, Tuvalu na Seychelles na Cyprus, kauli ambayo ilipingana na ile ya Marekani katika barua yake kwa Rais Kikwete iliyosema kuwa angalau meli sita kati ya hizo zilikuwa zinamilikiwa na makampuni ya Iran.

Waziri Hamad Masoud alisema meli hizo zimeandikishwa chini ya Sheria ya Usafiri wa Bahari Zanzibar (Zanzibar Maritime Transport Act) ya mwaka 2006 ambayo inasimamiwa na    Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) ya mwaka 2009) ambayo ina mamlaka kamili ya kusajili meli katika daftari la kimataifa (International Shipping Registry) zitakazopewa usajili chini ya jina ‘TANZANIA ZANZIBAR.’

Hata hivyo, baada ya kusajiliwa, meli hizi zilibeba bendera ya Jamhuri ya Muungano, na siyo ile ya serikali ya Zanzibar – kutokana na kwamba Zanzibar kama nchi haitambuliwi kimataifa.

Kwa hali yoyote ile kuna utata mkubwa hapa, hasa iwapo kunatokea mgogoro, kama ya namna hii. Ukiachilia mbali suala la kuwapo kwa uhalali au la kuhusu vitisho vya Marekani, swali ni nani ilikuwa abebe mzigo wa vikwazo kutoka Marekani? Serikali ya Muungano au ile ya Zanzibar?

Matukio ya namna hii, pamoja na kuiweka nchi mahali pabaya, pia yanatoa changamoto kubwa kuhusu mfumo wa muungano wetu hasa katika mahusiano ya kimataifa. Aidha ni sehemu ya matukio mengine yaliyowahi kutokea nyuma ambayo pande mbili za muungano zilijikuta katika makabiliano.

Mara kadha serikali ya Muungano imekuwa ikijitokeza na kubeba lawama kutokana na shutuma kutoka nchi na taasisi za kimataifa kuhusu madudu yanayotokea kule Visiwani hasa katika masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu – inafanya hivyo kwa sababu tu serikali ya Zanzibar haitambuliki kimataifa.

Na serikali ya Muungano imekuwa ikifanya hivyo kwa ‘utiifu’ mkubwa, tena kimya kimya bila yenyewe kulalamika. Ni vigumu kujua iwapo serikali ya Muungano imekuwa ikiikaripia serikali ya Zanzibar kwa mwenendo wa namna hii unaoiweka Tanzania katika mwanga hasi kimataifa. Nitatoa mifano.

Wakati wa utawala wa “komandoo” – Dk Salmin Amour, hasa katika kipindi cha baada ya ujio wa mfumo wa vyama vingi (1992-2000) kulikuwapo vitendo kadha vya ukiukwaji wa misingi ya haki za kibinadamu na sheria nyingine za nchi vilivyokuwa vinafanywa na watawala vilivyotokana na shughuli za kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani, hususan wakati wa zoezi la uandikishaji wapigakura, kampeni za uchaguzi na wakati wa uchaguzi wenyewe.

Zaidi ya mara moja au mbili katika kipindi hicho ripoti za kila mwaka za Shirika la Haki za Binadamu duniani (Amnesty International) zilikuwa zinaituhumu Tanzania (kwa maana ya Serikali ya Muungano) kwa ukiukwaji huo.

Nazo baadhi ya nchi za magharibi zinazotupatia misaada ya kiuchumi, kama vile Norway, zimewahi kuilalamikia Tanzania kwa uminywaji wa haki kule Visiwani, hasa katika uchaguzi wa mwaka 2000 na nchi hiyo ilidiriki hata kutishia kusimamisha misaada yake.

Lakini hakuna tukio kubwa lilioitia doa Tanzania kama lile la mauaji ya makumi wa wafuasi wa chama cha upinzani – Chama cha Wananchi – (CUF) wasiokuwa na silaha kule Pemba tarehe 27 Januari 2001 baada ya kupigwa risasi na polisi. Tukio hilo lilitokana na mwenendo wa uchaguzi wa mwaka 2000 na matokeo yake. Wafuasi hao walikuwa wakiandamana kudai, pamoja na mambo mengine, tume huru ya uchaguzi.

Itakumbukwa tukio hilo lilisababisha, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, wakimbizi kutoka nchi hii kwenda nchi ya jirani ya Kenya. Kuna baadhi ya watu, wakiwemo wanasiasa (na baadhi ya vyombo vya habari) walipenda kuonyesha kuwa wakimbizi hao ni wa kutoka Pemba. Isisahauliwe kwamba kwa miaka mingi Tanzania ndiyo ilikuwa mpokeaji mkubwa wa wakimbizi kutoka jirani waliokuwa wanayakimbia machafuko nchini mwao.

Hata hivyo tuhuma nyingi zilizokuja kutokana na tukio hilo kutoka nchi mbali mbali zilielekezwa kwa serikali ya Muungano, na siyo ile ya Zanzibar. Hii inatokana na ukweli kwamba kimataifa, inayotambuliwa ni Tanzania na siyo Zanzibar.

Hii ina maana kwamba wale wanaotetea kuvunjika kwa Muungano, pia wakubali kwamba itabidi wawe wanaubeba mzigo wao wenyewe, kujikosha au kujieleza mbele ya jumuiya ya ulimwengu iwapo wataendelea na mambo hayo.