Home Makala USHINDI WA CCM NA WALAKINI MKUBWA … (2)

USHINDI WA CCM NA WALAKINI MKUBWA … (2)

1059
0
SHARE

NA JULIUS MTATIRO


ALHAMISI iliyopita tuliangalia sababu za kidola zilizoibeba CCM kwenye uchaguzi wa marudio wa kata 20 Tanzania Bara na Jimbo la Dimani Zanzibar, lakini tulizitumia kujadili hali halisi ya sababu za ushindi wa CCM katika chaguzi mbalimbali.

Sababu hizo kwa kweli zilitaka kuonesha yanahitajika mabadiliko makubwa ya katiba ya nchi yetu, sheria zetu, kanuni zetu na mwenendo wa usimamizi kwa kusaidiwa na vyombo vyote vya dola.

Pamoja na kuonesha upande huo muhimu wa kwanini CCM inapata ushindi mkubwa, Alhamisi ya leo nataka tuangalie sababu za ndani ya vyama vya upinzani bila kuzingatia zile zinazosababishwa na dola.

Vyama vya upinzani vya Tanzania vina matatizo makubwa ya ndani ya kujisababishia na yanayotokana na sintofahamu nyingi ndani ya vyama vyenyewe. Sababu nyingi kati ya nitakazozieleza hapa ambazo zimesababisha vyama vya upinzani vianguke zinafahamika ndani na nje ya vyama.

Viongozi muhimu ndani ya vyama mbadala wanazijua sababu hizi na kwa kweli wameendelea kuzikalia. Hizi zisipofanyiwa kazi basi kuiondoa CCM madarakani itakuwa ni safari ndefu zaidi na itakayohitaji moyo mkubwa zaidi.

Sababu ya kwanza ni ubinafsi ndani ya vyama mbadala. Inafahamika walau kwa uzoefu wa bara la Afrika, kwamba vyama dola vilivyodumu muda mrefu madarakani viliondolewa kirahisi baada ya vyama mbadala kuungana au kushirikiana kwa dhati na kumaanisha.

Ukiangalia Ghana, Nigeria, Malawi, Msumbiji, Kenya, Zambia na kwingineko kanuni iliyotumika ni hiyo tu – unganeni, shikamaneni, aminianeni, gawaneni maeneo ya kupambana na ondoeni chama dola kirahisi.

Kinyume chake ni msiungane, msishikamane, msiaminiane na msigawane maeneo ya kupambana ili nyote mkiwa mmoja mmoja mwingie vitani dhidi ya chama dola muishie kugawana kura nyie kwa nyie na baadaye chama dola kishinde kirahisi.

Ubinafsi katika vyama mbadala ni sumu mbaya sana. Na ubinafsi huu upo wa aina mbili. Aina ya kwanza ni pale ambapo hata baada ya makubaliano ya ndani ya vyama ya namna ya kwenda kwenye mapambano, mshirika mmoja au wawili wanaamua kutoheshimu makubaliano hayo na kuvamia maeneo ya mshirika mwingine na kuweka mgombea.

Haya hutendeka huku viongozi wakuu wa vyama wakiyaona na wakikaa kimya, ama wakipiga kelele kidogo na kujificha au kunyuti kabisa.

Viongozi washirika ambao wagombea wao wameingilia maeneo yaliyo chini ya chama kingine mshirika hupenda kujidai kuwa hali hiyo inasababishwa na wanachama wa chini kwenye kitongoji/kijiji/mtaa/kata au jimbo na kwamba wao katika ngazi ya taifa hawahusiki.

Hii ni sababu ya kijinga sana kwani inafahamika kuwa kwa mifumo ya vyama vyetu hapa Afrika maamuzi mengi yanafanyika juu kwenda chini na hayaanzii chini kwenda juu.

Na ndiyo maana kwenye mazingira au masuala mengine yoyote yale, hata yakiwa muhimu kiasi gani, wanachama wa chini hukisikiliza chama chao ngazi ya taifa kinasema nini.

Kwa hiyo sababu ya viongozi wakuu wa vyama washirika kwenye miungano au mashirikiano ya vyama, ya kwamba wanachama wa ngazi ya chini ndiyo wameweka mgombea katika eneo lisilo lao, ni sababu ya ovyo kabisa na isiyo na maana yoyote.

Ukweli ni kuwa sababu hiyo huwa ina sababu nyingine ndani yake. Wazungu wangeliita hii sababu “protectionism” (kujilinda) au mimi nitaiita kwa kimombo “conservatism” (uhafidhina) na nakuomba wewe msomaji uiite “extreme selfishness” (ubinafsi uliopitiliza).

Vipo vyama vya siasa au viongozi wa vyama vya siasa ambao wanaamini kuwa ukombozi wa nchi utakapopatikana wao ndio wanapaswa kuwa na sehemu kubwa ya mchango, hili si wazo baya, ubaya wake ni pale ambapo chama au viongozi wake wanang’ang’ania kuwa na mchango hata katika maeneo ya wenzao au ambayo si ya kwao.

Ubinafsi wa namna hiyo ni adui mkubwa wa maendeleo ya mapambano dhidi ya vyama dola na vinavyotumia nguvu kubwa kubakia madarakani.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, vyama mbadala vilikosa majimbo zaidi ya 30 kwa sababu ya ubinafsi huu lakini usingeliweza kumlaumu mtu kwani vyama havikuwahi kufanya ushirikiano wa kweli hadi wakati huo.

Mwaka 2015 ambapo kulikuwa na ushirikiano wa maana na wa mara ya kwanza kihistoria vyama mbadala vilipoteza majimbo mengi zaidi kwa sababu ya ubinafsi huu na mwisho wa siku CCM ndiyo ilikuwa msheherekeaji.

Mathalani, CUF ilipoteza majimbo mengi kwa kuingiliwa na Chadema huku Chadema ikipoteza majimbo kadhaa kwa kuingiliwa na CUF, hapo hujataja NCCR pia n.k. Kwa kuyahesabu majimbo yaliyopotea kutokana na ubinafsi huo katika uchaguzi wa mwaka 2015 yanafika 30 tena. Hiyo ina maana kuwa bado kazi kubwa ya kuunganisha vyama mbadala Tanzania haijafanyika.

Ukizisogelea kata, vijiji na vitongoji utagundua kuwa hali ni mbaya zaidi. Vyama mbadala vinapambana vyenyewe kwanza karibia kila mahali nchini kwenye ngazi hiyo, halafu ndipo vinakuja kupambana na CCM, mchezo huo wa kijinga hauwezi kukuza upinzani nchini. Na kwa kweli kama vyama mbadala havitashughulikia “mchawi” huyu aitwaye ubinafsi, CCM itaendelea kutamba kwa sababu hakuna mbinu za kuiondoa. Kwa wale waliosomea masuala ya kijeshi na kivita wanajua, askari waliogawanyika na ambao hawana amri ya pamoja ni sawa na kundi la watu walioko mnadani, kila mtu anauza kitu chake kwa wateja wake kwa wakati wake na hata atakavyoondoka hapo mnadani na atakapokwenda, ni yeye mwenyewe ndiye anajua. Ukiwa na jeshi la namna hiyo vitani na hasa katika mapambano makubwa ya kuving’oa vyama vikubwa hapa Afrika, unakuwa umeshindwa kazi hiyo kabla vita haijaanza.

Ni upuuzi na ujinga wa kiwango cha shahada ya uzamivu na katika zama hizi ikiwa yupo kiongozi yeyote katika vyama mbadala aambaye bado anaamini kuwa yeye peke yake au chama chake au genge lake vinaweza kuiondoa CCM madarakani bila msaada wa pamoja wa kuviunganisha vyama vyote vyenye nguvu, asasi za kiraia, za kidini n.k, katika safari ya kuikomboa mama Tanzania, kiongozi huyo atizamwe kwa jicho kali sana na darubini zinazopenya miamba maana huyo si mmoja wa wasafiri wa ngalawa ya vyama mbadala.

Alhamisi ijayo tutaendelea kujadili sababu za ndani ya vyama vya upinzani wakiwemo mapandikizi, wasaliti na mambo mengine mengi kama sababu zinazokwamisha safari ya mapambano ya kidemokrasia nyakati za uchaguzi hapa Tanzania.

Tukutane tena Alhamisi ijayo.